Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yamwachia huru Alhaj Shaban Mintanga

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaj Shaban Mintanga aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya nchini Mauritius baada kumuona hana kesi ya kujibu.

Alhaj Mintanga, hadi kuachiwa jana, alikuwa amesota Gereza la Ukonga kwa takribani miaka minne, kabla ya kesi yake kutolewa hukumu.

Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib na kusababisha mtuhumiwa huyo aliyekuwa akitetewa na mawakili maarufu wa kujitegemea nchini, Jerome Msemwa na Yasin Memba, kurejea uraiani na kuungana na familia yake.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Dk.Twaib alisema, ameisikiliza kesi hiyo tangu ilipohamishiwa mahakamani hapo mwaka juzi, ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako upande wa Jamhuri ili kuthibitisha kesi yao, walileta mashahidi wanne na vielelezo.

Dk. Twaib alisema, baada ya kupitia kwa kina vielelezo na ushahidi uliotolewa na mashahidi hao wa upande wa Jamhuri, imebaini ni havifu na umeshindwa kuishawishi mahakama imuone Mintanga ana kesi ya kujibu, hivyo inamwachilia huru.

Jaji Dk.Twaib, akiuchambua ushahidi huo, alisema kwa mujibu wa cheti kilichotolewa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania na ambacho kilikuwa kimesainiwa na Mkuu wa tume hiyo, Christopher Shekiondo, kinaonesha dawa za kulevya alizokuwa akituhumiwa Mintanga kuzisafirisha kwenda Mauritius, zina uzito wa kilo 4.9 na cheti kilichotolewa na Interpol, kinaonesha zilikuwa na uzito wa kilo 6.

“Kwanza mahakama hii imejiuliza ni Shekiondo ndiye aliyethibitisha dawa zile aina ya Heroin zina uzito huo ambao unatofautiana na uzito wa ulitolewa na Interpol, mahakama imejiuliza ni kwanini basi upande wa Jamhuri umeshindwa kumleta mahakamani hapa Shekiondo ambaye anaishi Dar es Salaam ili athibitishe ni yeye ndiye aliyetoa cheti hicho, kinachoonesha uzito huo na kama kweli aliziona dawa hizo kwa zilizokamatwa kwa macho na kisha akazipima na kutoa hati ile.

“Kwani kuna baadhi ya mashahidi waliieleza mahakama kuwa, Shekiondo licha kutoa cheti kile cha kuonesha thamani ya dawa zile, hakuwahi kuziona kwa macho dawa hizo,” alihoji Jaji Dk.Twaib.

Jaji huyo alisema, hata hivyo ushahidi wa mashahidi hao umekuwa ukipingana, kwani mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya, lakini shahidi wa nne ambaye ni ofisa wa Jeshi la Polisi, Charles Ulaya, aliiambia mahakama kuwa, Mintanga alipaswa kushitakiwa kwa kosa kula njama tu, sio kusafirisha dawa hizo.

“Hata kama hivyo ndivyo kama alivyoeleza Ulaya, lakini mahakama hii imeona pia upande wa Jamhuri umeshindwa kulithibitisha kosa hilo la kula njama, kwani wameshindwa kuleta ushahidi unaoonesha Mintanga na wenzake hao walikaa wapi, lini, saa ngapi na wakapanga njama za kusafirisha dawa hizo haramu aina ya Heroin na kwa sababu hiyo, mahakama hii inamwachilia huru mshitakiwa, kwa sababu imemuona hana kesi ya kujibu,” alisema Jaji Dk.Twaib.

Aidha, Jaji huyo alisema, karibu mashahidi wote walikuwa wakilitaja jina la mtu mmoja aitwaye (Michael), ambaye hakuwepo mahakamani.

Naye Charles Ulaya ambaye ndiye alikuwa akipeleleza kesi hiyo, alisema jina la Michael walipewa na Interpool na siyo jina la Mintanga katika sakata hilo la kusafirisha dawa za kulevya, ambalo mwisho wake lilisababisha Mintanga kufunguliwa kesi hiyo mahakamani hapo.

Jaji huyo akipangua hoja ya mawakili wa Jamhuri, iliyodai kuwa namba ya simu ya Mintanga ndiyo iliyotumika kufanyia ‘booking’ kwenye kampuni za usafirishaji kwa njia ya ndege, alisema, baada ya kupitia vielelezo, amebaini ile namba ya simu ni mali ya ofisi ya BFT, na ndiyo maana namba hiyo ipo kwenye ‘headpaper’ za shirikisho hilo na kwamba, mfanyakazi yoyote wa shirikisho hilo anaweza kuitumia, hivyo simu ile siyo mali ya Mintanga binafsi ni mali ya shirikisho.

Source: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO