Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

RAIS MAGUFULI AINGIA CHATO KWA MARA YA KWANZA ATAKA WATANZANIA WASHIKAMANE KUJITEGEMEA BADALA YA KUTEGEMEA MISAADA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefika nyumbani kwake katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, ambapo akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Chato, ametoa wito kwa kila mtanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na utegemezi wa misaada ya wafadhili ambayo huambatana na masharti.
Dkt. Magufuli amesema jukumu kubwa lililo mbele ya watanzania kwa sasa, ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
"Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali yake imeamua kuchukua hatua kudhibiti nidhamu serikalini, kwa kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa hatua hizo maarufu kwa jina la "Kutumbua Majipu" zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo hilo likomeshwe.
Dkt. Magufuli pia amekumbusha viongozi wote wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali popote ambapo hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa aliopewa.


Rais Magufuli amewapongeza walimu kote nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu, lakini ametaka Wazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.


"Niziombe kamati za shule zote Tanzania nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni, zile kamati za shule zijiuzulu. Lakini pia kama wewe ni Mwalimu Mkuu, shule yako kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka, sioni sababu ya wewe kuendelea kuwa Mwalimu Mkuu" Alisisitiza Dkt. Magufuli.


Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, Rais Magufuli amesema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni 800, na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za watanzania.


Ametolea mfano wa mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani.


Pia Rais Magufuli amesema serikali yake imejiandaa kuboresha maslai ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini amesema kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi shilingi milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi shilingi milioni 15.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato

29 Machi, 2016
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO