Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

TAMKO LA UKAWA JUU YA AMRI YA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUHUSU MAMLAKA YA BUNGE MAALUMU NA "RASIMU YA BUNGE LA SITTA"

UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI

(UKAWA)

TAMKO LA UKAWA JUU YA AMRI YA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUHUSU MAMLAKA YA BUNGE MAALUM

&

RASIMU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA ILIYOWASILISHWA KWENYE BUNGE MAALUM NA MWENYEKITI WA KAMATI YA UANDISHI YA BUNGE MAALUM

Dar es Salaam, 26 Septemba 2014:

Hapo jana tarehe 25 Septemba, 2014, Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa amri kuhusu maombi yaliyofunguliwa na Bwana Saed Kubenea, mwandishi habari mwandamizi na mhariri wa gazeti la Mwanahalisi kutaka Mahakama Kuu itoe ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za nchi yetu. Katika amri yake hiyo, Mahakama Kuu imesema yafuatayo kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum:

(a) “Kwamba kuna mgongano katika maana ya maneno yaliyotumika kwenye kifungu cha 25 cha Sheria hiyo kwenye toleo la Kiingereza la Sheria hiyo. Hata hivyo, licha ya mgongano huo, tafsiri sahihi ya maneno ya kifungu hicho ni kwamba:

(i) “Mamlaka ya ‘kujadili na kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa’ maana yake ni mamlaka ya kutunga na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi wa Tanzania ili kupigiwa kura ya maoni;

(ii) “Mamlaka hayo yatatekelezwa kwa kutumia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Katika kufanya hivyo, Bunge Maalum linaweza kuboresha na/au kurekebisha Rasimu ya Katiba. Mamlaka hayo yanamewekewa mipaka, kama ilivyokuwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tunu na maadili ya taifa yaliyopo kwenye kifungu cha 9(2) cha Sheria;

(b) “Mahakama haina mamlaka ya kuamua aina na upeo wa maboresho na/au marekebisho ambayo Bunge Maalum linaweza kuyafanya kwenye Rasimu ya Katiba kwa sababu hilo ni suala la kisiasa na wala siyo la kisheria, ilimradi maboresho na/au marekebisho hayo hayaendi kinyume na matakwa ya kifungu cha 9(2) cha Sheria.”

Uamuzi huu ni muhimu kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu zifuatazo:

(1) Tangu kuanza kwa Bunge Maalum mwezi Februari mwaka huu, kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wajumbe wa UKAWA na wajumbe wa CCM na mawakala wao katika Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum kama yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Wakati UKAWA imeshikilia msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum yana mipaka kisheria na Bunge hilo halina mamlaka ya kubadilisha misingi mikuu ya Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, CCM na mawakala wake imeshikilia msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum hayana mipaka na Bunge Maalum lina uwezo wa kufanya marekebisho au mabadiliko yoyote kwenye Rasimu ya Katiba. Uamuzi wa Mahakama Kuu unathibitisha usahihi wa hoja ya UKAWA kwamba mamlaka ya Bunge Bunge Maalum yana mipaka kisheria;

(2) Kwa kusema kwamba Bunge Maalum lina mamlaka ya kufanya maboresho na/au marekebisho kwenye Rasimu ya Katiba, Mahakama Kuu imekataa dhana ya CCM na mawakala wake kwamba Bunge Maalum lina mamlaka ya kubadilisha Rasimu ya Katiba. Amri ya Mahakama Kuu haijataja kabisa neno ‘kubadilisha’ ambalo liliingizwa kwa nguvu kwenye Kanuni za Bunge Maalum. Kwa maana hiyo, kanuni ya 3 ya Kanuni za Bunge Maalum inayotafsiri neno ‘hoja’ kuwa ni pamoja na mamlaka ya Bunge Maalum kubadilisha Rasimu ya Rasimu inakwenda kinyume na matakwa ya kifungu cha 25 cha Sheria na kwa hiyo tafsiri hiyo ni batili;

(3) Kama ilivyokuwa kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu iliyokuwa inahusu suala la mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya Tanzania imekwepa kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata Katiba na Sheria za nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘maamuzi ya kisiasa.’ Mamlaka ya Bunge Maalum yamewekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mipaka yake imewekwa na Sheria hiyo pia. Mahakama Kuu, kama ilivyo kwa Mahakama nyingine zote, ilikuwa na wajibu wa kutafsiri Sheria hiyo kwa kutamka bayana aina na upeo wa mamlaka ya kisheria ya Bunge Maalum kufanya maboresho na/au marekebisho ya Rasimu ya Katiba. Badala ya kutekeleza wajibu wake huo, Mahakama Kuu imekwepa lawama za CCM na mawakala wake kwa kusema kwamba aina na upeo wa maboresho na/au marekebisho ya Rasimu ya Katiba utategemea matakwa ya kisiasa, yaani ya CCM na mawakala wake, badala ya kutegemea lugha ya Sheria yenyewe. Aidha, Mahakama Kuu imekwepa lawama za UKAWA kwa kukubali hoja kwamba mamlaka ya Bunge Maalum yana mipaka, hata hivyo bila kuifafanua mipaka hiyo;

KATIBA MPYA INATENGENEZWA KWA MTUTU WA BUNDUKI!!!

Hali ya kisiasa katika nchi yetu kwa sasa ni tete kwa kiasi kikubwa. Nchi yetu sasa iko chini ya utawala wa kijeshi usiokuwa rasmi. Kila mahali katika makao makuu ya mikoa, wilaya na majimbo, askari wa Jeshi la Polisi wakiwa na mabomu na risasi za moto, magari ya deraya, farasi na mbwa wametanda kila mahali ili kujaribu kuzuia maandamano na mikutano ya wananchi wanaopinga mchakato wa Katiba unaoendelea.

Mjini Dodoma, Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linatumiwa na Bunge Maalum limezingirwa na vikosi hivyo vya Jeshi la Polisi. Katika hali hii, ni wazi kwamba mchakato wa Katiba umekuwa mateka wa Jeshi la Polisi, Bunge Maalum lenyewe ni mateka na Watanzania wote ni mateka wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya mabavu. Katiba mpya inatengenezwa kwa mtutu wa bunduki. Katika hali tete kama hii, kitu cha ajabu kabisa ni kwamba Rais Jakaya Kikwete – kama ambavyo imekuwa kawaida yake sasa – amekimbia nchi na kwenda Marekani kwa ziara ya wiki mbili.

Kama ambavyo UKAWA imesema katika kipindi chote hiki, chochote kitakachotokana na mchakato huu wa kimabavu hakitakuwa na uhalali wowote wa kisiasa. Sasa, baada ya mabadiliko mbali mbali ya Kanuni za Bunge Maalum kuruhusu uchakachuaji sio tu wa Rasimu ya Katiba bali pia uchakachuaji wa maamuzi ya wajumbe waliobakia wa Bunge Maalum, ni wazi pia kwamba chochote kitakachotolewa na Bunge Maalum kwa sura ya Katiba inayopendekezwa kitakuwa batili kisheria vile vile.

Kwa sababu hizo, tunawaomba Watanzania wote wenye nia njema na nchi yao kupinga nchi yetu kugeuzwa kuwa dola ya kipolisi na nchi ili chini ya utawala wa kijeshi usio rasmi. Tunawaomba wanachama na viongozi wote wa vyama vya UKAWA kufanya maandalizi ya kupinga vitendo hivi kwa njia mbali mbali za kidemokrasia. Aidha, wanachama na viongozi wetu wafanye maandalizi kwa pamoja kwa ajili ya Uchaguzi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliotangazwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo uwe ni fursa ya kwanza ya kuiondoa CCM katika utawala wa nchi yetu kabla ya kuiondoa kabisa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

-----------------------------------------------------------

Mh. Freeman Aikaeli Mbowe

MWENYEKITI MWENZA

Mh. Profesa Ibrahim Haruna Lipumba

MWENYEKITI MWENZA

--------------------------------------------------------------------

Mh. James Francis Mbatia

MWENYEKITI MWENZA

Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO