Yafuatayo ni baadhi ya majibu ambayo bado yamejaa maswali kuhusiana na anayeidaiwa kuwa mwekezaji wa "Treni ya Uwanja wa Ndege" nchini Tanzania, mradi ambao tayari umeshatiliwa saini.
Maswali ya baadhi ya watu wanaojadili suala hili yanauliza ikiwa hii ilikuwa ni bahati mbaya ama ni makusudi kama ilivyofanyika mikataba mingine mibovu na kuigharimu Serikali na Taifa fedha nyingi.
Fuatana na Evarist Chahali katika chapisho hili akitafuta majibu kwa maswali ya mambo 'yale yale' kama vile watu hufanya kwanza ndipo wakafikiri baadaye kana kwamba viongozi wetu wamekuwa ni "sikio la kufa, dawa halisikii."
Rasi Jakaya Kikwete akipokea zawadi ya saa kutoka kwa Robert Shumake, ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya M/S Shumoja inayotajwa kuwa itawekeza katika mradi wa usafiri wa treni ya kisasa Dar
Hebu soma kwanza habari ifuatayo kisha tujadili 'sintofahamu' kuhusu mwekezaji wa mradi huo
SERIKALI imetia saini mkataba wa uwekezaji wa pamoja kati yake na kampuni ya Marekani kwa ajili ya kuanza mradi wa usafiri wa treni ya kisasa itakayoanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesisitiza ni lazima kufanya haraka kwani mwekezaji, Kampuni ya Ms Shimoja ya Marekani, iko tayari hata sasa kuleta treni hizo aina ya Diesel Multiple Unit (DMU) ambazo ni za kisasa, itakayopita kila baada ya nusu saa.
Usafiri huo wa treni kwenye njia ya umbali wa kilometa 13 kutoka uwanja wa ndege hadi katikati ya jiji, unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu au mapema mwakani ukilenga kubeba abiria kati ya 800 na 1,000.
Katika hafla ya kutia saini kati ya mwekezaji huyo na Shirika la Reli Tanzania (TRL) jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe aliwaambia watendaji kwamba ikiwa watafanya haraka, baada ya wiki mbili watasaini makubaliano ya mwisho na kuanza urekebishaji na ujenzi wa vituo sita vya kupandia treni kwa kadi.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Ms Shimoja, Dk Robert Shumake na Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu walitia saini jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Waziri Mwakyembe na Katibu Mkuu wake, Dk Shaaban Mwinjaka.
Waziri Mwakyembe alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kusafisha njia ya kupata wawekezaji, akiwemo mfanyabiashara huyo mkubwa ambaye ametajwa kuwa na imani kuwekeza katika mradi huo utakaogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 35.
Kwa mujibu wa waziri, waliamua kuanza mradi huo baada ya kuhamasisha mashirika makubwa ya ndege kufanya safari katika kiwanja hicho cha ndege. Hata hivyo, alisema wasafiri wanapata kero ya usafiri kufika katikati ya jiji jambo wanalotegemea mradi kuondoa kero hiyo.
“Mabehewa hayo yataunganishwa kulingana na idadi ya abiria waliopo na muda, huku mwekezaji akiwekeza bila masharti kama walivyo wengine; kama vile kutaka dhamana ya serikali,” alisema Mwakyembe.
Hata hivyo alisisitiza, “lakini ni lazima watendaji waache ukiritimba kwa kufanya utaratibu haraka ili kazi zianze.”
Alisema katika utaratibu wa PPP, uwekezaji na idara nyingine lazima wafanye haraka. Aidha alitaka watendaji TRL kumsihi mfanyabiashara huyo kuleta treni nyingine mbili za Ubungo mpaka Stesheni na kwingineko.
Treni hiyo itasaidia kupunguza adha kwa abiria wanaosafiri kwa ndege, ambapo katika kituo cha Karakata, itajengwa njia ndogo ya treni mpaka barabarani. Pia litajengwa daraja kwa ajili ya wasafiri kuvuka na mizigo yao.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kisamfu alisema watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha usafiri huo unaanza mapema iwezekanvyo kutoka katikati ya jiji hadi Pugu kupitia maeneo ya Karakata, kwenye Uwanja wa Ndege kwa kutumia Reli ya Kati.
Mwekezaji Dk Shumake ambaye ni Balozi wa Heshima Tanzania nchini Marekani, alisema wako tayari kuanza mradi huo hata leo kama utaratibu utakamilika.
Alisisitiza kwamba uwekezaji huo utaondoa tatizo la foleni barabarani kutoka uwanja huo wa kimataifa wa ndege hadi katikati ya jiji.
CHANZO: Habari Leo
Sasa twende hatua kwa hatua kutafuta ukweli wa habari hii.
1. Nenda kwenye tovuti ya kusaka habari ya Google, kisha ingiza jina 'm/s shumoja.' Mie nimetumia siku nzima ya jana ku-search na sikuambulia kitu. Habari pekee kuhusu 'kampuni' hiyo ni za kutoka Tanzania kuhusu kusainiwa mkataba huo. Uthibitisho huu hapa chini (bonyeza picha kuikuza)
2. Hivi inawezekana kweli kwa kampuni kubwa 'yenye uwezo wa kuendesha mradi mkubwa kama huo' isiwe na tovuti? Mhusika Robert Shumake, ana akaunti katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Hata hivyo, ukibonyeza website yake (niliyoizungushia duara jekundu), hupati kitu
Kadhalika, katika ku-search orodha ya makampuni yaliyosajiliwa Marekani, matokeo ni hayo hayo
Lakini kingine kinachotia mashaka zaidi ni wasifu wa 'mwekezaji' huyo. Kwa ku-search jina lake, kuna habari mbalimbali zinazozua wasiwasi. Moja ni hii HAPA na nyingine ni hii HAPA
3. Ukisoma habari ya mwanzo kuhusu maelezo ya Waziri Mwakyembe, anadai kuwa mwekezaji huyo yupo tayari kunza huduma ya treni hizo hata leo. Pengine ni kweli lakini twajuaje ilhali hiyo kampuni yake haina hata tovuti mtandaoni? Je kampuni hiyo ina-exist kweli? Ukiangalia wasifu wake kwenye mtandao wa kijamii wa LinkedIn hakuna habari zozote kuhusu kampuni hiyo.
4. Pamoja na nia nzuri ya kuleta wawekezaji, lakini kinacholeta wasiwasi ni uharaka wa mradi huo. Ndio twafahamu umuhimu wa kuboresha usafiri kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, lakini ni muhimu kuzingatia taratibu, kwani sote twakumbuka jinsi tulivyoingizwa mkenge katika suala la Richmond kwa kisingizio kama hicho cha uharaka (wa kutatua tatizo la umeme wakati huo, na matokeo yake tatizo hilo laendelea hadi leo). Je Idara ya Usalama wa Taifa imeshafanya vetting ya kutosha kuhusu mwekezaji huyo hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo unahusu eneo nyeti (vital installation) la Uwanja wa Ndege?
Enewei, mie binafsi ntaendelea kuchunguza zaidi kuhusu suala hili ikiwa ni pamoja na kusaka taarifa zaidi kuhusu kampuni hiyo ya uwekezaji na mwekezaji mwenyewe. Endelea kutembelea hapa kwa taarifa zaidi.
Maswali ya msingi: Katika michoro tunaona jina la Shumake Rails, lakini taarifa pia zasema kampuni husika ni m/s shumoja. Je mwekezaji ni Shumake Rails (soma HAPA) au m/s shumoja/ shimoja (soma HAPA)? Kwa hakika haiwezekani tuwe tunazungumzia kampuni mbili tofauti au kampuni moja yenye majina mawili.
Tukiangalia hiyo michoro twaweza kujiuliza, huyo mwekezaji alikuja lini Tanzania kabla ya kuiandaa na kuiwasilisha siku ya kuwekeana mkataba? Je mpango huu ulikuwepo kitambo lakini sasa ndio twafahamishwa? Taratibu za zabuni zilikuwaje?
Na pengine picha hii ya mwezi Septemba mwaka jana kati ya Waziri Mwakyembe na 'mwekezaji' wakati waziri alipozuru nchini Marekani yaweza kutoa 'clues' flani.
Hapa chini ni uchunguzi nilioufanya kuhusu tovuti ya shumoja.com. Kama unavyoona, tovuti haina anwani ya ofisi za kampuni hiyo wala namba za simu.
Na kingine cha kukanganya zaidi ni ukweli kwamba licha ya tovuti hiyo kutokuwa na taarifa zozote za kuonyesha uzoefu wa mradi kama huo tunaoambiwa utawekezwa huko nyumbani, jina hapa ni SHUMOJA RAILS ilhali katika picha za hapo juu tunaona michoro ikiwa na jina la SHUMAKE RAILS
Lakini licha ya tovuti hiyo kutokuwa na habari za kutosha kuhusu kampuni hiyo, picha zifuatazo zaonyesha bayana kuwa ilisajili hivi majuzi tu, yaani mwezi uliopita. Hivi yawezekana kwa kampuni 'kubwa' ya uwekezaji kutokuwa na tovuti muda wote huo, na ghalfa kutengeneza tovuti mpya isiyo na maelezo ya kutosha takriba mwezi mmoja tu kabla ya kutangazwa kuwa itawekeza kwenye mradi wa treni za kisasa huko Dar?
Taarifa hizi zimenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Chahali kupitia www.wavuti.com:
0 maoni:
Post a Comment