Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Chadema yataka mfumo CCM kukabidhi madaraka

SERIKALI imetakiwa kuandaa mfumo wa kikatiba utakaowezesha chama cha upinzani kuongoza iwapo kile kinachotawala kitaondolewa madarakani. Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipokuwa akihutubia mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata za Mpapa, wilayani Momba na Myovizi, Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya.

Alisema kutokana na vuguvugu la siasa za mabadiliko zinazoendelea nchini, ni wakati mwafaka nchi ikawa na mfumo wa kikatiba na sheria kwa ajili ya kusimamia mabadiliko ya uongozi kufanyika kwa amani ili kuepusha nchi kuingia katika vurugu na mkanganyiko wa kisiasa.

Mbowe alisema ingawa hiyo inaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya, kutokana na umuhimu wake kwa ajili ya mustakabali mwema wa Taifa, ni vyema Watanzania wakaanza kuitafakari.
Alitola mifano wa Ghana ilivyopitia misukosuko kutoka utawala wa Jerry Rawlings kwenda chama cha upinzani cha Rais John Kufour.

Akiwanadi wagombea wa Chadema katika maeneo hayo, Mbowe alisema ni hatari kwa nchi kama Tanzania ambayo sasa inapitia kwenye wimbi kubwa la mabadiliko, kukosa mfumo huo wa kuhakikisha mabadiliko ya mpito kutoka utawala wa Serikali moja kwenda nyingine yanafanyika kwa amani na kulinda masilahi ya nchi bila vurugu.
“Ni muhimu sana kuwa na sheria itakayohakikisha 'transition' (kipindi cha mpito) kutoka Serikali ya chama fulani kwenda chama kingine au Serikali moja kwenda Serikali nyingine, kufanyika kwa amani na kwa kuhakikisha masilahi ya umma na nchi yanazingatiwa,” alisema na kuongeza:

“Lazima tuepuke hali kama hiyo. Wenzetu wale (Ghana) walijifunza, walipoingia madarakani wakaamua kutunga sheria ya kusimamia ‘transition period’ kutoka uongozi wa Serikali moja kwenda nyingine.”

“Watanzania wanaweza kujiuliza kwa nini Marekani inachukua siku 72 kwa Rais kuapishwa na kukabidhiwa rasmi mamlaka ya kuongoza nchi tangu achaguliwe? Ni kwa sababu kuna vitu vya muhimu sana vya kusimamiwa na kufanyiwa kazi kabla utawala mpya haujakabidhiwa Ikulu.”

Mbowe alisema hapa nchini upo mfano mzuri wa madhara ya kukosekana kwa sheria ya namna hiyo ya kusimamia kipindi hicho cha mpito.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alidai kwamba sehemu ya mabilioni ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) yalihamishwa kutokana na kukosekana kwa mfumo huo.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema wakati Marekani inachukua takriban siku 72 tangu uchaguzi na uongozi mpya kukabidhiwa madaraka ya kuongoza nchi, Tanzania inachukua wastani wa saa 48 pekee, akisema hali hiyo ni hatari kwa nchi kwani, kuna masuala ya msingi ambayo yanahitaji muda wa kutosha katika kufanya makabidhiano kutoka Serikali moja kwenda nyingine.

“Ni wakati mwafaka kuanza kufikiria kuwa na mfumo huu wa kikatiba na kisheria. Huwezi kutumia saa 48 tangu uchaguzi kufanyika kumkabidhi Rais mpya madaraka. Kwanza kwa muda huo nani anasimamia kikamilifu rasilimali za umma, nini hatma ya watumishi wa umma. Kuna masuala ya majeshi, nyaraka za siri na kila kitu, vitu ni vingi. Wenzetu walio makini na nchi zao wanajua umuhimu wa masuala kama haya. Wanapata muda wa kufanya 'orientation' (uelewa wa mazingira), alisema Mbowe na kuongeza:
“Ndiyo maana hapa kuna wakati watumishi wa Serikali wakaamua tu kuikumbatia CCM hata kama nao wameichoka, kwa sababu wanakuwa hawajui hatma yao ni nini kwenye Serikali au uongozi mpya, baada ya uchaguzi.

“Ghana katika kipindi hicho cha mpito kutoka Serikali moja hadi nyingine wameweka utaratibu wa mamlaka inayoongozwa na mtu ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa anasimamia rasilimali zote, nyaraka zote, zinakuwa zimeandikishwa, zinajulikana zikoje.”

Alisema lazima hatari hiyo izuiliwe kwa kuwa wakati Serikali mpya ilivyoingia Ghana, waliokuwepo madarakani walichoma moto nyaraka muhimu na kuharibu vitu, kitendo kilichosababisha Serikali iliyoingia madarakani kuhangaika kuanza upya.

Alisema kutokana na hali kama hiyo ni lazima wananchi waanze kudai mfumo huo kwani hivi sasa Katiba na sheria ziko kimya kitu kinachoweza kusababisha siku moja mtu akakabidhi ukuta wa Ikulu tu kukiwa hamna kitu ndani.

“Mfumo huo utahakikisha 'smooth exit' yaani wanaoondoka au anayeondoka aondoke kwa amani. Kwa sasa hakuna 'mechanism' (mfumo) yoyote ile, hakuna utaratibu, hakuna sheria, Katiba iko kimya. Tunataka 'smooth exit', 'smooth entry' (Kutoka kwa amani, kuongia kwa amani).”

“Watumishi wa umma wawe na uhakika wa kuwepo kwa Serikali, bila hivyo nchi inaweza kuingia kwenye machafuko kwa sababu tu watawala waliokuwepo hawataki kuondoka.”

Mwenyekiti huyo yuko kwenye ziara ya kuwanadi wagombea udiwani wa chama hicho katika kata mbalimbali za Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa, katika uchaguzi mdogo unaohusisha kata 29 nchini ambao umepangwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Source: Mwananchi 24 Oktoba 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO