Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Sokoine azikwa upya • Mazishi yake yafanyika saa saba za usiku Monduli

WAKATI Aprili 12 mwaka huu Watanzania wanatimiza miaka 29 tangu Waziri Mkuu aliyeweka historia ya pekee nchini, Edward Moringe Sokoine alipofariki dunia kwa ajali ya gari, mwili wake umehamishwa kutoka kwenye kaburi la awali na kuzikwa katika kaburi jipya, Tanzania Daima Jumapili limebaini.

Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa marehemu Sokoine, zililiambia gazeti hili kuwa mwili wa waziri mkuu huyo ulizikwa kwenye kaburi jipya mwishoni mwa mwaka jana mjini Monduli.

Kwa mujibu wa habari hizo, mwili wa Sokoine umezikwa upya baada ya kaburi lake la awali kupasuka na kuharibika kutokana na tetemeko la ardhi lililotikisa milima ya Oldonyo Lengai mwaka jana na kusababisha maji kuingia ndani.

Mmoja wa watoto wa kiongozi huyo wa zamani, aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kaburi hilo kuharibika na kuchakaa, Rais Jakaya Kikwete aliagiza lijengwe upya.

“Lilipasuka kiasi kwamba ukimwaga maji yalikuwa yanaingia hadi ndani. Rais Kikwete aliagiza lijengwe upya na baadaye walitumwa wanajeshi ambao pamoja na ndugu tulikubaliana kuchimba kaburi jipya na kuhamishia mwili huo katika kaburi jingine,” alisema mtoa habari wetu.

Kwa mujibu wa habari hizo, shughuli za kuhamisha mabaki ya mwili huo na kuuzika upya katika kaburi jingine ilifanyika saa saba usiku na kushuhudiwa na watoto wote na baadhi ya ndugu wa marehemu walioko ndani na nje ya nchi.

Pia baadhi ya viongozi, akiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa walikuwapo.

Inaelezwa kuwa mwili huo uliozikwa ndani ya jeneza miaka 29 iliyopita bila kufukiwa na udongo, bado uko katika hali nzuri kabisa na hii inatokana na sindano aliyochomwa ambayo ina uwezo wa kuhifadhi mwili huo katika hali nzuri ndani ya miaka takriban 40.

“Sanduku lake bado zito na mwili upo kama ulivyokuwa wakati ule anaagwa. Tulitaka kuufungua na kuhamishia kwenye jeneza jingine la kisasa tuliloandaa, lakini mzee Lowassa ambaye ni baba yetu, alituzuia,” alisema mtoa habari wetu.

Alisema hivi sasa kaburi la awali alimozikiwa limefukiwa na kaburi jipya lipo jirani na lile la zamani likiwa katika hali na mwonekano mzuri.

Katika hali ya kushangaza, watoto wa marehemu Sokoine pamoja na baadhi ya ndugu bado wanakusudia kufanya uchunguzi upya wa mwili huo ili kubaini kama kweli kifo chake kilitokana na ajali aliyoipata au la.

Ikumbukwe kuwa wakati wa kifo chake kulikuwa na mjadala mzito, wengi wakidai aliuawa na kwamba kifo chake kilipangwa na mahasimu wake ndani na nje ya serikali ambao walikerwa na operesheni yake ya kupambana na wahujumu uchumi na mali za taifa.

Kwa mujibu wa habari hizo, wapo baadhi ya watoto na ndugu wanaoamini kuwa kwa jinsi msafara wa kiongozi mkubwa kama waziri mkuu unavyowekewa ulinzi, ni vigumu gari jingine kutoka upande wa pili na kuligonga gari lake, hivyo wanaamini aliuawa.

“Siku tuliyozika upya, ndugu wote tulikubaliana mwakani tuombe kibali cha serikali kuleta wataalamu kuchunguza ili kubaini chanzo cha kifo chake kama kilitokana na ajali au la.

“Lakini mzee Lowassa alituzuia, na kwa vile tunamheshimu sana kama baba yetu tuliukubali ushauri wake, lakini mwakani tumepanga tuufanyie uchunguzi mwili huo,” alisema mtoa habari wetu.

Kwa mujibu wa sheria, mwili ukishazikwa unaruhusiwa kufanyiwa uchunguzi baada ya miaka 30 na mwakani mwili wa Sokoine utafikisha umri wa miaka 30 tangu ulipozikwa na huo utakuwa muda muafaka kwa wana ndugu hao kutaka kujua ukweli wa kifo cha ndugu yao.

Sokoine alifariki dunia Aprili 12 mwaka 1984 eneo la Wami-Dakawa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Ilikuwa majira ya saa kumi jioni, Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza kifo chake kwa sauti ya huzuni.

Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma.

Wengi wanamuelezea kwamba alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa kwani aliishi kama alivyohubiri.

Sokoine si tu kwamba hakujilimbikizia mali, bali pia alipunguza hata mali zake ili apate nafasi zaidi ya kuwatumikia Watanzania.

Itakumbukuwa kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili 1984, Sokoine alikabiliana na hoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao ambapo alitamka: “Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge posho ya chakula chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea mishahara na marupurupu mengine.”

Baada ya kikao kile cha Bunge, Sokoine badala ya kupanda ndege ya serikali kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi kwa njia ya barabara, apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo.

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO