Dar es Salaam.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia mashtaka raia wa Kenya, Joshua Mulundi kuhusu kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka na sasa atakabiliwa na mashtaka ya kuidanganya polisi kuhusika kumteka daktari huyo.
Hakimu Warialwande Lema aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alifikia hatua hiyo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), kuwasilisha hati ya kumfutia mashtaka hayo.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Beatha Kitau kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika.
Akiwasilisha hati hiyo mahakamani, Wakili Kitau alisema DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa, chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka. Kutokana na uamuzi huo wa DPP, Hakimu Lema alimfutia mashtaka Mulundi na kumwachia huru.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, alikamatwa na kufunguliwa kesi nyingine ya kutoa taarifa za uongo kwa Jeshi la Polisi.
Katika kesi hiyo mpya inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai, 2012, katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Wakili Kweka alidai kuwa siku hiyo mshtakiwa akiwa kituoni hapo alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa polisi kuwa yeye na wenzake ndiyo waliokodiwa ili kumteka na kumdhuru Dk Ulimboka wakati akijua kuwa si kweli.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo.
Wakili Kweka alisema upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili waweze kuandaa maelezo ya awali ya kesi hiyo. Pia aliweka pingamizi la dhamana dhidi ya mshtakiwa akidai hana makazi ya kudumu kwa kuwa si raia pia kwa ajili ya usalama wake kulingana na mazingira ya tukio hilo.
Kauli hiyo ya Wakili Kweka ilimfanya mshtakiwa huyo alipuke na kudai kuwa wanamfungulia kesi za uongo ambazo hahusiki na kudai kwamba wamepanga kumpoteza.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba unisamehe, kwa kile nitakachokifanya, kwani nikirudi mahabusu mimi itaniumiza,” alidai mshtakiwa huyo na kusisitiza kuwa hahusiki na kwamba bado ni kijana mdogo.
Baada ya mshtakiwa huyo kulalamika hivyo, Hakimu Katemana aliutaka upande wa mashtaka uwasilishe hati ya kuzuia dhamana ambayo hata hivyo, hawakuwa nayo licha ya kuwaongezea saa mbili kuandaa.
Baada ya kushindwa, Hakimu Katemana alimpa mshtakiwa masharti ya dhamana, ambayo hata hivyo, naye hakuweza kuyatekeleza hivyo kurudishwa mahabusu, hadi Agosti 20, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
Masharti hayo ya dhamana yalikuwa ni kuwa na wadhamini wawili, mmoja akitoka katika taasisi inayofahamika, ambao wote na yeye, watasaini hati ya Sh5 milioni kila mmoja na kuwasilisha mahakamani hati zake za kusafiria.
Mulundi alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Julai 14, 2012 na kusomewa mashtaka mawili ya kumteka na kutaka kumuua Dk Ulimboka.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakimu Mkazi, Agnes Mchome, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya alidai kuwa Mulundi ambaye ni mkazi wa Murang’a, Kenya, alimteka Dk Ulimboka Juni 26, 2012 akiwa eneo la Leaders Club, Kinondoni.
Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta, Dar es Salaam kinyume na sheria, mshitakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk Ulimboka.
Dk Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema Juni 27, 2012 akiwa hajitambui katika msitu huo wa Mabwepande huku akiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mshtakiwa alifikishwa polisi, baada ya kwenda katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Kawe la Josephat Gwajima, ambako alidai kuwa anataka kutubu kwa kuwa yeye na wenzake ndiyo waliomteka Dk Ulimboka.
STORY NA PICHA: MWANANCHI
0 maoni:
Post a Comment