Jana tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya mahojiano katika kipindi cha PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya habari vimeandika mahojiano yale. Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu msimamo wangu kuhusu mchakato wa Katiba.
Kwanza, Mimi sijawahi kuwa UKAWA wala kundi lolote lile katika Bunge Maalumu la Katiba isipokuwa kundi linalotaka maridhiano. Msimamo wangu kuhusu Muungano ni Serikali ...Tatu Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na Muungano imara usio tegemezi wala egemezi kwa Washirika wake.
Pili, Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupinga lugha za matusi na lugha za kibaguzi zilizokuwa zinaendelea ndani ya mkutano ule. Vilevile niliunga mkono kwamba Rasimu inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu iliyotokana na Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba. Nasisitiza umuhimu wa kupata Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tatu, kwa hali ya sasa kuna mkwamo katika kupatikana kwa Katiba Bora. Mkwamo unaotokana na kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano ya pande zinazopingana. UKAWA hawataki mazungumzo na Viongozi wa Bunge la Katiba badala ya kujenga maridhiano kila siku wanawabeza UKAWA jambo ambalo kamwe haliwezi kujenga mwafaka. Ushauri wangu ni kuahirisha mchakato mzima wa kuandika Katiba mpaka mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho machache kama ifuatavyo;
i) Tume ya Uchaguzi ili iwe huru na ionekane kuwa huru, ikiwemo kuwaondoa watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika kusimamia uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii) Kuondoa Mafuta na Gesi kama Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze mara moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa Mafuta katika vitalu vilivyopo upande huo wa Muungano
Mkutano wa Bunge Maalumu utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano utakuwa hauna maana yeyote na itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kununua madawa vijijini. Mimi binafsi sitahudhuria mkutano wa Bunge Maalumu kama makundi hasimu hayatakuwa yamefikia maridhiano.
Kabwe Zitto, MB/MBMK
0 maoni:
Post a Comment