Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Ikulu yaguswa kwenye ujangili Ndege ya Rais wa China yadaiwa kutumika kubeba pembe za ndovu; Kikwete atajwa kuwakumbatia majangili, Ikulu yasema haina taarifa

Ikulu yaguswa kwenye ujangili

Rais wa China Xi Jinping na Rais Kikwete wa Tanzania wakati alipozuru nchini (Picha ya Maktaba)

****

 

MIEZI tisa tangu mwandishi wa Uingereza, Martin Fletcher wa gazeti la The Mail on Sunday, kuchapisha makala akidai Serikali ya Tanzania inabariki ujangili wa meno ya tembo, gazeti la New York Times la Marekani, nalo limechapisha habari ikihusisha ndege ya Rais wa China, Xi Jinjing kuhusika kubeba pembe za ndovu alipokuwa Tanzania.

Katika toleo la Novemba 5 mwaka huu, mwandishi wa New York Times, Dan Levin alinukuu ripoti ya Shirika la ujasusi la mazingira lenye makao yake mjini London, akisema kwamba China ilinunua maelfu ya kilo za pembe za ndovu na kuzitorosha kwa kutumia ndege ya Rais huyo wakati alipozuru Tanzania Machi 2013.

Machi 2013, Rais wa China, Xi Jinping, aliwasili Tanzania katika ziara yake ya kwanza kwenye Bara la Afrika akiwa ni kiongozi wa nchi ambayo ni ya pili kiuchumi duniani. Katika ziara hiyo aliambatana na ujumbe wa maofisa wa serikali na wafanyabiashara ambao walikuwa maalum kwa ajili ya kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa mwandishi huyo, ripoti mpya ya shirika la ujasusi la mazingira inaonesha kuwa ujumbe wa Rais Jinping ulitumia ziara hiyo kama nafasi ya kufanya biashara haramu ya pembe za ndovu kwa kupandisha bei yake mara mbili kufikia dola 70,000 za Marekani kwa kilo, au dola 31,800 kwa kila paundi.

Kwamba, wiki mbili kabla ya Rais Jinping kuwasili, wanunuzi wa Kichina walikwenda kwenye maeneo mbalimbali yanayojihusisha na biashara hiyo na kununua maelfu ya pembe hizo ambazo baadaye zilipelekwa China kwa kutumia mabegi ya wanadiplomasia kwenye ndege ya Rais.

“Rais wenu alikuwa hapa,” ananukuliwa Suleiman Mochiwa, Mtanzania anayedaiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu, akimaanisha Rais Jinping. “Akiwa hapa, kilo nyingi zimekwenda nje kwenye ndege pasipo ulinzi. Walinunua kutoka kwetu.”

Ripoti hiyo inaitaja Tanzania kama chanzo kikuu duniani kwa uharamia wa pembe za ndovu na kwamba, China imekuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa hizo kimagendo.

Kwa miaka minne iliyopita, Tanzania inatajwa kupoteza tembo wengi katika uwindaji huo haramu zaidi ya nchi yoyote duniani, ambao wanakaridiwa kufikia 10,000 mwaka 2013 pekee, sawa na kusema kuwa tembo 30 wanauawa kila siku.

Kundi la wana mazingira wa kimataifa kwa muda mrefu limeituhumu Beijing kwa kufumbia macho wajibu wa China katika biashara haramu ya pembe za ndovu.

Katika ripoti hiyo, chanzo cha tembo wa Tanzania kuwa hatarini ni kutokana na serikali kushindwa kuchukua hatua, rushwa iliyokithiri na uhalifu.

Inaelezwa kuwa rushwa imewafanya maofisa wa ngazi zote wa serikali ya Tanzania kushiriki katika biashara hiyo, askari wa wanyamapori wanapeana taarifa na wawindaji haramu kwa kuonyeshana maeneo.

Livin katika habari hiyo aliongeza kuwa ripoti inaonyesha kwamba maofisa wa polisi nao wanatajwa kujihusisha na ujangili kwa kuwakodishia silaha na kuwasafirishia pembe hizo huku maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), nao wanatuhumiwa kutoa vibali vya kusafirisha makontena ya pembe hizo kwenye nchi za nje kiholela.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa watendaji wanaonekana kuwa makini katika kulinda tembo wasiuawe, wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi na kwamba hapo ni bila kutaja fedha ambazo zingeweza kushawishi maofisa wanaolipwa kidogo kukataa rushwa.

Mwandishi huyo anaongeza kuwa ripoti hiyo inasema kwamba, kutokana na uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii mapema mwaka huu, askari wa wanyamapori walifukuzwa kazi wakidaiwa kushirikiana na majangili.

Shirika hilo limehusisha rushwa na biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu nchini Tanzania hususani kwa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa, kutoka Chama tawala cha Mapinduzi (CCM), kinachoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Kwamba, Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, kulikuwa na tembo nchini takribani 142,000 na wakati huu ambako amebakiza mwaka mmoja kuondoka, idadi hiyo inakadiriwa kupungua na kubakia 55,000.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Kikwete alikabidhiwa orodha ya siri na vyombo vya usalama ikiwataja wahusika wakuu walioko nyuma na biashara hiyo ya ujangili wa tembo, yakiwemo ya wanasiasa mashuhuri na wafanyabiashara waliokaribu na CCM, lakini ni watuhumiwa wachache kati ya hao waliochunguzwa na kuchukuliwa hatua.

“Biashara hii inawahusisha matajiri na wanasiasa ambao wamejenga mtandao mkubwa,” ananukuriwa Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ambaye aliwataja wabunge wanne waliyopo kwenye biashara hiyo.

Ikulu yajitetea

Alipotafutwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuzungumzia kashfa hiyo kwa Tanzania, alisema kuwa; “Sijaona hiyo habari ila nimesikia, lakini kama serikali hatuna uhakika wa kama hilo kutokea serikalini”.

Balozi Sefue, alihoji lengo la wachapisha habari hiyo lilikuwa nini na alipoulizwa kama kweli Rais Kikwete aliwahi kupatiwa orodha ya majangili lakini akakwepa kuwachukulia hatua kutokana na ukaribu walionao kwa serikali yake na kwenye chama, alisema; “Sina taarifa kama alikabidhiwa majina akakaa kimya bila kuifanyia kazi”.

Kwa mujibu wa Balozi Sefue, Rais anapelekewa taarifa nyingi, kwamba kwa taarifa nyeti kama hiyo akiipata lazima aliwasilishe kwenye vyombo vya dola ili ifanyiwe uchunguzi na hatua zichukuliwe.

Februari 9, 2014 Tanzania ilichafuliwa na kudhalilishwa mbele ya uso wa dunia baada ya mwandishi Martin Fletcher, kuchapisha makala kuwa Serikali ya Tanzania inabariki ujangili wa meno ya tembo.

Taarifa hiyo iliikera Serikali ya Rais Kikwete, ambapo wakati akihojiwa na vyombo vya habari akiwa jijini London kuhusu mapambano ya vita ya ujangili, alisema kuwa anayo orodha ya majina 40 ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo na kwamba kinara wao yuko jijini Arusha.

Katika kuweka mambo sawa, ilibidi Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa asafiri kwenda Uingereza kwenye mkutano ulioandaliwa kujadili vita dhidi ya Ujangili, kuahirisha safari hiyo kwanza ili akanushe tuhuma hizo nzito.

Pia akiwa nchini Uingereza, Nyalandu alikatoa mwaliko kwa mwandishi Martin Fletcher aje Tanzania kujionea jitihada za kupambana na ujangili.

 

CHANZO: TANZANIA DAIMA

Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO