Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

ZIJUE SABABU ZA CHADEMA KUUNGA MKONO MUUNDO WA SERIKALI TATU.. SOMA HAPA

SABABU ZA KUUNGA MKONO MUUNDO WA SERIKALI TATU

1. MUUNDO WA SERIKALI MBILI UMESHINDWA KUTEKELEZEKA

(A) TANGU KUSAINIWA KWA HATI ZA MAKUBALIANO YA MUUNGANO, HATI HIZO HAZIJAHESHIMIWA NA MAMLAKA ZA SERIKALI YA MUUNGANO NA YA ZANZIBAR KAMA IFUATAVYO:

(i) Mamlaka ya kutunga sheria ya iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar haikutunga sheria ya kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano na kwa hiyo Muungano haukupata uhalali wa kisheria kwa upande wa Zanzibar;

(ii) Orodha ya Mambo ya Muungano imeongezwa kinyume na Hati za Makubaliano ya Muungano kutoka mambo 11 yaliyoko kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano hadi mambo 22 yaliyoko katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya sasa. Lengo na athari ya kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano imekuwa ni kuipokonya Zanzibar mamlaka yake katika mambo ambayo hayakuwa ya Muungano;

(iii) Utaratibu wa kikatiba wa kutatua migogoro ya Muungano haujawahi kuheshimiwa wala kufuatwa badala yake migogoro ya kikatiba ya Muungano inajadiliwa kwa taratibu za kirasimu ambazo zimeshindwa kuitatua;

(B) ZANZIBAR HAIRIDHIKI TENA NA MUUNGANO NA INATAKA UHURU

Mabadiliko ya kikatiba ya hivi karibuni, pamoja na madai ya Zanzibar juu ya ‘Kero za Muungano’ yanaonyesha dhahiri kwamba Zanzibar hairidhiki tena na misingi mikuu ya Muungano iliyoko kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya sasa:

(i) Katiba ya sasa ya Zanzibar inaitangaza Zanzibar kuwa ‘nchi’ na kutangaza mipaka yake na eneo lake la bahari;

(ii) Katiba mpya ya Zanzibar inatamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Kama Zanzibar ni moja ya ‘nchi mbili’, nchi ya pili ni Tanganyika ambayo ndiyo ilikuwa Mshirika wa Zanzibar katika Hati za Makubaliano ya Muungano;

(iii) Zanzibar ni dola, hata kama haina mamlaka kamili, kwa sababu ina vyombo vyote vya dola kama Serikali, Bunge na Mahakama. Aidha, Zanzibar ina viashiria (trappings) za dola kama Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Rais wake hukagua gwaride la heshima wakati wa Sherehe za Mapinduzi;

(iv) Katiba ya sasa ya Zanzibar inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Nchi ya Zanzibar na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Idara Maalumu, yaani vikosi vya kijeshi vya Zanzibar;

(v) Katiba ya sasa ya Zanzibar inaunda vikosi vya kijeshi vya Zanzibar vinavyoitwa vikosi vya Idara Maalumu na kumfanya Rais wa Zanzibar Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi hivyo mwenye mamlaka ya kutangaza hali ya hatari au kutangaza na kuendesha vita;

(vi) Katiba ya sasa ya Zanzibar inakataa mamlaka ya Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano kwa kukataza rufaa kwenye Mahakama hiyo kwa kesi zinazohusu haki za binadamu, tafsiri ya Katiba ya Zanzibar, mambo ya Kiislamu yanaoanzia katika Mahakama za Kadhi na mambo mengine yanayoweza kuainishwa kwenye Katiba ya Zanzibar au kwenye sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi;

(vii) Katiba ya sasa ya Zanzibar imemnyang’anya Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine, na Rais wa Zanzibar hahitaji tena kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati anapofanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa Zanzibar;

(viii) Katiba ya sasa ya Zanzibar imekataza kutumika kwa sheria zinazohusu mambo ya Muungano zitakazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano mpaka kwanza zipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar;

(ix) Katiba ya sasa ya Zanzibar imekataa mamlaka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya kutoza kodi zinazohusiana na Mambo ya Muungano mpaka kwanza kuwepo mashauriano na makubaliano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

(x) Katiba ya sasa ya Zanzibar inaweka msimamo kwamba mambo yote yaliyoorodheshwa katika kipengele (i) – (ix) hayawezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko hayo;

(x) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayaita ‘Kero za Muungano’ Mambo mbali mbali ya Muungano yaliyomo katika Hati za Makubaliano ya Muungano na yalioongezwa baada ya Hati hizo. Mambo ya Muungano ambayo sasa ni ‘kero’ ni hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, masuala ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa Zanzibar na mgawanyo wa mapato kati ya Zanzibar na Tanzania Bara; ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili na uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu; na ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.

MADAI YA MUUNDO WA SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU NI YA MUDA MREFU

Mapendekezo ya Rasimu juu ya muundo wa shirikisho lenye serikali tatu sio mapya, bali ni madai ya miaka mingi ya wananchi wa Tanzania:

i. Mwaka 1984 Rais wa pili wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Kwaw Swanzy waling’olewa madarakani na Wazanzibari wengine wengi kuwekwa kizuizini kwa sababu ya kuhoji muundo wa Muungano wa Serikali Mbili kwa madai kwamba Hati za Makubaliano ya Muungano zilikuwa zimeweka muundo wa shirikisho la Serikali Tatu;

ii. Mwaka 1991 Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa iliyoundwa na Rais Ali Hassan Mwinyi ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu;

iii. Vyama vya siasa vikuu vya upinzani, yaani CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi, vimekuwa na msimamo wa kuundwa kwa shirikisho la serikali tatu tangu vilipoanzishwa mwaka 1992;

iv. Mwaka 1993 Wabunge 55 kwa pamoja walitoa taarifa ya kuwasilisha hoja Bungeni iliyodai kwamba kuendelea na mfumo wa Muungano wa serikali mbili usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano. Hivyo Wabunge hawa waliliomba Bunge liazimie kwamba Serikali ilete Muswada Bungeni kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika’ ndani ya Muungano;

v. Mwaka 1998 Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 iliyoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuchunguza masuala mbali mbali ya kikatiba, nayo ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu;

SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU HALIWEZI KUWA NA GHARAMA KUBWA KULIKO MUUNGANO WA SERIKALI MBILI WA SASA

Tangu kuchapishwa kwa Rasimu, viongozi wa CCM na baadhi ya wananchi na wanazuoni wamedai kwamba muundo wa Muungano wenye serikali tatu utakuwa na gharama kubwa kwa nchi maskini kama ya kwetu. Hata hivyo, uchambuzi wa Rasimu yenyewe unaonyesha kwamba gharama za kuendeshea muundo wa shirikisho lenye serikali tatu zinaweza kuwa hata ndogo kuliko gharama za kuendeshea muundo wa Muungano wa serikali mbili za sasa:

(i) Hadi sasa hakuna mtu yeyote au taasisi iliyofanya uchambuzi wa ulinganifu wa gharama za kuendesha serikali – iwe moja, mbili au tatu – katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni ghali zaidi kuliko kuendesha serikali mbili;

(ii) Kama suala la gharama za kuendeshea serikali ndio jambo muhimu zaidi katika kuamua muundo wa Muungano, wanaopinga shirikisho la serikali tatu wangeeleweka kama wangependekeza muundo wa serikali moja tu, badala ya serikali mbili za sasa wanazoziunga mkono, au tatu zilizopendekezwa na Rasimu;

(iii) Kama mapendekezo ya Rasimu juu ya Mambo ya Muungano yakichukuliwa kuwa kigezo cha kupima ukubwa wa serikali – na kwa hiyo gharama za kuiendeshea – basi gharama za serikali ya Muungano zinaweza kuwa ndogo sana:

a. Kwa mambo saba ya Muungano yanayopendekezwa na Rasimu, hakutakuwa na zaidi ya wizara nne za Serikali ya Muungano. Hivyo, kwa mfano, kutakuwa na wizara ya katiba na sheria itakayoshughulikia masuala ya Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano; wizara ya ulinzi itakayokuwa na majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano; wizara ya fedha itakayoshughulikia masuala ya sarafu na benki kuu, na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano; na wizara ya mambo ya nje. Masuala yaliyobaki, yaani uraia na uhamiaji na usajili wa vyama vya siasa hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea kwa hiyo yanaweza kuwekwa chini ya mojawapo ya wizara zilizotajwa hapo juu;

b. Aya ya 93(2) ya Rasimu inapendekeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kuwa mawaziri wasiozidi kumi na tano. Hata hivyo, aya ya 93(3) inaelekeza kwamba “Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na Wizara kwa kuzingatia mamlaka ya Serikali kwa mujibu wa Katiba hii.” Kwa maana nyingine ukubwa wa Serikali lazima uzingatie Mambo saba ya Muungano. Kwa sababu hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano haiwezi kuwa na mawaziri wengi kuliko Mambo saba ya Muungano;

c. Kwa mtazamo huo huo wa aya ya 93(3) na orodha ya Mambo ya Muungano kama kipimo cha ukubwa wa Serikali ya Muungano, haiwezekani Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu wanaopendekezwa katika aya za 98 na 99 za Rasimu kuwa zaidi ya wanne;

d. Kwa kuzingatia idadi ya Makatibu Wakuu wenyewe, Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu inayoelezwa katika aya ya 100 na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri inayotajwa katika aya ya 101, hazina maana wala umuhimu wowote kikatiba;

e. Kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu kuhusu Bunge la Jamhuri ya Muungano katika aya ya 105, kwa idadi ya sasa ya mikoa ya Tanzania Bara na wilaya za Zanzibar, Bunge la Jamhuri ya Muungano litakuwa na wabunge 75. Kwa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, endapo Bunge la Zanzibar litakuwa na Wabunge hamsini wa majimbo ya sasa ya uchaguzi, wakati bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya sasa. Kwa maana hiyo, muundo wa Muungano wa serikali tatu utakuwa na mabunge matatu yenye jumla ya wabunge 314;

f. Kwa kulinganisha, Bunge la Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya wabunge 357 – 189 wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Bara na hamsini ya Zanzibar; 102 wa Viti Maalumu; 10 wa kuteuliwa na Rais; watano wanaowakilisha Baraza la wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu. Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuna jumla ya Wawakilishi 81 - 50 wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, 10 wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, 20 wa Viti Maalum na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwa maana hiyo, kwa muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana idadi ya wabunge 438. Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge matatu yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124!

g. Taasisi nyingine za Muungano zinazopendekezwa kama vile Tume ya Mahusiano na Uratibu wa Serikali (aya ya 102); Tume ya Utumishi wa Mahakama (aya ya 172); na Tume ya Utumishi wa Umma (aya ya 178) haziwezi kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu;

h. Taasisi nyingine kama vile Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji (aya ya 188) na Tume ya Haki za Binadamu (aya ya 194) hazipo kwenye orodha ya Mambo ya Muungano na uwepo wao kwenye Rasimu unakinzana na matakwa ya aya za 59(1) na 60 za Rasimu. Kama majukumu ya taasisi hizo hayahusu Mambo ya Muungano, Tume hizo haziwezi kugharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

i. Majukumu ya utekelezaji wa Mambo mengine ya Muungano kama uchaguzi na usajili wa vyama vya siasa yanaweza kutekelezwa na taasisi husika za Washirika wa Muungano kwa makubaliano na masharti maalumu chini ya aya ya 59(3) ya Rasimu. Hii nayo itapunguza gharama za kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

MUUNDO WA SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU UTALETA VITA???

Kumejitokeza hoja kwamba muundo wa shirikisho la serikali utapelekea Muungano kuvunjika, na “Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa Zanzibar.” Dhana hii ya ‘serikali tatu ni kiama’ na mifano inayotolewa kuiunga mkono ina malengo ya kiitikadi ya kuwatisha wananchi wasijadili Muungano na masuala muhimu yanayouhusu:

(i) Kuna mifano ya nchi zilizovunja muungano wao bila kuwepo vita au migogoro ya mipaka. Jamhuri za Czech na Slovakia zilizotokana na kuvunjika kwa Jamhuri ya zamani ya Czechoslovakia ni mojawapo ya nchi hizo;

(ii) Kuna nchi nyingi ambazo zimepigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu ya kulazimisha muungano usiokubaliwa na upande mmoja au mwingine katika umoja huo. Ethiopia na Eritrea; Sudan na Sudan Kusini, na hata Yugoslavia ya zamani ni mifano ya nchi hizo;

(iii) Zipo nchi ambazo zinaendelea kuwa na vita kwa sababu ya kulazimisha umoja ambao upande mmoja unaukataa. India (mgogoro wa Jimbo la Kashmir), Hispania (Jimbo la Basque) na Angola (Jimbo la Cabinda) ni mifano mizuri.

Tumaini Makene

CHADEMA Senior Information(Press) Officer

0752 691569/ 0688 595831

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO