Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Simulizi za polisi kuua gaidi Arusha

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas

Mkazi wa Mianzini, jijini Arusha, Yahaya Sendei (31), anayedaiwa kuwa kiongozi wa watuhumiwa ulipuaji mabomu nchini na umwagiaji tindikali watu, ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati akidaiwa kujaribu kuruka kwenye gari lao kwa lengo la kutoroka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,  Liberatus Sabas (pichani),  jana alisema kuwa mtuhumiwa huyo aliuawa  juzi  saa 5:30 usiku katika barabara ya Arusha- Babati eneo la Kisongo, wilayani Monduli, wakati wakimpeleka kijijini alikozaliwa Chemchem, wilaya ya Kondoa, mkoa  Dodoma, kuwaonyesha askari bomu jingine aliloficha.

Alidai kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa wakati wa uhai wake alikuwa mwalimu wa karate na judo ni mwasisi na kinara wa matukio ya ugaidi yaliyotokea jijini Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.

“Huyu tulimpata kutokana na intelejensia imara ya polisi ya kisasa na ya hali ya juu na tulimkamata mkoani Morogoro Oktoba 6, mwaka huu na kusafirishwa Oktoba 11 mwaka huu kuletwa Arusha na alipohojiwa alikiri kuhusika na kuratibu matukio ya ugaidi na alikuwa akijificha kwenye nyumba tofauti na porini, ” alisema kamanda huyo.

Alidai mtuhumiwa huyo alipigwa risasi kwenye mguu wa kulia na kalio la kulia alipojaribu kutumia uzoefu wake wa kuruka judo na kupiga karate kutaka kuwazidi polisi ili atoroke na kwamba alifia njiani wakati akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa matibabu.

Hata hivyo, hakueleza sababu za kumpiga risasi mtuhumiwa huyo ambaye hakuwa na silaha yoyote na kama alijeruhi askari yeyote zaidi ya kudai kuwa maiti yake imehifadhiwa hospitalini hapo kwa uchunguzi zaidi na kusubiri ndugu kuichukua kwa maziko.

Vile vile Kamanda Sabas hakueleza kama hatua ya kuuawa kwa mtuhumiwa huyo muhimu itawakosesha polisi taarifa muhimu katika mchakato wa upelelezi wao.

Awali Kamanda huyo alitaja baadhi ya matukio ambayo mtuhumiwa huyo inadaiwa alikiri kuhusika nayo kuwa ni la Oktoba 25 mwaka 2012 lililotokea saa 5:30 usiku katika mtaa wa Kanisani Paloti, kata ya Sokoini One, jijini Arusha.

Katika tukio hilo, yeye na wenzake inadaiwa walitega bomu kwenye chumba cha Sheikh Abdulkarim Idd Jonjo (52) nyumbani kwake na kumjeruhi baada ya kulipuka.

Inadaiwa tukio la pili na wenzake ambao wamefikishwa mahakamani, lilitokea Mei 5 mwaka jana saa 10:30 maeneo ya Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti jijini Arusha.

Katika tukio hilo inadaiwa kuwa  aliratibu kurushwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi  56.

Juni 15 mwaka 2013 saa 11:50 jioni katika viwanja vya Soweto, kata ya Kaloleni, jijini Arusha na wenzake, wanadaiwa kurusha bomu na kuua watu wanne, kujeruhi 60.

Julai 11 mwaka 2013  saa 5:00 eneo la Kwa Mrombo, jijini Arusha na wenzake wanadaiwa walimwagia tindikali usoni Sheikh Said Juma Makamba.

Februari 12 mwaka 2014 saa 3:45  katika eneo la Tindigani, Unga Ltd, jijini humo,  kwenye msikiti wa Sawiyatu Qadiria, wanadaiwa kumwagia tindikali usoni Sheikh Hassan Bashir.

Februari 28 mwaka 2014 saa 5:15 alfajiri katika msikiti wa Bondeni, wanadaiwa kumwagia tindikali Mistapha Mohamed Kiago na kumjeruhi usoni na shingoni.

Aprili 13 mwaka 2014 saa 1:30 usiku, eneo la Mianzini kwenye nyumba ya wageni na Baa ya Niht Park, wanadaiwa walirusha bomu na kujeruhi watu 11 na kusababisha kifo cha mmoja.

Aprili 13 mwaka 2014 la saa 5:00 katika eneo la Majengo, jijini Arusha, anadaiwa alirusha bomu kwa kushirikiana na wenzake na kuwajeruhi watu wawili Sudi Ali Sudi (37) ambaye ni Mkurugenzi wa Answar Muslim Kanda ya Kaskazini na mwenzake Muhaji Hussein Kifea (38),  mkazi wa Dar es Salaam. Julai 7 mwaka huu,  saa 4:15 usiku eneo la

Uzunguni, mgahawa wa Vama Traditional Indian, uliopo jirani na Viwanja vya Gymkhana, wanadaiwa walirusha bomu na kujeruhi watu wanane.

Kamanda huyo polisi alisema wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaojihusisha na kikundi hicho ambacho mtuhumiwa huyo alikiri kuendesha mafunzo ya karate na judo kwenye baadhi ya misikiti jijini Arusha.

Hata hivyo, alisema vikundi hivyo vimesambaratishwa na polisi.

Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi ili kuendelea kudumisha amani jijini Arusha na maeneo mengine ya nchini.

“Hawa watu hawakuwa wanafadhiliwa nje ya nchi  ila walikuwa wanajifadhili wenyewe na kwa faida zao wenyewe” alisema Kamanda Sabas.

SOURCE: NIPASHE

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO