TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: UVCCM MKOA WA ARUSHA.
Tarehe 22/01/2015
Ndugu wanahabari, leo tumeona vyema tutumie fursa hii ili tuweze kuzungumza machache na pongezi zetu kuhusiana na mustakabali wa chama chetu cha Mapinduzi kwa maamuzi stahiki na kuelekea uchaguzi wa 2015
Tutazungumzia mambo mawili makuu:
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Arusha tunaunga mkono hatua iliyochukuliwa na Katibu mkuu wa CCM Taifa Mh A. Kinana kwa kuona umuhimu wa kulinda na kuhifadhi katiba, miongozo na miiko ya chama kwa kusitisha ziara za Mh Mwigulu Nchemba ambazo kimsingi zilikuwa zinakwenda kinyume na miiko na miongozo ya chama.
Hatua hii ni muhimu katika kipindi hiki kwani umoja wetu ndio nguzo ya ushindi wetu hapo Oktoba 2015. Tunampongeza komredi Abdulrahman Kinana kwa hatua hii madhubuti, ni lazima tuzuie aina yoyote ya mgawanyiko unaoletwa na watia nia hawa wasiofuata miiko ya chama kwa kutumia taaluma,nafasi zao ndani ya chama, serikalini na kete ya ujana katika kuwania madaraka huku wakitaka kuwaonea wengine.UVCCM Arusha tulijiuliza,angefanya haya Lowassa angeeleweka?
Pia tunaipongeza kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kumaliza kikao chake kule Kisiwandui Zanzibar kwakuja na maazimio makini yenye kujenga Chama na kurejesha imani kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu, Tarehe 13/01/2015 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake wa Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku moja Kisiwandui Mjini Zanzibar. Pamoja na mambo mengine baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ni pamoja na suala la SAKATA LA AKAUNTI YA ESCROW.
Chama Cha Mapinduzi kilisikitishwa sana na sakata hili. Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu iliamua yafuatayo:-,
i). Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu iliitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya bunge juu ya swala hilo.
ii). Kamati Kuu iliwataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha.
iii). Aidha Kamati Kuu iliiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama. Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kilifanyika tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha tunasisitiza serikali izingatie haya na kufanyia kazi mapendekezo haya kama yalivyo.Pia tunamsihi katibu mkuu aendelee kushughulikia watovu wapya wa nidhamu wanaojitokeza huku wenzao wakitumikia adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi ambapo adhabu yao inafika ukingoni mwezi ujao kama ambavyo kamati ndogo ya maadili itakavyoamua baada ya tathmini ya utekelezaji wa adhabu hizo
Robinson Meitinyiku.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha
Chanzo: Taarifa hii imepatikana kupitia Mtandao wa Jamii Forums
0 maoni:
Post a Comment