Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza bodi na menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujirekebisha kwa kuondokana na matumizi mabaya ya fedha na kuwasilisha upya ombi lake la kutaka kibali cha kukopa fedha kwa ajili ya kumalizia miradi yake ya ujenzi iliyokwama kutokana na ukosefu wa fedha.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 13 Desemba, 2017 katika sherehe ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi wa Iyumbu Mjini Dodoma baada ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia Mchechu kuomba Serikali itoe kibali kwa NHC kukopa Shilingi Bilioni 232 kwa ajili ya kumalizia miradi minne mikubwa ya ujenzi wa majengo iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na agizo hili Mhe. Rais Magufuli pia amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Bodi ya NHC kuchukua hatua dhidi ya migogoro iliyopo ndani ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watendaji wanaoleta chokochoko.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia Mchechu na wafanyakazi wa NHC kwa kazi nzuri wanazofanya ikiwemo ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Bilioni 34 hadi 154.
“Mambo mengi mnafanya vizuri, naifahamu NHC najua mmepiga hatua kubwa ya kujenga nyumba sehemu mbalimbali, lakini jirekebisheni kwenye matumizi ya fedha, nataka Waziri Lukuvi ukakae na bodi ya NHC na Mkurugenzi Mkuu mfanye tathmini na mniletee maelezo ya namna mtakavyozirudisha hizo Shilingi bilioni 232 mtakazokopa, nikipata maelezo vizuri nitatoa maelekezo Wizara ya Fedha na Mipango iwape kibali” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia Mchechu amesema katika awamu ya kwanza mradi wa makazi wa Iyumbu unajenga nyumba 300, ambapo 150 zimekamilika na zimeshanunuliwa na nyingine 150 ujenzi wake umeanza.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuanzisha ujenzi wa nyumba za makazi Dodoma hata kabla ya mradi wa Iyumbu na amebainisha kuwa ili kuwafikia Watanzania wengi ameshatoa maelekezo kwa NHC kuachana na ujenzi wa majengo marefu na badala yake kujielekeza katika ujenzi wa nyumba za kawaida zitakazouzwa kwa gharama nafuu.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameufuta mpango wa kuwepo eneo la makaburi ya viongozi na kuagiza eneo lenye ukubwa wa ekari 129 katika kata ya Iyumbu lililochukuliwa na Serikali lirudishwe kwa wananchi na waruhusiwe kulitumia kwa shughuli zao.
Mhe. Rais Magufuli pia ametaka mchakato wa kubadili sheria ya makaburi ya viongozi wa kitaifa ufanye kwa kuwa amejiridhisha kuwa viongozi wote hawana nia ya kuzikwa katika eneo hilo.
Sherehe za uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa makazi wa Iyumbu Mjini Dodoma umehudhuriwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
0 maoni:
Post a Comment