Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

RIPOTI YA UCHUNGUZI WA KAMATI NDOGO YA BARAZA LA MADIWANI ILIYOUNDWA KUCHUNGUZA UHALALI WA UFUTAJI WA MADENI YA MAPATO YA HALMASHAURI YA ARUSHA MJINI



RIPOTI YA UCHUNGUZI WA KAMATI NDOGO YA BARAZA LA MADIWANI ILIYOUNDWA KUCHUNGUZA UHALALI WA UFUTAJI WA MADENI YA MAPATO YA HALMASHAURI MWAKA WA FEDHA 2009/10, 2010/11, 2011/2012 NA KUPITIA MADENI INAYODAI HALMASHAURI KUFIKIA JUNI, 2016

1.0.    UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha uliofanyika tarehe 07/05/2016, Baraza liliteua Wajumbe watano (05) wakiwemo Mhe. Nanyaro E. Japhet, Mhe. Zakaria A. Mollel, Mhe. Credo A. Kifukwe, Mhe. Amani E. Reward na Mhe. Ricky N. Moiro kuunda Kamati ndogo kufuatilia uhalali wa ufutaji madeni ya Halmashauri katika miaka ya fedha 2009/10, 2010/11, na 2011/2012 na pia kupitia madeni yote ya Halmashauri kufikia Juni, 2016.

Katika kutekeleza kazi zake, Kamati imeshirikiana na Wataalam wa Halmashauri wakiwemo Ndg. Kessy Mpakata (Mweka Hazina wa Jiji), Bahati Chonya (Mwanasheria wa Jiji), Amos Ackim (Mkaguzi wa Ndani) na Tibilengwa S.K. Stephen (Mwandishi wa Kamati).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati hii walipokea barua ya uteuzi yenye Kumb.Na.CD/C.90/11/171 ya tarehe 16 Juni, 2016 iliyoiruhusu Kamati kuanza kazi ya uchunguzi. Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji iliipatia Kamati hadidu nne (04) za rejea kama ifuatavyo:-

i)             Kuchunguza uhalali wa kufutwa kwa madeni ya Mapato ya Ndani kati ya Mwaka wa Fedha 2009/10 – 2011/12 kiasi cha Tshs.843,137,112.00

ii)           Kupitia na kutoa mapendekezo juu ya madeni ambayo Halmashauri inavidai Vikundi vya Wanawake na Vijana hadi kufikia Juni 2016.  Kupendekeza namna bora ya kufuatilia madeni hayo na kupendekeza mfumo sahihi wa utoaji wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake na Vijana.
iii)          Kupitia na kutoa mapendekezo juu ya madeni mengine tofauti na yanayotajwa katika kipengele cha (i) na (ii) ambayo Halmashauri inadai hadi kufikia Juni, 2016.

iv)          Mambo mengine kama yanavyoweza kujitokeza wakati wa uchunguzi na kama Kamati itakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya uchunguzi wake, Kamati imepitia na kuchambua nyaraka mbalimbali ikiwemo barua ya Halmashauri kwenda kwa Katibu Mkuu TAMISEMI kuomba kufutwa kwa madeni hayo ya tarehe 28/02/2013, mikataba yote kati ya Halmashauri na Mawakala waliofutiwa madeni; Hati za Makubaliano zilizoondoa kesi Mahakamani, Muhtasari wa Kikao cha Kawaida cha Kamati ya Fedha na Utawala kuidhinisha kufutwa kwa madeni hayo cha tarehe 22/06/2011, Muhtasari wa Kikao cha Kamati ndogo ya usuluhishi cha tarehe 23/06/2011, Muhtasari wa Kikao Maalum cha Kamati ya Fedha na Utawala cha tarehe 30/06/2011, Muhtasari wa Baraza Maalum la Madiwani la tarehe 30/06/2011, Muhtasari wa Baraza la Kawaida la Madiwani la tarehe 08/09/2011 na 12/09/2011, ambapo vikao vyote hivyo vilijadili na kuidhinisha  kufutwa kwa madeni hayo ya Mawakala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilikutana na kuwasikiliza Viongozi wa Vikundi mbalimbali vinavyodaiwa na Halmashauri mnamo tarehe 15/07/2016 na ilipitia nyaraka mbalimbali zinazohusu madeni ya vikundi hivyo ikiwemo mikataba kati ya vikundi hivyo na Halmashauri. Kamati pia ilikuatana na wadaiwa wa madeni mbalimbali ya Halmashauri tarehe 17.08.2016 na kuwasikiliza juu ya sababu za kutolipa madeni ya Halmashauri hadi Juni 2016, kwa lengo la kutoa maoni stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuikamilisha kazi hii ya uchunguzi, Kamati ilikutana katika vikao saba (07) ambapo Kamati ilianza kazi katika kikao chake cha kwanza cha tarehe 24/06/2016 kwa Wajumbe kupokea nyaraka mbalimbali, kujadili mfumo upi utumike kufanya uchunguzi na Mawanda ya uchunguzi huo na kisha Wajumbe walimchagua Mhe. Nanyaro E.J. kuwa Mwenyekiti wa Kamati na Ndg. Kessy mpakata kuwa katibu. 

Katika kikao chake cha tarehe 28/06/2016, Wajumbe walipitia na kutengeneza hojaji kuhusu madeni ya Mawakala.  Tarehe 05/07/2016 Wajumbe walikutana na kujadili wakala mmoja baada ya mwingine.  Mnamo tarehe 15/07/2016 Kamati ilikutana na vikundi vya wanawake na vijana, tarehe 03/08/2016 Kamati ilipitia Ripoti ya awali juu ya madeni yaliyofutwa. Tarehe 17/08/2016 Kamati ilikutana na kuhojiana na wafanyabiashara wanaodaiwa na Halmashauri kufikia Juni, 2016 na Jumapili ya tarehe 28/08/2016 kamati ilikamilisha uchunguzi wake kwa kupitia ripoti ya mwisho na kuiidhinisha.





2.0.      UHALALI WA KISHERIA AU VINGINEVYO JUU YA HALMASHAURI KUYAFUTIA MADENI MAKAMPUNI SABA (07) YA UKUSANYAJI MAPATO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilipitia na kuchunguza nyaraka mbalimbali zilizoyahusu Makampuni yote saba (07) yaliyofutiwa madeni yakiwemo; Mkomilo Trade Centre (T) Ltd. (Wakala wa kukusanya ushuru wa mabasi madogo kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2009/2010), Makumira Filling Station (Wakala wa kukusanya ada na ushuru wa maegesho ya taxi, pick up na magari kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2010/2011), M/S Pigadeal Investment Ltd. (Wakala wa kukusanya ushuru wa Mapato Soko la Kilombero kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2010/2011, Jamahedo Health food Company (Wakala wa kukusanya ada ya maegesho ya magari kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2009/10, Aquiline Traders (T) Ltd. (Wakala wa kukusanya ushuru wa pango kwenye maduka, mabucha na migahawa kwa Mwaka wa Fedha 2009/10 na New Metro Merchandise Ltd. ambaye alikuwa Wakala wa kukusanya ushuru wa mabango/matangazo kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2010/11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia hitimisho la ama ilikuwa halali au vinginevyo kwa Halmashauri kuwafutia madeni Mawakala hao, Kamati ilitengeneza hojaji/maswali (issues) zifuatazo ambazo ndizo zilikuwa Msingi wa mapendekezo ya Kamati.

i)             Kulikuwa na uhalali gani na sababu gani toshelezi za Halmashauri kufikia maamuzi ya kuwafutia mawakala hao madeni baada ya mawakala hao kushindwa kulipa kwa malalamiko mbalimbali; Ni kwa namna gani ama kwa uzembe au kwa makusudi watumishi wa Halmashauri walishindwa kutekeleza wajibu wao?

ii)           Kulikuwepo na uhusiano gani ama wa kibiashara/kimaslahi kati ya mawakala na Halmashauri (Watumishi na Madiwani) katika mchakato mzima wa kufuta madeni hayo?

iii)          Je, makubaliano yote yaliyoingiwa kati ya Halmashauri na Mawakala na kupelekea Mawakala kufutiwa madeni yalisajiliwa Mahakamani?

iv)          Je, Kamati hii, na kwa mantiki hiyo Baraza lina uwezo kisheria kupendekeza suala hili kurejeshwa/kupelekwa Mahakamani kuwadai Mawakala hao waliofutiwa madeni endapo itaonekana kuna ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa kufuta madeni hayo?

v)            Je, Kamati na kwa mantiki hiyo Baraza lina uwezo kisheria na kikanuni kupendekeza Watumishi wote wa Halmashauri wakiwemo mkurugenzi aliyekuwepo, mwanasheria aliyekuwepo, waliohusika na kutoa Zabuni kwa Kampuni zinazomilikiwa na mtu mmoja, Afisa biashara aliyekuwepo kuchukuliwa hatua stahiki kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kutoa ushauri wa kitaalam?. Kama wataalam hawa wataonekana walikosea kutoa ushauri na kuhitajika kupendekezwa hatua za kinidhamu/kisheria kuchukuliwa dhidi yao, nini kifanyike juu ya kamati ndogo ya baraza la madiwani iliyoundwa hapo awali na kupendekeza kwa baraza mawakala hao kufutiwa madeni?
vi)          Je, Baraza lina uhalali kisheria wa kupendekeza Makampuni hayo yote yaliyokuwa mawakala wa Halmashauri katika ukusanyaji ushuru, yatangazwe kuwa Makampuni yasiyo na uaminifu “to be black listed” ili kuiepusha Halmashauri kufanya nayo biashara kwa siku zijazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutoa mapendekezo na maoni ya Kamati kwa mtiririko sahihi Kamati ilipitia nyaraka na maelezo kwa kila Wakala kama ifuatavyo:-

WAKALA MKOMILO TRADE CENTRE (T) LTD KUFUTIWA DENI LA TSHS.29,139,000.00
Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa, Kamati ndogo iliyoundwa, Kamati ya Fedha na Utawala na Baraza la Madiwani walifikia maamuzi ya kufuta madeni kwa sababu kuwa Wakala aliingiliwa kwenye eneo lake na Wakala aliyekuwa anakusanya ushuru wa mabasi stendi kubwa aitwaye DRM Investment na kwamba Wakala hakuonyeshwa mipaka ya kazi yake. 

Mheshimiwa mwenyekiti, kamati iliamua kupitia mikataba yote miwili yaani Mkataba Namba AMC/MAPATO-MABASI MADOGO/1/2009/2010      wa M/S MKOMILO TRADE CENTRE (T) na Mkataba Namba.AMC/MAPATO-MABASI MAKUBWA/1/2009/2010  wa M/S DRM INVESTMENTS  ili kujiridhisha juu ya maelezo yaliyotolewa hadi kufikia maamuzi ya kufuta deni hilo.

Kifungu cha kwanza (1) cha mkataba wa Mkomilo Trade Centre (T) kinasema, “Wakala atakusanya ushuru na ada hizo za Mabasi Madogo katika eneo la Halmashauri ya Maspaa ya Arusha kwa kuzingatia masharti yaliyomo kwenye mkataba huu”…… na kifungu cha kwanza (1) cha mkataba wa M/S DRM Investments kinasema, “Wakala atakusanya ushuru na ada hizo za Mabasi Makubwa katika eneo la Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kwa kuzingatia masharti yaliyomo kwenye mkataba huu”...

Sababu zilizotolewa kuhalalisha kufuta deni zinanukuliwa kama ifuatavyo, “sababu za kufuta deni ni kutokana na wakala wa stendi ndogo kuingiliwa kukusanya ushuru kwenye eneo lake na wakala aliyekuwa anakusanya ushuru wa Mabasi stendi kubwa aitwaye DRM Investment na kuwa hakuonyeshwa mipaka ya kazi yake madai ambayo Halmashauri iliyaona ni ya msingi na kukubali kufuta deni”.

Mhe. Mwenyekiti, Kamati inaona sababu zilizotolewa kuhalalisha kufuta deni hilo hazina msingi wowote. Hii ni kwa sababu, ukisoma vifungu viwili vya mikataba kama vilivyonukuliwa hapo juu, iko wazi kwamba mikataba ya mawakala hao wawili ilihusu aina ya magari na wala siyo aina ya stendi wala mipaka inayoongelewa. Mkomilo alipaswa kukusanya ushuru wa mabasi madogo na kwa maana hiyo mipaka yake ilihusu mabasi madogo tu. Na M/s DRM Investment alipaswa akusanye ushuru toka mabasi makubwa kwa maana hiyo mipaka yake ilikuwa mabasi makubwa tu. Katika mikataba yao hakukuwa na haja ya kuainisha maeneo ya mipaka ya ardhi bali walipaswa kukusanya ushuru eneo lote la Halmashauri wakitenganishwa tu na ukubwa wa magari.
Katika maelezo yaliyotolewa na Nyaraka zilizopitiwa ingawa Mkomilo alidai kuwa DRM Investment alikusanya ushuru wa mabasi madogo yaliyokuwa yanakwenda Namanga, hakuna mahali panapoonyesha kuwa Mkomilo aliwasilisha risiti inayoonyesha kuwa M/S DRM investment amekusanya ushuru toka mabasi hayo madogo.
Katika mazingira haya kamati haikubaliani kabisa na maelezo yaliyotolewa kuhalalisha kufuta deni hilo. Inaonekana dhahiri kuwa kamati iliyosuluhisha mgogoro ama haikuisoma mikataba hiyo, au ilikuwa na maslahi binafsi na Mkomilo Trade Centre (T) Ltd na kwa sababu hiyo kuamua kumpendelea na kuiumiza Halmashauri. Maelezo yaliyotolewa hayakuwa na msingi kwani waliyakubali tu malalamiko ya Mkomilo Trade Centre (T) Ltd bila kuyachambua kwa mujibu wa mikataba.
Kwa mazingira hayo ni dhahiri kuwa haukuwepo uhalali wa namna yoyote wa kuidhinisha kufutwa kwa deni hilo. Kamati haielewi hoja za kwamba mawakala waliingiliana katika stendi ndogo na stendi kubwa zilitoka wapi.  Inaonekana maamuzi yalifikiwa kwa shinikizo la kimaslahi au la uzembe kwa upande wa Halmashauri na Kamati ndogo iliyoundwa na kupendekeza madeni yafutwe. 
Hata kama ingedhihirika kuwa DRM investment ameingilia mkataba wa Mkomilo, ni kwa nini isingependekezwa DRM amfidie Mkomilo kiasi alichokusanya kimakosa badala ya kumsamehe Mkomilo deni la halmashauri ambayo haikuwa na makosa yoyote? Azimio la kamati ndogo kuwa, “ilionekana kuwa pande zote mbili kutokudai upande wa pili kwa sababu ya kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa mkataba huo” halina msingi wowote kimkataba na kwa hali hiyo, kuwepo kwa maslahi binafsi hakuepukiki. 


WAKALA MAKUMIRA FILLING STATION KUFUTIWA DENI LA TSHS.18,500,000.00
Sababu zilizotolewa ni kuwa Halmashauri ilipanda miti katika maeneo ya maegesho na hivyo kumpunguzia Wakala eneo la makusanyo. Baada ya kupitia kifungu cha kwanza (1) cha mkataba wake Namba. AMC/MAEGESHO/1/2008/2009 Kamati iliridhika kuwa ni kweli wakala alikuwa amepewa kazi ya kukusanya ushuru katika maeneo yote ya maegesho katika eneo zima la Halmashauri. Kwa maana hiyo, ni kweli kuwa zoezi la upandaji miti liliathiri makusanyo yake.

Hata hivyo, Kamati hairidhishwi na kiasi cha fedha ambacho alifutiwa. Hii ni kwa sababu katika nyaraka zilizowasilishwa, zinaonyesha kuwa baada ya zoezi la kupanda miti kuathiri kazi zake, wakala aliwasilisha malalamiko Halmashauri.
Halmashauri ilitoa wataalam ambao waliungana na wataalam wa wakala huyo kufanya tathimini ya namna gani zoezi la kupanda miti liliathiri mkataba. Kilichogundulika katika tathimini hiyo ni kuwa zoezi la upandaji miti lilimsababishia wakala hasara ya Tshs. 5,000,000.00. Swali la msingi hapa ni je, ni kwa nini alisamehewa Tshs. 18,500,000.00 badala ya Tshs. 5,000,000.00 ambayo ndiyo hasara aliyoipata?

Katika mazingira haya ni dhahiri kulikuwepo na msukumo fulani nyuma ya kamati na watendaji wa Halmashauri kufikia maamuzi hayo. Kwa maoni ya kamati wakala huyo angesamehewa hasara ya Milioni tano aliyoipata na kiasi cha Tshs. 13,500,000.00 kilipaswa kulipwa na hivyo Halmashauri haikustahili hasara hiyo iliyosababishwa kwa makusudi. Hata hivyo licha ya kuamua kumsamehe deni hilo na kuamua kumuongezea mwezi mmoja wa mkataba ili ajifidie, badala ya kuongezewa mwezi mmoja ofisi ya sheria ilimuongezea  miezi miwili na kukusanya kiasi cha Tshs.29,500,000.00 bila uhalali wowote na kinyume na maagizo ya baraza lililomfutia wakala huyo deni na kumpa mwezi mmoja ili ajifidie.

Ingawa kamati inakubaliana na ukweli kuwa kwa kawaida Halmashauri inabadilisha mipango yake mara kwa mara,  Kamati inashauri wakati mwingine Halmashauri iwe na mipango thabiti na pale inapolazimika kufanya shughuli fulani mfano matengenezo ya barabara, upandaji miti n.k. shughuli ambazo zinaathiri mikataba iliyoingiwa, ikutane na Mawakala ili kurekebisha mikataba hiyo kuepusha kuwepo migogoro isiyo na sababu na kuikosesha Halmashauri mapato.



WAKALA M/S PIGADEAL INVESTMENT LTD KUFUTIWA DENI LA TSHS.231,000,000.00
Sababu mbili zilitolewa katika kufikia maamuzi ya kufuta deni hilo ambazo ni kuwepo kwa masoko bubu yaliyosababisha Wafanyabiashara kushusha mazao katika masoko tofauti na Soko la Kilombero ambalo lilikuwa linatambulika kuwa ndilo Soko la mazao ya jumla, na pili kuwa maduka yaliyokuwa yamepangishwa kwa Watumishi wa Halmashauri na Waheshimiwa Madiwani yaligoma kulipa kodi.
Baada ya kupitia mkataba wa wakala huyo Namba.AMC/MAPATO-SOKO KILOMBERO/1/2010/2011 kamati iligundua kuwa ulikuwepo uzembe mkubwa kwa upande wa watumishi wa Halmashauri katika kutekeleza wajibu wao. Kulikuwepo na matatizo kuanzia jinsi mkataba ulivyoingiwa hadi jinsi ulivyotekelezwa.
Kwa mfano kifungu cha sita (6) cha mkataba kinasema, “Wakala atailipa fedha hizo mwezi mmoja kabla ya kuanza kukusanya mwezi mwingine,” lakini kifungu cha 9 (2) kinasema, “sababu mojawapo itakayoweza kupelekea kuvunjika mkataba huu iwapo wakala atashindwa kulipa hadi kufikiwa kwa kiwango cha dhamana yake ya kazi, dhamana hiyo itachukuliwa na manispaa na mkataba kuvunjwa wakati huohuo”.

Vifungu hivyo vya mkataba vikisomwa kwa pamoja, vinaonyesha mkanganyiko wa hali ya juu. Wakati kifungu cha 6 kinambana wakala kuhakikisha analipa kila mwezi, kifungu cha 9 (2) kinampa njia ya kutokea na kukwepa kwa kumpa mwanya wa kuegemea “bond”anayoiweka.

Mhe. Mwenyekiti, ukifanya mahesabu katika mkataba huu utagundua kuwa walioandaa na kusaini mkataba huo ama hawakujua wanachokifanya ama walikuwa wazembe, au walikuwa na maslahi binafsi. Hii ni kwa sababu wakala huyo alipaswa kulipa Tshs.576,000,000.00 kwa mwaka mzima (yaani 48,000,000.00x12). Asilimia 15 ambayo wakala alipaswa kuweka “bond” ni Tshs.86,400,000.00. Kwa kuchukua kiasi kilichopaswa kulipwa kwa mwezi (yaani 48,000,000.00) kiasi hiki cha “performance bond” ni Tshs.9,600,000.00 pungufu ya kodi ya miezi 2 (yaani 48,000,000x2 =96,000,000.00). 

Katika mchanganuo huo wa kihesabu, kipengele cha 9(2) hakikuwa na maana yoyote badala yake kipengele Namba 6 kilipaswa kiboreshwe kwa kuongeza maneno kuwa “wakala akishindwa kurejesha ushuru kwa mwezi husika hataruhusiwa kukusanya mwezi mwingine na hivyo atakuwa amevunja mkataba na kuwa wakala hatarudishiwa kiasi chochote alicholipa kwa ajili ya (‘performance bond’)”. Kama mkataba ungekuwa hivi, halmashauri isingepata hasara iliyoipata kwani ingeweza kuvunja mkataba mapema baada ya mwezi mmoja na kupata faida ya Tshs.38,400,000.00.
Mhe. Mwenyekiti, pamoja na kuandaliwa kwa mikataba inayoiumiza Halmashauri, kamati iligundua uzembe mkubwa uliofanywa na watendaji wa Halmashauri katika utekelezaji wa mkataba huu. Hii ni kwa sababu, mkataba ulianza kutekelezwa mnamo tarehe 09.08.2010, lakini hadi kufikia tarehe 4/02/2011 ambapo barua ya kumdai wakala iliandikwa (takribani miezi 6 baadae), Mkurugenzi alikuwa hajafanya chochote licha ya kuwa wakala huyo alikuwa hajawasilisha ushuru hata wa mwezi mmoja.

Licha ya kuwa tarehe 4/02/2011 Mkurugenzi alimwandikia wakala barua akimpa ilani ya kulipa deni ndani ya siku saba, na ingawa wakala hakulipa chochote, bado ilimchukua zaidi ya mwezi mmoja baadae kuvunja mkataba tarehe 09.03.2011.
Katika uchunguzi wake kamati ilikutana na kiinimacho ambacho ilishindwa kuelewa ni kwa namna gani Halmashauri ilifikia maamuzi hayo. Hii ni kwa sababu baada ya Halmashauri kufungua kesi mahakamani na baadae kuamua kuelewana nje ya mahakama, kamati ya usuluhishi ilipendekeza fedha kiasi cha Tshs. 102,000,000.00 zilizopaswa kulipwa na SGR/NFRA kama ushuru wa mazao zigawanye kati ya Halmashauri na Wakala.

Ingawa ni kweli kuwa wakala alipaswa kukusanya ushuru huo toka NFRA, kamati haielewi ni kwa nini Halmashauri ilikubali kugawana fedha na wakala ambaye tayari alikwisha isababishia hasara ya kiasi kikubwa cha fedha badala ya kiasi hicho kupunguzwa kwenye deni.

Mhe. Mwenyekiti, kamati inaamini kuwa kilichofanyika hapa ni ujanjaunja wa kutumia mali za umma kwa maslahi binafsi ambao kwa bahati mbaya ulibarikiwa na baraza baada ya kupotoshwa na kamati hiyo ndogo. Maelezo ya kuwa madeni yalifutwa kwa vile maduka ya watumishi na madiwani hayakulipa ushuru nayo hayana maana kwa sababu kama hilo kweli lilitokea, kilichotakiwa ilikuwa ni kufanya hesabu ya maduka hayo na kuondoa katika deni kiasi ambacho maduka hayo yalikuwa yanadaiwa na siyo kusamehe deni zima.
Hata hivyo, lilikuwa jukumu la Halmashauri kushirikiana na wakala kuhakikisha kodi inalipwa kwa mujibu wa sheria bila kujali maduka hayo kumilikiwa na watumishi au madiwani. Kuhusu hoja ya masoko bubu, Halmashauri ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha masoko yote bubu yanakomeshwa na mazao yote yanashushwa Soko la Kilombero badala ya kufikia hatua ya kusamehe deni.

Katika mazingira hayo inaonekana ni dhahiri aidha kwa uzembe au kwa makusudi kuwa Mkurugenzi na watumishi wake, walishindwa kuisimamia Halmashauri na kushindwa kuzuia kupenyeza kwa maslahi binafsi katika utekelezaji wa mkataba huo na hivyo kuisababishia Halmashauri hasara.

WAKALA JAMAHEDO HEALTH FOOD COMPANY KUFUTIWA DENI LA KIASI CHA TSHS.256,510,032.00
Sababu za kufutwa kwa deni la Wakala huyu zinaelezwa kuwa Wakala alisitishiwa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari katika maeneo kadhaa kama vile ICTR, TASO, Kilombero na TANESCO kinyume na makubaliano ya mkataba. 
Mhe. Mweneyekiti, kamati ilipitia mkataba wa wakala Namba. AMC/MAPATO-MAEGESHO/1/2009/2010 ambapo kwenye kifungu cha kwanza (1) wakala alipewa kukusanya ushuru na ada za maegesho katika eneo lote la Halmashauri. Kamati imejiridhisha kuwa ni kweli kuwa Halmashauri iliingilia mkataba kwa kumsitishia wakala maeneo ya kukusanya bila makubaliano.
Katika mazingira hayo, na ikizingatiwa mahakama iliweka zuio la kuweka wakala mwingine baada ya wakala huyo kufungua kesi akidai aendelee kukusanya ili ajifidie hasara ya Tshs. 100milioni ambayo kwa makusudi Halmashauri ilimsababishia, Halmashauri haikuwa na jinsi zaidi ya kutekeleza agizo la mahakama.
Kutokana na hali hiyo kamati haikuona tatizo kufanya makubaliano na wakala huyo nje ya mahakama ila kamati inaona tatizo katika maeneo mawili.
Kwanza, kamati imeshindwa kupata sababu za msingi zilizosababisha kumsitishia wakala maeneo ya kukusanya kama yalivyoainishwa hapo juu. katika mkataba wake ilikuwa wazi kuwa wakala atakusanya katika maeneo yote ya halmashauri, hivyo mabadiliko ya namna yoyote ile ilikuwa ni lazima yamhusishe wakala.
Mazingira haya yanajenga dhana kuwa ama watendaji wa Halmshauri walikuwa na maslahi ya kirushwa kwa wakala wa pili waliyehitaji kumpatia uwakala ambaye alizuiwa na mahakama, au ulikuwa ni mchezo uliotengenezwa ili ionekane wakala ameingiliwa utendaji wake kwa kumnyanganya maeneo kadhaa ya kukusanya  ili apeleke kesi mahakamani ili wagawane pesa za Halmashauri na hatimaye Halmashauri ipate hasara.

Pili, kamati haikubaliani na kipindi cha miezi minne (4) aliyopewa wakala katika makubaliano ili ajifidie hasara aliyopata kama ilivyoelekezwa na mahakama (ieleweke mahakama haikuelekeza apewe miezi mingapi.  Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa mkataba wake kifungu cha tano (5), wakala alipaswa kuilipa Halmashauri kiasi cha Tshs.52,900,000.00 kwa mwezi. Kwa vile makubaliano yalihusu hasara ya Tshs.milioni 100, inamaana kuwa alipaswa kupewa miezi miwili tu akusanye ajifidie (yaani 52,900,000x2=105800000.00) kiasi ambacho angejifidia na faida juu. Badala ya miezi miwili wakala alipewa miezi 4 aendelee kukusanya (yaani 52,900,000x4=211,600,000.00) ambapo kwa makusanyo haya alipewa fedha za bure kiasi cha Tshs.111,600,000/=. Haiingii akilini kuwa watendaji wa Halmashauri walimwachia wakala achukue bure kiasi hicho chote cha pesa bila wao kuhusika/kuwa na maslahi.
Kutokana na vitendo hivyo vyenye viashiria vya rushwa, Halmashauri ilipoteza Jumla ya Tshs.368,110,032.00 (yaani Tshs. 111,600,000.00 alizokusanya bure kwa kupewa miezi 4 na deni la awali la Tshs.256,510,032.00 alilokuwa anadaiwa bila kuhusisha Tshs.milioni 100 amabazo alistahili kujifidia kwa maelekezo ya mahakama ingawa hata kiasi hiki Kilipaswa kupungua kwani baadhi ya maeneo aliyolalamikia kupata hasara kama vile maeneo ya nyumba za ibada hayakuwa miongoni mwa maeneo aliyostahili kukusanya kwa mujibu wa mkataba wake).
Mhe.mwenyekiti, iko wazi hapa kuwa Halmashauri ilipata hasara kubwa namna hii kutokana na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watumishi wa Halmashauri na ni mapendekezo ya kamati kuwa wahusika hawana budi kuchukuliwa hatua stahiki.

WAKALA AQUILINE TRADERS (T) LTD – PANGO (MADUKA, MABUCHA NA MIGAHAWA TSHS.27,485,500.00
Sababu zilizoipelekea Halmashauri kufuta deni hilo ni kuwa Wakala alidai kuwa baadhi ya Wafanyabiashara walikuwa wanalipa kodi ya duka moja wakati wameunganisha maduka matatu hivyo kusababisha kurejesha mapato pungufu.  Sababu zingine zilikuwa maduka 43 ya jengo la ghorofa stendi ndogo kutokulipiwa kodi ya pango, jengo la choo ambalo Wapangaji wake walidai gharama zao za kujenga na Wafanyabiashara wa maduka ya UWT yaliyopo stendi kubwa kutolipa kodi ya pango.

Mhe.mwenyekiti, kamati ilijielekeza kwenye Mkataba wa wakala huyo; Mkataba Namba.AMC/MAPATO-PANGO/1/2009/2010 ambapo kamati haikuona kifungu chochote ambapo halmashauri ilikuwa inawajibika kumsaidia kukusanya ushuru toka kwenye maduka aliyokuwa anayahudumia.

Kama baadhi ya maduka kama vile maduka 7 ya UWT yalikataa kulipa (ingawa hata kama wasingelipa, kiasi ambacho kingelipwa toka vyumba 7 hakina maana ya msingi kwenye deni zima alilodaiwa), lilikuwa ni jukumu la wakala kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha maduka yote yanalipa ikiwemo kufungua kesi dhidi ya maduka yote ambayo yaligomea kodi na Halmashauri ingekuwa shahidi upande wake mahakamani kuhakikisha wahusika wote wanalipa.
Pia Madai kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliunganisha maduka matatu kuwa duka moja hayana msingi wowote kwani hakuna barua yoyote ambayo kamati imeiona aliyoiandika akiitaka Halmashauri kuingilia kati tatizo hilo na akanyimwa ushirikiano. Kuunganishwa kwa maduka hayo pia hakuna maana yoyote katika kodi kwani iko wazi kuwa aliyekuwa anaunganisha maduka hayo matatu ina maana alikuwa anayamiliki mwenyewe na hivyo hata kama angeyaunganisha angeendelea kulipa kodi ya maduka matatu bila kuathiri chochote katika kodi iliyopaswa kulipwa.

Hata hivyo kamati inapenda kuweka wazi kuwa maduka 43 ya jengo la ghorofa stendi ndogo ambayo wakala alidai yalikuwa hayamlipi, yalikuwa ya wakala mwenyewe na yeye ndiye aliyajenga. Ieleweke pia kuwa maduka hayo 43 hayakuwemo kwenye mkataba wa makusanyo kwani tangu 2009 majengo haya yalikuwa kwenye mkataba mwingine wa kujifidia gharama zao za ujenzi hivyo kwa vyovyote vile yasingehusishwa miongoni mwa maduka ambayo angekusanya kodi. 
Hata hivyo hali hii ilisababishwa na mwanasheria aliyeandaa mkataba kwani kimsingi kilipaswa kuwepo kifungu kwenye mkataba kinachoyaondoa maduka hayo 43 kwenye mkataba wake kwani kwa maana ya kifungu cha 1 cha mkataba kuwa, “wakala atakusanya ushuru wa pango katika eneo la Halmashauri” maana yake ni kuwa hata maduka 43 yako ndani ya kifungu hicho licha ya kuwa yalikuwa na utaratibu mwingine na hivyo kumpa mwanya wa ujanja wa kukwepa kwa kudai maduka hayo hayalipi.

Kiasi cha Tshs. Milioni 32 wakala alichodai anaidai halmashauri kwa sababu baadhi ya wapangaji hawakulipa hakieleweki na azimio lililofikiwa na kamati ndogo kuwa halmashauri ishirikiane na wakala kukusanya kiasi hicho toka kwa wapangaji halieleweki pia .Hivyo kuna haja ya kamati hiyo ndogo kuhojiwa na kuchunguzwa kwa kina ni kwa nini walifanya suluhu zilizolenga kuipotezea Halmashauri mapato. Pamoja na hayo, pia mfumo uliotumika katika kufanya majadiliano nao ni wa kutilia mashaka kwani makampuni manne (4) yaliyomilikiwa na mtu mmoja, yenye kesi tofauti na madai tofauti yalifanyiwa majadilianao kwa pamoja na makubaliano yaliyofikiwa hayaeleweki.
Mhe. Mwenyekiti, Kamati ilibaini uzembe mkubwa uliofanywa na Watumishi wa Halmashauri kuanzia hatua ya utoaji wa zabuni hadi kwenye utekelezaji wa mkataba wenyewe.  Hii ni kwa sababu ilikuwa inafahamika kuwa Mmiliki wa Kampuni ya Aquiline traders ndiye aliyekuwa amejenga baadhi ya maduka hayo ambayo inavyodaiwa alipewa ili akusanye ushuru.  Katika hali ya kawaida, haikutegemewa kuwa Wakala huyo angeweza kukusanya ushuru na kuuwasilisha Halmashauri kutoka kwenye majengo yake mwenyewe ambayo kwa vyovyote vile ingetegemewa ajifidie zaidi tofauti na kuifikiria Halmashauri. 

Kwa sababu ya kuwa na maslahi binafsi inaonekana dhahiri Wakala huyo hakuonyesha jitihada zozote katika ukusanyaji wa mapato.  Watumishi wa Halmashauri walionyesha uzembe katika usimamizi wa mkataba kwani licha ya kupokea malalamiko toka kwa Wakala kuwa baadhi ya vyumba vimeunganishwa (kama inavyodaiwa) na kuwa baadhi ya Wapangaji wanagoma kulipa kodi, Halmashauri ilipaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Wafanyabiashara hao wanalipa.

WAKALA MKOMILO TRADERS CENTRE (T) LTD – SOKO LA KILOMBERO TSHS.50,906,100.00
Kwa maelezo yaliyopitiwa na Kamati inadaiwa Wakala huyu alisamehewa deni baada ya kujitetea kuwa alishindwa kurejesha mapato hayo kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba baada ya kugundua kuwa kuna masoko bubu ambayo Wafanyabiashara waliyatumia kushusha mazao badala ya Soko la Kilombero.  Sababu nyingine ya kusamehewa ni kuwa baadhi ya maduka ya Watumishi na Madiwani yalikuwa hayalipi kodi husika. 

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno tu yaliyotumika “alishindwa kurejesha mapato….. baada ya kugundua kuwa kuna masoko bubu” tafsiri yake ni kuwa Wakala alikataa kulipa ushuru makusudi.  Maamuzi yaliyofikiwa kuwa Wakala alipe deni la milioni ishirini (20) badala ya milioni 50.9 ni maamuzi yaliyoghubikwa na maslahi binafsi.
Kamati pia haikuridhishwa na maamuzi ya Kamati ndogo iliyopendekeza kufutwa kwa madeni hayo kuwa kiasi cha milioni 36.5 zihakikiwe na Mkaguzi wa ndani kujiridhisha kama Wakala alipata hasara au la, kwani maelezo yake kuwa alipata hasara hayakuwa na msingi wowote.  Hata hivyo hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kama matokeo ya uchunguzi wa Mkaguzi wa Ndani.  Kamati hiyo ndogo pia ilionyesha wazi wazi kuwa na uhusiano wa kimaslahi na Wakala kwani wakati huo huo wanamuazimia Wakala alipe deni, wakati huo huo waliazimia shauri dhidi yake liondolewe Mahakamani, mazingira ambayo yalikuwa yanatoa mwanya kwa Wakala huyo kukwepa deni.

Kamati ilijiridhisha dhahiri kuwa maamuzi hayo yalifikiwa kwa sababu Madiwani na Watumishi walikuwa na maslahi kwenye kodi hizo kwani pia walikuwa miongoni mwa wadaiwa.  Kwa tafsiri rahisi ni kuwa Wakala alikula njama na Madiwani na Watumishi kuiibia Halmashauri mapato yake.

WAKALA M/S NEW METRO MERCHANDISE LTD – MABANGO NA MATANGAZO TSHS.229,599,480.00
Kwa maelezo yaliyopitiwa na Kamati inadaiwa Wakala huyu alisamehewa deni baada ya kuwasilisha malalamiko kuwa aliingiliwa na watendaji wa Halmashauri wakati wa utekelezaji wa mkataba wa ukusanyaji wa ushuru wa mabango ambapo watumishi wa Halmashauri walikusanya viwango vya chini tofauti na makadirio ya wakala. Katika usuluhishi wakala alifutiwa deni la mwaka wa fedha 2009/2010 na 2010/2011 jumla ya Tshs. 229,599,480.00.

Pamoja na kufutiwa deni aliongezewa miezi minne (4) kuanzia Julai hadi Oktoba 2011 ili akusanye na kurejesha Halmashauri Tshs. 56,813,720.00 kwa mwezi. Hata hivyo nyaraka zinaonyesha kuwa licha ya kuongezewa miezi minne (4) alishindwa kuwasilisha makusanyo na hivyo anadaiwa Tshs. 227,254,880.00
Mhe. Mwenyekiti, maelezo ya ziada iliyoyapata kamati ni kuwa wakala huyo alikuwa anaidai Kampuni ya Zantel na Halmashauri ilikuwa inamtolea ushahidi mahakamani kwa vile ndiyo ilikuwa imempatia kazi. Hata hivyo kamati haijapata hatima ya deni hilo la makusanyo ya miezi minne aliyoongezewa wakala. Suala la kuwa wakala alikuwa anamdai Zantel halina uhusiano na deni alilokuwa anadaiwa na Halmashauri.
Kamati inapenda ieleweke vyema kuwa deni alilosamehewa wakala huyu ni deni la 2009/2010 na 2010/2011 kiasi cha Tshs. 229,599,480.00  na siyo deni la miezi minne aliyoongezewa na kushindwa kuwasilisha chochote.

Katika taarifa za kesi zilizopo mahakamani hadi sasa hakuna kesi ambayo Halmashauri inamdai wakala huyo kiasi cha Tshs.227,254,880.00 alizopaswa kulipa kwa miezi minne aliyoongezewa. Kamati inapata mashaka juu ya jinsi idara ya sheria/Halmashauri ilivyoshughulikia suala hilo kwani imeshindwa kuelewa ni kwa nini wakala huyo hakufunguliwa kesi ya madai. Katika mazingira haya, iko wazi kuwa mwanasheria aliyekuwepo alikula njama na wakala huyo kupoteza mapato ya Halmashauri kwa makusudi. Kwa vitendo hivyo vya kukosa uaminifu na uzembe, Halmashauri ilipoteza kiasi cha Tshs.456,854,360.00 likiwemo na deni la awali alilofutiwa kwa madai ya kuingiliwa na watendaji wa Halmashauri. Kwa sababu hiyo, kamati haioni sababu ni kwa nini watumishi waliokuwepo wakati huo wasichukuliwe hatua za kisheria na za kinidhamu.

MAPENDEKEZO
Mhe. Mwenyekiti, kamati inapendekeza kwa baraza kuwa liazimie/liielekeze ofisi ya Mkurugenzi imfungulie kesi ya madai wakala M/S New Metro Merchandise Ltd ya kiasi cha Tshs. 227,254,880.00 likiwa ni deni halali alilopaswa kulipa kwa miezi minne aliyoongezewa baada ya kusamehewa madeni ya awali. Kamati imejiridhisha kuwa suala hili linawezekana kisheria kwa sababu; kwanza deni hili la miezi minne halikuwemo miongoni mwa madeni yaliyosamehewa, na pili; kwa vile kesi hii itakuwa inatokana na wakala kuvunja mkataba (kwa kushindwa kulipa), bado iko hai (kwa mujibu wa sheria ya ukomo wa muda katika kesi za madai “The Limitatation Act”) kwani haijapita miaka sita ili kesi hii ifikie ukomo kwa mujibu wa sheria hiyo.

2.1       YALIYOBAINIKA KWA UJUMLA KATIKA UCHUNGUZI
Mheshimiwa Mwenyekiti katika uchunguzi wake, Kamati iligundua mapungufu yafuatayo yaliyoisababishia Halmashauri hasara:-

i)             Uandaaji na Usimamizi mbovu wa Mikataba kati ya Halmashauri na Mawakala:  Kamati ilibaini kuwa Idara ya Sheria haikuwajibika vilivyo katika suala zima la uandaaji na usimamizi wa mikataba. Ama kwa makusudi au kwa uzembe, mikataba iliyokuwa inaandaliwa haikuwa na vipengele vyovyote vya kuilinda Halmashauri.  Idara ya Sheria iliendelea kuisababishia Halmashauri hasara kwa kutoa ushauri mbovu wa kuondoa kesi Mahakamani hata kwa zile kesi ambazo zilikuwa wazi Halmashauri ingeshinda.  Halmashauri pia ilishindwa kuwajibika katika usimamizi wa makubaliano yake na Mawakala kwani ilionekana mara kwa mara inaingilia utendaji wa Mawakala kinyume na mikataba.
ii)           Uzembe/kukosa uadilifu miongoni mwa Watendaji wa Halmashauri:  Kamati imebaini wazi kuwa ulikuwepo uzembe wa hali ya juu katika suala zima la usimamizi wa mapato ya Halmashauri kwani inaonekana watumishi walitanguliza mbele maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.
iii)          Kuwepo kwa maslahi binafsi na viashiria vya rushwa katika zoezi zima la ukusanyaji wa mapato:  Kamati ilibaini kuwa mfumo mzima wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ulighubikwa na tatizo la maslahi binafsi au rushwa.  Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ndio walikuwa wanamiliki idadi kubwa ya maduka na hivyo kusababisha zoezi la kukusanya mapato kuwa gumu.  Maamuzi na mapendekezo ya Kamati ndogo ya Madiwani iliyoundwa kumaliza migogoro inaonekana ama Wajumbe wake walikuwa na maslahi ya kibiashara ama walijihusisha na vitendo vya rushwa kutoka kwa Mawakala kwani hakuna sehemu yoyote Kamati ilipopendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa Watumishi walioisababishia Halmashauri hasara.  Tatizo la maslahi binafsi pia linaonekana liliathiri hata maamuzi ya Baraza zima kwani kwa vile maduka mengi ya Waheshimiwa Madiwani na Watumishi yalikuwa yanadaiwa kodi, kuamua kutowasamehe kodi Mawakala ingeimanisha kulazimika kulipa kodi na hivyo njia ya kujilinda ilikuwa ni kufuta mapato hayo ya Halmashauri.

iv)          Makadirio ya mapato bila kuzingatia uhalisia:  Kamati imebaini kuwa baadhi ya vyanzo vya mapato vilikuwa vinakadiriwa kiasi kikubwa cha fedha tofauti na uhalisia hali iliyokuwa inachangia Mawakala wengi kushindwa kufikia viwango hivyo katika utekelezaji wa mikataba.  Idara ya fedha inaonekana ilitawaliwa na uzembe mkubwa katika utekelezaji wa shughuli zake na hivyo kuikosesha Halmashauri mapato.

2.2       USHAURI WA KAMATI
Kamati inashauri kuwa ili kuepuka tatizo kama hili kwa sasa na kwa miaka ijayo, Halmashauri ihakikishe inazingatia yafuatayo:-

i)             Wataalam wote wa Halmashauri na Waheshimiwa Madiwani wasijihusishe kwa namna yoyote ile na upangaji wa maduka ya Halmashauri na kama Mtumishi au Diwani ataamua kupanga duka au kibanda cha Halmashauri lazima atangaze na aweke wazi kuwa ana maslahi katika biashara hiyo “to declare interest” kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi zinazohusu maslahi binafsi katika utumishi wa Umma. Madiwani na watumishi wajiepushe na vitendo vya upendeleo kwa mawakala.
ii)           Idara ya Sheria na Manunuzi zihakikishe kanuni na taratibu za manunuzi zinafuatwa katika suala zima la manunuzi.  Mikataba yote ya Uwakala iwe na vipengele vinavyoilinda Halmashauri na Halmashauri ijiepushe daima kuingilia utekelezaji wa mikataba na pale inapobidi kufanyika shughuli yoyote inayoweza kuvuruga utekelezaji wa mkataba mfano ujenzi wa barabara, upandaji miti na mambo mengine kiasi cha kuathiri sehemu yoyote ya mkataba, Halmashauri ijadiliane na Wakala huyo kabla ya kutekeleza jambo hilo.
iii)          Nakala (“sample”) ya mikataba ya mawakala iwe inapelekwa kamati ya fedha na utawala kwa ajili ya kupitiwa na kuhakikiwa kama inalinda maslahi ya Halmashauri kabla ya kusainiwa au kabla ya kupelekwa kwa mwanasheria wa Serikali kupitiwa.
iv)          Ofisi ya Mkurugenzi ihakikishe inafuatilia na kutatua malalamiko ya Mawakala kwa maeneo ambayo itakuwa na Mawakala mapema kadri malalamiko hayo yanavyopokelewa ili mambo yanayolalamikiwa yapatiwe suluhisho kuepusha migogoro isiyo ya lazima.  Uzembe wa namna yoyote kwa upande wa Watumishi usipewe nafasi kuepusha Halmashauri kupata hasara kwenye suala zima la mapato.


2.3       MAPENDEKEZO YA KAMATI
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia kwa kina kesi kwa kesi kwa kila Wakala, Kamati sasa inatoa mapendekezo juu ya hojaji (issues) zake ilizoziainisha kabla kama ifuatavyo:-



i)             UHALALI, NA KAMA ZILIKUWEPO SABABU ZA KUTOSHA KUHALALISHA KUFUTWA KWA MADENI HAYO
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kamati hii, Halmashauri haikuwa na sababu za msingi za kufuta madeni hayo.  Hii ni kwa sababu mambo yote yaliyosababisha kufikia maamuzi ya kufuta madeni yalichangiwa na Watumishi wa Halmashauri.  La kusikitisha ni kuwa siyo Kamati ndogo iliyoundwa iliyosuluhisha migogoro, Kamati ya Fedha na Utawala ama Baraza waliofikiria kuchukua hatua zozote za kinidhamu kwa Watumishi wa Umma walioisababishia Halmashauri hasara kubwa kiasi hicho.  Hivyo ni hitimisho la Kamati kuwa madeni hayo yalifutwa bila uhalali na bila sababu za msingi.

ii)           UHUSIANO WA KIMASLAHI, UZEMBE AU RUSHWA KATI YA MAWAKALA, WATUMISHI WA HALMASHAURI PAMOJA NA MADIWANI
Kwa uchunguzi uliofanywa na Kamati ni dhahiri kuwa Halmashauri ilipata hasara na kupoteza mapato yake kwa sababu ya kuchanganywa kwa maslahi binafsi na vitendo vya rushwa katika kazi za Umma.  Jinsi Ofisi ya Sheria ilivyosimamia uandaaji, na usimamizi wa mikataba pamoja na uendeshaji wa kesi zilizokuwa Mahakamani, inaonyesha dhahiri kuwa Mwanasheria alikuwa na uhusiano wa karibu na Mawakala hao na kwa kutumia taaluma yake alihusika kutengeneza mazingira mbalimbali kuhujumu mapato ya Halmashauri. 
Pia kitendo cha Watumishi na Madiwani kuwa na maduka bila kuweka wazi maslahi yao “to declare interest” ulikuwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.  Pamoja na Kamati ndogo, Kamati ya Fedha na Utawala hata Baraza la Madiwani kufahamu juu ya suala la maslahi binafsi na mazingira ya rushwa yaliyoghubika zoezi zima la kukusanya mapato, hakuna hatua zozote za kinidhamu zilizochukuliwa hali iliyoifanya Kamati hii kuamini kuwa ulikuwepo mtandao wa wizi wa mali za Umma na uhujumu mkubwa wa ustawi wa Halmashauri kwa maslahi ya watu wachache. 

Hivyo Kamati imejiridhisha kuwa Mkurugenzi, Mwanasheria, Mweka Hazina, Afisa biashara na Afisa Manunuzi waliokuwepo katika kipindi hicho, iwe kwa makusudi au kwa uzembe walishindwa kutimiza wajibu wao wa kuishauri Halmashauri na hatimaye kuisababishia Halmashauri hasara.  Kamati ndogo pia ya Madiwani inaonekana ilikuwa na maslahi binafsi kiasi cha kutoa mapendekezo ya kulipotosha Baraza na hatimaye Baraza kufikia maamuzi yasiyo sahihi na yaliyohujumu mapato ya Halmashauri.

iii)         KUSAJILIWA  KWA HATI ZA MAKUBALIANO MAHAKAMANI NA ATHARI ZAKE KWA HALMASHAURI
Katika uchunguzi wake, ingawa inaonekana makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kesi kusajiliwa Mahakamani, Kamati haikuridhika vya kutosha kama makubaliano yote yalisajiliwa mahakamani kwani katika makubaliano yote ambayo kamati iliyapitia, makubaliano na kampuni ya “Pigadeal” tu ndiyo yanayothibitika kuwa yalipokelewa mahakamani. Hata hivyo, kutokana na mlolongo mrefu wa kupata nyaraka kutoka mahakamani, kamati haikuweza kufuatilia mahakamani kusajiliwa kwa makubaliano ya mawakala wengine na hivyo kamati inaliachia jukumu hili vyombo vingine vya uchunguzi kama itabidi uchunguzi wa suala hili kuendelea zaidi. Kama ni kweli makubaliano yote ya kumaliza kesi na kufutiana madeni yalisajiliwa Mahakamani kama ilivyo kwa kampuni ya pigadeal na kwa vile Halmashauri yenyewe ilikubaliana na kumaliza migogoro hiyo nje ya Mahakama, hakuna uwezekano wa namna yoyote kisheria kurejeshwa kesi hizo Mahakamani.

iv)         WATUMISHI WALIOKUWEPO KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU
Kamati imejiridhisha kuwa kwa mujibu wa taratibu, sheria na kanuni za Utumishi wa Umma, Watumishi waliokuwepo na ambao kwa makusudi waliisababishia Halmashauri hasara kwa kushindwa ama kwa makusudi au kwa uzembe kutimiza wajibu wao, wachukuliwe hatua za kinidhamu popote pale walipo baada ya uchunguzi na hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa.  Hatua za kisheria pia zinaweza kuchukuliwa kwa waliokuwa Wajumbe wa Kamati ndogo kama itaweza kuthibitika kuwa kulikuwepo na viashiria vya rushwa katika uchunguzi wao na kuwa kwa makusudi walilipotosha Baraza katika kufikia maamuzi ya kufuta madeni hayo bila uhalali.

v)           KUTANGAZA KUKOSA IMANI NA MAKAMPUNI YOTE YALIYOHUSIKA KUIPOTEZEA HALMASHAURI MAPATO (BLACK LISTING)
Kamati imejiridhisha kuwa upo uwezekano kisheria wa kuyatangaza Makampuni hayo yote kama Makampuni yasiyo na uaminifu katika biashara na hivyo kuyaondoa katika orodha ya Makampuni ambayo Halmashauri ya Jiji la Arusha inaweza kufanya nayo biashara.  Hata hivyo kama Baraza litaridhia utekelezaji wa jambo hili itabidi kuainisha Wamiliki wa Makampuni hayo ili kuepuka kufanya nao biashara kwa siku zijazo endapo watasajili Makampuni mengine.

2.3.1 MAPENDEKEZO YA JUMLA
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mazingira ya utata yaliyoghubika utaratibu mzima wa ufutaji madeni hayo, Kamati inapendekeza kwa Baraza kama ifuatavyo:-

i)             Suala hili lipelekwe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili uchunguzi ufanyike ili kubaini kama kuna vitendo vya rushwa vilivyofanywa na Watumishi wa Halmashauri, Mawakala na Madiwani waliounda Kamati ndogo iliyopendekeza kufutwa kwa madeni hayo ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
ii)           Kwa vile Watumishi wote wakiwemo Mkurugenzi, Mwanasheria, Mweka Hazina, Afisa Manunuzi na Afisabiashara waliokuwepo wakati huo (miaka ya fedha 2009/10, 2010/11 hadi 2011/2012) walishahamia sehemu nyingine, mawasiliano yafanyike ili kama itabainika baada ya uchunguzi wa TAKUKURU kuwa walikosea, hatua za kinidhamu/kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa uzembe na kwa kushindwa kuishauri Halmashauri ipasavyo na hivyo kuisababishia Halmashauri hasara.
iii)          Halmashauri iangalie uwezekano wa mikataba yote inayoiingia hasa ya mapato iwe na kipengele kinachoweka masharti kuwa unapotokea mgogoro, yafanyike majadiliano (“arbitration”) ili panapo uwezekano migogoro imalizwe kabla ya kupelekwa kesi mahakamani ili kuiepushia Halmashauri hasara zinazoweza kuepukika
iv)          Makampuni yote ya Uwakala yakiwemo Mkomilo Trade Centre (T) Ltd., Makumira Filling Station, M/S Pigadeal Investment Ltd, Jamahedo Health food Company, Aquiline Traders (T) Ltd, na New Metro Merchandise Ltd ambayo kwa vitendo vyake vya kukosa uaminifu yaliisababishia Halmashauri hasara kwa kuipotezea mapato, yawe “black listed” na katika mchakato huo, majina ya waliokuwa Wamiliki wa Makampuni hayo yawekwe wazi kuepusha Halmashauri kufanya biashara na watu hao kwa siku zijazo.

3.0 MADENI YA VIKUNDI VYA WANAWAKE NA VIJANA
Mhe. Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2009 hadi sasa (2016) jumla ya Tshs. 104, 985,900.00 Zinadaiwa kutoka vikundi mbalimbali vya wanawake na vijana ambapo vikundi vya wanawake vinadaiwa jumla ya Tshs.58,625,800.00 na vikundi vya vijana vinadaiwa jumla ya Tshs.46,360,100.00
Mhe, Mwenyekiti, tarehe 15.07.2016, kamati ilikutana na jumla ya viongozi 38 wa vikundi vya wanawake na vijana wanaodaiwa na Halmashauri zikiwemo Saccos na vikundi vya walemavu. Lengo la kamati kuamua kukutana nao ilikuwa nikutaka kujua sababu zinazosababisha vikundi hivyo kushindwa kurejesha fedha za Halmashauri ili kamati iweze kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuhakikisha fedha zote zilizokupwa kwa vikundi zinarejeshwa na mfumo gani utumike ili zinazotolewa kwa sasa na baadae ziweze kurejeshwa.

Baada ya majadiliano ya kina na viongozi wa vikundi hivyo, kamati iligundua mapungufu mbalimbali ambayo yamesababisha fedha za Halmashauri kutorejeshwa kwa wakati. Sababu zifuatazo zilibainiwa;-


MTAZAMO WA WANANCHI JUU YA MFUKO WA WANAWAKE NA VIJANA.
Kupitia mahojiano, kamati iligundua kuwa fedha zinazotolewa katika mfuko huu, wananchi wanazichukulia kama hisani na wanadhani hawapaswi kudaiwa. Wananchi hawatambui kama huu ni mkopo kama mikopo ya Benki au Saccos na hivyo kutotilia mkazo suala la kuzirejesha. Mtazamo huu umevifanya vikundi hivyo hata kutumia fedha hizo kinyume na mipango iliyokusudiwa ambayo waliombea fedha. Kwa mfano, katika mahojiano, kamati ilikutana na kesi ambayo kikundi kilibadili matumizi ya mkopo kiliopewa  kutoka biashara na kutumia fedha hizo kufanya utafiti wa mazingira kwa kutegemea kuwa kuna wafadhili (shirika) lingewapa fedha za kutunza mazingira ambapo wangepata fedha za kurejesha halmashauri lakini shirika halikuwapa fedha na fedha ikapotea bila kufanya jambo lolote la kuzalisha.

Licha ya kuwa huu ni mfano tu, kamati ilijiridhisha kuwa vikundi vilivyo vingi havitumii fedha kwa malengo waliyoziombea na badala yake huzigawana na kwa kufanya hivyo mwishoni hujikuta hawawezi kulipa na mwishowe vikundi kuvunjika.

MAPENDEKEZO YA KAMATI
Ili kutatua changamoto hii kamati inapendekeza elimu itolewe kwa kuwashirikisha wataalam husika, waheshimiwa madiwani kwenye kata zao, na viongozi wote ngazi ya mtaa kuwaelimisha wananchi juu ya madhumuni ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi ili kuondoa mtazamo hasi miongoni mwa wananchi ili hatimaye fedha hizi ziwe na tija.

MIKATABA MIBOVU ILIYOTOLEWA NA HALMASHAURI
Mhe, mwenyekiti, eneo hili la mikataba limekuwa tatizo kubwa katika mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ya wanawake na vijana. Katika uchunguzi wake kamati imegundua kuwa baadhi ya mikataba haikusainiwa na Meya wala Mkurugenzi licha ya kuwa ilipaswa kusainiwa lakini pesa zilitolewa. Katika mazingira mengine hata mikataba yenyewe haipo na kwa hali hiyo kuna watu walikopeshwa bila kuingia mikataba. Tatizo lingine ni kuwa katika mikataba hiyo hakuna dhamana ya kuamika inayowekwa na vikundi hivyo. Katika mazingira haya ya kimikataba, inakuwa vigumu na itaendelea kuwa vigumu kuvichukulia vikundi hivyo hatua za kisheria pale vinaposhindwa kurejesha.

Hii ni kwa sababu mbili; Mosi, hizi zinakuwa kesi za madai na hivyo ni vigumu kuihusisha polisi katika ufuatiliaji wa mikopo hiyo. Pili ni kuwa hata pale ambapo kuna mikataba, kesi zikipelekwa mahakamani, inakuwa vigumu Halmashauri kurejesha fedha zake kwani hakuna dhamana inayoweza kuuzwa. Kisheria Halmashauri inaweza kuomba mahakama iwafunge wadaiwa kwa kile kinachojulikana kama “Civil prison” ingawaje hili ni jambo gumu kutekelezwa kwani sera ya serikali ni kuviwezesha vikundi kiuchumi na siyo kufunga wananchi wake na pia kumfunga mtu kwa mfumo wa “civil prison”  Halmashauri inapaswa kugharamia matunzo ya huyo mtu kwa muda wote anaokuwa gerezani. Kwa mazingira haya ni vigumu kuchukua hatua za kisheria zaidi ya kusamehe madeni hayo na kuisababishia Halmashauri hasara.

MUDA UNAOTOLEWA KUREJESHA MIKOPO NA KIASI KINACHOKOPESHWA
Mhe, Mwenyekiti, kamati ilibaini kuwa muda unaotolewa kuanza kurejesha na muda kikundi kinapaswa kuwa kimerejesha mkopo ni tatizo kubwa. Kamati ilipata maelezo kuwa muda wa maandalizi unaotolewa kabla ya kuanza kurejesha (yaani “grace period”) ni mwezi mmoja tu na kuwa mkopo na riba unapaswa kurejeshwa ndani ya miezi 12 yaani mwaka mmoja na marejesho yanafanyika kila mwezi.
Kwa hali ya uchumi ya watu ambao halmashauri inawakopesha, muda wa maandalizi wa mwezi mmoja ni mfupi sana pungufu ya hata ule unaotolewa na benki za biashara. Kamati inaona pia kuwa muda wa miezi 12 ambayo kikundi kinapaswa kulipa mkopo wote na riba pia hautoshi kwani unaonekana ni pungufu zaidi ya hata wa benki za kibiashara kwa maana kwamba mikopo ya benki mteja anaamua mwenyewe muda gani atatumia kurejesha lakini kwa halmashauri vikundi vyote vinalazimishwa kulipa ndani ya muda wa miezi 12 bila kujali uwezo wake ingawaje riba ya halmashauri ni ndogo kulinganisha na riba za benki. 

Kamati ilijaribu kufanya uchambuzi huu wa kihesabu; kwa kikundi kinachokopeshwa Tshs. 5,000,000.00 kinapaswa kurejesha pamoja na riba ya 10% kiasi cha Tshs. 5,500,000.00 ambapo kila mwezi, kikundi kinatakiwa kurejesha Tshs. 458,333.33. Ikichukuliwa mfano wa kikundi chenye idadi ya watu 7, kama kila mmoja anafanya mradi wake ina maana atapata 714,285.71 na kila mmoja anapaswa kurejesha 65,476.19 kwa mwezi.

Mhe, mwenyekiti, hebu tufikiri kwa pamoja, ni biashara gani yenye mtaji wa takribani laki 7.1 ambayo mtu huyo ataianzisha katika Arusha hii na aweze kupata faida ya kumuwezesha kurejesha elfu 65 kwa mwezi na kwa muda wa maandalizi wa mwezi mmoja anaopewa?

Katika hesabu za kibiashara ya mtu mdogo ambaye halmashauri inafikiria kumkwamua toka kwenye umaskini ni vigumu mtu huyo kupata faida badala yake anabaki kuhangaikia jinsi ya kulipa mkopo maana kama ataamua kushona nguo kwa mfano, mtaji hautoshi kununua cherehani na vitambaa na hata akiweza itakuwa vigumu kupata fedha za kurejesha kila mwezi kwa utaratibu uliopo.

Kwa hali hiyo ni dhahiri kuwa, kiasi hiki cha marejesho kwa mwezi ni kikubwa sana kwa hali ya uchumi ya mwananchi anayelengwa kukopeshwa na Halmashauri ikizingatiwa anapewa tu mwezi mmoja wa kujiandaa. Kwa hali hii ni kuwa wanakikundi wanalazimika kurejesha mitaji ambayo wamekopeshwa badala ya kurejesha faida ambapo kwa vyovyote vile wanaishia kupata hasara na fedha hizo kwa mahesabu ya kibiashara haziwasaidii chochote zaidi ya kuwapotezea muda na kuwasababishia marumbano katika harakati za kuzirejesha na hatimaye kuvunjika kwa vikundi.

Kamati pia iligundua kuwa kiasi cha fedha kinachotolew kwa vikundi ni kidogo na hivyo hakikidhi malengo wanayokuwa wamejiwekea. Kwa mfano, tukichukua mfano mwingine wa kikundi chenye watu 25, kila mwanakikundi wakigawana anapata 200,000.00 ambapo kila mwezi atapaswa kurejesha 18,333.33. Kiasi hiki cha mkopo anachopewa ni kidogo sana na hakina maana yoyote ile katika dhana nzima ya biashara.
Baada ya kuhojiana na vikundi, kamati imegundua kuwa kupewa fedha kidogo kumekuwa kukisababisha watu wengine kuona wanapoteza muda katika vikundi hivyo na hivyo baadhi yao kuzikataa fedha hizo au kuzichukua na kisha kujiondoa kwenye vikundi na hatimaye kusambaratisha vikundi hivyo na mzigo wa kuzilipa kubakia kwa viongozi.

MAPENDEKEZO
Mhe, mwenyekiti, kamati ili kutatua tatizo hili, inapendekeza yafuatayo;-
i)             Muda wa maandalizi (grace period) uongezwe kutoka mwezi mmoja (1) hadi miezi minne (4) ili kumsaidia mkopaji apate muda wa kutosha ili hatimaye arejeshe faida  inayotokana na mkopo badala ya kurejesha mtaji
ii)           Muda wa kurejesha mkopo kuanzia mwaka huu wa fedha (2016/17) uongezwe kutoka mwaka mmoja (1) wa sasa hadi mwaka mmoja na nusu (yaani miezi 18) hali itakayotengeneza uwiano mzuri wa kurejesha kwa mwezi na hivyo kuwawezesha kurejesha bila matatizo makubwa.
iii)          Idadi ya wanachama katika kila kikundi isipokuwa kwa Saccos na Vikoba wasipungue na wasizidi watano (5) ili mradi wasiwe wa familia moja. Kamati inapendekeza hivyo kwa sababu zifuatazo;-
a)    Watu watano ni rahisi kuongozeka kwani karibia kila mmoja atakuwa kiongozi kwa maana ya mwenyekiti, mwenyekiti msaidizi, katibu, mwekahazina na mmoja tu ndiye atabakia mjumbe vyeo ambavyo watakuwa wanabadilishana kwa mujibu wa katiba zao.
b)   Kwa vile karibia wote wanakuwa ni viongozi, halmashauri itakuwa na picha zao na hivyo kuondoa tatizo la wanachama kukimbia na kuwaachia mzigo wa viongozi kulipa deni peke yao.
c)    Mfumo huu utasaidia kuondoa vikundi hewa ambapo watu wawili watatu tena wakati mwingine wenye uwezo kiuchumi, wamekuwa wakiunda vikundi na kujaza majina hewa na kuchukuwa fedha za umma kwa manufaa yao huku siyo lengo na sera ya serikali
d)   Kwa Saccos na vikoba, wanachama wanaweza kuwa wengi iwezekanavyo ikizingatiwa wanafanya biashara ya fedha ingawa kamati inaonelea wangekuwa watu 30 kwa Saccos zinazoanza na walau kati ya 10-20 kwa vikoba vinavyoanza na ushirika huu unaweza kutanuka kadri uchumi wao unavyokua ili kurahisisha suala zima la uongozi.
iv)          Vikundi vyote (vyenye idadi ya watu 5) vikopeshwe si chini na si zaidi ya Tshs. 5,000,000.00 kwa mkopo wa kwanza. Kamati inapendekeza hivyo kwa sababu za kibiashara na kimahesabu kuwa kwa kupewa million 5, kila mmoja kama wana miradi tofauti (ambapo kimsingi ndivyo inavyofanyika kwa mujibu wa mahojiano yaliyofanyika), atapata kiasi cha Tshs.1,000,000.00 na atapaswa kurejesha pamoja na riba kiasi cha Tshs.61,111.11 kwa mwezi. Ukizingatia atakuwa amepewa miezi minne (4) ya maandalizi, maana yake kibiashara ni kwamba atakuwa ameanza kupata faida na hivyo ni rahisi kurejesha fedha hizo bila tatizo. Halmashauri inaweza kufikiria kuongeza kiasi cha fedha kulingana na uaminifu na mtiririko mzuri katika suala zima la urejeshaji. Kwa upande wa Saccos na vikoba vinavyoanza na kwa pale zinapoomba kama zenyewe na siyo kama wakala wa halmashauri, visikopeshwe chini ya million 5 na zaidi ya millioni 10. Fedha zinaweza kuongezwa kulingna na uaminifu na mtaji ilionao Saccos hiyo.
v)            Kwa vikundi vyenye miradi ya kilimo na ufugaji vinapaswa kupewa masharti tofauti na vikundi vya biashara kuhusu kiasi cha mkopo (kiwango kiongezeke) na muda wa kurejesha unapaswa uwe mrefu zaidi na marejesho yao yanapaswa kufanyika kila mwishoni mwa msimu kama inavyofanyika kwa benki ya NMB.  Kamati inapendekeza vikundi vinavyoomba fedha kwenda kwenye miradi ya kilimo kusimamiwa hatua kwa hatua na kwa kilimo cha mazao, kianzishwe maeneo ambayo kikundi kinaweza kufanya umwagiliaji.

MFUMO MBOVU WA UANZISHWAJI NA USIMAMIZI WA VIKUNDI
Mhe, mwenyekiti, kamati iligundua kuwepo kwa tatizo kubwa kuanzia jinsi vikundi vinapoanzishwa, na mfumo mzima wa usimamizi wake. Vikundi vingi vimekuwa vikianzishwa kwa kufuata matukio ama ya kisiasa (kuelekea uchaguzi) au matukio ya kiserikali mfano mwenge. Historia inaonyesha kuwa kuelekea vipindi vya kampeini, madiwani wamekuwa wakihamasisha wananchi kuunda vikundi harakaharaka ili vipatiwe fedha kwa maslahi ya kisiasa. Wataalam pia wa halmashauri wamekuwa na tabia ya kuwa bize kuhamasisha jamii kuunda vikundi ama karibia na sherehe za mwenge au sikukuu za kitaifa kama nanenane ili waweze kupata miradi ya mwenge ya kuzindua.
Mfumo huo wa uanzishwaji wa vikundi umekuwa ukisababisha vikundi kuanzishwa kwa mtazamo wa kupata fedha za bure za serikali na hivyo kutokuwa na nia ya dhati ya kuendeleza ushirika hali inayosababisha mara nyingi vikundi hivyo kusambaratika mara tu baada ya kujipatia fedha.

Kamati pia imegundua kuwa idara ya maendeleo ya jamii haiwajibiki vya kutosha katika kusimamia vikundi. Baadhi ya kata hazina maafisa maendeleo ya jamii na hakuna mfumo mzuri wa mawasiliano kati ya kata na maafisa maendeleo ya jamii makao makuu. Kamati imegundua pia kuwepo kwa kasi isiyoridhisha ya utendaji kazi katika idara. Maafisa maendeleo ya jamii na ushirika wamekuwa wakitumia muda mwingi maofisini badala ya kuwatembelea na kuwahamasisha wananchi kuhusu ushirika na kushauri vikundi katika shughuli zake. Kamati imegundua kuwa wapo wananchi wengi ambao hawajui kabisa juu ya uwepo wa maafisa maendeleo ya jamii wa kata na wajibu wao. Inaonekana mawasiliano baina ya idara ya maendeleo ya jamii na vikundi yanakuwepo tu wakati wa kupatiana mikopo na wakati wa kudaina mikopo.

Hata hivyo, licha ya kuwepo hali ya kutowajibika vilivyo kwa maafisa maendeleo ya jamii, kuna changamoto ya kukosa rasilimali fedha na rasilimali watu katika idara ya maendeleo ya jamii. Baadhi ya kata hazina kabisa maafisa maendeleo ya jamii na pale walipo, hawana bajeti ya kuzungukia vikundi ikiwemo usafiri, na bajeti ya mawasiliano. Hali hii inawalazimu wataalam hao kutumia fedha zao kufuatilia maendeleo ya vikundi ikiwemo marejesho ya mikopo hali ambayo kwa vyovyote vile ni vigumu kufanikiwa.

MAPENDEKEZO YA KAMATI
Kamati inatoa mapendekezo yafuatayo;-
i)             Ofisi ya mkurugenzi ihakikishe kila kata inakuwa na afisa maendeleo ya jamii. Kwa vile taratibu za ajira zinahusisha ngazi za utumishi serikali kuu, kwa sasa maafisa maendeleo ya jamii waliopo wapewe maelekezo kwa maandishi ya kuhudumia kata za jirani na ili kuwafanya wafanye kazi hii kubwa kwa moyo, Halmashauri iwape posho maalumu kila mwezi kwani watakuwa wameongezewa majukumu tofauti na ajira zao
ii)           Idara ya maendeleo ya jamii itengeneze bajeti itakayoainisha gharama za usafiri, mawasiliano ya simu na ofisi ya mkurugenzi iipatie fedha idara ya maendeleo ya jamii ili kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii makao makuu na wale walioko ngazi ya kata kutembelea, kuhamasisha na kushauri vikundi katika shughuli zake.
iii)          Idara ya maendeleo ya jamii iongeze kasi katika utendaji wa kazi zake na utengenezwe mfumo imara wa mawasiliano ili kuondoa tatizo la wananchi kuchelewa kupata taarifa.
iv)          Utoaji wa mikopo uwe unasitishwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa na miezi mitatu kabla ya kuvunja baraza ili kuondoa tatizo la kuingizwa kwa maslahi ya kisiasa katika utoaji mikopo ya vikundi.
v)            Idara ya maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na idara ya Tehama, itengenezecomputerized data base” ya vikundi vyote vinavyosajiliwa, vinavyopatiwa mikopo na jinsi vinavyorejesha ili kuondoa tatizo la kukosekana kwa taarifa muhumu pale zinapohitajika na lakini pia kurahisisha uratibu wa vikundi.
vi)          Idara ya maendeleo ya jamii itengeneze “task force” ya kufuatilia madeni yote ambayo Halmashauri inavidai vikundi mpaka sasa. Kamati inashauri vikundi vyote vinavyodaiwa viainishwe kwa kata na WDC ihusishwe kikamilifu kukusanya madeni hayo ikibidi hata asilimia kadhaa ya makusanyo hayo ibaki ngazi ya kata kwa matumizi ya ofisi ya kata husika. Hii itasaidia kuongeza kasi ya kufuatilia madeni hayo ikizingatiwa vikundi vingine wahusika hawatambuliki hivyo ni lazima kuwahusisha wenyeviti na watendaji wa mitaa ili kuwabaini wahusika ambapo kwa vyovyote vile wahusika watapaswa kulipwa posho.

UKOSEFU WA ELIMU YA BIASHARA, KUTOJUA KANUNI ZA FEDHA NA UKOSEFU WA ELIMU YA UJASILIAMALI
Mhe, mwenyekiti, kutokana na mahojiano na vikundi, kamati ilibaini kuwepo kwa uelewa mdogo sana juu ya masuala ya biashara, miradi na mikopo. Vikundi vingi vimekuwa vikipatiwa fedha bila elimu ya kutosha juu ya uanzishaji wa miradi, usimamizi wa fedha na usimamizi wa mikopo hali ambayo imesababisha vikundi vingi kupata hasara na hivyo kushindwa kurejesha mikopo. Kwa mfano, kikundi cha “audepa” toka kata ya sombetini kiliomba million 15 ila kikapewa milioni 3 ili kifanye kilimo cha kisasa.

Licha ya kupata fedha kidogo sana, bado kikundi kiliendelea na mradi wa kilimo na mwishowe kikapata hasara na kusambaratika. Kwa maoni ya kamati ni kuwa kikundi hiki kilipata hasara kutokana na kukosa ushauri wa wataalam kwani kwa kiasi hicho cha fedha kilipaswa kushauriwa kubadili mradi au kubadili ukubwa wa eneo walilopanga kulima. Hata hivyo, eneo walilokuwa wanaendesha kilimo halikuwa na uhakika wa maji na hatimaye walikumbwa na tatizo la ukame. Kwa hali hiyo inaonekana dhahiri kuwa ulikosekana ushauri wa kitaalam ndiyo maana kikundi hicho kiliishia kupata hasara.
Mhe, Mwenyekiti, ni lazima ieleweke kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana ni nyingi  na hivyo ni lazima zisimamiwe vilivyo ili mwishowe zilete tija kama ilivyokusudiwa. Hata hivyo, fedha hizo zitaendelea kupotea kama halmashauri haitaweka mikakati madhubuti. Kamati imeshindwa kuona umuhimu wa kitengo cha ushirika katika jiji hili. Kamati ilitegemea maafisa ushirika wangekuwa wanashinda mitaani wakihamasisha wananchi umuhimu wa kuwa na ushirika badala ya kukaa ofisini na kazi hii kuiachia idara ya maendeleo ya jamii peke yao.

Ni lazima ieleweke kuwa idara ya maendeleo ya jamii ni idara mtambuka (“cross-cutting”) na hivyo haipaswi kuachiwa peke yake jukumu la usimamizi wa asilimia kumi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana.
Mhe, mwenyekiti, kamati pia iligundua kuwepo kwa tatizo kubwa la kutozifahamu kanuni za fedha miongoni mwa wanavikundi. Hili lilijidhihirisha katika uchunguzi kwani miongoni mwa vikundi mfano “Mbeshele Umoja group” kinadai kilishalipa na pamoja na vingine vya aina hii, vinadaiwa si kwa sababu havijalipa, bali ni kwa sababu ama hawajawasilisha “slip” za malipo za benki ili wakatiwe risiti za halmashauri, au walipoteza “bank slips”.

Kwa uelewa mdogo walionao wananchi ni kuwa wakishalipa benki kwenye akaunti ya halmashauri, wanaamini tayari wamekwishailipa halmashauri hadi kutoona umuhimu wa kutunza slip za benki. Kamati inaona kuwa tatizo hili linatokea kwa sababu wakati vikundi vinapewa elimu kabla ya kukopeshwa, hawaelimishwi vya kutosha jambo ambalo linawasababishia hasara ya ama kutakiwa kulipa tena au kutumia muda mrefu kufanya “reconciliation” ya malipo hayo.
Kutokana na changamoto zilizopo, Kamati inategemea idara ya uchumi, biashara, fedha, kilimo, ushirika, sheria na utawala zinapaswa kushirikiana kwa karibu kuanzia uundwaji wa vikundi, kujadili na kushauri miradi ya vikundi na katika usimamizi wa fedha na marejesho yake na siyo kuiachia idara ya maendeleo ya jamii peke yake.

Hii ni kwa sababu ya ukweli kuwa idara ya maendeleo ya jamii pekee haiwezi kuwa na weledi katika masuala yote yanayohusu uchumi, biashara, fedha, sheria, ushirika n.k. Wataalam wa idara zote hizi wanapaswa kushiriki hatua kwa hatua katika zoezi zima la kuelimisha vikundi kwani inaonekana elimu inayotolewa haikidhi matakwa kwa vile inatolewa na idara moja tu ya maendeleo ya jamii na mara chache hushirikisha wataalam wa idara zingine.

MAPENDEKEZO
Kamati inapendekeza kuwa;-
i)             Idara za uchumi, fedha, biashara, na sheria ziwe na mtu mahususi atakayekuwa anashirikiana na idara ya maendeleo ya jamii na ushirika kutoa elimu kwa vikundi na wananchi kuhusu uanzishwaji wa miradi, usimamizi wa fedha, mbinu za biashara na mifumo ya sheria ili kuvipa uelewa wa kutosha vikundi hivyo kabla ya kuvipa fedha ili fedha hizo ziwe na tija. Elimu hii itolewe kwa wanakikundi wote kwenye kata na siyo kuwaita viongozi wachache tu.
ii)           Idara ya uchumi isaidie kwa karibu kupitia miradi ya vikundi na kushauri kama miradi hiyo ina tija kibiashsra na juu ya njia nzuri ya utekelezaji ili hatimaye fedha zinazotolewa ziwe na tija.
iii)          Pale ambapo kuna uhitaji wa kualika wataalam wa masuala ya ujasiliamali kutoa elimu, Halmashauri iwaite hata kama ni wa nje ili kuongeza tija na kuhamasisha jamii katika suala zima la ujasiliamali
iv)          Halmashauri ipate kipindi katika redio walau mara moja kwa mwezi ili wataalam wa halmashauri waweze kutoa elimu kwa umma juu ya mambo mbalimbali yahusuyo mikopo ya vikundi kwani ni rahisi jamii kupata elimu hiyo kwa muda mfupi.

UONGOZI MBAYA NA USIMAMIZI MBAYA WA FEDHA MIONGONI MWA WANAVIKUNDI
Mhe. Mwenyekiti, Katika uchunguzi wake, kamati ilibaini kuwepo kwa uongozi mbaya na mfumo mbaya wa usimamizi wa fedha. Katiba za vikundi na Saccos nyingi hazijatengenezwa katika mifumo inayoweza kuwawajibisha wanavikundi pale wanapokimbia na fedha za vikundi. Kamati iligundua kuwa Saccos zilizo nyingi zinatoa fedha bila kufuata utaratibu wa uendeshaji Saccos. Kwa mfano “Sombetini Saccos” ilikopeshwa fedha na ikawakopesha wanachama wake bila kujali wana hisa na akiba kiasi gani. Kilichotokea ni kuwa Saccos ilisambaratika na wanachama wakapotea na fedha na wengine wakahama kabisa ikizingatiwa wengine wanakuwa wapangaji.

Katika mazingira haya mwishowe wanabakia tu viongozi ndio wanapaswa kulipa deni wakati fedha zilitumiwa na wanachama wote. Kinachoonekana hapa ni kukosekana uelewa wa kutosha katika usimamizi wa fedha na uratibu wa Saccos. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa taratibu za Saccos, mwanachama hawezi kukopeshwa fedha bila kuwa na akiba au hisa yoyote. Utaratibu uliozoeleka ni kuwa walau mwanachama anakopeshwa mara mbili ya akiba aliyonayo. Kama utaratibu huu ungefuatwa na Saccos hiyo, maana yake ni kuwa walau ingepoteza nusu ya fedha ilizokopesha.

MAPENDEKEZO
Kamati inapendekeza kuwa;-
i)             Idara ya ushirika iwajibike kutoa elimu ya kutosha kwa Saccos hizo na izisimamie hatua kwa hatua pale Halmashauri inapopeleka fedha kwenye Saccos hizo.
ii)           Kwa vile halmashauri imeamua kuzitumia Saccos na vikoba kama mawakala wake, lazima uwepo usimamizi wa mara kwa mara kuhakikisha kuwa; kwanza vikoba/saccos hizo zinawapatia fedha walengwa (vikundi) na pili, kuhakikisha Vikoba/Saccos hizo zinavifuatilia vikundi hivyo ili viweze kurejesha mikopo hiyo. Kamati inapendekeza hivyo kwa kuuona ukweli kuwa kama usimamizi wa karibu hautakuwepo, na kwa kuzingatia kuwa si Saccos/Vikoba vinavyopewa fedha na Halmashauri kama wakala zinazoweka dhamana yoyote, basi fedha zote zitapotea na itafikia wakati halmashauri haitapata wa kumdai. Saccos zitasingizia vikundi na vikundi vitasingizia Saccos/Vikoba na mwishowe Saccos na vikoba zitavunjika na huo ndio utakuwa mwisho wa fedha za halmashauri.
iii)          Halmashauri iendelee kuwekeza zaidi katika elimu ya ushirika ili kujenga vikundi vyenye nguvu kuanzia chini, vyenye mtazamo chanya katika uchumi na biashara ili baada ya miaka kadhaa 10% ya mapato ya ndani iwe na matokeo yanayoweza kupimika kwa maslahi ya halmashauri ya jiji la Arusha na watu wake.
iv)          Halmashauri ianzishe mchakato wa kuanzisha benki ya wananchi wa jiji la Arusha yaani “Arusha Community Bank”. Kamati inapendekeza hivyo kwa sababu zifuatazo;-
a)    Asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri ni fedha nyingi zinazohitaji usimamizi wa kutosha kiasi cha kamati kuona kuwa haziwezi kuratibiwa kikamilifu na idara tu ya maendeleo ya jamii.
b)   Kuwepo kwa “Community Bank” kutaiwezesha halmashauri kuwaleta pamoja kiuchumi wanawake, vijana, na wananchi wote kwa ujumla kwani masuala mengi ya uhamasishaji na uundaji wa ushirika utafanywa na Benki hiyo badala ya watumishi tu ambao wana mambo mengi ya kushughulika nayo. Wataalam wa halmashauri watafanya kazi ya usimamizi tu wa benki hiyo ikizingatiwa kuwa Halmashauri kwa kupitisha 10% ya mapato yake katika benki hiyo, itakuwa na hisa nyingi.
c)    Halmashauri itakuwa na dirisha maalum la vikundi vya wanawake na vijana na hivyo shughului za uratibu na ufuatiliaji wa marejesho zitafanywa na benki kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa. Kazi ya Halmashauri itabakia kuidhinisha fedha na uratibu mzima kufanywa na Benki.
d)   Benk hiyo kwa kudhaminiwa na halmashauri inaweza kupata fedha toka taasisi zingine za kifedha ikiwemo Benki Kuu, mashirika ya kifedha ya kitaifa na kimataifa hali itakayoiwezesha kuongeza mtaji, kukua na kufanya mambo makubwa ya kiuwekezaji.
e)    Community Bank siyo tu itavisaidia vikundi vya wanawake na vijana tu bali wananchi wengine ambao kwa kununua hisa, benki itakuza mtaji wake zaidi na hivyo kuongeza uwezo wa kukopesha zaidi.

UKOSEFU WA UAMINIFU/UDANGANYIFU KATIKA MCHAKATO MZIMA WA KUANZISHA NA KUTOA MIKOPO NA TATIZO LA VIONGOZI KUINGILIA MICHAKATO YA UTOAJI NA USIMAMIZI WA MIKOPO
Mhe.mwenyekit, tatizo hili linaonekana katika sura tatu yaani kutokuwepo uaminifu miongoni mwa wanavikundi wenyewe, miongoni mwa watumishi, na miongoni mwa viongozi wakiwemo waheshimiwa madiwani na wenyeviti wa mtaa.
Wanavikundi wenyewe
Kamati imegundua kutokuwepo uaminifu baina ya wanavikundi pale wanapopatiwa fedha tatizo ambalo linaonekana katika sura mbili; Moja viongozi wa vikundi wakati mwingine hujipendelea na kujigawia fedha nyingi na kuwapatia wanachama wengine fedha kidogo. Hali hii husababisha migongano na hivyo kuwafanya wanachama wengine kujitoa uanachama na kukimbia na fedha kidogo wanazopatiwa.

Katika mazingira mengine viongozi uwasilisha mihtasari ya uongo ambayo hawajakubaliana na wanachama na mwishowe mambo yakiharibika wanachama hukana kuhusika kuamua jambo fulani na hivyo kikundi kusambaratika. Katika mazingira mengine pia viongozi huwasilisha majina ya kughushi ya wanachama ili kujipatia fedha na pale wanapotembelewa hutafuta watu wa kughushi kama wanachama wakati kimsingi siyo wanachama wa kikundi hicho hivyo maafisa maendeleo ya jamii wanahitaji kuwa makini sana katika uhakiki wa wanachama wa vikundi.
Mhe. Mwenyekiti, katika utafiti wake, kamati ilikutana na kisa cha kusikitisha kinachothibitisha jinsi ukosefu wa uaminifu unavyoathiri vikundi kutoka “Jakaya Walemavu Group” ambacho ni kikundi cha walemavu kutoka kata ya Sombetini ambapo kama ni kweli, basi Halmashauri inapaswa kukisaidia kikundi hiki.
Katika kisa hicho ni kuwa mnamo mwaka 2009 kikundi hicho cha walemavu kilianzishiwa mradi wa mashine za kusaga nafaka kupitia fedha za TASAF. Halmashauri pia ilikiongezea fedha kama mkopo ili kiendeleze mradi wake. Hata hivyo kwa mujibu wa maelezo ya mwenyekiti, katibu wa kikundi hicho alitoroka na fedha za kikundi zikiwemo Tshs. Milioni 10 za mtu binafsi ambazo hazikuwa na uhusiano wowote na mali za kikundi.
Mtu huyo alikipeleka kikundi hicho mahakamani na mwenyeti akaiomba halmashauri iwasaidie kwa kuzingatia fedha hizo zilikuwa mali ya umma (mradi wa TASAF). Hata hivyo, mwenyekiti huyo anadai idara ya sheria ya Halmashauri haikutoa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kutohudhuria mahakamani na mwishowe kikundi kilishindwa kesi, na mahakama iliufirisi mradi huo kwa kumpa mdai huyo asiye halali mashine za kikundi kufidia fedha zake zilizoibwa na katibu wa kikundi wakati hakuna uhusiano wowote na kikundi.
Licha ya kuwa kamati haina uhakika wa asilimia zote na maelezo hayo ya mwenyekiti, kama kweli ndivyo ilivyotokea, halmashauri ilishindwa kusimamia fedha za umma kwani licha ya kuwa vikundi hivyo vinapewa mikopo, lazima ieleweke kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya huduma kwa umma hivyo ni lazima Halmashauri iingilie pale inapoona mali ya umma inahujumiwa kwa namna yoyote ile.
Sura ya pili ni kuwa wanachama wanapewa fedha kwa makubaliano lakini kwa vile wanajua waliosaini mkopo huo ni viongozi, na kwa vile wanatambua hakuna picha zao kwenye fomu za mikopo, wanajitoa kwenye vikundi na kuwaachia viongozi mzigo wa madeni wakiamini hawatagushwa na sheria. Tatizo hili limechagizwa pia na watendaji wa kata na mitaa kwani pale viongozi wanapochukua hatua juu ya wanachama wenzao na kuomba msaada kwa viongozi wa serikali, wamekuwa wakikatishwa tamaa kwa kuelezwa kuwa wao ndio walisaini fedha za serikali hivyo wawajibike kuzilipa wakati viongozi hao walipaswa kuwapa ushirikiano.

Katika tatizo hili pia kamati ilikutana na kesi moja toka kata ya sombetini, ambapo kikundi kinachojiita “Sombetini youth group” wahusika wote hawajulikani walipo. Katika ofisi ya kata hiyo kuna mkataba ambao una picha za wahusika lakini cha kushangaza ni kuwa hakuna kiongozi hata mmoja kwenye WDC anayezitambua picha za vijana hao. Maelezo yaliyopatikana ni kuwa watu hao walikuwa waendesha bodaboda tu na kwa sasa hawajulikani walipo. Ni vigumu kuelewa katika mazingira haya ni kwa namna gani watu wasiofahamika na wasio na mdhamini wa uhakika walipewaje fedha za umma.


Watumishi
Mhe. Mwenyekiti, Kamati iligundua kuwepo kwa baadhi ya watumishi ambao siyo waaminifu. Baadhi ya maafisa watendaji hushirikiana na wananchi kuunda vikundi hewa kwa maslahi yao. Watendaji wanawasilisha mihtasari ya uongo kuhalalisha vikundi ambavyo wana maslahi navyo na kupoteza kabisa kumbukumbu za vikundi hivyo.
Katika uchunguzi wake, kamati ilikutana na kesi ya aliyekuwa afisa maendeleo ya jamii wa kujitolea katika kata ya kati aliyetajwa kwa jina moja la “Leah” ambaye aliunda vikundi vyake mwenyewe vitano na kuchukua fedha za halmashauri kupitia mgongo wa vikundi hivyo. Kwa muda wote huo amekuwa anasuasua kurejesha fedha hizo na kwa sasa bado anadaiwa na ingawa anakaa kata ya sekei hayuko tayari kueleza mahali anapoishi.

Hata hivyo kamati inashindwa kuelewa ni kwa jinsi gani huyo mtumishi angeweza kupata fedha za vikundi vyote 5 bila kumshirikisha mtendaji, na WDC. Kama angevidhulumu vikundi, kwa vyovyote vile vingelalamika na angechukuliwa hatua. Kinachoonekana hapa ni kuwa kwa vyovyote vile alishirikiana na viongozi wengine kutengeneza vikundi hewa kwa maslahi binafsi.
Viongozi
Mhe. Mwenyekiti, katika uchunguzi wake kamati ilikutana na kesi za kusikitisha zinazoonyesha kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa waheshimiwa madiwani, watumishi na wenyeviti wa mitaa. Maelezo yafuatayo yanathibitisha hoja hii;-

Katika kata ya Sekei, kikundi cha “Sekii Youth group” kinachodaiwa Tshs 732,000.00 diwani aliyekuwepo ndiye aliyechukua fedha kwa kutumia picha za watoto wa mama mwenye nyumba ambayo yeye alikuwa anapanga. Watumishi wamefanya mahojiano na huyo mama ambaye amekana kabisa watoto wake kuhusika na kikundi hicho na baada ya diwani huyo kujua kuwepo kwa suala hilo, aliwafuata watumishi ngazi ya kata (afisa mtendaji na afisa maendeleo ya jamii) na kuwaeleza kuwa yeye ndiye alikuwa anakidhamini kikundi hicho na kuwahaidi wasiwe na wasiwasi fedha hizo zitarejeshwa. Hata hivyo walipomtaka afanye hahadi hiyo kwa maandishi alikataa kufanya hivyo na mpaka sasa fedha hizo hazijalipwa.

Hata hivyo, kamati haikupata ushahidi wa mheshimiwa diwani kuzichukuwa fedha hizo kwa maslahi yake binafsi bali tatizo ni kuwa kama kweli alihusika kama inavyosemekana, alisaidia kikundi kupata fedha bila kupitia utaratibu unaotakiwa. Bila kujali alikuwa na nia njema kiasi gani ya kuwasaidia wananchi hao kama kweli alifanya hivyo, kutofuata utaratibu kunaleta tatizo.

Kamati imejiridhisha kuwa fedha zilichukuliwa na kugawanywa miongoni mwa wanawake watatu wa kikundi hicho na kwa bahati mbaya baada ya kupata fedha hizo, wote watatu waliingia katika migogoro ya ndoa na kuachika katika ndoa zao na kwa sasa hawaeleweki wanaishi wapi. Watumishi wamekuwa wakifuatilia deni hili kwa kuwapigia simu na licha ya kuhaidi watalipa hawajalipa bado na hata kama wangekuwepo ni vigumu kulipa kwani hakuna mkataba unaowadai.

Katika kesi nyingine ya kusikitisha, vikundi vya “maendeleo group”, na “two in one women group” inasemekana viliundwa na mheshimiwa diwani marehemu mawazo. Vikundi hivi havijarejesha fedha na kimsingi hakuna wa kumdai.

Katika kesi nyingine, kikundi cha “Omega” toka kata ya elerai kinachodaiwa 1,425,000.00, mwenyekiti alitoa maelezo kuwa kikundi hiki kilihusisha pia watumishi wawili wa Halmashauri ambao nao walipata mgao wa fedha ila kati yao mmoja alifariki dunia na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Kweka alihamia mwanza na hakuna mawasiliano ya jinsi gani ya kurejesha deni hili. Ingawa kamati haikupata ushahidi wa namna gani watumishi hao walijipatia fedha, kama kweli hili lilitokea, ni tatizo kubwa sana kwani itakuwa vigumu kumsurutisha mwanachama mmoja aliyebaki kulipa fedha zote hizo ambazo zilichukuliwa hata na watumishi wa Halmashauri yenyewe.

Kikundi cha “Maisha plus” toka kata ya Elerai kinachodaiwa Tshs. 550,000.00, inasemekana kiliundwa na aliyekuwa diwani viti maalum aliyetambulika kwa jina moja la “Mama Choga” na wanachama wote walikuwa wa familia yake isipokuwa mwenyekiti.  Wanachama wote akiwemo diwani hawatoi ushirikiano kwa mwenyekiti huyo na hivyo ndiye peke yake anayetakiwa kulipa mkopo. Kinachoonekana hapa ni kuwa mwenyekiti wa kikundi alishawishiwa na kudanganywa na diwani huyo, pesa waligawana wote lakini katika kulipa diwani huyo haonyeshi ushirikiano.

Kikundi cha “Tareto na Kisetu youth groups” toka kata ya Unga Ltd navyo vina tatizo la kukosekana uaminifu. Kinachodaiwa hapa ni kuwa wahusika wa vikundi hivi hawajulikani. Hata hivyo kwa maelezo iliyoyapata kamati ni kuwa wahusika wanajulikana ila viongozi wa mtaa hawako tayari kuwataja.  Vikundi hivyo inasemekana vilidhaminiwa na Diwani aliyepita na inaonekana Afisa mtendaji wa kata aliyekuwepo alihusika kwa namna moja ama nyingine katika uovu huo.
Mhe. Mwenyekiti, Kamati pia iligundua kuwepo kwa tatizo la viongozi ngazi ya kata hasa weheshimiwa madiwani na watendaji wa kata kuingilia shughuli za maafisa maendeleo ya jamii wa kata au kufanya maamuzi mbalimbali yanayohusu masuala ya vikundi bila kuwashirikisha maafisa maendeleo ya jamii. Kwa nafasi ya afisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata, anapaswa kuhusika na kutoa mapendekezo yake kabla vikundi havijatumwa Halmashauri ili vipewe fedha kwani kimsingi yeye ndiye ana wajibu wa kutembelea vikundi hivyo ili kujiridhisha juu ya uhai wa vikundi hivyo. Kamati imepata taarifa zenye uhakika kuwa mpaka sasa zipo WDC ambazo haziwashirikishi maafisa maendeleo ya jamii katika mchakato mzima wa kujadili vikundi na hata pale wanaposhirikishwa maoni yao hayazingatiwi.

Cha kusikitisha zaidi ni kuwa wapo waheshimiwa madiwani ambao wamediriki hata kuwatishia kuwahamisha vituo vya kazi baadhi ya maafisa maendeleo ya jamii wanaojaribu kushauri utaratibu ufuatwe katika mchakato mzima wa kuibua na kuidhinisha vikundi na wakati mwingine kuwalazimisha kusaini mihtasari ambayo wao hawakuhusika katika kuvijadili vikundi hivyo.
Kamati inatoa rahi kwa waheshimiwa madiwani wote kuwahusisha na kutowaingilia maafisa maendeleo ya jamii katika utendaji wa kazi katika kata zao ili kuhakikisha yaliyotokea katika kipindi cha nyuma kwenye zoezi la kutoa mikopo hayajirudii katika kipindi hiki.

Mhe, mwenyekiti, katika orodha hii ya vikundi vyenye utata, vikundi vifuatavyo pia vinahitaji mjadala wa kina;-

Kikundi cha “Batiki Olasiti”: Kikundi hiki kiliundwa na wanawake 9 waliokuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi ili kutengeneza batiki. Kabla hawajapewa mkopo wanachama 5 walijitoa uanachama kutokana na hali yao ya kiafya kuwa mbaya zaidi. Wanachama waliobaki 4 walikopeshwa fedha na wanadaiwa Tshs. 1,255,000.00. Hata hivyo kwa bahati mbaya wanachama hao waliokuwa wamebaki (waliokopeshwa fedha) wote wamekwishafariki dunia. Katika mazingira haya, halmashauri haina wa kumdai zaidi ya kusamehe deni.

Kikundi cha “Imanuatha group”:  Kwa maelezo iliyoyapata kamati, Kikundi hiki kipo kata ya Terrat na kina wanachama 2 wanaotambulika. Hata hivyo                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                      mwanachama mmoja alikufa na mwingine inasemekana alihamia kondoa Dodoma. Inasemekana pia kuwa kuna wanachama wengine waliokuwa katika kikundi hiki na wanafanya biashara ya nguo lakini hakuna ushahidi wowote wa maandishi au mkataba kuthibitisha ukweli wa watu hao kuwa wanachama wa kikundi hicho. 
       
Kikundi cha “Faraja walemavu group”: Kwa maelezo iliyoyapata kamati, kikundi hiki kipo kata ya Levolosi na kinadaiwa Tshs.1,150,000.00. Kikundi hiki ni cha walemavu wakiwemo walemavu wa viungo na mmoja ni mlemavu wa ngozi (Albino). Inasemekana kikundi kilipopata fedha kilimpatia mwanakikundi mmoja kwanza ili afanye biashara na baadae wachukue wengine. Aliyepewa fedha hakuweza kuwapatia wenzake na fedha zilipotea katika mazingira yasiyoeleweka.
                                                                                                                                                                                                              
Katika kata ya Terrati na Murriet kuna vikundi saba (7) vyenye utata: Vikundi hivyo inasemekana vilipewa fedha wakati wa mwenge. Vikundi hivyo havina usajili, hakuna mikataba, wala hakuna picha za wadaiwa na inasemekana hata baadhi ya wahusika waliokuwa wanafahamika wamehamia kata nyingine au wamehama kabisa mkoa ikizingatiwa wengine wanakuwa wapangaji.

Katika kata ya Kimandolu wataalam wanakutana na changamoto kubwa kutoka kwa kikundi kimoja ambacho inasemekana kilipewa fedha kwa shinikizo la mwenyekiti, hawakufanya mradi wa kuzalisha na kwa sasa kiuhalisia wanakikundi hali zao za maisha ni mbaya sana kiasi kwamba inaonekana hawawezi kabisa kulipa hata wakipelekwa mahakamani.

Mhe. Mwenyekiti, ni maoni ya kamati kuwa baadhi ya vikundi havitaweza kabisa kurejesha fedha za Halmashauri kulingana na hali ilivyo. Katika mazingira hayo, kamati inalishauri baraza kama litaona inafaa, lianze kufikiria kufuta madeni kwa vikundi ambavyo iko wazi kuwa haviwezi kulipa.

MAPENDEKEZO YA JUMLA YA KAMATI
Mhe. Mwenyekiti, kamati inatoa mapendekezo ya jumla kama ifuatavyo;-

a)    Ndani ya miezi mitatu(3) kuanzia tarehe 15.07.2016 hadi tarehe 15.10.2016 vikundi vyote  vinavyodaiwa na Halmashauri viwe vimelipa madeni yote na vitakavyoshindwa kulipa vichukuliwe hatua za kisheria.  
b)   Iundwe “Task force” ya kufuatilia madeni yote amabayo Halmashauri inavidai vikundi. Task force hiyo iundwe ngazi ya kata na mitaa kwa kuwashirikisha wataalam na viongozi wote ili kupata ushirikiano wa kutosha katika zoezi la kuwatambua wahusika ikizingatiwa wengine hawajulikani.
c)    Vyombo vya dola vitumike kusaidia kukusanya madeni hayo ya Halmashauri kwani historia inaonyesha pale vyombo vya dola vinapohusishwa wahusika huweza kurejesha fedha hizo hata kwa kulipiwa na ndugu zao
d)   Baada ya muda wa miezi mitatu kuisha, wale wote waliojipatia fedha kwa kughushi  picha ikiwa hawatakuwa wamelipa, wakamatwe na wafunguliwe kesi za kujipatia fedha kwa udanganyifu bila kujali wadhifa wao walionao au waliokuwa nao
e)    Viongozi wote ngazi ya kata waache tabia ya kuingilia utendaji kazi wa maafisa maendeleo ya jamii katika kata zao. Ni wajibu wa WDC kuhakikisha utaratibu unafuatwa katika hatua zote zinazohusu uratibu wa vikundi kwa mujibu wa kanuni na taratibu na siyo kuingilia mchakato kwa maslahi binafsi.
f)     Idara ya maendeleo ya jamii makao makuu ikishirikiana na maafisa maendeleo ya jamii ngazi za kata, watendaji wa kata na waheshimiwa madiwani wahakikishe Saccos na Vikoba vyote vinavyopewa fedha kwa sasa vinazifikisha kwa vikundi lengwa na marejesho yanafanyika kwa wakati.
g)    Muda wa maandalizi (“grace period”) uongezwe toka mwezi mmoja hadi miezi minne (4) na muda wa kurejesha uongezwe kutoka mwaka mmoja (miezi 12) hadi mwaka mmoja na nusu (miezi 18)                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                  
h)   Vikundi vitatu vya Walemavu vikiwemo Batiki Olasiti, Faraja walemavu group, na Jakaya Walemavu Group, baraza livifutie vikundi hivi deni kwani kamati imejiridhisha kuwa hakuna namna ya kurejesha fedha hizi toka kwa walemavu hao hata wakifunguliwa kesi mahakamani; kwani kwa jinsi ilivyo hawana uwezo wa kulipa na kwa kikundi cha ‘batiki’ wanachama wote walikufa. Kamati inashauri hivi ili kuondoa hoja za ukaguzi. Kamati pia inashauri kuwa wakati mwingine vikundi vya namna hii vikikopeshwa fedha vifuatiliwe kwa umakini sana ili kuhakikisha shughuli zake zinasimamiwa kwa mujibu wa malengo yaliyoombewa fedha ili ziweze kurejeshwa kuepusha walemavu kutumia hali yao ya ulemavu kupoteza fedha za umma.

Pamoja na vikundi hivyo vitatu kamati inashauri baada ya “task force” kufanya kazi yake, vikundi ambavyo vitashindikana wahusika wake kupatikana, vianishwe ili uangaliwe uwezekano wa kufuta madeni hayo kuliko kuendelea kudai madeni yasiyowezekana kulipika na pengine kutumia fedha nyingi kufuatilia kikundi zaidi ya ambazo kinadaiwa lakini pia kuondoa hoja za ukaguzi na kwa kuzingatia ukweli kuwa matatizo yote yanayosababisha kutorejeshwa kwa fedha hizo yamechangiwa na uzembe wa Halmashauri yenyewe.

i)     Halmashauri ianzishe mfumo wa kompyuta wa kanzi data “Computerized Data base” ya vikundi vyote vilivyopo, vinavyosajiliwa na vinavyokopeshwa na mikataba na nyaraka mbalimbali ili kuweza kufuatilia kwa karibu masuala yote yanayovihusu vikundi.
j)     Idara ya sheria ifanye utafiti kujiridhisha juu ya madai ya Kikundi cha “Jakaya walemavu group” na ikibainika ni kweli mahakama haikutenda haki iangalie namna gani ya kukisaidia kikundi hiki cha walemavu ikizingatiwa kuwa mradi huu ulianzishwa kwa fedha za umma chini ya TASAF ambapo halmashauri inawajibu wa kuzisimamia kwa kushirikiana na TASAF.
k)   Wanasiasa wote wakiwemo wenyeviti wa mitaa na waheshimiwa madiwani wajiepushe kuwa wanachama kwenye vikundi ili kurahisisha uratibu wa vikundi hivyo. Wanasiasa wabaki na kazi ya kuhamasisha wananchi kuunda vikundi na siyo kuunda vikundi vyao wenyewe.
l)     Wanachama wote wanaopewa mikopo picha zao na mawasiliano yao wote yawepo ngazi ya kata ili iwe rahisi kuwasiliana nao na wanaposhindwa kulipa iwe rahisi kuwapata. WDC zihakikishe watu wote wanaokopeshwa wawe wanafahamika makazi yao na visiwepo vikundi ambavyo wanachama wake wote ni wapangaji.

4.0 MADENI MENGINE YA HALMASHAURI KUFIKIA JUNI, 2016
Mhe. Mwenyekiti, kamati pia ilipewa kazi ya kupitia madeni yote ambayo Halmashauri inadai ili kutoa mapendekezo stahiki. Kamati katika kikao chake cha tarehe 5/08/2016 ilipitia orodha ya madeni mbalimbali ambapo hadi kufikia Juni 30, 2016, Halmashauri ilikuwa inadai kiasi cha Tshs.18,953,500.00 kwa soko la Killombero, Tshs.74,890,000.00 kwa maduka ya Stendi Ndogo, Tshs.41,175,000.00 maduka ya Jengo la Ghorofa (maduka 42-stendi ndogo ambao hawajaanza kulipa kabisa), Tshs.9,205,000.00 maduka 27 ya ghorofa stendi ndogo, Tshs.1,125,000 stendi ndogo mzunguko, Tshs. 3,801,000.00 Maduka Soko la  Kijenge, Tshs.14,690,000.00 maduka soko kuu, Tshs.960,000.00 maduka soko la sanawari, Tshs.43,040,000 maduka ya Rangers Safari, Tshs. 25,470,000.00 Standi kuu.

Katika orodha hiyo ya madeni zipo pia Tshs.579,729,090.92 kwa ajili ya ushuru wa mabango, Tshs. 350,961,000.97 deni la kodi ya majengo, Tshs.64,820,000.00 anadaiwa wakala wa taa za barabarani aitwaye Masoko Agencies Ltd, na Tshs.61,960,000.00 anadaiwa wakala wa taa za barabarani aitwaye Kiliative Solution. Kwa upande wa Service Levy kiasi kinachodaiwa hakijulikani kutokana na mfumo unaotumika kulipia ushuru huo.

Mhe. Mwenyekiti, kamati ilipitia madeni ya kila chanzo na kutoa mapendekezo yake kama ifuatavyo;-


4.1 WADAIWA WA MABANGO 2015/2016
Mhe. Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016, Halmashauri ilikuwa inadai jumla ya Tshs.579,729,090.92 toka kwa jumla ya wateja 1045. Kamati iliona ni vyema kuwaita wadaiwa wote wanaodaiwa kuanzia Tshs. Milioni 1 na zaidi ili kuongea nao ili kujua ni kwa nini hawalipi madeni yao. Halmashauri iliwaandikia barua za wito na mnamo tarehe 17.08.2016 kamati ilikutana na jumla ya wadaiwa 10 na kuzungumza nao. Kutokana na kikao hicho kamati ilibaini changamoto zifuatazo kukwamisha kutokusanywa kikamilifu ushuru wa chanzo hiki;-

Kuwepo kwa mamlaka mbili zinazokusanya ushuru wa mabango
Wadaiwa takribani wote walioitikia wito walidai kuwa tayari wamekwisha lipia mabango yao na kuwa wamefanya malipo hayo kwa wakala wa barabara TANROAD.  Madai haya yalithibitishwa na watumishi wanaohusika na ushuru wa mabango walioeleza kuwa mara kadhaa wamekuwa wakikutana na watumishi wa TANROAD nao wakikusanya ushuru wa mabango kutoka kwenye mabango yaliyopo kwenye eneo lao. Ingawa hapo awali ushuru huu ulikuwa unakusanywa na Halmashauri husika, baadae serikali iliagiza TANROAD kuwa inakusanya yenyewe ushuru wa mabango yote yaliyowekwa kwenye barabara zake.

 Utapeli katika Ukusanyaji wa ushuru.
Utapeli umekuwa changamoto kubwa kiasi cha kuathiri mapato ya chanzo hiki. Kwa muda sasa wakusanyaji wa ushuru wa mabango wamekuwa wakikutana na kesi za wenye mabango kulipa fedha kwa watu wanaotumia risiti bandia za halmashauri. Imekuwa rahisi sana kwa wananchi kutapeliwa kutokana na ukweli kuwa hapo awali chanzo hiki kilikuwa kwa wakala hivyo baada ya kuanza kukusanywa na halmashauri yenyewe, baadhi ya mawakala walibaki na nakala za risiti za halmashauri na nakala za “bill” na kuwa bado wananchi wanawatambua kama wakusanya ushuru wa mabango.

Kwa sababu hiyo wameendelea kugawa ‘bill’ na kukusanya ushuru kwa kutoa risiti bandia. Ingawa Halmashauri imefanya vya kutosha kuwasaka na kuwakamata matapeli hao ambao wanaendelea na kesi, bado halmashauri inapaswa kutoa elimu zaidi kwa umma juu ya utapeli huo. Inaonekana wakati chanzo hiki kinachukuliwa na Halmashauri elimu haikutolewa kwa wananchi juu ya kuondolewa kwa mawakala hao ndiyo maana wameendelea kuwatapeli wananchi.
Vitendea kazi visivyotosheleza mahitaji ya wakusanya ushuru wa mabango
Mhe. Mwenyekiti, kitengo cha mabango kinakabiliwa na tatizo la kutokuwa na gari maalum kwa kazi hiyo kwa muda mrefu sasa. Watumishi katika eneo hili wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kutegemea magari ya idara nyingine ambazo nazo zinayahitaji magari kwa shughuli mbalimbali za Halmashauri. Kwa sababu hiyo wamekuwa wakishindwa kuzunguka kupeleka “bili” na kufuatilia masuala yote yanayohusu ushuru wa mabango ikiwemo kupima “size”. Ikumbukwe pia kuwa mabango yanawekwa kila siku hivyo unahitajika ukaguzi wa kila siku.
Mhe. Mwenyekiti, tatizo la kukosekana kwa vitendea kazi siyo tu linaathiri makusanyo katika chanzo cha mabango, bali vyanzo vingine vya mapato. Kamati imegundua kuwa walipakodi wengi wamekuwa wakichelewa kulipa kodi kutokana na kutopelekewa bill mapema tatizo linalosababishwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana usafiri wa uhakika kwa watumishi wa ukusanya ushuru.

Ushirikishaji mdogo wa Utawala wa ngazi za chini katika ushuru huu
Ushuru wa mabango ungekusanywa kwa urahisi zaidi kama viongozi wa ngazi za kata na mtaa wangehusishwa kikamilifu. Hii ni kwa sababu mabango yanawekwa kila siku kwenye mitaa yao hivyo inakuwa rahisi kwa wao kuyaona na kutoa taarifa mara moja ili yapimwe na kulipia ushuru.

4.2 MGOGORO WA HALMASHAURI NA KAMPUNI YA SKYTEL
Katika orodha ya wadaiwa kamati imeona ni vyema kuongelea juu ya wakala wa kuwasha taa za barabarani Skytel kutokana na utetezi wake aliouwasilisha mbele ya kamati lakini pia umuhimu wa kuwa na taa za barabarani zinazowaka. Baada ya kumsikiliza wakala huyo, kamati ilijiridhisha kuwa mgogoro kati ya wakala huyo na halmashauri umekuwepo kutokana na pande mbili kutoamua kukaa pamoja kujadili mgogoro huo. Baada ya kupitia nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mbele ya kamati, kamati ilijiridhisha pia kuwa yalikuwepo mapungufu kadhaa kwa pande zote mbili ambayo yangeweza kumalizwa kama wahusika wangekaa katika meza ya mazungumzo. Ni kweli kuwa Halmashauri inamdai Skytel lakini pia baadhi ya madai ya Skytel yana msingi na kwa vile anaonekana yuko tayari kwa mazungumzo na bado ana nia ya kuendelea kuwa mdau wa maendeleo katika masuala ya taa za barabarani na kwa kuzingatia pia kuwa halmashauri inaendelea kupata hasara kutokana na mgogoro huo kwa yeye kutolipia mabango yake na kwa kutowasha taa za barabarani, ipo haja ya kukaa naye meza moja kutanzua mgogoro huo wa muda mrefu.

Mhe. Mwenyekiti, ili kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabiri chanzo hiki cha mapato, kamati inapendekeza mambo yafuatayo;-
a)    Ofisi ya Mkurugenzi iunde timu itakayopitia barabara kuu zote zinazomilikiwa na TANROAD ili kujiridhisha kama kuna mabango ambayo TANROAD wanakusanya lakini hayamo kwenye mita za barabara ya TANROAD (mita 60).
b)   Gari maalum la kisasa ambalo ni wazi, lenye “cren” linunuliwe kwa ajili ya kukusanyia ushuru wa mabango tu. Kwa sasa litafutwe gari la muda ambalo wakusanya ushuru wa mabango watakuwa wanalitumia wakati utaratibu wa kupata gari kwa ajili ya kazi hiyo unasubiriwa.
c)    Mabango yote ya Halmashauri yawekewe “stika zenye barcon” ili kuonyesha mabango ambayo tayari yamelipa kiurahisi.
d)   Ushuru wote wa mabango ambao ushuru wake uko chini ya milioni 1 ukusanywe kwa kushirikiana na uongozi ngazi ya kata hata ikibidi kata ibakiziwe 10% ya makusanyo hayo kama motisha.
e)    Kwa kushirikiana na uongozi ngazi ya kata na mitaa Halmashauri ihakikishe mabango yote mapya yanasajiliwa mara tu baada ya kuwekwa.
f)     Halmashauri iendelee kutoa elimu ya kutosha juu ya utapeli unaoendelea katika ushuru wa mabango ili kuwaepusha wananchi na utapeli huo
g)    Halmashauri iangalie uwezekano wa kuanzisha “Business forum” ambapo wafanyabiashara watakuwa wanakutana na Halmashauri kujadili juu ya mambo mbalimbali ili kujenga mahusiano mazuri na kuiweka Halmashauri karibu na wafanyabiashara ili kurahisisha zoezi la kulipa kodi.
h)   Uangaliwe uwezekano wa kuanzisha mfumo mpya wa malipo wa “e-wallet” ambapo malipo yanaweza kufanyika kwa njia za M.pesa, Tigo.pesa n.k ili kuwaondolea usumbufu wananchi kupanga mstari benki kulipia ushuru huo ikizingatiwa wengine wanakuwa wanadaiwa fedha kidogo.
i)     Agenda ya Mabango iwe agenda ya kudumu katika vikao vyote vya WDC na mikutano ya mitaa ili kuwaepusha wananchi na utapeli unaoendelea na pia kuhamasisha kulipa ushuru wa mabango.
j)     Kanzi data (data base) ya mabango ihuishwe kwa kutumia GIS na picha
k)   Mchakato wa sheria ndogo ukamilishwe ili kurekebisha viwango vinavyolipwa kwa sasa
l)     Mgogoro wa Skytel na Halmashauri ufuatiliwe kwa kina na ikiwezekana umalizwe mapema na taarifa yake ipelekwe kamati ya fedha mwezi ujao ili kuiondolea Halmashauri hasara kwa kuwa mmiliki wa Skytel aliongea na kamati na kuonyesha nia ya kujadiliana na Halmashauri ili mgogoro uishe.
m)  Taarifa za madeni yote ziwasilishwe kila mwezi katika kamati ya fedha na utawala ili kamati ya fedha iweze kushauri




4.3 MADENI YA MAWAKALA WA TAA ZA BARABARANI
Mhe.Mwenyekiti, hadi kufikia Juni 2016, jumla ya Tshs.126,780,000.00 zinadaiwa kutoka kwa mawakala hao. Mawakala hao si tu wameshindwa kulipa ushuru kwa Halmashauri bali pia wameshindwa kuwasha taa kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za TANESCO. Tatizo lililobainika hapa ni kuwa biashara ya mabango ambayo kimsingi ndiyo ingewawezesha kupata mapato na wao kulipa mapato ya Halmashauri inabadilika kila mara na hivyo kuwafanya washindwe kupata faida na hivyo kushindwa kulipa ushuru.
Kamati inapenda kulishauri baraza kuwa uwashaji wa taa usiangaliwe kama chanzo cha mapato bali ichukuliwe kama huduma. Ingekuwa vyema kama wakala angepewa eneo, awashe taa na ushuru utolewe pale tu anapopata bango la matangazo na Halmashauri kupima mabango hayo.

MAPENDEKEZO YA KAMATI
Kufuatia changamoto ya baadhi ya mawakala wa uwashaji wa taa kushindwa kukusanya mapato ya matangazo na hivyo kushindwa kuwasha taa, kamati inapendekeza menejimenti kupitia upya vigezo vya zabuni za uwakala wa uwashaji wa taa ili kufanywa kwa ufanisi zaidi. Pia katika mkataba kuwe na kifungu ambacho kitamtaka wakala katika kila mita ya umeme (luku) kuwa na umeme usiopungua wastani wa matumizi ya wiki moja. Pia Halmashauri iwe na uwezo wa kukagua mita za umeme ili kuona kama umeme uliopo unatosha kwa matumizi ya zaidi ya wiki moja. Aidha adhabu iwekwe kwa wakala atakayekiuka kipengele hiki.

4.4 KODI YA MAJENGO
Mhe. Mwenyekiti, hadi kufikia Juni 2016, Halmashauri ilikuwa inadai kiasi cha Tshs. 350,961,001.97 kwa chanzo hiki. Hata hivyo kwa vile chanzo hiki cha mapato tayari kimekwishachukuliwa na serikali kuu chini ya TRA, kamati haikujadili kwa kina chanzo hiki zaidi tu ya madeni inayodai.

Kamati inatoa Mapendekezo yafuatayo kuhusu madeni ya kodi ya majengo;-
a)    Watu wote waliokuwa wanadaiwa na Halmashauri hadi kufikia Juni 30, 2016, kesi zote zipelekwe mahakamani ili madeni yote hayo yaweze kulipika
b)   Taarifa za madeni hayo na mienendo ya kesi hizo iwe inapelekwa kwenye vikao vya kamati ya fedha kila mwezi
c)    Majengo yote ya Taasisi za umma, na vyama vya siasa bila kujali itikadi hasa kwa yale yaliyokwishafanyiwa tathimini, Halmashauri ihakikishe yanalipa madeni ya majengo na viwanja vyao kwani vyama vya siasa (kama vile , CCM vimekuwa na tabia ya kutolipa kodi mbalimbali za Halmashauri na kuwa vyama vyote vya siasa vijenge tabia ya kutoa ushirikiano kwa maofisa wa serikali katika ufuatiliaji wa masuala mbalimbali.Kamati imegundua kuwa ccm haijawahi kulipa kodi ya majengokwa kipindi chote cha uhai wake,majengo ya ccm ambayo yanatumika kibiashara,ccm mkoa,Ccm Vijana,Ccm Wilaya,ccm kwa mtei,uwanja wa stadium,Hospital ya Soweto,majengo ya ofisi za kata Kuanzia kaloleni,Levolosi,Sekei,Ngarenaro,Daraja Mbili,Themi,Elerai,etc kwa ujumla wake ni Jumla ya deni la Zaidi ya 507,289,100(507mil).Hizi ni fedha nyingi sana ambazo ccm hawajalipa.

4.5 KESI ZA MADAI ZILIZOKO MAHAKAMANI
Mhe. Mwenyekiti, pamoja na kuwa Halmashauri inadai fedha nyingi kutoka kwa walipa kodi mbalimbali, ukweli kuwa Halmashauri nayo inadaiwa hauepukiki. Ingawa kamati isingependa kuzungumzia kwa kina mashauri yaliyoko mahakamani, ni ukweli kuwa mpaka sasa zipo kesi mbalimbali mahakamani ambazo Halmashauri inadaiwa kihalali baada ya kupewa huduma mbalimbali.

Kamati inapenda kushauri kuwa Halmashauri ijitahidi kadri iwezavyo kuwa inawalipa watoa huduma mbalimbali kwani kutowalipa wazabuni siyo tu kunaipotezea Halmashauri uaminifu, bali pia kuisababishia kesi ambazo zingeweza kuepukika. Kwa sababu hiyo, pamoja na ushauri ambao tayari kamati imeutoa juu ya kuwepo matakwa ya usuruhishi katika mikataba (“arbitration”) ni maoni ya kamati kuwa Halmashauri iangalie uwezekano wa kupitia upya kesi zilizoko mahakamani ambazo Halmashauri inadaiwa kihalali yafanyike mazungumzo ili madai yao halali yalipwe kwa kuzingatia ukweli kuwa siyo vyema Halmashauri kuwadhulumu wananchi wake.

4.6 LESENI NA MFUMO WA HUDUMA YA BIASHARA WA HALMASHAURI
Mhe. Mwenyekiti, kutokana na changamoto mbalimbali wanazozikabili wafanyabiashara katika jiji letu, na kwa kutumia hadidu ya rejea namba (IV) kamati imeona ni vyema japo kwa ufupi kuongelea suala la biashara katika jiji letu. Katika suala la biashara Kamati ingependa kusisitiza juu ya mambo mawili;
i)             Leseni Ndogo
Kamati inasisitiza Halmashauri kutekeleza azimio la kuanzisha leseni ndogo. Kamati inasisitiza juu ya jambo hili kutokana na ukweli kuwa wapo wafanyabiashara wengi wanaofanya biashara ndogondogo ambao hawawezi kukata leseni ya kawaida. Kwa wafanyabiashara hao wadogo kutokuwa na Leseni, siyo tu wanashindwa kupata huduma za kifedha, bali pia Halmashauri inakosa mapato. Kamati inasisitiza jambo hili lifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.
ii)           Kutawanyika kwa ofisi za fedha na Biashara katika Halmashauri yetu
Mhe. Mwenyekiti, kamati imegundua kuwa umbali uliopo kati ya ofisi za fedha na biashara unawatatiza wananchi. Mwananchi anapowasilisha Halmashauri ‘slip’ ya benki ya malipo ya leseni kwa mfano, anapaswa aanzie kwa “cashier” halafu aelekezwe kwenda ofisi ya biashara. Kutokana na jinsi korido ya kuelekea ofisi za biashara ilivyo, uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi wananchi huenda ofisi za masjala au za waandishi wa mikutano kutokana na kuonekana moja kwa moja kutokea ofisi za ‘cashier’.

Kamati inashauri  menejimenti, izihamishie ofisi za biashara kutoka zilipo sasa kwenda ofisi namba 2 (ya mazingira/mipangomiji kwa sasa) na ofisi ya mishahara na hizo ofisi zihamie ofisi za biashara. Kamati inashauri hivyo ili kuziweka pamoja ofisi za fedha na biashara kutokana na shughuli zake kuelekeana na kwa kuzingatia pia kuwa ni idara moja lakini pia kuwaondolea wananchi usumbufu. Hii pia itaondoa msongamano usiopendeza wa wananchi katika kurido za ofisi za biashara za sasa.
Kamati pia inapendekeza kuwa menejimenti ofisi namba 2 na ile ya mishahara zitengenezwe ili yawekwe madirisha huduma zitolewe kwa nje na eneo la nje litengenezwe katika hali inayoweza kuwaruhusu wananchi kupata sehemu za kukaa wakati wanasubiria huduma.

4.7 TAARIFA YA UTEKELEZAJI
Mhe. Mwenyekiti, wakati kamati ikiendelea na uchunguzi wake, masuala mengine ilielekeza wahusika kuendelea na utekelezaji. Mpaka kamati inakamilisha ripoti yake baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wanadaiwa na Halmashauri ambayo kamati ilielekeza waandikiwe barua za kulipa madeni yao yakiwemo mabenki na baadhi ya vikundi vya wanawake na vijina tayari wamekwishalipa madeni yao na wanaendelea kulipa. Kamati inaipongeza menejimenti kwa ushirikiano ilioutoa kwa kamati katika kufanikisha suala hili.

5.0 HITIMISHO
Mhe. Mwenyekiti, kamati inapenda kuhitimisha kazi yake kwa kusema maneno machache kama ifuatavyo;-

Kwanza; wajumbe wa kamati wanapenda kulishukuru baraza lote kwa kuwaamini wajumbe wa kamati na kuwateua kufanya kazi hii ngumu. Kamati inatoa taarifa kuwa imeifanya kazi hii kwa uaminifu wa hali ya juu na kamati imetoa maoni yake kwa hekima kubwa na kwa kuzingatia heshima kubwa iliyopewa na baraza.

Pili; kamati inapenda kuwaomba wajumbe wote wa baraza kuisoma kwa kina ripoti hii pamoja na mapendekezo yake ili hatimaye wafanye mjadala wa kina kwa manufaa mapana ya Halmashauri yetu na kwa manufaa ya walipa kodi wa jiji la Arusha.

Tatu; kamati inalisii baraza kutambua kuwa wajumbe katika kamati hii wamefanya kazi kwa kujitolea muda wake mwingi kwa maslahi ya Halmashauri yetu, hivyo inategemea baraza litaazimia kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wale wote ambao kwa makusudi na uzembe wa hali ya juu waliisababishia Halmashauri hasara ya mamilioni ya fedha. Kamati inategemea baraza litatoa maamuzi ambayo ni fundisho kwa watu wengine wote wanaojihusisha ama wanaotarajia kujihusisha na vitendo viovu kama hivyo.
Nne; kamati inapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa ofisi ya Mkurugenzi na wataalam wa Halmashauri kwa ushirikiano mkubwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi iliyopatiwa kamati.

Mwisho; Napenda kuwashukuru wajumbe wangu wa kamati wote kwa ushirikiano wao mkubwa waliouonyesha kuanzia mwanzo kamati ilipoanza uchunguzi hadi kukamilika kwa ripoti hii. Ni matumaini yangu kuwa wajumbe walikuwa na kazi nyingi zinazowakabili lakini waliziacha na kutoa muda wao mwingi katika kuifanya kazi hii kwa maslahi ya Halmashauri yao na kwa ajili ya wananchi wa jiji la Arusha. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape afya njema na Baraka tele katika maisha yao ya sasa na yajayo.

Kwa niaba ya kamati, ripoti hii inathibitishwa leo tarehe 28 Agosti 2016 na;



………………………………………..
Nanyaro E.J
Mwenyekiti wa Kamati










































VIAMBATANISHO
Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO