Kuna taarifa za upotoshaji zinasambazwa kwa nia ya kuwachanganya wananchi kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na viongozi wake wakuu.
Ni wazi taarifa hizo zinasambazwa na 'wale wale' ambao hali yao ya kisiasa iko mtanzikoni na hatma yao ya kubaki madarakani iko hatarini, kadri UKAWA unavyozidi kuimarika na viongozi wakuu wa umoja huu wakizidi kushirikiana kwa dhati kuwaonesha Watanzania njia sahihi ya kufikia mabadiliko ya kweli ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.
Hofu ya watawala kutokana na uimara wa UKAWA ni kubwa. Uoga wa kushindwa uchaguzi wa mwaka huu umezidi kuwakumba tangu baada ya anguko kubwa walilopata kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hawana tena hoja za kushawishi. Kutunga uongo kama huo wa 'Dkt. Slaa na James Mbatia', ndiyo kete zao zilizobakia.
Imani na matumaini ya Watanzania kwa UKAWA na viongozi wake ni kubwa mno. Kila mara viongozi wa UKAWA wanaposikika wamekutana kujadili masuala makubwa ya kitaifa kwa maslahi ya wananchi, watawala wanaweweseka.
Taarifa za upotoshaji eti kwamba hakuna maelewano kati ya Katibu Mkuu wa Makatibu Wakuu wa UKAWA, Dk. Slaa na Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA James Mbatia, si uongo wa kwanza wa 'watawala waliojawa uoga'. Wamejaribu mara kadhaa. Hawajafanikiwa. Hawataweza. Kwa sababu UKAWA ni tumaini la watu.
Waliojawa uoga kwa sababu ya uimara wa UKAWA, wamejaribu mara kadhaa kutunga maneno ambayo wanadhani yanaweza kuwakatisha moyo. Ni wale wale ambao huko nyuma walieneza chuki ndani ya jamii kwa kusema chama fulani cha dini fulani, kabila fulani, kanda fulani. Kote huko wameshindwa. Wanabuni ugomvi usiokuwepo wala usiotarajiwa kuwepo.
UKAWA unasonga mbele. Ndilo tumaini la Watanzania. Maelewano miongoni mwa viongozi wote wakuu yanazidi kuongozwa kwa dhamira na nia safi ya kuwaongoza wananchi kupigania matamanio ya haki na matumaini waliyonayo.
Badala ya kuzubaishwa na uzushi wa 'ugomvi' miongoni mwa viongozi wa UKAWA, unaoratibiwa na makanika wa uongo walioko madarakani, Watanzania waendelee kusimama bega kwa bega na viongozi wa UKAWA kuendelea kushusha tumaini hili la Watanzania nchi nzima na kuzidi kuchochea moto wa mabadiliko unaokwenda kuwachoma watawala, Oktoba, mwaka huu.
Ni hayo kwa sasa.
Makene
Afisa Habari Chadema
0 maoni:
Post a Comment