Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

TASWIRA YA TUKIO LA MH FREEMAN MBOWE ALIPOKWENDA KUHOJIWA MAKAO MAKUU YA POLISI

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe akiwasili kwenye makao makuu ya Jeshi la Polisi nchini,Mapema leo asubuhi tayari kwa kwenda kuhojiwa juu kauli aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho hivi katibuni,kuwa watafanya maandamano nchini nzima bila kikomo.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema,Prof. Abdallah Safari na Wakili wa Chama,Wakili Mabele Marando wakiwasili kwenye Makao Makuu wa Jeshi la Polisi mapema leo.

Baadhi ya wapenzi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakishangilia baada ya gari lililokuwa limembeba Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alipowasili leo Makao Makuu wa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, kwa mahojiano.

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari waliokuwepo kwenye eneo la makao makuu ya Jeshi la Polisi,juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwenye mahojiani katika ya Mwenyekiti wa Chama hicho na Jeshi la Polisi.

Mwenyekiti wa Chama cha DP, Christopher Mtikila akihojiwa na askari Polisi, alipowasili Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa bajaji, ambako Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alihojiwa na Polisi.

 

Dar es Salaam. Shughuli za kiserikali katika Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi jirani, jana zilisimama kwa siku nzima kutokana na hekaheka zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema pale mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipojisalimisha polisi.

Hekaheka hizo ziliibuka kuanzia saa 5.10 asubuhi baada ya Mbowe akiongozana na wanasheria wa chama hicho, kufika katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi ambako pia zipo ofisi za wizara hiyo kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.

Kabla ya Mbowe kuwasili, alifika Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Benson Kigaira na alipojitambulisha akakataliwa kuingia.

Baadaye waliwasili mawakili, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando ambao waliruhusiwa kuingia, kisha wakafuata Mbowe, John Mnyika na wanasheria wengine akiwamo John Malya na Peter Kibatala.

Wakati huo, Barabara ya Garden inayokatiza mbele ya wizara hiyo ilikuwa imefungwa na wafuasi wa Chadema walikuwa wamezuiliwa kwa mbali. Kila mwananchi aliyefika katika jengo hilo kupatiwa huduma, alijibiwa na askari waliokuwa na mbwa na silaha kuwa, “hakuna shughuli yoyote inayofanyika hadi kesho (leo)”.

Hali hiyo iliendelea hadi saa 9:10 alasiri baada ya Mbowe aliyehojiwa kwa saa mbili kuhusu tuhuma za uchochezi kuachiwa kwa dhamana.

Baada ya kuachiwa, Mbowe alisindikizwa kwa msafara wa magari manne ya polisi akielekea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, ambako alipanda ndege kwenda Afrika Kusini kwa shughuli za kichama.

 

Ilivyokuwa

Ombi lililotolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika kuwataka wanachama wa Chadema kujitokeza kumsindikiza Mbowe polisi, liliitikiwa kwani zaidi ya wanachama 100 walijitokeza katika ofisi hizo.

Walianza kukusanyika mmoja baada ya mwingine nje ya makao mkuu ya jeshi hilo kuanzia saa 4:30 asubuhi na kujichanganya katika kundi la waandishi wa habari, hali iliyosababisha askari polisi waliokuwa na bunduki na mabomu ya machozi kuwataka wanahabari wajitambulishe kwa kuonyesha vitambulisho ili wawatenge na wafuasi hao.

Licha ya juhudi hizo, hawakufanikiwa kuwatawanya wanachama hao ambao awali, walijieleza kuwa walikuwa wamefuata hati zao za kusafiria katika Ofisi za Uhamiaji zilizopo eneo hilo.

Hali ilibadilika baada ya Mbowe kufika katika ofisi hizo akiwa katika msafara wa magari matano huku ukiongozwa na Mnyika na wanachama hao kuanza kuimba nyimbo za chama hicho na kumsifu kiongozi wao.

 

Msafara huo ulizuiwa kwenye lango la ofisi hizo na askari wa FFU waliwazuia viongozi wengine, wakisema anayetakiwa kuingia ndani ni Mbowe na wanasheria wake pekee.

Baada ya gari la Mbowe kuingia, viongozi na baadhi ya wafuasi wa chama hicho nao walipenya kwa nguvu getini na kuingia ndani ya uzio huku wakisema ‘people’s power’ (nguvu ya umma). Kitendo hicho kiliwatibua FFU na kuanza kutumia nguvu kuwatoa nje, hali iliyozua vurugu kubwa.

Kutokana na mvutano huo, askari zaidi wa FFU waliokuwa katika Land Rover mbili wakiwa na mbwa waliongezeka na kuanza kuwashushia kipigo wafuasi hao huku wakiwataka kusimama umbali wa mita 100 kutoka lilipo jengo hilo.

Baada ya kutolewa ndani ya uzio baadhi ya wafuasi wa Chadema walikaa chini wakisema hawatafanya vurugu na wako tayari kuingia ndani wakiwa wamenyoosha mikono juu.

Katika kundi la wafuasi hao walikuwamo pia baadhi ya wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana).

Wabunge waliofika baadaye na kuruhusiwa kuingia ndani ni Suzan Lyimo (Viti Maalumu) na Halima Mdee (Kawe).

Miongoni mwa walioathirika na hekaheka hizo ni wanahabari ambao pamoja na kuonyesha vitambulisho na kamera, baadhi yao walishushiwa kipigo na askari hao.

Katika kipigo hicho, mwandishi wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima, Josephat Isango na Mwandishi gazeti la Hoja, Shamimu Ausi walijeruhiwa. Isango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na jicho la kulia.

Wakati Isango alisema alivamiwa na askari wawili wa FFU na kwamba hata alipojitambulisha na kuwaonyesha kitambulisho waliendelea kumpiga, Ausi alisema alipigwa rungu usoni na akashangazwa na nguvu kubwa iliyotumika wakati awali, aliruhusiwa kusimama katika eneo alipokuwa akiendelea na kazi.

Baada ya vurugu hizo waandishi wa habari na wafuasi wa chama hicho walitakiwa kusimama katika makutano ya Barabara ya Ghana na Ohio umbali wa mita 100 kutoka yalipo makao makuu ya jeshi hilo kusubiri mahojiano yaishe.

Ilipofika saa 8.45, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alitoka nje ya ofisi hizo na kuzungumza na waandishi wa habari na wafuasi wa chama hicho.

Alisema mahojiano kati ya Mbowe na Jeshi la Polisi yalikwenda vizuri huku akiongozwa na wanasheria na kwamba polisi wamekubali kumpa dhamana lakini kabla hajaondoka, wafuasi wote wanatakiwa kuondoka eneo hilo bila maandamano.

 

“Polisi wanaomba mtawanyike, hawataki maandamano, wao watamsindikiza hadi makao makuu ya chama yaliyopo Kinondoni, mkifanya maandamano watatumia nguvu kuyazuia na hilo hawataki litokee. Nawaomba mtawanyike,” alisema Lissu.

Baada ya tangazo hilo, wafuasi hao kwa shingo upande, walikubali ushauri huo na kuondoka katika eneo hilo saa 9.00 alasiri.

Ilipofika saa 9.20 Mbowe alitoka katika ofisi hizo akisindikizwa na magari ya polisi aina ya Land Rover zilizojaa askari na baadaye ilielezwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliyekuwa makao makuu ya chama hicho kuwa mwenyekiti huyo alikwenda moja kwa moja Uwanja wa Ndege kwa safari ya kikazi Afrika Kusini.

 

Mtikila azua gumzo

Wakati hekaheka zikiendelea, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alifika katika ofisi hizo saa 7.26 akiwa katika Bajaj lakini alizuiwa kuingia ndani na akaondoka.

Akizungumza na wanahabari, Mtikila alisema, “Ni lazima Watanganyika tuidai Tanganyika yetu kwa gharama yoyote, aluta continua.”

 

Makao Makuu

Baada ya kuondoka eneo hilo, wafuasi wa Chadema walikwenda katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni na kupewa maelekezo na Dk Slaa na Lissu.

Lissu alisema Mbowe anatuhumiwa kwa uchochezi kwa kauli yake kuhusu kufanyika maandamano nchi nzima, huku akisisitiza kuwa tuhuma alizopewa “ni za wizi wa kuku”.

“Mbowe aliposema kufanyika maandamano alikuwa na maana kuwa maandamano hayo yatafanyika baada ya Chadema kutoa taarifa, kauli yake haikuwa ya uchochezi hata kidogo,” alisema Lissu.

Aliongeza, “Kama polisi wakitueleza ni sheria ipi inakataza maandamano, sheria ipi inalazimisha wanaotaka kuandamana lazima wawe na kibali na sheria ipi inakataza watu kugoma, watakuwa na ruksa ya kumfunga Mbowe.”

Kwa upande wake, Dk Slaa alisema, “Mbowe baada ya kutoka polisi ameomba nimwagie kwa wanachama wa Chadema. Amekwenda Afrika Kusini katika mkutano wa chama. Safari yake ilikuwa imepangwa tangu juzi na ingeahirishwa kama angenyimwa dhamana leo.”

Dk Slaa alimwagiza Kigaira kuhakikisha kuwa wanachama wawili wa chama hicho waliokamatwa na polisi wanaachiwa kwa dhamana. Zoezi la kufanya maandamano likifanyika kama hivi Taifa hili litabadilika,” alisema.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge na Susan Mwillo wa MWANANCHI

 

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO