Na Gazeti Mwananchi, Dar es Salaam 30 Machi 2016Wakati serikali ikihaha kubana matumizi ili kupata fedha za miradi ya maendeleo, Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) limesitisha rasmi mkataba wa awamu ya pili wa kutoa zaidi ya dola 700 milioni za Marekani (Sh1.4 trilioni) kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya umeme.
Uamuzi huo, ambao Balozi Augustine Mahiga ameuelezea kuwa “unamuumiza mtu pale panapouma katika suala la maendeleo”, umetokana na bodi hiyo kutoridhishwa na kitendo cha kurudia uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani bila ya kushirikisha wadau na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa kiti cha urais, akisema sheria na kanuni za uchaguzi zilikiukwa.
Hata hivyo, hakutaja ukiukwaji huo ulivyofanyika na wakati chama kikuu cha upinzani, CUF kikipinga uamuzi huo kuwa haukuwa halali kikatiba, Jecha alitangaza tarehe mpya ya uchaguzi. CUF ilisusia uchaguzi huo uliomalizika kwa CCM kushinda urais kwa asilimia 91 na viti vyote vya uwakilishi.
“Desemba 2015, bodi ya Millennium Challenge Corporation (MCC) iliahirisha kupiga kura ya kuiwezesha Tanzania kuwa na sifa za kupata mradi wa pili, ikirejea kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar na haja ya kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi kwa haki na amani,” inasema taarifa ya MCC.
“Bodi pia ilitaka kuhakikishiwa na Serikali ya Tanzania kuwa Sheria ya Mtandao haitatumika kukandamiza uhuru wa kujieleza na wa kuungana, kwa kuangalia ukamataji wa watu uliofanyika wakati wa uchaguzi. Jambo hili lilisisitizwa mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na taarifa ya Balozi (wa Marekani) Mark B. Childress.
“Machi 20, 2016, “Tanzania pia iliendelea na uchaguzi mpya licha ya Serikali ya Marekani na Jumuiya ya Kimataifa kushauri juu ya suala hilo. Serikali ya Tanzania pia haijachukua hatua zozote kuhakikisha uhuru wa kutoa maoni na kuungana vinaheshimiwa katika utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao.”
Taarifa hiyo inaeleza kuwa nchi ambazo ni washirika wa MCC hazina budi kuhakikisha zinakuwa na chaguzi ambazo ni huru na za haki kwa kuwa suala hilo ni kubwa katika miradi hiyo.
“Uchaguzi wa Zanzibar na matumizi ya Sheria ya Mtandao vilikwenda kinyume na suala hilo,” inasema taarifa hiyo.
“Matokeo yake, wakati Marekani na Tanzania zitaendelea kushirikiana katika mambo mengi ya kipa umbele, bodi ya MCC imeamua kwamba Serikali ya Tanzania imefanya vitendo ambavyo haviendani na sifa za kuwa mnufaika wa MCC, na imepiga kura ya kusitisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania. Kwa maana hiyo, MCC itasitisha shughuli zote zinazohusu maendeleo ya awamu ya pili ya miradi ya Tanzania.”
Tayari MCC ilishapitisha kutolewa kwa dola 9.8 milioni kwa ajili ya shughuli za upembuzi wa miradi ambayo Tanzania ilitaka itekelezwa kwenye awamu ya pili.
Tanzania ilipendekeza kuwa fedha ambazo zingetolewa kwenye awamu ya pili ya mkataba wa MCC zielekezwe kwenye miradi ya umeme na barabara baada ya mradi wa kwanza kujikita kwenye miradi ya ujenzi wa barabara, miundombinu ya maji na umeme vijijini.
Katika bajeti ya mwaka 2015/16, Serikali ilitenga Sh916.7 bilioni (sawa na asilimia 5.7 ya bajeti) kwa ajili ya miradi ya umeme na uamuzi huo unaifanya ipoteze takriban asilimia 10 ya bajeti yake, ambayo pia ingeweza kuendesha takriban wizara nane zilizotengewa fedha chini ya Sh150 bilioni.
Kwa mujibu wa tovuti ya MCC, awali Tanzania ilifikia vigezo vya kunufaika na awamu ya pili ya fedha za shirika hilo ambazo zingetumika katika sekta ya nishati, kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya umeme pamoja na kuboresha sera, sheria na kufanya mabadiliko ya sekta, ambayo ni pamoja na kuboresha utaalamu, masuala ya kifedha, na uendeshaji wa Tanesco na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na kuwezesha umeme kuwafikia wananchi wa vijijini.
‘Wametuumiza panapouma’
“Kitendo hiki ni kibaya. Unamuumiza mtu pale panapouma katika suala la maendeleo,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, balozi Augustine Mahiga alipoulizwa kuhusu uamuzi huo wa bodi ya MCC.
“Kitendo hicho kinafuta imani na uelewano kati yetu (Marekani na Tanzania) kwa sababu suala la nishati ni nyenzo ya maendeleo. Fedha hizo zingesaidia miradi ya umeme vijijini kwa hiyo watoto wetu wangesoma, wangepata elimu bora na zingeboresha huduma ya afya.
“Walitutamanisha kuwa watatupa hizo fedha, lakini wanafuta pale ambapo maendeleo yetu yamejikita.”
Lakini Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango alikuwa na maoni tofauti.
“Serikali tayari imejipanga katika kuongeza makusanyo ya ndani na hata bajeti ijayo haitategemea fedha za MCC. Tunategemea fedha za ndani na kwa wadau wengine wa maendeleo ndiyo maana tunajitahidi kukusanya fedha za ndani,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alisema Serikali ikipata taarifa rasmi ya MCC itafanya mazungumzo kuhusu suala hilo.
Akizungumzia Tanzania kuzikosa fedha za MCC, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felschemi Mramba alisema baadhi ya miradi itaathirika lakini si kwa kiwango kikubwa kwa sababu fedha hizo zilidhamini miradi ya miaka mitano.
“Tulishaanza kuona dalili, tukaanza kutafuta namna ya kuziba mianya. Kwa hiyo baadhi ya miradi itadhaminiwa na Benki ya Dunia (WB), na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB),” alisema.
Alisema wameshazungumza na WB kuhusu kufadhili miradi ya kuunganisha umeme mjini na wamekubali na wameahidi kutoa fedha kwenye mradi wa kuunganisha umeme kutoka Zambia.
Kadhalika alisema ADB imeonyesha nia ya kutoa fedha katika mradi wa kuimarisha miundombinu ya umeme.
“Ingekuwa ni miradi ya mwaka mmoja, kweli tungeathirika kwa sababu tungekuwa hatujajipanga, lakini kwa sababu ni miaka mitano, tuna nafasi ya kutafuta mbinu nyingine,” alisema.
Awamu ya kwanza ya MCC
Katika awamu ya kwanza iliyokwisha mwaka jana, MCC ilitoa Dola za Marekani 698 milioni (Sh1.46 trilioni) ambazo zilitumika katika miradi mbalimbali ya barabara, huduma ya maji na umeme vijijini.
Fedha hizo zilijenga barabara ya Tunduma – Sumbawanga yenye urefu wa kilomita 230 kwa kiwango cha lami. Pia, zilijenga Barabara ya Tanga – Horohoro (kilomita 65.14) na Namtumbo – Songea – Mbinga yenye urefu wa kilomita 139.
Vilevile, fedha za MCC zilijenga barabara zote kuu zilizoko Pemba kwa kiwango cha lami na baadhi ya Barabara za Unguja. Pia, miradi ya huduma ya maji ilitekelezwa katika mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam.
MCC ilianza pia kufadhili miradi ya umeme vijijini katika mikoa 10 ya Tanzania. Mikoa iliyonufaika na hatua ya awali ya umeme vijijini ni Singida, Tanga, Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza, Lindi, Mtwara, Shinyanga na Mara.
Awamu ya pili ya MCC ingejikita zaidi katika miradi ya umeme vijijini kama Serikali za Marekani na Tanzania zilivyokubaliana kuwekeza kwenye sekta ya nishati hasa kwa wananchi waishio vijijini.
Maoni ya wanasiasa
Akizungumzia hatua hatua iliyofikiwa na MCC, mwenyekiti wa chama cha UDP, John Cheyo alisema kila nchi duniani ina uhuru wa kuamua mambo yake ya ndani bila kuingiliwa na nchi nyingine.
Cheyo alisema sababu walizozitoa MCC ni kuingilia uhuru wa Tanzania katika kuendesha mambo yake. Alisisitiza kwamba pamoja na kuzuia fedha hizo, Serikali itaweza kutekeleza mradi wa umeme vijijini kwa fedha zake za ndani.
“Tunaamua mambo yetu kulingana na mazingira yetu,” alisema.
Cheyo, ambaye alikuwa mbunge katika bunge lililopita alisema MCC haina nia njema na Tanzania kwa sababu wanajihusisha pia na masuala ya ndani ya nchi. Alisisitiza kwamba sheria ya makosa ya jinai siyo mbaya hata Marekani yenyewe imeweka udhibiti wa maovu katika sheria yao.
Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini,(NCCR), David Kafulila alisema kitendo cha MCC kusitisha misaada si suala la kifedha tu bali linaathiri uhusiano kati ya Tanzania, Marekani na mataifa mengine.
Alisema kitendo cha MCC kusitisha msaada ni zaidi ya fedha kwani mahusiano mabaya ni jambo baya hasa pale ambapo tunaharibu mahusiano hayo kwenye suala la kidemokrasia.
“Tanzania haikupaswa kuwa hivi kwa sababu ni nchi kiongozi barani Afrika kwa kupigania uhuru na ni mfano bora kwa wengine,” alisema na kumshauri Rais John Magufuli kuingilia kati.
“Ingawa Rais si mwanasiasa, lazima ajue kuwa amekabidhiwa Tanzania kama Taifa, aangalie pale CCM ilipoishia, aangalie mahusiano ya Tanzania na wengine, kila zama na kitabu chake, asifungwe na historia,” alisema.
Kafulila aliongeza kuwa Tanzania iliwahi kukosa mikopo ya kibajeti ya riba nafuu ya kiasi cha dola 800 milioni kwa sababu za ukosefu wa demokrasia na rushwa.
Katika tamko la ACT-Wazalendo lililotolewa na makamu mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje, Theopista Kumwenda chama hicho kimesema uamuzi wa bodi ya MCC utawaumiza na kukwaza juhudi za wananchi wa vijijini katika kujikwamua na umaskini.
“Tunasikitika kwamba ubabe wa Serikali ya CCM na woga wake wa kushindana kidemokrasia umesababisha nchi yetu ikose pesa za MCC ambazo zingesukuma mbele juhudi za kupambana na umaskini,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Tamko hilo lilieleza zaidi na kuitaka serikali ya CCM kuacha ubabe na kufifisha juhudi za miaka 20 za ujenzi wa demokrasia hapa nchini.
“Tunatoa wito maalumu kwa wadau wote wa siasa visiwani Zanzibar kurudi mezani na kutatua mgogoro wa kisiasa kwa njia za kistaraabu na katika hali ambayo itarudisha heshima ya nchi yetu katika kukuza demokrasia nchini,” lilisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo), Zito Kabwe alisema suala la uzalendo ni kutaka haki ya kidemokrasia Zanzibar ya Wananchi waliochagua viongozi wao oktoba 25, 2015.
Zito amewaomba Wazanzibari kuwa na subira, akisema siku moja haki itapatikana.
Aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Segerea kwa tiketi ya CUF na mchambuzi maarufu wa masuala ya siasa, Julius Mtatiro amesema kunyimwa kwa fedha za MCC kunawaumiza wananchi na wala si viongozi.
Alisema kitendo hicho ni dhambi ya CCM ambayo inabebwa na Watanzania wote kwa kuwa CCM ndio waliopora haki na kweli ya Wazanzibari kwenye masanduku ya kura katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.
“Kuna watakaokimbilia hoja ya umuhimu wa kutolilia misaada ya wazungu, hao pia tuwaulize, kwani hii misaada ya sasa ya MCC aliyeenda kuiomba ni nani? Si ni hao hao ambao ikishafungwa wanageuka, wanasema hawana shida nayo?” alihoji Mtatiro.
“Tunawauliza swali jingine, ni nani amekuwa na mamlaka ya kulifanya Taifa lijitegemee kiuchumi kwa miaka 50 iliyopita? Si ni nyie nyie? Tena hamtaki kusaidiwa na mawazo mapya hata baada ya kushindwa na kuendelea kuwalamba miguu wahisani.”
Takriban Sh1.5 trilioni zilizozuiwa zingeweza kusaidia zaidi ya wizara nane ambazo zilitengewa chini ya Sh150 bilioni katika bajeti ya 2015/16. Wizara hizo ni kama:
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (Sh38.8 bilioni)
Wizara ya Kazi na Ajira (Sh17.6 bilioni)
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (Sh66 bilioni)
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sh68.8 bilioni).
Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (Sh43 bilioni)
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi (Sh83 bilioni)
Wizara ya Viwanda na Biashara (Sh116.4 bilioni)
0 maoni:
Post a Comment