Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

BUNGE LA KATIBA:Mpasuko mkubwa

Wakati kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba za kupitia Rasimu ya Katiba zikitarajiwa kujulikana leo, hali ya mpasuko katika Bunge hilo imezidi kuwa dhahiri ikichochewa zaidi na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Ijumaa iliyopita.
Mpasuko huo unajidhihirisha dhahiri baada ya sasa kuibuka makundi kinzani ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
Wakati kundi la wabunge wanalounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) likijitokeza juzi na jana kuelezea kutoridhishwa kwao na hotuba hiyo kiasi cha wengine kujuta kushiriki katika maridhiano, kundi jipya la Tanzania Kwanza limeanzishwa.


TANZANIA KWANZA
Umoja wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaojiita ‘Tanzania Kwanza‘ wameeleza kusikitishwa na kauli za baadhi ya wajumbe wenzao zenye muelekeo wa kuhujumu mchakato wa kupata Katiba mpya ambazo wamekuwa wakizitoa baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge hilo Maalum.


Umoja huo ambao unaundwa na wajumbe kutoka chama tawala-CCM unadai kuwa na wajumbe 400, umedai kuwa viongozi waliotoa kauli hizo walionekana awali wakishangilia hotuba ya Rais pale aliposema yale waliyokuwa wanakubaliana nayo, lakini sasa watishia vurugu na kususia baadhi ya mambo wasiokubaliana nayo.

MKUMBA

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja huo, Said Mkumba, alisema wameshangazwa na wajumbe hao waliotoa kauli nzito na kuacha kuweka utaifa mbele kwa kushawishiana hoja kuliko kulazimisha kutunga Katiba itakayoimarisha Taifa.


Alisema kuwa wajumbe walionekana kukerwa na baadhi ya maneno yaliyotamkwa na Rais Jakaya Kiwete ya kuwa na ustahimilivu wa kidemokrasia, ustaarabu na hekima ya uongozi na utu uzima.
Mkumba alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya Muungano wa nchi kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana zaidi ya kutafakari na mwisho kuamua, hivyo wanashangazwa na baadhi ya wajumbe wenzao kutoa matamko hayo.


Naye Dk. Emanuel Nchimbi ambaye ni Mjumbe wa Umoja huo, aliwataka Wajumbe wa Bunge Maalum wasivumilie wala kuendekeza vitendo vya vurugu za makusudi vitakavyozuia au kuruhusu watu wachache waliweka rehani Bunge kwa kutengeneza mtaji wa kisiasa.

MBATIA AJUTA
Hali ilizidi kudhihirisha mgawanyiko mkubwa ndani Bunge hilo, Mjumbe wa Bunge hilo, James Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, ameowaomba radhi Watanzania kwa kushiriki kikao cha Kamati ya Maridhiano, ambacho kiliridhia kuvunjwa kwa kanuni ya 7 (1) ya Bunge hilo.


Kanuni hiyo inataka Rais azindue Bunge Maalum kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba haijawasilisha Rasimu ya Katiba.
Akizungumza na wandishi wa habari mjini Dodoma, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema anajutia uamuzi wake wa kushiriki kwenye maridhiano hayo.


Mbatia ambaye pia ni mmoja wa Ukawa, alisema maridhiano hayo yamekuwa na athari kubwa kwa wananchi kwa kuwa hakutarajia kwamba Rais Kikwete angekwenda kulihutubia Bunge kama Mwenyekiti wa CCM.
“Mimi nikiri na niombe radhi kuwa ni mmojawapo wa watu nilioamini kuwa anakuja kama Rais akiwa juu ya itikadi ya chama chake kuwaunganisha Watanzania. Naomba radhi sana, mimi ni mmojawapo ninayeamini hivyo. Lakini amekuja na kudiriki kusema kwamba, sisi ndani ya CCM,” alisema Mbatia.


Alisema kwa matamshi hayo, Rais Kikwete alikwenda bungeni kurasimisha Rasimu ya CCM ndani ya Bunge Maalum la Katiba na kuikanyaga rasimu ya wananchi, jambo ambalo wao hawawezi kulikubali.


Mbatia alisema katika hotuba yake, Rais Kikwete alitumia maneno, ambayo yanaidhalilisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa hiyo, akasema kitu hicho ni sawa na kuwatukana Watanzania, ambao ndiyo waliotoa maoni yaliyowasilishwa na Tume.
Alisema hotuba ya Rais Kikwete imekwenda kinyume cha hotuba alizozitoa Dedemba 30, mwaka jana, wakati akipokea Rasimu ya Pili ya Katiba na Februari 6, mwaka huu wakati akizungumza na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam akitaka kuwaunganisha Watanzania na kuelezea thamani ya katiba na mchakato wake wote unaoendelea.


Mbatia alisema maneno yale ya busara, Rais Kikwete aliyasahau na kujikuta akitoa hotuba inayowagawa wananchi, akiegemea zaidi kwenye msimamo wa chama chake.

“Rais aligeuka akawa mwenyekiti wa chama na kuanza kuzungumza propaganda. Huwezi kuleta propaganda kwenye katiba, huwezi kuleta propaganda kwenye uhai wa taifa,” alisema Mbatia.

MZEE MOYO: NI MAONI BINAFSI YA JK
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassoro Moyo, amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kufahamu kuwa hotuba aliyoitowa Rais Kikwete ni maoni yake mwenyewe.
Akizungumza na NIPASHE jana nyumbani kwake Fuoni mjini Zanzibar, Moyo ambaye ni mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, alisema wajumbe hao wanapaswa kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba na siyo kujadili maoni ya Rais Kikwete.
“Ni vyema wajumbe wa Bunge la Katiba kuzungumzia jambo ambalo limewapeleka bungeni ili kupata katiba bora kwa manufaa ya wananchi,” alisema Moyo.
Alisema ni muhimu kwa wajumbe kujua kwamba Watanzania wanasubiri mwelekeo watakaoutoa wakati wa majadiliano.
Kiongozi huyo alisema mabadiliko ndani ya Muungano ndio pekee ya kuondoa kero za Muungano ambazo zimekuwa zikijitokeza tangu kuundwa kwake mwa 1964.

“Mabadiliko yenyewe ni ama kuwa na serikali ya mkataba au angalau serikali tatu kama ilivyopendekezwa katika Rasimu,” alisema Moyo.
Alisema anashangwazwa na baadhi ya watu wanaomtupia lawama Jaji Warioba kwani Rasimu imependekeza mfumo wa serikali tatu kutokana na maoni ya wananchi na siyo maoni ya Warioba kama wanavyodai.
Alisema msimamo wa Kamati  ya Maridhiano ni serikali ya mkataba, lakini kwa kuwa Rasimu imependekeza serikali tatu, kamati hiyo imeunga mkono mapendekezo hayo.
Alisema  serikali mbili haziwezi kuleta haki na usawa baina ya Zanzibar na Tanganyika, hivyo mapambano ya hoja ya kutaka serikali tatu yataendelea na waamuzi wa mwisho ni wananchi wakati watakapopiga kura ya maoni kuhusu katiba waitakayo.

MSIMAMO WA UKAWA
Juzi Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema katika hotuba yake, Rais Kikwete alitumia muda mwingi kuweka vitisho kuhusu uanzishwaji wa muundo wa serikali tatu kuwa endapo utapitishwa, unaweza kusababisha nchi kupinduliwa na jeshi huku akitoa maelekezo ya kuwapatia Wazanzibari mamlaka zaidi ya kujitawala kama nchi inayojitegemea.
“Sisi tulitarajia kwamba Rais atakuja kutuunganisha, badala yake hotuba aliyoitoa ni ya kututenganisha na hatuwezi kukubali kutumiwa kupitisha mambo wanayoyataka CCM badala ya Rasimu ya wananchi iliyowasilishwa na Jaji Warioba,” alisema Profesa Lipumba, ambaye ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.


ASKOFU DK. SHAO
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Martin Shao, hutuba ya Rais Kikwete bungeni Ijumaa ilikisemea zaidi Chama chake, CCM, badala ya kulishauri Bunge hilo kutumia fursa liliyonayo kupima mawazo ya wananchi na kuyachuja ili walipeleke taifa kwenye hatma njema.
Dk. Shao alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ibada ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 ya Injili ya Dayosisi hiyo jana.
Alisema kilichofanywa na Rais Kikwete ni kukitetea chama chake licha ya kwamba, Watanzania wengi wanajua mabadiliko hayawezi kupatikana kwa siku moja.
“Tunajua kwamba, Mheshimiwa Rais anapaswa kukitetea chama chake. Kwa hiyo, hatukushangazwa na hotuba yake, ingawa tumeongozwa na changamoto nyingi kwa miaka 50. Na katika hili, walipaswa watoe elimu kwa wananchi mapema kuhusu sura ya Muungano,” alisema Askofu Shao.

Aliongeza: “ Rais Kikwete amekuwa mwaminifu sana kwa chama chake na ndiyo maana ametoa msimamo wa chama badala ya kuhimiza mawazo ya wananchi yaheshimiwe.”
Alisema Rais Kikwete alipaswa kutumia nafasi yake kulihimiza Bunge hilo kupima mawazo ya wananchi kwa kutazama wanataka nini na kisha kuheshimu mawazo yao.


KIKWETE
Mwishoni mwa wiki akilizindua rasmi Bunge hilo, mjini Dodoma, Rais Kikwete aliweka wazi kuwa CCM wanaunga mkono mfumo wa Muungano wa serikali mbili na kuadharisha kuwa serikali tatu hazitekelezeki.
Alisema serikali ya tatu ya Muungano inayopendekezwa haina dhaifu, haina vyanzo vya kuaminika vya mapato, haiwezi kukusanya kodi zake, haikopesheki, ni dhaifu na ni rahisi kusababisha jeshi kufanya mapinduzi.

Source: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO