Hatua ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba, Mwamtumu Dau imezua gumzo nchini na wadau wakitoa maoni tofauti.
Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara zilizopokewa kwenye halmashauri zao walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Alipoitwa mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi cha fedha zilizotolewa katika halmashauri kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara, Mwantumu alijibu kuwa ana idara nyingi anazozisimamia hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina.
Alipohojiwa kwa nini anamjibu hivyo, akasema hawezi kusema uongo kauli ambayo ilionekana kumkera Dk Magufuli lakini akasema amewasamehe lakini baadaye iikatolewa taarifa na Ikulu kuwa wametenguliwa.
Mwamtumu alisema fedha hizo zipo chini ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) na kwamba yeye kama mkurugenzi hafahamu ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya mradi huo.
Akizunguzia tukio hilo Rais wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema shirikisho hilo limepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo.
Nyamhokya alisema ingawa ukurugenzi ni nafasi ya kuteuliwa na kwamba anayeteua ana mamlaka ya kumsimamisha wakati wowote kulingana na vigezo vyake, lakini kilichotokea ni cha kusikitisha.
“Ukiangalia tukio lenyewe, Rais alimuuliza hadharani na baadaye akasema amewasamehe lakini muda mfupi baadaye akatengua nafasi zao, hii siyo sawa.”
Aliongeza kuwa Tucta wanaamini wakurugenzi hao bado wapo katika utumishi wa umma na kwamba watapangiwa shughuli nyingine kama alivyoahidi Rais mwenyewe.
Nyamhokya anaungwa mkono na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji aliyesema kitendo hicho hakikuwa cha kiungwana.
Dk Mashinji alisema kwake kiasi cha fedha hakikuwa muhimu badala yake cha msingi ni kujua iwapo fedha hizo zipo au hazipo na kwamba wakurugenzi wote walijieleza vizuri.
“Siyo dhambi kusema hujui ni kiasi gani kwani yeye siyo ofisa mtendaji mkuu, kiongozi mjanja angebadili swali kwani alichofanya ni kuidhalilisha Serikali na si kumdhalilisha mkurugenzi yule.”
Dk Mashinji alisema kilichotokea katika mkutano ule ni matokeo ya jambo wanalolilalamikia kila kukicha la kuwateua makada ambao wamekosa vyeo na kuwaweka katika nafasi za utendaji matokeo yake wanashindwa kusimamia vitu vinavyohusu kazi yao.
Hata hivyo, Dk Mashinji alimpongeza Mwamtumu kwa majibu yake na kuonyesha si mnafiki na yupo tayari kusimamia ukweli anaouamini.
“Hakuona busara kumdanganya Rais badala yake alionyesha yeye ni kiongozi kwa kuwaita watu walio chini yake watoe ufafanuzi. Mimi nampa sifa ila ningemwambia ajitahidi kujua hata vitu vidogo vinavyohusu wilaya yake.”
Mashinji pia alishangaa Rais kuwa na misimamo ya aina mbili, awali akitangaza kuwasamehe viongozi hao lakini muda mfupi baadaye akatengua uteuzi wao.
“Kama kiongozi hutakiwi kuonyesha sura mbili katika maamuzi yako, hii inasababisha kuwa na watumishi waoga na wasiojiamini kwa kuwa hawajui kesho yao,” alisisitiza.
Akitoa maoni yake, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema Serikali ilianzisha Wakala wa Barabara mjini na vijijini (Tarura) ambao ndiyo wasimamizi wa fedha za miradi ya barabara na wakati mwingine wakurugenzi wa halmashauri wanakuwa hawazijui.
“Yale maswali waliyoulizwa wakurugenzi wa manispaa ya Bukoba na Bukoba si ya kwao, kuna Tarura ambayo kuanzia Julai Mosi ilianza kufanya kazi kwa hiyo hao ndio walipaswa kuulizwa na si wakurugenzi,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini
“Kilichofanyika ni kuwadhalilisha watumishi wa umma, kunahitajika kuwa na heshima kwa watumishi wenzako, kwa nini wasingeulizwa Tarura ambao ndiyo hasa fedha hizi wanazipokea,” alihoji Zitto
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Hamad Salim alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya nafasi za uteuzi, anaweza kukuteua na kutengua.
“Tatizo linakuja pale ambapo unamteua baada ya kumfanyia vetting (kumchunguza) halafu unamtengua katika mkutano wa hadhara. Maelezo yote ya mama alikuwa wazi kuwa anasimamia idara nyingi na alikuwa tayari kumwita mhazini,” alisema Dk Salim
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema; “ule mkurugenzi alisema hana takwimu na hataki kusema uongo, mbona kuna mawaziri huwa wanaulizwa maswali na wanashindwa kujibu na wakati mwingine maswali hujiandaa au huomba kupewa muda, hakukuwa na kosa la kumtengua.”
0 maoni:
Post a Comment