RAIS Jakaya Kikwete, alfajiri ya juzi alifanyiwa upasuaji wa tezidume (prostrate), katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari jana, ilisema kuwa Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake, kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.
“Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja nusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa. Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo pia iliwataka wananchi kuwa watulivu, kwani wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Wiki iliyopita kupitia taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema kuwa aliondoka Jumatano na kwamba kulingana na ratiba ya uchunguzi wa afya yake angerejea nchini Alhamisi wiki hii.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, haikueleza bayana tatizo linalomsumbua Kikwete mbali ya kusisitiza kuwa amekwenda huko kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
Taarifa za hali ya afya ya Rais Kikwete kwa mara ya kwanza ziliwahi kutolewa mwaka 2009, muda mchache baada ya kushindwa kukamilisha hotuba aliyokuwa akiitoa kwenye sherehe za miaka 100 ya Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT), kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
CHANZO: Tanzania Daima
ANGALIA ZA RAIS DK. J.K KIKWETE BAAADA NA KABLA YA KUFANYIWA UPASUAJI
0 maoni:
Post a Comment