Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

News Updates: Kinachojiri Mkutano wa Saed Kubenea na Waandishi wa Habari Jijini Dar

Ndugu waandishi wa habari,
Natumaini mna taarifa kwamba tangu Ijumaa iliyopita, nimefungua shauri Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, kupinga kinachofanywa na Bunge Maalum la Katiba. Shauri hilo, limesajili kwa Na.28 la mwaka 2014.

Katika kesi hiyo, nimeomba Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi juu ya mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba, chini ya kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya mwaka 2011.

Aidha, nimewasilisha maombi madogo nikiomba Mahakama kutoa zuio la muda la kusimamisha Bunge Maalum la Katiba, wakati tukisubiri uamuzi wa kesi ya msingi. Maombi ya zuio yamepangwa kutajwa tarehe 4 Septemba na kesi ya msingi itatajwa 15 Septemba 2014.

Ndugu waandishi wa habari,
Tangu kuripotiwa kufunguliwa kwa shauri hili mahakamani, yapo mengi yaliyosemwa. Wapo walionipongeza na kunifariji. Wapo walionitia moyo na kuniomba nisirudi nyuma. Wapo walionidhihaki na kunikatisha tamaa. Wapo walionitisha.

Lakini wapo walioahidi kuniombea kwa Mwenyezi Mungu ili jambo hili kubwa nililolifanya kwa maslahi ya taifa langu, niweze kulifikisha mwisho nikiwa mzima na mwenye amani.

Ninafahamu jukumu hili nililolibeba ni zito sana. Linaweza likasababisha baadhi ya watu kukosa posho ikiwa mahakama itaridhia ombi langu la usitishaji wa Bunge la Katiba. Linaweza kunitenganisha na baadhi ya ndugu na marafiki zangu. Linaweza kuhatarisha hata maisha yangu.
Lakini kwa kuwa maisha yangu hayajawahi kuwa salama kwa zaidi ya miaka tisa sasa; nimesema Mungu ndiye atakayenilinda.

Ninajua kuwa kesi hii, inaweza kusababisha gazeti langu la ----------- ambalo limefungiwa kwa muda usiojulikana na watawala kwa kuitumia sheria katili ya magazeti, linaweza lisifunguliwe kabisa. Hii ni kwa sababu, waliofungia ----------- ndiyo haohao niliowashitaki.
Hata hivyo, nimesema niko tayari kwa lolote. Nitakabaliana nalo kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniongoza.

Ndugu waandishi wa habari,
Nimefungua shauri hili kwa kusukumwa na uzalendo wangu na kulinda heshima ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano waliotoa maoni yao mbele ya Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, nami nikiwamo.

Nimefungua shauri hili baada ya kujiridhisha kuwa wananchi waliowengi, kutoka makundi mbalimbali – serikalini hadi chama tawala – wanakiri kuwapo tatizo katika tafsiri ya sheria kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba.

Baadhi ya walioko bungeni wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta, wanasema wanaweza kufanya lolote katika rasimu. Wanaweza kufuta rasimu; kubandua sura yote na wanaweza kubandika sura mpya.

Siyo hivyo tu: Wanaweza hata kukusanya maoni upya kutoka makundi mbalimbali. Kazi hii, ndiyo inayofanyika sasa bungeni.
Lakini wapo wanaoamini kuwa Bunge Maalum la Katiba, halina mamlaka ya kufanya kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Halina uwezo kukusanya maoni upya.

Bunge Maalum la Katiba, haliwezi kunyofoa moyo wa rasimu ya katiba kama ilivyowasilishwa na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba na kuleta kitu kipya ambacho hakikutokana na wananchi; na ambacho kimekusanywa kinyume cha sheria.

Nimekwenda mahakamani baada ya kumuona Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema akishindwa kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Badala yake, Jaji Werema amempotosha rais kuwa hana mamlaka ya kusimamisha mchakato wa Katiba.

Sheria inayosimamia mchakato wa katiba mpya ni sheria tofauti na sheria nyingine katika nchi. Sheria nyingine zote zinasimamiwa na vyombo vya serikali. Hii inasimamiwa moja kwa moja na wananchi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotumika sasa, haina kifungu chochote kinachoruhusu kutungwa katiba mpya. Wabunge wote wa Bunge la Muungano ambao sasa wamefanywa wajumbe wa Bunge la Katiba, akiwamo Werema, waliapa kulinda katiba iliyopo na kuitetea. Rais wa Jamhuri ya Muungano ameapa kulinda katiba iliyopo.

Lakini kwa kuwa Bunge la Jamhuri liliridhia kutunga katiba mpya kwa kutumwa na wananchi – siyo kwa kutumwa na katiba iliyopo – rais anayo mamlaka mapana ya kusimamisha mchakato huu.

Rais anaposimamia mchakato huu, hafanyi hivyo kama rais binafsi. Anatekeleza matakwa ya wananchi ambao wote kwa umoja wao, wamempa yeye mamlaka yao kusimamia raslimali, ulinzi na usalama wa mali za raia wa Jamhuri ya Muungano.

Kwahiyo, ni ujuha kuacha mabilioni ya shilingi ya wananchi kuteketea, kisha watawala wakadai kuwa “rais hana mamlaka ya kusimamisha mchakato wa katiba mpya.”

Kutokana na mgongano huo, kama mwananchi wa Jamhuri ya Muungano nimewasilisha malalamiko yangu mahakamani kwa nguvu ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba inayosema: “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya katiba na Sheria za nchi.”

Suala zima la maoni ya wananchi haliwezi kuachwa mikononi mwa watu wachache. Mamlaka ya kutafsiri sheria za nchi, hawezi kuachwa mikononi mwa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum la Katiba wala chombo kingine kilichojinyakulia mamlaka hayo kinyemela.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Ibara ya 107 A (1), “mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni mahakama.”

Kwa msingi huo, iwapo tafsri yangu ni sahihi, kinachofanywa na Bunge la Katiba sasa, ni uvunjaji wa Sheria Na. 83 ya mwaka 2011, inayounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuanisha majukumu yake na Bunge la Katiba.

Kama tafsiri yangu ni sahihi, kinachofanywa na Bunge Maalum la Katiba, ni kuvunja Katiba. Hakikubaliki.
Hivyo basi, kupitia kwenu, nichukue nafasi hii, kuwaomba wananchi wote wanaolitakia mema taifa letu, kusimama pamoja nami katika kusaidia taifa kupata katiba inayoheshimu maoni ya wananchi.

Ninawashukuru wote waliofariji; wanaonitia moyo na walioahidi kuniombea katika hili. Ninawaomba waniunge mkono kwa hali na mali. Nchi hii ni yetu sote.

Saed Kubenea,
Mkuregenzi Mtendaji,
HHP Limited.

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO