Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mwisho wa Bilionea Sambeke; Mfanyabiashara Aliyefariki kwa ajali ya Ndege Arusha

 

Arusha/Moshi

Kwa mara nyingine, Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imetikiswa, kutokana na kifo cha mfanyabiashara maarufu katika mikoa hiyo, Joseph Sambeke (49) maarufu kama Bob Sambeke.

Bob Sambeke alifariki dunia juzi jioni baada ya kuanguka na ndege ndogo aliyokuwa akiiendesha, kilomita moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Arusha wakati akitokea mkoani Kilimanjaro.

Huu ni msiba wa tatu katika muda wa mwezi mmoja kwani mwishoni mwa mwezi jana, Wakili na Mfanyabiashara maarufu mkoani Arusha, Nyaga Mawalla alifariki dunia, ikiwa ni siku moja tagu kufariki ghafla kwa mfanyabiashara mwingine wa madini wa mkoani humo, Henry Nyiti.

Ndege ya Sambeke aina ya MT 7- namba 5H-QTT ilianguka saa 12.34 jioni baada ya bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na uwanja huo.

Alijeruhiwa na baadaye alifariki akiwa njiani wakati akiwahishwa hospitalini na askari wa Magereza ambao wanaishi katika kambi alipoanguka. Mazishi yake yamepangwa kufanyika Alhamisi eneo la Karanga, Moshi.

Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo, na kueleza kuwa taarifa za awali zinaonyesha ndege hiyo ni mali ya marehemu Mawalla ambaye alikuwa mbia wa biashara na Bob Sambeki na imesajiliwa kupitia Kampuni ya Quality Tours & Travellers.

Hata hivyo, Wakili Alex Msando, ambaye pia alikuwa mshirika wa Mawalla, aliliambia gazeti hili kuwa Sambeke alikuwa ameinunua ndege hiyo kutoka kwa marehemu.

Dede alisema ndege hiyo, ilianguka mita 200 kutoka njia namba 8 ya kuruka ndege katika uwanja huo ikitokea Kilimanjaro, katika dakika 15 za muda wa nyongeza wa matumizi ya uwanja huo.

Alisema ndege hiyo ikiongozwa na rubani Bob Sambeki ina uwezo wa kubeba watu wanne akiwamo rubani. Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, walisema kabla ya kuanguka ndege hiyo, ilikuwa ikiyumba na iligonga mti mkubwa katika moja ya mabawa yake na kupoteza mwelekeo.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Julias Laizer alisema kwamba aliona ndege hiyo ikigonga mti na kuyumba, kisha kudondoka chini na ndipo askari wa magereza walipojitokeza kutoa msaada. Laizer alisema Sambeki alikuwa peke yake na alijeruhiwa kichwani.

Kifo chake

Taarifa za kifo chake zilianza kuzagaa kwa kasi juzi saa 2:00 usiku na kusababisha taharuki katika Miji ya Moshi na Arusha.

Mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Peter Kisima au Papaa aliyekuwa naye uwanja wa ndege muda mfupi kabla ya kuruka, alikuwa katika wakati mgumu kuamini kilichotokea. “Yaani naona kama vile naota siamini hizi taarifa mtu niliyekuwa naye muda mfupi tu uliopita sasa hivi ni marehemu? Hapana siamini, ”alisema Papaa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alisema kumbukumbu zinaonyesha ndege aliyokuwa akiendesha marehemu iliruka saa 10.00 jioni kwenda West Kilimanjaro.

Marehemu Sambeke ameacha wake watatu na watoto watatu ambao ni Sia, Getrude na Jamal ambaye amefuata nyendo za marehemu baba yake katika fani ya urubani.

Jamal ambaye anajifunza urubani katika Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) alisema amepokea msiba wa marehemu baba yake kwa mshutuko mkubwa.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Moshi, Mussa Juma na Moses Mashallah, Arusha.


Imeandikwa na MWANANCHI

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO