Tanzania imeondolewa rasmi kuwa mwanachama wa Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani kutokana na kushindwa kutekeleza maagizo iliyotoa, mojawapo likiwa ni kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Pia MCC iliitaka serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi juu ya Sheria ya Makosa ya Mtandaoni (Cyber-Crime Law) katika kipengele cha kuchapisha kanuni za utekelezaji zinazozingatia mchango wa wadau na kuendelea kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kulinda uhuru wa kujieleza.
Aidha, MCC ilitaka kupata ufafanuzi wa kina juu ya watu kadhaa walioshikiliwa na vyombo vya dola mwaka jana kwa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni iliyoanza kutumika Septemba Mosi, mwaka jana kabla ya Bodi ya MCC kukutana.
Uamuzi huo ambao unaifanya Tanzania ikose misaada mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na shirika hilo, ulifikiwa katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa MCC kilichofanyika juzi nchini Marekani.
Awali kulikuwapo na matumaini kwamba Tanzania ingeidhinishiwa msaada wa mabilioni ya Shilingi baada ya kusitishwa kuipa muda wa kutekeleza mambo ambayo shirika hilo lilielekeza yafanyiwe kazi na Serikali ya Tanzania.
Shirika hilo lilisitisha kutoa msaada wa Dola za Marekani milioni 472 (Sh. trilioni 1) za awamu ya pili zikiwa ni fedha za maendeleo katika kikao chake cha bodi kilichofanyika Desemba 16, mwaka jana, baada ya Tanzania kushindwa kutimiza maelekezo iliyotoa.
Bodi ya Wakurugenzi ya MCC imesema kuwa, licha ya wasiwasi ulioelezwa mara kwa mara na Serikali ya Marekani na Jumuiya ya Kimataifa, Machi 20, mwaka huu Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar, ambao haukuwa shirikishi wala wenye uwakilishi unaostahili.
Pia bodi hiyo imesema Serikali ya Tanzania haijachukua hatua zinazostahili kuhakikisha kuwa uhuru wa kujieleza na kujumuika unalindwa katika utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao na kwamba mojawapo kati ya vigezo vya msingi ambavyo MCC hutumia kuingia ubia na nchi yoyote, ni dhamira ya dhati ya nchi hiyo kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na haki.
Uamuzi huo dhidi ya Tanzania ni mgumu kwa kuwa ni dhahiri kwamba utawaumiza wananchi wengi maskini. Tunasema hivyo kwa kuwa misaada inayotolewa na MCC ni ya msingi na inawagusa moja kwa moja wananchi maskini.
Itakumbukwa kwamba misaada hiyo inahusisha ujenzi wa barabara, maji na nishati hususan ya umeme na umaskini, hivyo Tanzania kuondolewa katika MCC maana yake ni kuwa miradi yote iliyokuwa inatekelezwa na mfuko huo itasimama na kuiathiri nchi na wananchi wake.
Miradi ya barabara, maji na nishati (umeme) ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, hivyo kwa Tanzania kuikosa kupitia MCC ni pigo kubwa, kwani kutaathiri jitihada za serikali ya Rais John Magufuli za kuipaisha nchi kiuchumi na kuipeleka katika uchumi wa kati.
Pamoja na kutambua kuwa kila nchi ina haki ya kufanya maamuzi yake bila kuingiliwa na mataifa ya nje, lakini tunaishauri serikali itafakari kuhusiana na uamuzi huo na ikiwezekana ifanye mashauriano na shirika hilo kuhakikisha inarejeshewa uanachama.
Kama alivyoeleza Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, kwamba Tanzania inaisihi Marekani ibadilishe maamuzi yake, tuna amini kuwa jitihada zaidi zitafanywa na Serikali ili Tanzania irejeshewe uanachama wake katika MCC.
CHANZO: NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment