CHAMA cha Mabadiliko na Uwazi (ACT), kimetangaza rasmi kuwa muasisi wa chama hicho ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ambaye kwa sasa bado anatambulika kuwa mwanachama wa Chadema.
Siri hiyo iliwekwa hadharani jana na Makamu Mwenyekiti wa ACT, Shabani Mambo, wakati akinadi kwa wananchi wagombea wa uenyeviti wa serikali za mitaa kupitia chama hicho kipya, katika mitaa ya Majengo pamoja na Nyasubi katika uwanja wa Lumambo.
Kutokana na kauli hiyo, gazeti hili lilimtafuta Zitto atoe ufafanuzi, ambapo alikataa kukiri wala kukanusha madai hayo ya ACT.
Hii si mara ya kwanza kwa Zitto kuhusishwa na chama hicho, ambapo Mei mwaka huu alipohojiwa na kituo cha redio cha Clouds Fm, kiongozi huyo kijana wa Chadema alikaririwa akisema hawezi kukubali au kukanusha kuwa mwanachama wa ACT, mpaka hapo kesi ya msingi dhidi ya uanachama wake Chadema itakapotolewa uamuzi mahakamani.
Aliulizwa swali hilo, baada ya kiongozi ambaye alitimuliwa Chadema pamoja na Zitto, Profesa Kitila Mkumbo, kumtaka rafiki yake Zitto kuhamia ACT na kugombea nafasi ya uenyekiti.
Profesa Mkumbo katika maoni yake kwa Zitto, alikaririwa akisema kiongozi huyo kijana hawezi kupata mafanikio zaidi ya kisiasa ndani ya Chadema, isipokuwa kama ataamua kuhama chama hicho.
Zitto alipohojiwa na Clouds kuhusu kauli ya Profesa Mkumbo, alisema yeye na Profesa Mkumbo wana mrengo wa siasa unaofanana, unaoamini katika maendeleo na maslahi ya jamii kwa ujumla na sio chama wala watu wachache.
Kampeni
Akiendelea na kampeni baada ya kueleza kuwa bosi wao ni Zitto, Mambo alidai watumishi wa Serikali iliyopo madarakani, wamekuwa na jeuri ya fedha kuliko wafanyabiashara hata kama wana mishahara midogo na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na ubadhirifu uliopo katika sehemu zao za kazi.
“Unakuta mfanyakazi mdogo wa halmashauri lakini unakuta anamiliki mali nyingi na huku mshahara wake ukiwa ni mdogo, ukiambiwa unaweza kushangaa hata mfanyabiashara mkubwa anaweza kutokuwa nazo sasa hebu fikiri mtu huyu anatoa wapi fedha hizo?” Alihoji.
Katika Mkutano huo Makamu Mwenyekiti huyo aliwanadi wagombea uenyekiti kupitia ACT kutoka katika ya Majengo Kati, Ali Shango pamoja na mgombea mwingine wa Mtaa wa Nyasubi, Idsam Mapande na kuongeza kuwa chama hicho ambacho ni kipya kimejipanga kuhakikisha kuwa kinashinda viti hivyo.
Source: HabariLeo la leo Disemba 13, 2014
0 maoni:
Post a Comment