Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Jaji Mkuu mstaafu Samatta ‘apanda kizimbani’ Moshi Kumtetea Dr Slaa

samatha

Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kupanda kizimbani na kutoa ushahidi  mahakamani hapo katika kesi ya jaribio la kutapeli viongozi wa Chadema. Kushoto ni shahidi namba mbili wa kesi hiyo, Profesa Abdalah Safari. Picha na Dionis Nyato 

****

Moshi. Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta jana alipanda kizimbani kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Hai tukio lililovuta hisia za wananchi wengi kwani ni la kwanza na la aina yake kwa kiongozi wa juu wa mhimili huo wa dola.

Jaji Samatta aliingia eneo la Mahakama saa 2.40 asubuhi akifuatana na Profesa Abdallah Safari na baadaye kwenda moja kwa moja chumba cha mapumziko kabla ya kuingia mahakamani.

Baada ya kula kiapo kutoka kwa karani wa Mahakama hiyo, Baltazar Buretta, Jaji Samatta alianza kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Adam Abeid (25) ya kujifanya jaji huyo na kutaka kuwatapeli viongozi wa Chadema, akisema alishtuka alipoelezwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa kuna mtu ambaye amempigia simu akijitambusha kuwa ni Jaji Samatta.

Abeid pia anakabiliwa na shtaka kutaka kumtapeli Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa ilisikilizwa chemba huku Jaji Samatta akiongozwa kutoa ushahidi wake na Mwanasheria wa Takukuru, Susan Kimario anayesaidiana na Furahini Kibanga akikana kumfahamu wala kuwa na uhusiano na mshtakiwa huyo.

Jaji Samatta ambaye sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na mjumbe wa Bodi ya Kuchuja Mahakimu na Majaji Kenya, alisema kati ya Aprili na Mei 2012, Dk Slaa alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms) akiambatanisha na ujumbe unaodaiwa kutumwa na mshtakiwa, akimtaka athibitishe kama ndiye aliyeutuma kwake.

Ujumbe huo ulisomeka: “Hali yako Dk Slaa, kesho nataka nikamuone Jaji Mkuu Chande, naomba nichangie nauli (ili) nikashughulikie yale masuala yetu.”

Jaji Samatta alisema alishtuka na kuamua kumpigia simu Dk Slaa na kumweleza kuwa ujumbe huo haukuwa umetoka kwake na kumtaka alifikishe suala hilo kwenye vyombo vya dola.

“Nilimpigia pia Wakili Profesa Safari (Abdallah) nikamuomba ahakikishe suala hilo haliishi kisiasa, bali upelelezi ufanyike kwa sababu hadhi yangu na heshima yangu ilikuwa at stake (shakani),” alisema.

Maswali kati ya mshtakiwa na Jaji Samatta yalikuwa kama ifuatavyo;

Mshtakiwa: Je, katika zile meseji alizokutumia Dk Slaa unazo kwenye simu yako?

Jaji Samatta: Zile meseji ziko katika simu yangu ya zamani ambayo niliacha kuitumia baada ya kuzeeka.

Mshtakiwa: Wakati Dk Slaa anakupa taarifa hizo, nani alikuwa wa kwanza kulifikisha suala hilo Takukuru?

Jaji Samatta: Sijui kwa sababu niliwaambia Dk Slaa na Profesa Safari walipeleke hilo suala kwenye vyombo vya dola na mimi ningeitwa kuandika maelezo.

Profesa Safari ambaye ni shahidi wa pili, aliiambia Mahakama kuwa kati ya Aprili na Mei, 2012, alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni Jaji Samatta akiomba simu ya Lema.

“Aliniambia anataka azungumze na Lema ili kumsaidia kwenye kesi yake ya Arusha (ya kupinga ubunge wake). Nilimpa na nikampigia pia Lema kuwa kuna mtu anamtafuta,” alisema.

Profesa Safari alisema hata hivyo, alishuku kuwa mtu huyo hakuwa Jaji Samatta kutokana na kwamba alikuwa akiifahamu sauti yake na ni mtu ambaye wamefanya naye kazi kwa muda mrefu.

Baadaye Profesa Safari alisema aliamua kumjulisha Dk Slaa kuhusiana na jambo hilo kwa vile lilikuwa linaonekana kuwa na sura ya utapeli na rushwa na Chadema hakijihusishi na mambo hayo.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka unadai kuwa mshtakiwa alijifanya ni Jaji Samatta akitaka kumsaidia Lema katika rufaa yake namba 47/2012 ya kupinga hukumu iliyokuwa imemvua ubunge wa Arusha Mjini.

Pia, upande wa mashtaka unadai pia katika kipindi hicho, mshtakiwa huyo ambaye alikana mashtaka hayo, alijifanya kuwa ni mkuu wa Takukuru Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Abel Kibaso.Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Januari 14.

CHAZO: MWANANCHI

 

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO