Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

BIASHARA KIMATAIFA: MADINI YA TANZANITE YAPETA MJINI BANG KOK

Tanzanite

Mfanyabiashara wa madini na Afisa Masoko wa Kampuni ya Tom Gems Tanzania, akimwonesha mgeni aliyefika katika banda la Tanzania kuona madini ghafi ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee. Wageni wengi wamefika katika banda hilo kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania.

Baadhi ya madini ya Tanzanite ambayo yanapatikana katika mabanda mbalimbali katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya Bangkok Gems and Jewelry Fair.


Mwenyekiti wa Madini ya Viwandani Bw. Kassim Iddi Pazi, akimwonesha mgeni madini ya Ruby. Kutokana na maelezo ya Bw. Pazi, ameeleza kuwa, madini hayo yametoka katika maeneo ya Winza Dodoma na Matombo Morogoro.



Mfanyabiashara wa Madini kutoka Kampuni ya Tom Gems Bw.Benjamin Mtalemwa akimwonesha mgeni madini mbalimbali alipotembelea banda la Tanzania. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Mthamini wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini Bw. Edward Rweymamu, Wa pili kulia ni Afisa Madini kutoka Shirika la Madini Tanzania (STAMICO). Bw. Peter Maha, na wa kwanza kulia ni Afisa toka Wizarani Bibi. Margareth Muhony.

Na Asteria Muhozya, Bangkok

**********

Madini ya Tanzanite yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya 53 ya Kimataifa ya‘’Bangkok Gems and Jewelry Fair’’, yanayoendelea katika eneo la kibiashara la ‘Impact Challenger’, jijini Bangkok.


Madini ya Tanzanite yanayozalishwa nchini Tanzania pekee duniani, yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea maonesho hayo ikiwemo wauzaji, wanunuzi na wafanyabiashara ambao wamefika katika banda la Tanzania kutaka kuona Tanzanite halisi kutoka Tanzania.


Aidha, pamoja na kwamba madini ya Tanzanite yanazalishwa na Tanzania pekee, lakini katika maonesho hayo ya Bangkok, madini hayo yanapatikana kwa kiasi kikubwa katika mabanda ya washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani jambo ambalo linaonesha namna madini hayo yalivyo na muhimu katika sekta za kibiashara na kiuchumi.


Akizungumzia suala la uwepo wa madini ya Tanzanite kwa kiasi kikubwa katika soko la kimataifa, na katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini , Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Hamis Komba, ameeleza kuwa, uwepo wa Tanzanite katika soko la kimataifa unaashiria mahitaji makubwa ya madini hayo duniani na umuhimu wake katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania, na nchi nyinginezo ikiwemo thamani yake katika soko la kimataifa na upekee wake.


Aidha, , aliongeza kuwa, hiyo ni changamoto katika uthibiti wa madini hayo katika soko la kimataifa kutokana na uwiano wa takwimu za kiasi cha madini kinachotoka kwa kufuata taratibu za usafirishaji madini hayo nje ya nchi na uwingi halisi unaoonekana katika soko la Kimataifa.


“Uwiano wa takwimu za uzalishaji Tanzania na idadi halisi ya madini iliyopo katika maonesho ya kimataifa ni tofauti. Hii ni changamoto katika udhibiti wa madini haya” Amesema Kamishna Komba.


Hivyo, ameongeza kuwa, Serikali inalifanyia kazi suala hili kwa lengo la kufanikisha usimamizi na biashara endelevu ya madini ya Vito na usonara.


Mbali na madini ya Tanzanite kuwa kivutio, katika banda la Tanzania, vinyago vinavyotengenezwa kutokana na mawe aina ya Zoisite, Basalt, Limestone, Travertine, Granite na White marbale yanayopatikana Tanzania ambayo yametengenezwa mapambo mbalimbali ya majumbani yamekuwa kivutio kikubwa katika maonesho hayo kwa wageni waliotembelea banda la Tanzania kutoka nchi za Ulaya na Asia, akiwemo pia Rais wa Shirikisho la wafanyabiashara wa vito na usonara Bw. Somchai Phornchindarak, ambaye pia alitembelea Banda la Tanzania na kuonesha kuvutiwa na kushangazwa na mapambo hayo.


Akizungumzia kuhusu ushiriki wake katika maonesho hayo, Mratibu wa kituo cha Tanzania Geomological Center, Bw. Musa Shanyangi, amesema kuwa, maonesho hayo yamekuwa ya manufaa katika soko la madini ya mawe kutokana na wageni wengi kuonesha kuvutiwa nayo.


Shanyangi, ameongeza kuwa, tayari kituo hicho kimeanza kufanya ukarabati wa miundombinu na kuandaa mitaala ya kufundishia , hivyo chuo kitaanza kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago, ukataji wa madini ya vito, uchongaji wa mawe, mafunzo ya utambuzi wa madini ikiwemo pia maabara itakayotumiwa kwa ajili ya shughuli hizo.


Hivyo, amewataka vijana wa kitanzania kuitumia fursa hiyo kupata mafunzo hayo ili waweze kuingia katika sekta ya madini kwa kuwa itawasiadia kujiajiri, kuinua vipato vyao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Aidha, amewataka wadau katika sekta ya madini kuona umuhimu wa kuongeza thamani ya madini.


“ Maonenesho hayo, yamekuwa na manufaa kwa Tanzania, kituo chetu kimepata fursa ya kufaa kwa bidhaa za mawe, kwasababu nimejaribu kuzunguka katika mabanda mengi sana sijaona bidhaa kama hizi. Hiyo ni fursa kwetu na kwa vijana wa Tanzania katika soko hili. Amesema Shanyangi.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Madini ya Viwanda Tanzania (FEMATA), Bw. Kassim Iddi Pazi akielezea ushiriki wake katika maonesho hayo na soko la madini kimataifa ameeleza kuwa, maonesho hayo yamefungua fursa kubwa ya biashara kutokana na kupata oda nyingi za madini mbalimbali yakiwemo madini ya ruby na zoisite.

Ameongeza kuwa, wamegundua mambo mengi ya muhimu yatakayowasaidia wachimbaji katika sekta hiyo na hasa madini ya viwandani.


“Hakuna kitu muhimu kama kushiriki maonesho. Ruby yetu ni bora na imependwa sana hapa. Wengi walijua Ruby inatoka Bama lakini uwepo wetu umewafanya kujua Ruby safi inatoka Tanzania. Namshukuru Sana Mhe. Rais na Wizara kwa kutuwekea mazingira mazuri katika sekta hii na kutuwezesha kushiriki maonesho haya”. Amesema, Pazi.


Aidha, ameongeza kuwa, kama viongozi wa shirikisho hilo, wanao wajibu wa kuwasaidia wachimbaji wengine kupata taarifa mbalimbali kuhusu sekta hiyo kutokana na uzoefu walioupata na hivyo amewataka kufanya kazi na Serikali kwa ushirikiano.


Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza maonesho hayo ya 53 ya Kimataifa ya ‘Bangkok Gems and Jewelry Fair, ambapo mwaka 2013 ilishiriki kama nchi mwalikwa ambapo kiongozi wa ujumbe wa Tanzania alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Mhe. Stephen Masele.

CREDIT: WOINDE SHIZZA “LIBENEKE LA KASKAZINI”

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO