Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

TAARIFA YA JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) KUHUSU VIJANA WALIOHITIMU MAFUNZO KWA KUJITOLEA NA KUTAKA KUAJIRIWA NA SERIKALI

Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa Julai 10, 1963 na serikali kwa lengo la kuwaweka pamoja vijana wa nchi hii na kuwapa malezi kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za matabaka zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.

Baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa JKT ni:

Kubadili fikra za vijana wa nchi hii kutoka ile hali ya ukoloni kutegemea nchi nyingine kuleta maendeleo.

Kukusanya nguvu za vijana wote wa nchi hii na kuzielekeza kwa umoja wao kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya taifa.

Kuwafunza vijana kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, ili kulinda uhuru wa Taifa lao.

Jeshi la Kujenga Taifa linaunganisha vijana bila kujali itikadi zao, dini, elimu, jinsia na mali ili kuwalea kuwa wazalendo kwa taifa lao na kupenda kuitumikia nchi yao.

Pamoja na dhana ya kufunzwa uzalendo, pia stadi mbalimbali za kazi hufundishwa kwa vijana hao ili waweze kujiajiri, pindi wamalizapo mkataba yao ya kujitolea kwa miaka miwili.

Serikali ilirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001, baada ya kusitishwa mwaka 1994.

Masharti ya Kujiunga na JKT kwa vijana wa Kujitolea

Kijana kabla ya kujiunga na JKT hutakiwa kuyajua masharti na kuzifahamu taratibu za kujiunga na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira.

Moja ya kipengele cha masharti ya kujiunga na JKT kinasema kuwa ‘Kwa kipindi chote nitakachokua ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie ajira/kazi’.

Kipengele hiki kinaainisha masharti ya makubaliano kati ya Jeshi la Kujenga Taifa na kijana kabla ya kujiunga na kupatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.

Aidha, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na viongozi wengine mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza kuwa, JKT halitoi ajira.

Lakini hivi karibuni wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka huu, umezuka mtindo wa makundi ya vijana waliopitia JKT katika Operesheni mbalimbali kuomba kuandamana kwenda Ikulu kudai ajira.

Madai yanayopingana na dhana ya JKT na kauli ya Mhe. Rais kuwa Jeshi la Kujenga Taifa haliajiri, bali vijana hujiunga kwa hiari kwa kujitolea na baada ya mkataba wa miaka miwili wanatakiwa kurejea walikotoka.

Aidha, Mhe. Rais Kikwete, amewahi kutoa agizo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, taasisi za Serikali na kuziomba zile zisizo

za kiserikali kutoa ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya JKT kulingana na sifa za kijana na nafasi zilizopo.

Takwimu zinaonesha kuwa tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi mwaka jana, jumla ya vijana 104,594 wamejiunga na JKT wakiwemo wavulana 76,832 na wasichana 27,762.

Katika kipindi hicho, jumla ya operesheni 13 katika mafunzo ya JKT zimefanyika, Operesheni hizo ni pamoja na Operesheni Mkapa mwaka 2001, Miaka 40 ya JKT mwaka 2002, Utandawazi mwaka 2004 na Operesheni Jiajiri mwaka 2005.

Zingine ni pamoja na Kasi Mpya mwaka 2006, Maisha Bora mwaka 2007, Uadilifu mwaka 2008, Kilimo Kwanza mwaka 2009 na Operesheni Uzalendo mwaka (2010), Miaka 50 ya Uhuru (2011), Sensa mwaka 2012, Miaka 50 ya JKT (2013) na Miaka 50 ya Muungano (2014).

Vijana wa Kujitolea walioajiriwaTangu mwaka 2003 hadi 2014 jumla ya vijana 24,708 wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670 wameajiriwa na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Jeshi la Polisi vijana 3,965 wavulana wakiwa 2,943 na wasichana 1,022, Magereza vijana 2,139 wavulana 2,044 na wasichana ni 95, Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa ni 78 na wasichana ni 22 na taasisi zingine vijana 592 Vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama TANAPA, GEITA GOLD MINE, BANDARI na AFRICAN GOLD MINE.

Ni vema vijana hao wakatambua kuwa tatizo la ajira sio kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania ikiwemo, wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.

Aidha, vijana hao watambue kuwa walikula kiapo cha UTII, wakati wa kuhitimu mafunzo ya JKT, hivyo suala la kuandamana ni kinyume cha kiapo chao. Vijana hao walitumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na kumaliza mkataba wa miaka miwili. Shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.

Kwa maelezo ya hapo juu utaona kuwa Jeshi la Kujenga Taifa, halina dhamana ya kuajiri bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada ya hapo wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za serikari na binafsi.

Taarifa hii Imetolewa na

Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO