JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Tanzania imeridhia rasmi Itifaki ya Umoja wa Fedha ambayo ni sheria muhimu katika utekelezaji wa hatua ya tatu ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Itifaki hiyo iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 25 Juni 2014.
Itifaki ya Umoja wa Fedha ilisainiwa na Wakuu Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Novemba 30, 2013 Jijini Kampala, Uganda wakati wa Mkutano wa 15 wa Kilele wa Wakuu wa Nchi hizo. Baada ya kusainiwa na Wakuu wa Nchi, Nchi wanachama zilitakiwa ziwe zimeridhia Itifaki hiyo ifikapo Julai 1, 2014 ili kuruhusu kuanza kwa utekelezaji wake.
Baada ya kuridhiwa kwa Itifaki, Nchi wanachama zitatakiwa kufuata mpango mkakati wa utekelezaji ambao umeelezwa bayana kwenye Itifaki hiyo.
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha utapelekea Nchi wanachama yaani Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda kuwa na sarafu moja ifikapo mwaka 2024. Ili kufikia hatua ya kuwa na sarafu moja mwaka 2024 baadhi ya mambo muhimu yanayotakiwa kufanyika ni pamoja na uanzishwaji wa Taasisi za Kifedha.
Taasisi hizo ni pamoja na Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki (ambayo baadaye itakua Benki Kuu ya Afrika Mashariki), Taasi ya Takwimu ya Afrika Mashariki, Tume ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Udhibiti na Tume ya Huduma za Kifedha ya Afrika Mashariki.
Utekelezaji wa Itifaki utahusisha pia uhuishaji wa sera zao za kifedha zikiwemo za kubadilisha fedha, sera za malipo kupitia benki, sera zinazohusu uzalishaji na usambazaji wa takwimu na sera za masoko ya fedha.
Izingatiwe kuwa, kabla ya kuingia kwenye Sarafu moja mwaka 2024, nchi wanachama zitatakiwa kukidhi vigezo vya Muunganiko wa uchumi mpana (Microeconomic Convergence Criteria) vilivyowekwa ambavyo ni pamoja na:
i. kuwa na mfumuko wa bei usiozidi 8%;
ii. Kuwa na nakisi ya Bajeti isiyozidi 3% (pamoja na misaada);
iii. Kuwa na deni la taifa lisilozidi 50% ya Pato la Taifa;
iv. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni ambazo zinatosheleza manunuzi ya bidhaa kutoka nje kwa kipindi cha miezi minne na nusu.
Vigezo hivyo vinatakiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kukaribia 2024. Kama kutakua angalau na nchi tatu za Jumuiya zitakazoweza kufikia vigezo hivyo basi zitaweza kuanza kutumia sarafu moja.
Umoja wa Fedha ni hatua ya tatu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki baada ya hatua za awali, Umoja wa Forodha (2005) na Soko la Pamoja (2010) kutekelezwa. Hata hivyo ili hatua ya Umoja wa Fedha iweze kufanikiwa inategemea utekelezaji wa hatua za awali za mtangamano na ushiriki wa wananchi katika kuzitumia fursa zitokanazo na mtangamano. Wizara inawahamasisha Watanzania kutumia fursa mbalimbali zitokanazo na Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja.
Imetolewa na
KATIBU MKUU
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
0 maoni:
Post a Comment