TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kampuni ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya
JamiiForums.com na FikraPevu.com imejijengea heshima na umaarufu kwa muda mrefu
kutokana na namna inavyoendesha na kusimamia shughuli zake ambazo kwa kiwango
kikubwa ni za kimtandao.
Mtandao wa JamiiForums ni mtandao mkubwa wa
Kiswahili kwa Afrika Mashariki na Duniani ukiwa na wasomaji wasiopungua Milioni
4 kwa mwezi ambapo kwa mwaka 2016, mtandao huu unatimiza rasmi miaka 10 tangu
uanzishwe. Mtandao huu unasifika kwa kutoa fursa ya kipekee kwa watumiaji wake
kutoa yaliyo mioyoni mwao huku wengine wakijifunza mbinu kadha wa kadha za kijasiriamali,
afya, elimu na hata kuibuka wanasiasa wapya waliofundwa na wana JamiiForums.
Pamoja na kuendelea kutoa huduma hata katika nyakati ngumu, mtandao
wa JamiiForums unakumbana mara kwa mara na changamoto nyingi zinazopelekea
waanzilishi na waendeshaji wake kuwa katika misukosuko mara kwa mara.
Kwa takribani miezi mitatu iliyopita, Jeshi la Polisi limekuwa
likiushinikiza mtandao huu (kwa njia ya barua rasmi) kutoa taarifa za baadhi ya
wateja wake wanaoonekana kutoa taarifa zile ambazo kwa namna moja ama nyingine
zinaibua ufisadi mkubwa na ukwepaji wa kodi.
JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri (privacy) wa wateja
wake, imekuwa ikihoji mashinikizo hayo yanazingatia sheria gani na kutaka kujua
ni vifungu gani vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja bila kupewa
maelezo yanayoridhisha zaidi ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama
hautatolewa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Baada ya kupata mashinikizo takribani manne yanayoashiria kuwa haki
ya watanzania watumiao mtandao wa intaneti na hasa watumiaji wa mtandao wa
JamiiForums, Jamii Media imeshauriana na Wanasheria wake na kuona ni wakati
sasa wa Kuilinda haki ya wananchi kupata taarifa na kulindwa kwa Uhuru wao wa
Maoni na Kujieleza inayolindwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ibara ya 18 ambapo
imefungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Kesi namba 9 ya mwaka 2016);
kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya
kwakuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za watanzania watumiao mitandao
ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
Mtandao wa JamiiForums utaendelea na shughuli zake kama kawaida na
utaendelea kuwahakikishia watumiaji wake kuwa mahala salama pa kutolea
madukuduku yao na hata kuisaidia Serikali kuonyesha nyufa zilipo kwa maslahi
mapana ya Taifa (wakizingatia mwongozo wa ushiriki wa mijadala anuai).
Mwisho, JamiiForums inamuunga na itaendelea kumuunga mkono Rais
Magufuli katika jitihada zake za kupambana na ufisadi kwa kutoa uwanja/fursa
salama na rahisi kwa wananchi kuweza kuyaainisha yale wanayoyabaini kuwa
yanachelewesha maendeleo ya Taifa lao.
Imesainiwa na
Maxence M. Melo
Mkurugenzi Mtendaji – Jamii Media
Machi 04, 2016
0 maoni:
Post a Comment