Raia wa Vietnam, Dong Van (47) amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na meno 65 na kucha 447 za simba zenye thamani ya Sh189.4 milioni.
Van alikamatwa juzi saa 10 jioni akijiandaa kwa safari kuelekea Vietnam kwa kutumia ndege ya Shirika la Qatar kupitia Doha.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema raia huyo alikamatwa na nyara hizo akiwa amepakia katika begi lake la nguo huku zikiwa zimefungwa vizuri katika pakiti za mchele na kahawa. Selemani alisema baada ya kupita kwenye mashine za ukaguzi walibaini kwenye begi lake kulikuwa na pakiti 22 kati ya hizo saba zilikuwa na meno pamoja na kucha za Simba.
“Katika begi lake tulikuta suruali mbili, vyakula vyake pamoja na pakiti za mchele na kahawa ambazo zilikuwa zimechanganywa na kucha na meno ya Simba,” alisema Selemani.
Alisema walimkagua na kukuta baadhi ya pakiti zikiwa na meno 65 ya Simba ambayo yalifungwa kwa nailoni ili kuficha
harufu na kucha 447 zilichanganywa na mchele wa aina ya basmat.
Selemani alisema hiyo ni aina nyingine ya ujangili ambayo imeibuka baada ya ujangili wa tembo.
“Huyu raia alitumia mbinu kutudanganya alichukua mchele wa basmat alichanganya na kucha ili asigundulike kwa sababu zinafanana na tuligundua kuwa kuna meno ambayo hayajang’olewa muda mrefu. Yalikuwa yanatoa harufu, yalichanganywa na kahawa ili yasigundulike,” alisema Selemani.
Alisema mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Vietnam, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda Selemani alisema hilo ni tukio la tatu kutokea tangu Januari na raia kadhaa kutoka nchi za Asia walikamatwa na meno pamoja na kucha za wanyama. Alisema polisi wataimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kudhibiti aina hiyo ya utoroshaji wa nyara.
Hivi karibuni, Wizara ya Maliasili na Utalii ilifuta kibali cha uwindaji cha kampuni ya uwindaji ya Green Miles Safaris kwa kuendesha uwindaji kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na kuwinda wanyama ambao hawaruhusiwi na kuruhusu watoto chini ya miaka 16 kuwinda.
CHANZO: GAZETI MWANNCHI
0 maoni:
Post a Comment