Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

POLISI WA ARUSHA WAAMUA KUWAFUATA WANANCHI MITAANI

GEDSC DIGITAL CAMERA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas akiongea na askari, viongozi wa vyama na serikali, vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na wananchi wa eneo la Tarafa ya Themi wakati wa kuwatambulisha askari 15 watakaoungana na wananchi wa eneo hilo katika utendaji wa kazi za kipolisi za kila siku.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

GEDSC DIGITAL CAMERA

Viongozi wa serikali za mitaa,Askari, vikundi vya ulinzi pamoja na wananchi wakimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas wakati akielezea mikakati ya Polisi 15 watakaokuwa wanafanya kazi katika tarafa ya Themi pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Jumla ya askari 45 ambao walikuwa wanafanyakazi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na Kitengo cha Usalama Barabarani wametawanywa katika tarafa tatu za jijini hapa. Askari hao kutoka vitengo mbalimbali wamesambazwa katika tarafa za Themi, Elerai na Suye wakiwa ndani ya kikosikazi ambacho kinajumuisha askari wa Upelelezi, Usalama barabarani na askari wa kawaida ambapo lengo kubwa ni kushirikiana kwa ukaribu na wananchi.

Akizungumza na wananchi katika matukio ya ukaguzi wa tarafa hizo pamoja na kuwatambulisha askari hao jana tarehe 10.01.2014 katika tarafa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas amesema kwamba, jamii katika maeneo yao ikiamua kupinga uhalifu toka ngazi ya familia kwa kushirikiana na nguvu ya askari hao hakika uhalifu utapungua kama si kutokuwepo kabisa.

“Hapo awali jeshi la Polisi lilikuwa na askari kata lakini baadae likawa na askari tarafa na kuona kwamba hiyo haitoshi sasa limeamua kuanzisha kanda za kitarafa ambapo kila tarafa itakuwa na askari 15 kutoka vitengo mbalimbali watakaoongozwa na Mkaguzi wa Polisi, hali hii itasaidia kujenga ukaribu kati ya wananchi na jeshi la Polisi na kutatua matatizo mbalimbali ya kiusalama kabla hata ya kufika ngazi ya wilaya”. Alifafanua Kamanda Sabas.

Kamanda Sabas aliendelea kusisitiza kwa kuwaomba viongozi wa tarafa hizo kuhakikisha kwamba, vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimeundwa viendelee kuwa hai ili ustawi wa usalama wa watu na mali zao uendelee kuwepo. Pia aliwaomba waendelee kukusanya michango toka kwa wananchi wa maeneo yao ili zisaidie kuwapa posho askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi na kununulia vitendea kazi kwani jukumu la ulinzi ni watanzania wote na hasa wazalendo na kila mmoja aone umuhimu wa amani na usalama.

Alisema pamoja na wananchi hao kujitahidi kupambana na uhalifu na kuwakamata wahalifu lakini baadhi yao huwa hawajitokezi kutoa ushahidi mahakamani hali ambayo inasababisha watuhumiwa waachiwe huru na kupata ujasiri hivyo kuweza kujiunga na makundi mengine kuendelea kufanya uhalifu.

Kamanda Sabas alitoa namba zake tatu za simu kwa wananchi hao ili ziweze kusaidia katika mawasiliano na kuongeza kwamba, japo kuwa askari hao 15 wapo katika maeneo yao, bado wapo huru kuwasiliana naye na viongozi wengine katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu huku akisisitiza pia ofisi yake ipo wazi kwa wale watakaotaka kwenda kumuona.

Kwa upande wake Diwani wa Tarafa ya Themi kutoka kata ya Unga Limited Mh.Issa Omari (CCM) alisema kwamba mpango huo wa askari 15 kupelekwa katika tarafa hiyo utasaidia katika kudhibiti vitendo vya uhalifu kwani kutakuwa na nguvu ya pamoja ya ulinzi ambayo itakuwa inajumuisha askari wa Jeshi la Polisi na vikundi vya ulinzi shirikishi.

Diwani huyo wa Unga Ltd aliwataka askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi wasirudi nyuma bali wanatakiwa kusonga mbele na yeye pamoja na wananchi wanaliunga mkono Jeshi la Polisi kwa mpango huo; huku akiongeza kwa kusema kwamba katika kata yake uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kuwepo kwa ushirikiano kati ya jeshi la Polisi, viongozi wa mtaa huo na vikundi vya ulinzi shirikishi.

Naye Diwani wa kata ya Elerai Mh. Mhandisi Jeremiah Mpinga wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tarafa ya Elerai alisema, sasa umefika wakati wananchi wa eneo lake waondoe itikadi zao za vyama badala yake wote washirikiane katika suala zima la kuimarisha ulinzi huku akiwata viongozi wa mitaa kuhamasisha uanzishaji zaidi wa vikundi vya ulinzi shirikishi ili washirikiane na askari wa jeshi la Polisi huku akiunga mkono mpango huo kwa kauli mbiu yake isemayo “ULINZI KWANZA MAISHA SALAMA”.

Source: Bertha Blog, Arusha

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO