Jeneza likiwa na mwili wa Marehemu tayari kwa Ibada ya Mazishi iliyofanyikia Nyumbani kwao Chiwanda.
Mchungaji wa Kanisa la Africa Mission Church wanakosali wazazi wa Marehemu akiongoza ibada ya Mazishi.
baadhi ya Waombolezaji wakielekea Makaburini.
Joseph Mwaisango akiwa amebeba Jeneza lenye mwili ya marehemu kuelekea Makaburini tayari kwa safari ya mwisho
Mchungaji akisoma neno la Mungu kutoka kwenye Biblia lenye ujumbe kwa Waombolezaji na wafiwa ambapo alisema hata kama alikuwa ni mtoto mchanga alikuwa akivuta pumzi kama sisi hivyo naye amepaswa kupewa heshima zote kama binadamu.
Mwili wa Marehemu ukishushwa kaburini.
Kaburi likifukiwa baada kukamilika kwa taratibu zote ambapo mwili wa marehemu ulizikwa katika makaburi ya Kijiji wanakozikwa Wananchi wengine.
Kwa mujibu wa mila za kabila la Wanyamwanga vijana hawa walikuwa wakisiliba kaburi baada ya kumaliza mazishi.
Ezekiel Richard Kamanga ambaye ni mwandishi wa Habari kutoka redio ya Bomba fm ya Jijini Mbeya akizungumza machache kwa wafiwa na wanakijiji kwa niaba ya Wanahabari wenzao ambao hawapo pichani Venance Matinya wa gazeti la JamboLeo na Joseph Mwaisango wa mbeya yetu blog
KATIKA hali ya kusikitisha Watoto wawili kati ya Wanne ambao ni mapacha waliozaliwa kwa pamoja na mwanamke Aida Nakawala Mkazi wa Kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoani Mbeya wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Nimonia.
Watoto hao wamefariki kwa mida tofauti ambapo Mtoto wa Kwanza alifariki Nyumbani kwao baada ya kuugua ghafla ndipo hali za wengine zilipoanza kutia shaka na kulazimu Waandishi wa Habari wa Mtandao wa Mbeya Yetu, Gazeti la Jambo Leo na Redio ya Bomba Fm waliohudhuria mazishi ya Mtoto huyo kulazimika kuwakimbiza katika Hospitali ya Wazazi Meta kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo baada ya kupokelewa kwa watoto hao Watatu mtoto mmoja aliaga dunia baada ya kuchelewa kupata matibabu kutokana na kubanwa na kifua na kusababisha kushindwa kupumua vizuri.
Hali za watoto wawili waliobaki wanaendelea vizuri na matibabu na kwa mujibu wa Daktari anayewatibu amesema taratibu za Hospitali hiyo ni kupokea watoto waliochini ya Miezi miwili lakini hao wamezidi umri huo hivyo badala ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya wataendelea kuwepo Meta hadi hapo hali zao zitakapoimarika.
Baadhi ya wananchi na wauguzi katika Hospitali ya Wazazi Meta wamesema sababu ya watoto hao kuugua ni kutokana na kukosekana kwa uangalifu wa karibu katika malezi ya watoto hao ukilinganisha na maisha ya vijijini kukosa watu wenye uelewa wa afya za watoto.
Wengine wameitupia lawama moja kwa moja Serikali kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka tangu watoto walipozaliwa ili kujiridhisha na mazingira wanayopaswa watoto hao kuishi kwa kuwapatia msaada wa karibu na ushauri wa kitaalamu.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Thobias Mwalwego, alikiri kuwepo kwa urasimu katika Idara yao kwa madai kuwa tangu watoto hao walipokuwa wamezaliwa walipata taarifa na kuchukua hatua kwa afisa mmoja kufika kijijini na kuchukua picha zao.
Alisema urasimu unakuja kutokana na Ofisi ya Wilaya na Mkoa kukosa fungu la dharula ambapo barua za maombi zote hupelekwa makao makuu kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii ambapo Ofisi yake huchukua muda mrefu kurudisha majibu kutokana na waombaji kuwa wengi.
Alisema kila ofisi katika Ngazi ya Mkoa ingekuwa na fungu la Dharula kama ilivyo katika Ofisi zingine hali ambayo ingeweza kusaidia kuepusha vifo vya watoto hao kutokana na kupatiwa msaada wa ushauri na makazi rafiki kwa malezi ya mapacha wanaozidi wawili.
Aidha alishauri kila Halmashauri Nchini kutenga bajeti za kusaidia majanga kama hayo na vitu vya dharula wakati Serikali inajipanga kutekeleza kutokana na taratibu zake kuchukua muda mrefu ili kuweza kukabiliana na hali yoyote na muda muafaka.
Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Ahmed Issa katikati na Joseph Mwaisango wa Mbeya yetu Blog wakimkabidhi Aida Nakawala msaada wa pesa kiasi cha shilingi laki tano 500,000/ toka wa watanzania waishio nchini Uswisi
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini wakiwa wamewabeba watoto hao
Joseph Mwaisango alipokwenda kuwatembelea Hospitali ya wazazi Meta watoto wawili waliobakia na hali zao kwa sasa zinaendelea vizuri
Wakati huo huo Umoja wa Watanzania waishio nchini Uswisi (TAS) wametoa msaada wa Fedha taslimu shilingi Laki tano(500,000/=) kwa mama Aida Nakawala kwa ajili ya kusaidia kulea watoto wengine waliobaki.
Akikabidhi msaada huyo kwa mama huyo kijijini kwao Chiwanda Wilayani Momba, Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Ahmed Issa kwa niaba ya Watanzania hao alisema wameguswa sana na hali hiyo na kuahidi kuendelea kuchangia kila mara.
Aidha alisifu utendaji kazi wa Waandishi wa Habari hususani Mbeya yetu Blogwaliofanikisha kuibua jambo hilo na kulitolea taarifa kila wakati jambo lililosaidia kufahamisha watu wengi wakiwemo wanaoishi nje ya Tanzania na kutuma kile wanachokuwa wameguswa nacho.
Mbali na Hilo, Meneja wa TMA Kanda ya Mbeya, Ahmed Issa, pia amejitolea kuusafirisha mwili wa Marehemu kutoka Hospitali ya Meta Mbeya hadi Kijijini kwao Chiwanda Wilayani Momba kwa ajili ya taratibu za Mazishi.
Na Mbeya yetu
0 maoni:
Post a Comment