Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

TAMKO LA USHIRIKIANO WA VYAMA VYA UPINZANI VYA CHADEMA, CUF NA NCCR MAGEUZI JUU YA MUSTAKABALI WA MCHAKATO WA KATIBA MPYA

TAMKO LA USHIRIKIANO WA VYAMA VYA UPINZANI VYA CHADEMA, CUF NA NCCR MAGEUZI JUU YA MUSTAKABALI WA MCHAKATO WA KATIBA MPYA KUFUATIA KUPITISHWA KINYEMELA KWA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA WA MWAKA 2013

1234803_239687566179450_573999025_nPicha kutoka mtandao wa Jamii forum ikionesha viongozi wa vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi wakiwa katika kikao cha pamoja kwa nia ya kutoka na makubaliano ya pamoja kufuatia mapungufu yaliyomo kwenye muswada wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, muswada unaosubiri kusainiwa na Rais Kikwete uwe sheria.


Leo tarehe 15 Septemba ni siku ya demokrasia duniani; Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kwamba ujumbe wa siku hii kwa mwaka huu ni “Kuzipa nguvu sauti kwa demokrasia” (Strengtherning Voices for Democracy).

Sisi, Chama Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR Mageuzi tuliokutana kwa nyakati mbalimbali Jijini Dar Es Salaam tangu kupitishwa kinyemela kwa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 tumetafakari, kujadili, kuzingatia yafuatayo juu ya mustakabali wa mchakato wa katiba mpya ya taifa letu:

KWAMBA Katiba ya Nchi ni mali ya wananchi na sheria mama ya taifa hivyo mchakato wa mabadiliko yake haupaswi kuhodhiwa na chama chochote, taasisi yoyote, kundi lolote au mtu yoyote. Mchakato wa katiba mpya unapaswa kuwapa wananchi mfumo shirikishi na utaratibu jumuishi wa kuwawezesha kuandika katiba yao wakiongozwa na misingi ya maridhiano.

KWAMBA Mchakato wa katiba mpya unahitaji uvumilivu, stahamala, hekima, kuheshimiana na kamwe usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala na wadau wengine. Misingi hii ikipuuzwa mchakato wa mabadiliko ya katiba unaweza kutumbukiza taifa letu katika mipasuko, migogoro au hata machafuko.

KWAMBA Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 uliopitishwa katika mkutano wa kumi na mbili wa Bunge tarehe 6 Septemba 2013 na yaliyojiri kabla, wakati na baada ya kupitishwa kwa muswada huo yameweka mustakabali wa mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba mashakani.

KWAMBA, Ikumbukwe kwamba kabla ya muswada huo kusomwa kwa mara ya pili, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo ilijadiliwa katika mabaraza ya katiba yaliyosimamiwa na tume na mabaraza ya katiba ya taasisi, asasi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana. Kinyume na maoni ya makundi mengi mengine, Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliweka msimamo wa kupinga mambo makuu muhimu yaliyopendekezwa na rasimu hiyo na kujadili mikakati ya kukwamisha mabadiliko makubwa kuanzia katika Bunge Maalum la Katiba.

KWAMBA, Muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 umepitishwa ukiwa na marekebisho yaliyomo kwenye muswada wenyewe na yaliyoongezwa kupitia majedwali ya marekebisho yaliyowasilishwa na wabunge wa CCM kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka makubwa zaidi katika uteuzi wa wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka katika taasisi, asasi na makundi mbalimbali. Marekebisho hayo yamefanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala baada ya kupokea maoni ya wadau wa Tanzania Bara. Aidha, kamati haikukutana kabisa na wadau wa Zanzibar wala wawakilishi wa wananchi wa upande wa pili wa Muungano.

KWAMBA, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikushirikishwa kikamilifu katika kuandaa muswada uliopelekwa wa mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopelekwa Bungeni. Mwezi Mei 2013, Serikali ya Muungano ilipeleka Muswada wa mabadiliko ya sheria ya mabadiliko ya Katiba uliokuwa na vifungu sita. SMZ waliujadili na kupeleka mapendekezo yao ya rasimu ya muswada huo. Muswada uliopelekwa bungeni uliongezwa vifungu vingi ambavyo havikuwemo katika rasimu iliyopelekwa SMZ. Mathalani kifungu cha 26 cha sheria mama kurekebishwa kuruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazikupatikana kwamara mbili, basi sasa kura kwa mara ya tatu itakuwa kwa uwingi wa kawaida (“simple majority”) ya kila upande. Pia, Kifungu cha 37 kinachohusu kuvunjwa kwa Tume ya Katiba ambacho kimerekibishwa bila mashauriano na SMZ ambapo sasa Tume ya Katiba itavunjwa baada ya Rasimu kuwasilishwa katika Bunge la Katiba na sio kama SMZ ilivyoafiki awali kuwa Tume itavunjwa baada ya matokeo ya kura ya maoni. Ikiwa serikali ya Muungano inaidanganya hata SMZ kuhusu suala muhimu la katiba tutawezaje kufikia muafaka wa kitaifa katika suala zima la katiba ya nchi inayotokana na wananchi.

KWAMBA Yaliyojiri bungeni tarehe 4, 5 na 6 Septemba 2013 na yanayoendelea kusemwa na kutendwa na CCM na Serikali inayoongozwa na chama hicho juu ya muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba ni matokeo ya mikakati hiyo. Hivyo, nguvu za pamoja za wananchi, wadau na wote wenye kuitakia mema nchi yetu zinapaswa kuunganishwa kunusuru mchakato wa katiba mpya uliotekwa na kuhodhiwa na CCM na Serikali yake.

Kwa kuzingatia masuala hayo na mengine, Vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR- Mageuzi vinaazimia yafuatayo:

Mosi; Tunapongeza na kuunga mkono hatua ya wabunge wa vyama vyetu kuweka pembeni tofauti zao na kutumia njia za kibunge kutaka mjadala wa muswada huo usiendelee bungeni kwa lengo la kuhakikisha masuala muhimu kwa niaba ya wananchi yanazingatiwa. Vyama vyetu vimeamua kuendeleza ushirikiano huo kwa kuweka pembeni tofauti zetu na kuunganisha nguvu za pamoja kunusuru mchakato wa katiba mpya kwa maslahi ya wananchi na nchi kwa ujumla. Aidha, Tunalaani ukiukwaji wa kanuni za Bunge na mila desturi za kibunge uliofanywa wa kuingiza vifungu vipya kinyemela, kukiuka masharti ya kushughulikia madai ya taarifa za uongo kutolewa bungeni, kuzuiwa kwa wabunge wa upinzani kusema juu ya masuala ya utaratibu na kutoa hoja za kusimamia haki na taratibu za kibunge, kushambuliwa kwa baadhi ya wabunge, pamoja na kudhalilishwa kwa hadhi ya Bunge kwa ujumla.

Pili; Tunatoa mwito kwa Rais asisaini muswada huo kuwa sheria kwa kuwa marekebisho yaliyofanyika na utaratibu uliotumika kuyapitisha ni kinyume cha dhamira na dhima ya majadiliano aliyofanya na vyama vyetu na wadau wengine kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2011 na 2012. Rais arejeshe muswada huo bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuamiana na muafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Tatu; Tunaanza kuunganisha umma kufanya maamuzi ya kunusuru mchakato wa katiba mpya kuendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka yote ni wananchi na Serikali inapaswa kuwajibika kwa wananchi. Mkutano wa hadhara wa pamoja tutakaoufanya Uwanja wa Jangwani Jiji Dar Es Salaam tarehe 21 Septemba 2013 utakuwa ni mwanzo wa hatua za kwenda kwa wananchi. Njia zitakazotumika kuunganisha wananchi kuchukua hatua na ratiba ya vyama kuzunguka katika maeneo mengine nchini ni kati ya masuala yatakayoelezwa katika mkutano huo.

Nne; Tunaomba asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, taasisi za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, jumuiya za wafugaji, jumuiya za wavuvi, taasisi za sekta binafsi, jumuiya za watu wenye ulemavu, asasi za wataalamu wa masuala mbalimbali, jumuiya za wanawake, jumuiya za vijana, vyama vya wastaafu na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana tuweke pembeni tofauti zingine na kuungana nasi kukataa mchakato wa katiba kuhodhiwa kwa matakwa ya CCM na Serikali yake.

Tumalizie kwa kunukuu maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki-Moon kwenye ujumbe wake juu ya siku ya leo tarehe 15 Septemba 2013, “ On this International Day of Democracy, I call on Leaders to hear, respect and respond appropriately to the voices of the people, whether expressed directly or through elected representatives” .

Tunatarajia kwamba viongozi watasikiliza, kuheshimu na kuitikia sauti za watu na wawakilishi wao za kunusuru mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi yetu usihodhiwe na chama kimoja au kikundi cha wachache bali wananchi wote.


________________________
Prof. Ibrahimu Haruna Lipumba
M/kiti wa CUF Taifa
_________________________
James Francis Mbatia (Mb)
M/Kiti wa NCCR –Mageuzi Taifa
________________________
Freeman Aikaeli Mbowe(Mb)
M/kiti wa CHADEMA Taifa

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO