Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Uchaguzi Serikali za Mitaa shakani Pinda asema hatma yake inategemea mchakato wa katiba

pinda

UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, upo shakani kufanyika.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na mameya wa majiji, manispaa na wenyeviti wa halmashauri za miji na wilaya Tanzania katika kikao cha siku moja kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.

Pinda ambaye ni mara yake ya pili kutilia shaka uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo, alisema hatma yake kwa kiasi kikubwa inategemea kukamilika kwa mchakato wa katiba mpya.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea sana kukamilika kwa mchakato wa Bunge la Katiba,” alisema na kuongeza:

“Kama wizara tunaendelea na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande wetu. Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha wadau wote.”

Kwa mujibu wa Pinda, maandalizi ya uchaguzi huo muhimu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea vizuri.

Hii ni mara ya pili kutilia shaka uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo.

Akiwa bungeni, Waziri Pinda aliwahi kutamka kwamba ucheleweshaji wa kupatikana kwa katiba mpya utaathiri uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unaweza kufanyika mapema mwakani.

Aliliambia Bunge kabla ya serikali kuongeza muda wa Bunge la Katiba kwamba watamwomba Rais Jakaya Kikwete aongeze muda wa Bunge la Katiba na endapo litaongezewa muda, litaathiri uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa ratiba, Bunge la Katiba linatarajiwa kuanza mapema Agosti na kuendelea hadi Oktoba na baada ya hapo itafuatiwa na kura ya maoni ili kupata katiba mpya.

Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema kuwa ukiangalia ratiba ya Bunge la Katiba, ni vigumu kwa uchaguzi huo kufanyika Oktoba na kuna uwezekano mkubwa ukafanyika mapema mwakani.

Waziri Mkuu yuko Tanga kwa ajili ya sherehe za Serikali za Mitaa ambazo kilele chake kitafanyika leo kwenye viwanja vya Tangamano.

Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya kukutana nao aliyoitoa Mei 14 mwaka huu wakati akifungua mkutano mkuu wa ALAT.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali ambapo alisema katika mwaka wa fedha unaoisha, hali ya ukusanyaji mapato haikuwa nzuri.

Kutokana na hali hiyo, amewaandikia barua wakuu wa mikoa akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo ya halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.

“Katika taarifa hizi itabidi kila halmashauri ieleze ilipanga kukusanya kiasi gani, je imefikia lengo na kama sivyo ni kwanini. Nia yetu ni ku-track down makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa na nini,” alisema.

Kuhusu udhibiti wa matumizi, aliwataka mameya na wenyeviti hao kuendelea kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi yasiyofaa.

“Lazima muendelee kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalamu wa kwenye halmashauri zenu. Fanyeni kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale wanaoharibu.

“Ili muweze kuwabana vizuri, lazima mdai kupatiwa taarifa za fedha kutoka kwa mkaguzi wa ndani (Internal Auditor)… kuna baadhi ya watendaji wanadai kuwa hizi taarifa ni siri wakati siyo siri,” alisema.

Aliwaeleza washiriki wa kikao hicho kwamba taarifa hizo ni muhimu kwao kuzipata na zitawasaidia kuonyesha mapungufu yoyote kama yapo.

Aliwataka kila mmoja wao kwa nafasi zao za meya na mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato la wananchi wanaowaongoza.

 

CHANZO: TANZANIA DAIMA

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO