Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Tundu Lissu: Jeshi la polisi lirudishe simu yangu, liache kuingilia mawasiliano yangu


Wandugu wapendwa,

Nimetoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar sasa hivi (jana). Polisi wamekataa kunirudishia simu yangu waliyoinyang'anya kwa nguvu tarehe 6 Machi, siku waliyonikamata nikiwa mahakamani Kisutu.

Mimi sijatuhumiwa wala kushtakiwa kwa kosa lolote la mtandao chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao au Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Kiposta.

Badala yake nimeshtakiwa kwa makosa ya uchochezi yanayohusiana na kauli zangu juu ya Serikali ya Rais Magufuli. Aidha, nimeshtakiwa kutokana na msimamo wangu na kauli zangu juu ya siasa za Zanzibar na masuala ya Muungano.

Kwa sababu hizi, Jeshi la Polisi halikuwa na, na halina, sababu wala haki ya kuchukua simu yangu na kuendelea kukaa nayo hadi sasa, siku 17 baadae.

Nimepata taarifa kwamba tangu walipoichukua kwa nguvu karibu wiki tatu zilizopita, simu hiyo imekuwa inaonekana inatumika kwa mawasiliano ya whatsapp.

Maana yake ni kwamba polisi wanasoma na au kusikiliza mawasiliano yangu ya simu na ya kielektroniki. Hii ni kinyume cha sheria za nchi yetu.

Simu hiyo ni chombo changu cha mawasiliano ya kikazi na binafsi. Kama mbunge, ninaitumia simu hiyo kwa ajili ya mawasiliano yangu na wananchi walionichagua na viongozi wengine wa kiserikali na kichama.

Jeshi la Polisi halina haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo.

Kama wakili ninatumia simu hiyo kwa ajili ya mawasiliano na wateja wangu, wengi wao wakiwa na kesi mahakamani dhidi ya Jeshi la Polisi au Serikali hii.

Mawasiliano hayo yanalindwa kwa mujibu wa sheria na polisi hawana sababu wala haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo na wateja wangu.

Vile vile ninatumia simu yangu kwa mawasiliano yangu binafsi na familia yangu, marafiki zangu na jamaa zangu wengine.

Mawasiliano haya nayo yanalindwa na Katiba yetu na polisi hawana sababu wala haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo binafsi.

Kwa vyovyote vile, kitendo cha Jeshi la Polisi kuchukua na kuendelea kuishikilia simu yangu bila sababu wala haki ni mfano mwingine wa matumizi mabaya ya mamlaka ya kiupelelezi ya Jeshi hili la Polisi.

Badala ya kushughulikia wahalifu wa wazi kama akina Daudi Bashite na wenzake, polisi wetu wanahangaika na viongozi waliochaguliwa na wananchi wanaotumia haki na wajibu wao kikatiba kuikosoa serikali ya Rais Magufuli kwa sababu ya matendo yake ya hovyo.

Ninafahamu polisi wanafikiri kwamba kwa kunifanyia vitendo hivi basi nitaogopa na kulegeza msimamo wangu katika masuala mbali mbali yanayolisibu taifa letu.

Ninawaomba wajiulize kwa nini imeshindikana hadi sasa kulegeza msimamo wangu huo kwenye masuala hayo, licha ya kunikamata na kuninyanyasa mara nyingi kwenye vituo vya polisi na mahakamani. Sitishiki na sitatishika na mambo yao haya.

Hata hivyo, naomba niseme wazi ili mwenye kusikia na asikie. Vitendo hivi vya Jeshi la Polisi havifai na vinatakiwa kukoma kabisa. Polisi wanirudishie simu yangu mara moja na bila masharti yoyote.

Ninaendelea kutafuta mawasiliano ya IGP Mangu na wakubwa wenzake ili wanieleze kwa nini simu yangu inashikiliwa na maofisa wao.

Endapo na wao watashindwa kutoa maelekezo sahihi kwa waliochukua simu yangu na wanaendelea kukaa nayo, nitalazimika kwenda Mahakama Kuu ili kuomba mahakama iingilie kati na kutamka kama ni sahihi kisheria kwa mapolisi wa nchi hii kuingilia mawasiliano ya sisi wananchi kwa namna ya hovyo namna hii.

Naomba mnaopata ujumbe huu mnisaidie kupaza sauti zetu ili matendo haya mabaya yakome katika nchi yetu.

Wasalaam,

Mh. Tundu AM Lissu
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO