Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

WAMILIKI WA MABASI YA ABIRIA ARUSHA WAPEWA ONYO; UHALIFU WAPUNGUA KWA 24%


 

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa onyo kwa wamiliki wa mabasi ambayo yanavunja sheria za usalama barabarani. Akizungumza  na waandishi wa habari leo mchana ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ukaguzi wa mabasi ya abiria uliofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 22 mwezi huu hadi 24, Kamamda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo  alisema kwamba, wamiliki wa magari wanatakiwa wahakikishe mabasi yao yanazingatia ubora unaokubalika hali ambayo itasaidia abiria wanasafiri salama.

“Mbali na ubora wa gari lakini pia madereva wanatakiwa wazingatie sheria za usalama barabarani kama vile kuendesha kwa kufuata maelekezo ya alama“. Alisema Kamanda Mkumbo.

Alisema katika ukaguzi huo wa kushtukiza uliojumuisha mabasi yaliyokuwa yanakwenda mikoani na yale yaliyokuwa yanaingia jijini hapa, jumla ya mabasi 77  yalikamatwa kwa makosa ya ubovu na mwendokasi.

“Kati ya hayo mabasi 25 yalikamatwa kwa makosa ya mwendokasi ambapo 20 kati yao yalilipiwa tozo na matano wahusika walipelekwa mahakamani, wakati mabasi 52 yalikutwa na makosa ya ubovu ambapo 41 yalitozwa tozo na mabasi 11 toka makampuni mbalimbali tumeyasitishia kutoa huduma mpaka hapo yatakapofanyiwa marekebisho”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.

Kamanda Mkumbo alisema kwamba pamoja na ukaguzi wa magari hayo ambao unafanywa kila siku lakini Jeshi hilo litaendelea kufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara ili kuhakikisha abiria wa mabasi hayo wanasafiri salama, huku akitoa wito kwa abiria watoe taarifa popote wanapogundua dereva anakwenda kinyume na sheria za usalama barabarani.

WAKATI HUO HUO, RPC ARUSHA ANASEMA: UHALIFU UMEPUNGUA KWA 24%

 Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupunguza makosa ya jinai kwa mwaka huu 2017 toka 1,378 yaliyoripotiwa mwaka jana 2016 hadi kufikia 1,041 na kufanya idadi ya makosa yaliyopungua  kufikia 337.

Akitoa takwimu hizo ofisini kwake  jana mchana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo, alisema kwamba punguzo hilo ni sawa na asilimia 24.4 huku akifafanua kwamba takwimu hizo ni kwa mujibu wa kuanzia  mwezi  Januari hadi Juni mwaka huu 2017.

“Huu upungufu wa makosa ya jinai ni takwimu za nusu mwaka, toka Januari hadi Juni mwaka huu 2017 ikilinganishwa na mwaka 2016 kwa muda kama huo, hivyo utaona tumejitahidi “. Alifafanua Kamanda Mkumbo, huku akiendelea kubainisha,

“Mwaka jana kwa nusu mwaka makosa ya mauaji yalikuwa 45 lakini mwaka huu kwa kipindi kama hicho makosa yalikuwa 36 pungufu ya makosa 9, wakati makosa ya kubaka yalikuwa 106 kwa mwaka jana lakini mwaka huu yameshuka hadi kufikia makosa 79 pungufu ya makosa 27, huku makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka jana yalikuwa makosa 16 na mwaka huu kwa kipindi kama hicho yamekuwa makosa matatu sawa na upungufu wa makosa 13”. Alisema Kamanda Mkumbo.

Akiendelea kutoa takwimu hizo Kamanda Mkumbo aliendelea kusema kwamba, makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu kwa miezi sita ya mwanzo wa mwaka jana yalikuwa 54 na mwaka huu kwa kipindi kama hicho yalifikia makosa 28 ni pungufu ya makosa 26, makosa ya wizi wa pikipiki kwa mwaka jana yalikuwa 54 lakini mwaka huu yamefikia 24 pungufu ya makosa 30 na makosa ya uvunjaji yalikuwa 453 kwa miezi sita ya mwaka jana lakini mwaka huu yameshuka hadi kufikia 195 pungufu ya makosa 258.

Akizungumzia mapambano dhidi ya dawa za kulevya Kamanda Mkumbo alisema kwamba ongezeko la ukamataji lilipanda toka kesi 295 hadi kufikia kesi 301 huku akielezea hilo linatokana na zao la ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi ambapo taarifa wanazozitoa zinafanyiwa kazi hasa kupitia misako inayofanyika katika maeneo mbalimbali.

Aidha kwa upande wa usalama barabarani Kamanda Mkumbo alisema jeshi hilo kwa miezi sita ya mwaka huu yaani Januari hadi Juni lilikusanya jumla ya Tsh 2,107,530,000/= (Bilioni mbili milioni mia moja na saba laki tano na elfu thelathini) kutokana na tozo za makosa ya usalama barabarani kiasi hicho ni tofauti na mwaka jana 2016 kwa miezi sita ya mwanzo ambapo tozo zilizokusanywa zilikuwa Tsh 2,520,180,000/= (Bilioni mbili milioni mia tano ishirini laki moja na elfu themanini).

Hii ni pungufu ya tozo zenye thamani ya Tsh 412,650,000/= (Milioni mia nne kumi na mbili laki sita na elfu hamsini) kwa mwaka huu na hali hiyo ilitokana na elimu iliyotolewa na Jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama barabarani kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wote wa barabara wa vyombo vya usafiri hasa waendesha pikipiki maarufu kama boda boda  na watembea kwa miguu.

Mafanikio hayo ni sehemu ya  muendelezo wa mapambano dhidi ya uhalifu ambapo takwimu za uhalifu  kwa  mwaka nzima wa 2016 zinaonyesha makosa ya jinai yalipungua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na mwaka juzi 2015.
Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO