Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI   KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA  MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
_________________________
1.   UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/18.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, napenda kutumia  fursa hii, kipekee kutoa pole nyingi kwa CHADEMA FAMILY, kwa kuondokewa na mmoja wa waasisi wa CHADEMA, Mzee Philemo Ndesamburo, aliyefariki dunia tarehe 31 Mei, 2017 huko Moshi, Kilimanjaro na hatimaye kupumzishwa katika nyumba yake ya milele tarehe 6 Juni, 2017. Marehemu Mzee Philemon Ndesamburo licha ya kuwa mwasisi wa CHADEMA, lakini pia alijitoa kwa hali na mali kukifadhili na kukilea Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kukifikisha hapa kilipo leo. Mafanikio tuliyo na yo leo kama chama, na kama wabunge wa CHADEMA na viongozi wa chama kwa ngazi mbali mbali, na mafanikio tuliyo nayo leo, katika siasa za vyama vingi hapa nchini,  kwa sehemu fulani yanatokana na juhudi za Mzee wetu huyu.
Mheshimiwa Spika, Taifa limempoteza mwanamageuzi wa karne, aliyekuwa tayari kupoteza maisha yake, kwa ajili ya mabadiliko ya kweli ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Taifa letu. Kama chama, tutamkubuka kwa kuyaenzi yale yote aliyoyaasisi kwa mustakabali mwema wa chama chetu na Taifa kwa jumla. Hakika ni vigumu kuziba pengo aliloliacha. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, AMINA.
Mheshimiwa Spika, baada ya salama hizo za rambi rambi, naomba nitambue mchango uliotukuka wa Mhe. Halima James Mdee (Mb) ambaye ndiye Waziri Kivuli mwenye dhamana ya kuisimamia Serikali katika masuala ya Fedha na Mipango, kwa kufanya kazi usiku na mchana kufanya tafiti na uchambuzi wa nyaraka mbalimbali na kupata takwimu ambazo zimejenga msingi wa hotuba hii kwa zaidi ya asilimia 90.
Mheshimiwa Spika, tofauti na nchi zilizoendelea ambapo watu wenye upeo na weledi wa kufanya kazi namna hii huenziwa na kujengewa mazingira mazuri ya kuwa bora zaidi, katika nchi zinazoendelea watu wa aina hii hukumbana na madhila mengi ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa sababu tu ya ujasiri wao wa kuisimamia na kuikosoa Serikali tena katika misingi ya kikatiba na kisheria. 
Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) anahitimisha hotuba yake kuhusu Bajeti ya Serikali hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017 alisema kwamba: “… ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kumfikia kila mwananchi ni lazima uchumi huo uwe shirikishi. Uchumi huo hauwezi kuwa shirikishi ikiwa tunabaguana kwa misingi ya tofauti za kisiasa au tofauti nyinginezo. Uchumi wa nchi yetu hauwezi kujengwa na kundi moja la jamii na kulibagua linguine. Hali kadhalika uchumi wa nchi yetu hautajengwa na chama kimoja cha siasa kwa kukibagua kingine au kuchochea migogoro ndani ya vyama vingine. Mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana katika kujenga uchumi ulio imara. Ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda haiwezi kufikiwa tukiwa na msigano wa namna hii”.  Aidha, aliongeza pia kwamba: “kutofautiana kifikra ni afya ya akili, na ili uvumbuzi utokee lazima kuwe na fikra mbadala – ‘alternative thinking’ Nilidhani kuwa Serikali na Chama cha Mapinduzi wangetambua kuwa uwepo wa watu wenye fikra mbadala katika taifa hili ni tuna na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; lakini badala yake Serikali wameona kuwa uwepo wa watu hao ni kama mwiba na kikwazo.”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kunukuu maneno ya Kitabu cha mwasisi wa Taifa la Afrika ya Kusini Hayati Nelson Mandela “No Easy Walk To Freedom” kama maneno ya faraja kwa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni waliopatwa na madhila mbalimbali kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na kufungiwa kuhudhuria vikao vya bunge au kuadhibiwa kwa namna nyingine yoyote ile, wakati wakitekeleza majukumu yao ya kibunge,  kwamba wasifadhaike; kwa kuwa imewapasa kupitia njia hiyo, ili kufikia lengo lililo kubwa zaidi la kutwaa madaraka ya dola kwa njia ya kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nitoe Bashraff ya Bajeti ya Serikali iliyowasilisha mbele ya Bunge lako kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuungana na waheshimiwa Wabunge ambao kwa umoja wao walisema kuwa bajeti hii haijawahi kutokea katika historia ya hivi karibuni ya bajeti za Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba ni kweli haijawaji kutokea bajeti ya namna hii na kwamba bajeti hii imevunja rekodi kwa sababu zifuatazo:-
1.   Bajeti hii ni bajeti ambayo takwimu za  vitabu vyake vya mapato na matumizi (Volume I, II, III &IV) zinatofautiana sana,  na pia sura ya bajeti iliyosomwa na Mheshimiwa  Waziri wa Fedha na Mipango inatofautiana pia na vitabu hivyo.  Wakati kitabu cha Mapato ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 itakusanya jumla ya shilingi trilioni 23.9; kitabu cha Matumizi ya Serikali kinaonyesha kuwa Serikali inakusudia kutumia jumla ya shilingi trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 3 ambayo vyanzo vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato. Wakati huo huo, sura ya bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango inaonyesha kuwa bajeti ya Serikali kwa maana ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni kiasi cha shilingi trilioni 31.7 – kiasi ambacho hakionekani popote katika vitabu vya mapato na matumizi ya Serikali. Hali kadhalika kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mikaka Mitano  tarakimu hii ya shilingi trilioni 31.7 inaonekana kwamba ni makisio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19. Hivyo, sasa hivi tunatekeleza mapendekezo ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2018/19 na sio 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea!!!


2.   Hii ni bajeti ambayo imedhamiria kuuwa kabisa dhana ya ugatuaji madaraka kwa Serikali za Mitaa (D by D) kwa kuziondolea Serikali za Mitaa madaraka yake ya kisheria ya kukusanya kodi ya Majengo, Kodi ya Mabango na Ushuru wa huduma mijini (City Service Levy) kwa malengo ya kujiendesha, na kurudisha madaraka hayo ya ukusanyaji kodi hizo Serikali Kuu kupitia TRA. Hii inadhihirisha kwamba yote yaliyofanywa  na Serikali za CCM zilizopita na gharama zote zilizotumika kuimarisha madaraka kwenye Serikali za mitaa yailikuwa hayana maana yoyote. Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kwamba haijapata kutokea bajeti ya Serikali yenye lengo la kuuwa Serikali za Mitaa kwa kuzipunguzia madaraka na kuziondolea vyanzo vyake vya mapato.

3.   Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania inawalipisha watanzania maskini wasio na uwezo wa kumiliki magari kodi ya ada ya mwaka ya leseni za magari (Annual Motor Vehicle Licence Fee) kwa kuihamishia kodi hiyo kwenye ushuru wa bidhaa za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa ambapo athari zake ni kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi masikini. Ieleweke kupanda kwa bei ya mafuta kutasababisha kupanda kwa nauli katika sekta ya usafirishaji jambo litakalosababisha kupanda kwa bei za vyakula, kupanda kwa bei za kusaga na kukoboa nafaka kwa kutumia mashine zinazotumia petrol au dizeli kwa wananchi waishio vijijini, kupanda bei kwa pembe jeo za kilimo, kushindwa kupata nishaati ya mwanga kwa wananchi waishi vijijini kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya taa nk. Kwa maneno mengine bajeti hii imelenga kuwabebesha wananchi masikini mzigo wa kodi kwa matumizi ya anasa ya watu wa tabaka la kati na juu wenye uwezo mkubwa kifedha wa kuweza kumiliki magari na vitu vingine vya thamani kubwa. Katika hili, Kambi Rasmi ya Upinzani inakiri kabisa kwamba haijawahi kutokea bajeti ya namna hiyo ya kuwanyonya masikini na kuwaneemesha matajiri. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona chombo chochote cha moto cha usafiri wa barabarani kinachotumia mafuta ya taa.

4.   Hii ni bajeti ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania Serikali itatoza kodi ya shilingi elfu kumi (10,000/=) kwa nyumba zote katika halmashauri zote nchini  ambazo hazijafanyiwa uthamini zikiwemo nyumba za tembe na tope kwa wananchi masikini waishio vijijini. (Hii iko katika ukurasa wa 48 kipengele cha iii cha hotuba ya Bajeti 2017/18) Badala ya Serikali kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wa vijijini waweza kuwa na nyumba bora zenye staha, na badala ya Serikali kufanya uthamini wa ardhi na nyumba za wananchi masikini waishio vijijini ili waweze kupata hati miliki itakayoongeza thamani ya ardhi na nyumba zao ili waweze kutumia hati hizo kupata mikopo itakayoboresha maisha yao; bado Serikali imeendelea kuwabamiza kodi katika ufukara na uduni wao. Haya ni mastaajabu!!!, na hakika Kambi Rasmi ya Upinzani haijawahi kuona bajeti ya namna hii.

5.    Hii ni bajeti ambayo imeendelea kupandisha kodi kwenye bidhaa ambazo uzalishaji wake hutumia malighafi inayozalishwa ndani ya nchi kama vile shayiri, zabibu, tumbaku n.k, jambo ambalo ni dhahiri litapunguza bei za mazao hayo, na hivyo kupunguza kipato cha wakulima wa mazao hayo. Kwa maneno mengine, bajeti hii haimjali mwananchi masikini ambaye ndiye mzalishaji wa malighafi hizo.

6.    Hii ni bajeti ambayo imejinasibu kama bajeti ya uchumi wa viwanda wakati haijaonyesha popote mkakati wa kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo ndiyo msingi wa uzalishaji  viwandani.

7.   Hii ni bajeti ambayo haijataja popote itaongeza ajira kiasi gani kwa watanzania na wala haijasema itapunguza umasikni wa watanzania wa kiwango gani kwa mwaka wa fedha 2017/18. Aidha, ni bajeti ambayo haikuzungumzia popote utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.

Mheshimiwa Spika, wahenga walisema,“ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni. Maajabu ya bajeti hii ni mengi lakini itoshe kusema tu kwamba “ukiwa mwongo, basi uwe pia na kumbukumbu nzuri” Waheshimiwa wabunge na hata wananchi wanaweza kusahau mengine, lakini hili la ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ni mapema mno kuweza kulisahau. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutolea maelezo ahadi hii ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili wananchi wajue kama wamekopwa fedha hii au wamedhulumiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, waliosema kwamba bajeti hii haijawahi kutokea walikuwa sahihi, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaunga mkono.

Mheshimiwa Spika, tofauti na bajeti mbadala za Kambi Rasmi ya Upinzani zilizopita ambazo ziliweka msisitizo katika Ukuaji wa Uchumi Vijijini (Rural Growth) safari hii bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebeba kauli mbiu ya Ukuaji Shirikishi wa Uchumi (Inclusive Economic Growth) ambapo watu wote wanatakiwa kushiriki katika kujenga uchumi katika mazingira yao na pia ukuaji wa uchumi unatakiwa uwaguse watu wote katika tabaka zote.

Mheshimiwa Spika, wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni akiwasilisha hotuba yake kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni tarehe 6 Aprili, 2017, alisema kwamba:  “tangu Serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikijigamba kuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ikilinganishwa na serikali za awamu zilizotangulia, lakini kumekuwa na kilio kikuu kwa upande wa wananchi kuhusu hali ya maisha kuendelea kuwa ngumu kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu”. Aidha, alisema kwamba: “kilio hiki cha wananchi kinamaanisha kwamba ukuaji wa uchumi unaohubiriwa na Serikali haujawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa nchi hii”.

Mheshimiwa Spika, Kiongozi wa Upinzani alinukuu maneno ya Wanazuoni wa uchumi wanaosema kwamba “Growth is inclusive when it takes place in the sectors in which the poor work (e.g. agriculture); occurs in places where the poor live (e.g. undeveloped areas with few resources); uses the factors of production that the poor possess (e.g. unskilled labour); and reduces the prices of consumption items that the poor consume (e.g. food, fuel and clothing).”  

Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi unapotokea kwenye sekta ambazo watu maskini wanafanya kazi kama vile kilimo; unatokea katika maeneo ambayo watu masikini wanaishi kwa mfano maeneo ambayo hayajaendelea na yasiyo na rasilimali; unatumia nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo kwa mfano nguvukazi isiyo ya kitaalamu; na unapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia kwa mfano chakula, mafuta na nguo.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ukipima hali ya Tanzania utaona kwamba uchumi wetu sio shirikishi kwa kuwa ukuaji wake hautokei katika sekta ambazo watu masikini wanafanya kazi au maeneo ambayo watu masikini wanaishi. Aidha, ukuaji wa uchumi wetu hautumii nyenzo za uzalishaji ambazo watu masikini wanazo na pia ukuaji huo haujapunguza bei za bidhaa ambazo watu masikini wanatumia. Kimsingi bajeti hii ambayo imeshabikiwa kwamba haijawahi kutokea, iko kinyume kabisa na mahitaji hayo ya ukuaji shirikishi wa uchumi.


2.   MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MIAKA MTATU ILIYOPITA 2014/15 – 2016/17
Mheshimiwa Spika, wahenga wetu walishasema kwamba “Sikio la kufa halisikii dawa” Nimeanza na methali hiyo, kwa kuwa, kwa miaka yote ya uhai wa Bunge la Kumi na mpaka bunge hili la kumi na moja, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kubana matumizi kwa kupunguza bajeti ya matumizi  kawaida yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, lakini kinyume chake Serikali hii ya CCM imeendelea kuongeza bajeti matumizi ya kawaida hata kwa matumizi yasiyo ya lazima  na kupunguza bajeti  ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefanya tathmini ndogo ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa maana ya matumizi ya kawadia na matumizi ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo iliyopita na kubaini kwamba utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeweka matumizi ya kawaida kama kipaumbele kuliko bajeti ya maendeleo ambayo ndiyo dira ya ujenzi wa uchumi katika nchi yetu.  Kwa mfano mwaka 2014/15 utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ulikuwa ni asilimia 40, mwaka 2015/16 asilimia 31.24 na mwaka 2016/17 asilimia 35.26. Ukitafuta wastani wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta kwamba utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa miaka hiyo haujawahi kuzidi asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, wakati utekelezaji wa bajeti ya maendeleo uko chini ya wastani, utekelezaji wa bajeti ya matumizi ya kawaida yakiwemo matumizi yasiyo ya lazima umebaki kuwa juu. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2014/15 matumizi ya kawaida yaikuwa ni asilimia 91, mwaka 2015/16 asilimia 81 na mwaka 2016/17 asilimia 68.7. Ukitafuta wastani kwa kutumia takwimu hizi kwa miaka tajwa utakuta bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikitekelezwa kwa kwa takriban asilimia 80.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuweka rekodi sawa kwamba; utekelezaji wa asilimia 68.7 wa  bajeti ya matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2016/17, haumaanishi kwamba Serikali imebana matumizi bali imegoma kutoa fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kutumiwa na kwa maana hiyo, fedha hizo zinabaki kuwa ni deni la Serikali. Kwa maneno mengine matumizi ya kawaida bado yako juu ukilinganisha na matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, mwenendo huu wa kutumia mapato yetu kwa matumizi ya kawaida kwa takriban asilimia 80 na kutoa fedha kiduchu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambazo nazo hazitolewi kwa wakati, kunaifanya nchi yetu kuwa na uchumi wa ‘mchumia tumbo’ – yaani hand to mouth economy.

3.   TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Mei, 2017 wakati nawasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha, nilieleza kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa ikipuuza utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ndiyo msingi wa uchumi wa wananchi kwa kutotoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo. Katika maelezo yangu nilitaja Wizara 10 za mfano kuonyesha tofauti ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge na fedha halisi zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bado Serikali haijatoa sababu za msingi za utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo, nitarudia sehemu hiyo, ili kwa mara nyingine kuipa Serikali nafasi ya kuwaeleza wananchi ina lengo gani hasa kwa kutotekeleza bajeti ya maendeleo kwa takriba asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, Wizara nilizozitolea mfano kwa kutopatiwa fedha za maendeleo kwa ukamilifu wake katika mwaka wa fedha 2016/17 ilikuwa ni kama ifuatavyo:
                     i.        Ofisi ya Makamu wa Rais  ( Mazingira)
Mheshimiwa Spika, nilieleza kuwa, kati ya  shilingi bilioni   10.9  za miradi ya Maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge katika ofisi hii,  ni shilingi  bilioni 1.2 tu  sawa na asilimia  11.3 ya fedha ya fedha hizo zilizotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kwa maneno mengine bajeti ya Maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira haikutekelezwa kwa asilimia 88.7.
Mheshimiwa Spika, nilitoa angalizo kwamba, fedha hizi ndizo hutumika kupambana na uharibifu wa mazingira yetu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi kama vile ukame, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, njaa nk na kwamba kitendo cha Serikali kutotoa fedha hizo maana yake ni kubariki athari mbaya zinazotokana na uharibifu wa mazingira ziendelee kuwaangamiza wananchi.

                   ii.        Tume ya Kudhibiti Ukimwi :
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni  10.1 za miradi ya maendeleo  zilizoidhinishwa na Bunge, ni shilingi  bilioni  2.7 tu sawa na asilimia 27  ya bajeti  ndio zimetolewa. Nilieleza kwamba tafsiri ya kutotekeleza bajeti hiyo kwa asilimaia 73, maana yake ni kwamba; vita dhidi ya maambukizi ya UKIMWI hapa nchini si kipaumbele tena cha Serikali hii ya awamu ya tano.
                   iii.        Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi:
Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, kati ya shilingi bilioni 897.6 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ni shilingi bilioni 500.4 sawa na asilimia 55 ndizo ambazo zilikuwa zimetolewa hadi kufikia Machi, 2017. Hata hivyo, mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba, shilingi bilioni 427 (asilimia 48) zilikuwa ni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na shilingi bilioni 470 (asilimia52) zilikuwa ni kwa ajili ya kugharamia miradi halisi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika sekta ya elimu zinaonekana kuwa nyingi kwa kuwa zimechanganywa pamoja na fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwmba; ni muhimu tukatenganisha  kati ya miradi ‘halisi ya maendeleo’ na ‘ Mikopo ya wanafunzi’ ili kuweza  kupata picha halisi  ya nini hasa kinakwenda kutumika kutatua changamoto za uboreshaji/ upanuzi/ujenzi  wa miundombinu na shughuliza utafiti  katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, tukija kwenye miradi halisi ya maendeleo, kati ya miradi 16 ambayo ilitengewa fedha  katika mwaka wa fedha  2016/17 Kamati ya Bunge ya Maendelelo na Huduma za Jamii  ilifanya  ukaguzi wa miradi 5 tu sawa na  na 12% ya miradi yote. Kati ya miradi hiyo  mitano , ni miwili tu iliyopatiwa fedha! Tena kwa kiwango kidogo sana. Ifuatayo ni Hali halisi ya miradi mitano iliyokaguliwa  :
§  Mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) – Mradi namba 6361. Bunge liliidhinisha  shilingi bilioni 4, hakuna fedha yoyote iliyopelekwa
§  Mradi wa ukarabati wa Chuo Kikuu  cha Dar es salaam  (Mradi namba 6350). Bunge iliidhinisha shilingi  bilioni 9.4, hakuna fedha yoote iliyopelekwa
§  Mradi wa Hospitali ya Mloganzila (Namba ya Mradi 6364).Chuo kiliomba shilingi 14,549,727,933 (BN. 14.5) hakuna fedha iliyopelekwa mpaka 13/Mei /2017 wakati wa hotuba ya bajeti ya wizara ya elimu inasomwa.
§  Mradi wa Mfuko wa Utafiti na Maendeleo wa COSTECH (Namba ya Mradi 6345. Katika Malengo ambayo nchi  nchi imejiwekea , ni kutenga 1% ya Pato la Taifa. Hata hivyo, mfuko huu ulitengewa  kiasi cha shilingi  bilioni 12.8 tu  sawa na 0.012% ya pato la Taifa . Pamoja  na udogo huo , kiasi kilichotolewa ni shilingi  bilioni 4.07 tu (sawa na 31.7%). Kati ya hizo fedha Mfuko mkuu wa hazina uliotakiwa kutoa  bilioni 8 ilitoa  shilingi bilioni 1.5 tu na TCRA iliyotakiwa kutoa   shilingi  bilioni 4.8 ilitoa shilingi bilioni 2.57 tu.
§  Mradi wa ujenzi wa DIT teaching Tower (Namba ya Mradi 4384). Mradi huu una umri wa miaka 11 (2006- 2017)…bado unasuasua, hakuna pesa na Matokeo  yake gharama za mradi zimeongezeka  toka bilioni 5 mpaka bilioni 9.

                  iv.        Wizara ya Maji
§  Tume ya Taifa ya umwagiliaji- Fungu 05:
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya Maji, kati ya shilingi bilioni 35.3 za miradi ya maendeleo zilizodhinishwa na Bunge, ni shilingi bilioni 2.9 tu sawa na asilimia 8.4 zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji  wa miradi hiyo. Kwa upande wa usambazaji wa maji ,mijini na vijijini kati ya shilingi bilioni 915.1  zilizotengwa,  zilizotolewa ni shilingi bilioni 181.2 sawa na 19.8% ya fedha  zote za miradi ya Maendeleo ndizo zilizotolewa. 
Mheshimiwa Spika, nilisema na narudia tena kusema kwamba; utekelezaji duni namna hii wa bajeti ya maendeleo katika sekta ya maji ni matusi kwa watanzania ambao uhaba wa maji umewafanya waishi kama wanyama; na kwamba;  ule usemi wa Serikali wa kumtua mama ndoo ya maji, kwa mazingira haya  ni dhihaka na ni ulaghai   kwa akina mama wote wa nchi hii ambao wanaendelea kusota  na kukumbana na kila aina ya kadhia katika kutafuta maji. Aidha, niliitahadharisha Serikali  Ikumbuke kwamba, hawa kina mama inaowafanyia mzaha kaatika suala la maji  ndio mtaji mkubwa wa kura waliyoipa ushindi, na sasa imeshindwa kutumiza ahadi yake ya kuwatuma ndoo za maji kichwani, kwa kushindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo iliyodhinishwa na Bunge.
                   v.        Wizara ya Viwanda na Biashara:
Mheshimiwa Spika, Kati ya shilingi bilioni 42.1 zilizotengwa, wizara ilipokea shilingi bilioni 7.6 tu sawa na 18.6%.  Nileeleza wazi na ninarudia tena kwamba; kwa utekelezaji huo wa bajeti, ni aibu kwa Serikali kutumia Kauli mbiu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ kama kampeni ya kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.

                 vi.        Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa:
Mheshimiwa Spika, nilieleza pia kwamba, pamoja na unyeti wa  Wizara hii, bado ilikumbwa na janga hili la kutopewa fedha za maendeleo. Moja ya mradi muhimu sana katika wizara hii  ni mradi wa  Defence Scheme ( mradi namba  6103)  ambao unatekelezwa chini ya  Kifungu namba  2002- Military Research  and Development Fungu 57. Mradi huu, ulitengewa jumla ya shilingi  bilioni 151.1. lakini Mpaka mwezi Machi,2017 wizara ilikuwa imepokea shilingi  bilioni 30 tu sawa na 20%  tu! Mbali na mradi tajwa hapo juu  kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje  Ulinzi na Usalama [1] fedha za miradi ya maendeleo ziliwasilishwa ni 14.5% tu, yaani Bunge liliidhinisha shilingi   bilioni 230, pesa zilizotolewa  hadi  Machi 2017 ni shilingi bilioni 33.9. Halafu tunaitangazia dunia kwamba tuna lengo la kuwa na jeshi dogo la kisasa lenye weledi, wakati Serikali haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kupitia miradi hiyo ndiyo tunaweza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa na hivyo kuwa na jeshi la kikisasa.
                vii.        Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi:
Mheshimiwa Spika,  Kilimo kiliidhinishiwa shilingi 101,527,497,000 (bilioni 101). Kiasi kilichotolewa ni  shilingi 3,369,416,66 (bilioni. 3.369) sawa na  3.31%. Kwa upande wa mifugo na uvuvi, kiasi cha shilingi 15,873,215,000 (bilioni 15.8) kiasi kilichotolewa  ni bilioni 1.2. Sawa na 8% . Kwa maneno mengine, Kilimo ambacho tunasema kwamba ndio uti wa mngongo wa uchumi wa Tanzania, bajeti yake ya maendeleo haikutekelezwa kwa takriban asilimia 97. Serikali inahubiri Uchumi wa Viwanda ikijua fika kwamba viwanda hivyo haviwezi kuendelea bila ukuaji katika sekta ya kilimo, lakini haitoi fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya Kilimo.  Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba;   ama Serikali imefilisika ila haitaka kukiri hivyo, au kuna tatizo kubwa la afya ya akili (mental health) miongoni mwa watendaji wa Serikali. Tulisema hivyo kwa kuwa  haingii akilini kwamba ile sekta ambayo inategemewa kuleta hayo mapinduzi ya viwanda haipewi fedha za kutosha, halafu Serikali inaendelea kuhubiri viwanda – vitatoka wapi mwenendo huo?
               viii.        Wizara ya Maliasili na Utalii , fedha za  ndani za miradi ya maendeleo  zilizotengwa ni shilingi  bilioni 2. Fedha zilizotolewa ni shilingi milioni 156,688,000 sawa na 8%
                  ix.        Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa ni shilingi bilioni 25.30 . Fedha zilizotolewa mpaka sasa ni shilingi  bilioni 7.63 tu.
                    x.        Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano:
Mheshimiwa Spika, wizara hii ilitengewa fedha za Maendeleo kwa mchanganuo ufuatao:

§  Ujenzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.17 zilizotolewa ni shilingi trilioni 1.07 sawa na asiliia 58.7
§  Uchukuzi iliidhinishiwa shilingi trilioni 2.49 zilizotolewa ni shilingi bilioni 761.5 sawa na asilimia 30.5
Mheshimiwa Spika, Uchambuzi uliofanywa hapo juu unaonyesha wazi kwamba, ufanisi wa Serikali ya awamu ya tano katika utekelezaji bajeti ya Miradi ya maendeleo na mpango wa kuwaondolea umasikini watanzania  ni  kwa wastani wa  0%- 20%. Wizara pekee iliyoweza kuvuka 50% ni Wizara ya Ujenzi na inafahamika kwamba yapo ‘maslahi mapana’ yanayohitaji kulindwa katika wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali hii ya awamu ya tano inashindwa kutekeleza bajeti ya maendeleo kwa takriban asilimia 70, ni Serikali hii hii ambayo kwa nyakati tofauti imekuwa ikijigamba kwamba imefanikiwa kukusanya mapato kwa kiwango cha hali ya juu kuzidi makisio iliyoyaweka kila mwezi.
 Mheshimiwa Spika, Swali la msingi la kujiuliza hapa ni kwamba; hizo fedha amabazo Serikali inajisifu kukusanya kwa wingi zinakwenda wapi??  Au zinatumika vibaya – kwa maana ya matumizi ambayo hayajaidhinishwa na bunge? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili, ni kwa nini haikutoa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa takriban wizara zote, kwa kisingizio kwamba kulikuwa na upungufu wa fedha lakini wakati huo huo inautangazia umma kwamba imekusanya mapato mengi kuzidi lengo la makusanyo.
Mheshimiwa Spika, Ni Serikali hii hii ambayo kupitia Ilani ya chama chake, na kupitia dira ya taifa ya maendeleo ya 2025 na 2020 kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imekuwa ikituambia  kwamba suluhisho la kuondokana na hali duni ya uchumi na utegemezi ni kuendesha modernization ya uchumi. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali iliahidi kufanya mambo yafuatayo:
i)             Kutilia Mkazo katika matumizi ya maarifa ya kisasa (Sayansi na Teknolojia)
ii)           Kuandaa rasilimali watu katika maarifa na mwelekeo
iii)          Kufanya mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi
iv)         Kufanya mapinduzi ya viwanda ambavyo ndivyo kiongozi wa uchumi wa kisasa
v)          Mapinduzi  katika nishati na miundombinu ya kisasa
Mheshimiwa Spika, Suala la Msingi ambalo wabunge wa pande zote mbili tunapaswa kutafakari na kujiuliza, kutokana na uchambuzi uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hapo juu, hivi kweli itakapofika 2020 na 2025 malengo (i-v) yatatimia? Na kama nafsi zetu zinatuambia kwamba hayatatimia, tunajipanga vipi kutumia kipindi hiki cha bajeti KUJISAHIHISHA ili mwaka ujao wa fedha TUSIJIULIZE maswali hayahaya?!

4.   HOJA ZA NYUMA ZA KAMBI YA  UPINZANI KUHUSU BAJETI YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti Mbadala za mwaka 2011/12 na 2012/13 Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza masuala kadhaa ili kusaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa upande mmoja na kwa upande wa pili kusaidia kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wa kawaida na hivyo kuboresha maisha yao. Masuala tuliyoyapendekeza ni pamoja na:
1.   Kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia  asilimia moja (1%) ya pato la Taifa kama wenzetu wa Uganda na Kenya.
2.    Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitakiwa kufanya ukaguzi maalum (special audit) katika kitengo cha Deni la Taifa (fungu 22) ili kujua mikopo inayochukuliwa kila wakati inatumika kufanyia nini, na miradi iliyotekelezwa kama ni miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Bado ukaguzi maalum haujafanyika hadi sasa.
3.   Kuongeza Kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma hadi Tsh 315,000 kwa Mwezi. Inashangaza kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali imeshindwa hata kutangaza nyongeza ya Mishahara licha ya ukweli kwamba hali ya maisha imezidi kuwa ngumu.
4.   Kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwa kufuta sehemu ya Kodi ya Mapato inayotoa fursa kwa kampuni za madini kutumia sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 iliyofutwa (grandfathering). Pendekezo letu lilikuwa na lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100 percent depreciation’ kwenye mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax’. Pendekezo hili ambalo lingeipatia Serikali mapato mengi na kwa sasa bado halijatekelezwa kwa Kampuni za madini zenye mikataba.
5.   Kuanzisha Real Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili kutokana na biashara ya kupangisha nyumba/vyumba. Serikali bado haijatekeleza pendekezo hili, hakuna sera ya nyumba na hivyo Serikali hupoteza mapato mengi sana kwenye sekta ya nyumba, kodi za nyumba kuwa juu sana na kuumiza vijana wanaoanza maisha na kutozwa kwa mwaka mzima.
6.   Kushushwa kwa tozo ya kuendeleza stadi (Skills Development Levy – SDL) kutoka asilimia sita (6) ya sasa mpaka asilimia nne (4). Katika pendekezo hilo tulishauri kuwa waajiri wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali imechukua pendekezo hili kwenye mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2013/14 lakini bila kuhusisha mwajiri Mkuu, Serikali. Ni vema kodi hii ilipwe na waajiri wote nchini na ishuke kuwa asilimia 4.
7.   Kuwepo na utaratibu wa kuweka stiker maalumu kwa kazi za sanaa zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi hizo ili wasanii wanaozitengeneza wanufaike na kazi zao. Pendekezo hili lilikubaliwa na Serikali na hivi sasa TRA na COSOTA wameanza kufanya kazi hii ili kuhakikisha wasanii wetu wanafaidi jasho lao.(ufanisi wake ukoje?)
8.   Kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje ya nchi na badala yake kuwe na mpango wa kuziongezea thamani na kuzitumia ngozi ghafi hapa nchini ili kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje. Serikali iliamua kupandisha ushuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Bungeni inaamini kuwa kuna haja kubwa ya kuzuia kuuza mazao ghafi nje ili kukuza ajira za ndani na kuongeza thamani ya mauzo yetu nje.
9.   Kujenga Mazingira ya ukuaji wa uchumi vijijini (Rural Growth) kwa kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na Umwagiliaji. Sambamba na kuundwa  kwa  Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural Development Authority) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.Lengo likiwa kuwe na fedha mahsusi, kutoka chanzo mahsusi zinazotengwa na kuwekewa uwigo (ringfenced ) wa kutotumika kwa shughuli nyingine yoyote zaidi ya kufanya maendeleo vijijini. Pendekezo hili Serikali imelidharau na madhara yake ni kuwa maendeleo ya vijijini hayana uratibu mzuri na hivyo kusahaulika kabisa.
10.               Kukarabati Reli ya Kati na matawi yake.
11.               Kujenga uwezo wa viwanda vya ndani ili kuviwezesha kuzalisha na kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa thamani. Tuliitaka serikali kupiga marufuku uuzaji nje wa korosho ghafi kama ilivyovyo kwa ngozi ghafi kwa kuanzia. Serikali haijaweka mkakati wowote wa kuhakikisha korosho yote nchini inabanguliwa kabla ya kuuzwa nje.
12.               Kuboresha elimu na afya hasa kwa shule na zahanati/Vituo vya Afya vilivyo katika maeneo ya vijijini kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa sekta hizi walio kwenye Halmashauri za Wilaya. Tulipendekeza pia kuanzishwa kwa posho za mazingira magumu. Serikali haijatekeleza pendekezo hili.
13.               Kuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60. Serikali  ipo kimya kuhusu suala hili muhimu sana kwa wazee nchini.
14.               Tulipendekeza kwamba utaratibu wa vitambulisho vya Taifa uoanishwe na mfumo wa kutoa namba ya utambulisho kwa mlipa kodi (TIN Number) ili kila mwananchi awajibike kujaza fomu za taarifa za kodi  ‘tax returns’ bila kujali kipato chake. Suala hili lingewezesha kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi nchini na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi. Pendekezo hili bado halijatekelezwa na serikali.
15.               Ilipendekezwa kwamba misamaha yote ya kodi iwekwe wazi na ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Bajeti ya mwaka 2014/2015 imeridhia pendekezo hili na kuahidi kuwa misamaha ya kodi itawekwa wazi. Utekelezaji wake bado unasuasua!
16.               Kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kufundisha wataalamu wa kutosha wa sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na utajiri wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu. Serikali ipo kimya kuhusu pendekezo hili kama ambavyo imekuwa kimya KABISA kwenye suala la Mafuta na Gesi katika hotuba   za wizara ya Nishati na Madini na Hotuba ya Bajeti. Wakati miaka michache iliyopita ilikuwa inalipigia upatu kwa mbwembwe  nyingi sana.

5.   HALI YA UCHUMI WA TAIFA -   TAARIFA YA BENKI KUU YA TANZANIA YA  MWEZI  - APRIL 2017  
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwezi Aprili, 2017, hali ya uchumi wa Taifa ilikuwa kama ifuatavyo:
                                     i.        Mfumuko wa Bei: katika Mwezi Machi,  2017 mfumuko wa bei ulikuwa kwa wastan wa 6.4%  ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo  mfumuko ulikuwa kwa 5.4%. Ongezeko husika limesababishwa  na ongezeko la bei ya chakula   kama vile unga, mahindi, mihogo, ndizi, mbogamboga, sukari n.k
                                    ii.        Akiba ya chakula:  kwenye ghala la Taifa (National Food reserve Agency  NFRA) kulikuwa na akiba ya chakula ya  tani 86,444. Hii haijumuishi maghala ya watu binafsi.
                                   iii.        Mzunguko wa fedha:  Mzunguko wa fedha na upatikanaji wa fedha (Money Supply and Credit ), ulikuwa kwa 4.1% (22,539) mwaka 2017 ikilinganisha na  15.5% mwaka 2016 ( 21,648.5)
                                 iv.        Upatikanaji wa  fedha  katika sekta binafsi: Nyongeza ya upatikanaji wa fedha wa sekta binafsi  kutoka kwenye taasisi za fedha ilikuwa  kwa kiwango cha 3.7% kwa mwaka 2017 . Ukuaji ulikuwa wa kiwango cha chini ikilinganishwa  na ongezeko la 23.6% mwezi Machi 2016. Hali hii ni kiashiria cha kusua sua kwa sekta ya fedha nchini na mzunguko /upatikanaji wa fedha kwa wafanyabishara.
                                   v.        Mwenendo wa kibajeti:  Makusanyo ya mwezi Machi, 2017 yalifikia shilingi trilioni 1.45 ikilinganishwa  na shilingi Trillion 1.325 mwaka 2016. Mapato yaliyotokana na kodi  ni shilingi trilioni 1.3  ikiwa ni ongezeko la 7.1%. Serikali za mitaa toka vyanzo vya ndani shilingi bilioni 45.3.
                                  vi.        Usafirishaji wa Bidhaa Nje : Mauzo ya nje yaliinza dola za kimarekani milioni 8,921 mwaka  2017  ikiwa ni pungufu kwa 3% ikilinganishwa na mwezi Machi, 2016.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo za hali ya uchumi, wala haihitaji kuwa na shahada ya uchumi kujua kama hali ya uchumi wa nchi yetu sio nzuri. Kwa mwenendo huo, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unaporomoka na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza bunge hili juu ya mikakati iliyopanga ili kunusuru hali ya uchumi wetu ambayo kwa vigezo vyote inaporomoka.

5.1.      HALI YA UCHUMI WA TAIFA – TAARIFA YA  BENKI YA DUNIA
Mheshimiwa Spika, Tarehe 11 Aprili, 2017 - Benki ya Dunia ilitoa Ripoti yake juu ya uchumi wa Tanzania na ilikuwa na haya ya kusema :
                                     i.        Kukua kwa uchumi kumepungua kutokana na upatikanaji wa fedha kuwa hafifu na kutotabirika/kutokueleweka  kwa Rais Magufuli.
                                   ii.        Kuubadilika badilika kwa sera za serikali na ukuaji kwa kasi ndogo kwa sekta binafsi ilipunguza  ukuaji wa pato la ndani  toka 7.2% ( 2015)  mpaka 6.9% (2016)
                                  iii.        Wawekezaji  wana wasiwasi/ mashaka na  sera zisizotabirika  kutoka za serikali ya Rais Magufuli.
                                 iv.        Kuporomoka /kushuka kwa kasi kwa mzunguko wa fedha na kuongezeka kwa Mikopo isiyolipwa kumeiathiri sana sekta binafsi.
                                   v.        Kubadilika badilika kwa sera kunapotokea mara kwa mara kunasababisha sintofahamu  kwa sekta binafsi na sintofahamu husika zina athari katika maamuzi ya wawekezaji.
                                 vi.        Mabenki ya Tanzania yanajilinda /yanajiwekea wigo Mkubwa (LARGE BUFFER) dhidi ya hasara inayopatikana kwa Mikopo isiyolipwa (kutokana na hali mbaya ya kibiashara tokea awamu ya tano iingie madarakani) kwa kutoza riba kubwa katika Mikopo.
                                vii.        Baadhi ya wawekezaji wa kigeni wameamua/ wanataka kupunguza  shughuli zao za uzalishaji  au  kusitisha mipango ya kupanua shughuli za uwekezaji kwa sababu ya masharti mapya magumu na kutozwa kodi kubwa. Tanzania inatajwa kuwa nchi ambayo sio rahisi  kufanya biashara ikiwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya malipo (the highest number of payments) katika ukanda wa Afrika Mashariki.[2] Kuna malipo tofauti tofauti zaidi 48 ya kikodi.Na ni nchi ya pili  kwa kuwa na kiwango kikubwa cha kodi (44.9%) katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Hii ndio taswira ya hali ya mwenendo wa uchumi wetu kutokana  na uchambuzi uliofanywa na wataalam wa fedha na uchumi  kitaifa  na kimataifa. Pamoja na yote hayo tunaambiwa kila kitu kinakwenda vyema!! Uongo huu na upotoshwaji unaofanya na serikali hii kupitia wizara ya fedha lazima ufike mwisho!!
6.      MAENDELEO YA KISEKTA – SEKTA YA UZALISHAJI – VIWANDA
Mheshimiwa Spika, baada ya hotuba za wizara mbalimbali kukamilika tumegundua yafuatayo:
                                     i.        Kwamba, kwa mwaka wa fedha 16/17 serikali imeweza kutekeleza 30% tu ya miradi ya Maendeleo
                                    ii.        Kilimo Kinachoajiri 75% ya watanzania kimezidi kudorora.. ukuaji umeporomoka mpaka 1.7 % toka 6% iliyotarajiwa
                                   iii.        Viwanda vingi vilivyosajiliwa TIC ni viwanda ambavyo havina uhusiano wa moja kwa moja na shughuli pana za kiuchumi za nchi yetu.
                                  iv.         Viwanda vya usindikaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo, Mifugo na uvuvi  sio kipaumbele cha serikali
                                   v.        Hakuna uhusiano  wa moja kwa moja kati ya sekta ya kilimo , sekta ya viwanda na nishati. Viwanda haviwezi kuwa imara bila kuwa ma malighafi za kutosha kutoka kwa wazalishaji na Umeme wa kuweza kuviendesha.
                                  vi.        Hakuna dhamira ya serikali kufufua kilimo. Kijiografia Tanzania ilipaswa kuwa kapu  la nafaka la Afrika ya Mashariki na Kati , yenye uwezo wa kuzalisha  chakula kitakachotosheleza mahitaji ya ndani na zida kwa ajili ya nchi Jirani
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya waziri mkuu, ukurasa  wa 19 iliainisha kwamba  katika kuhakikisha  watanzania wanashiriki  kikamilifu  kwenye uchumi  wa viwanda , serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi  ya hapa  nchini Pamoja  na Mashirika  ya umma inajenga viwanda. Na kwamba jitihada hizo zimewezesha  Mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF, LAPF,LAPF,GEPF ,PSPF na NHIF kuanza kufufua, kuendeleza  na kujenga   viwanda  vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali nchini!
Mheshimiwa Spika, Taarifa  ya mwaka ya shughuli za Kamati nya kudumu  ya Bunge  ya uwekezaji wa mitaji ya umma (PIC ) kwa kipindi  cha Januari  ,2016  hadi  Januari 2017 ikizungumzia madeni  makubwa  ambayo serikali inadaiwa na Mashirika  na Taasisi zake inaainisha kwamba  Kamati ilipokea  taarifa  ya msajili wa hazina kuhusu utendaji  wa taasisi mbalimbali za umma  na kubaini madeni  makubwa ambayo serikali inadaiwa  na Taaasisi hizo. Taarifa ya Kamati inasema…. Kwa ujumla uchambuzi wa Kamati  umebaini kuwa  serikali imekuwa  na tabia ya kutumia huduma au kukopa  kutoka katika taasisi zake bila kufanya malipo. Serikali imekuwa ikidaiwa fedha nyingi  na madeni hayo yamekuwa yakilimbikizwa  mwaka hadi mwaka . Hali hii inadidimiza  ukuaji wa Taasisi hizo na kusababisha  hasara kuwa katika utendaji wao.
Mheshimiwa Spika, Mfuko ambao unaonekana kuathirika zaidi ni Mfuko wa PSPF ambao unaidai serikali zaidi  ya shilingi Trillion 3.3. ambayo yanajumuisha Madeni yanayotokana na dhima  ya mafao  ya watumishi  wa serikali ambao  walirithiwa  na mfuko wa PSPF kipindi iliyoanzishwa mwaka 1999 (pre 1999).
Mheshimiwa Spika, Mpaka kufikia Juni 2015, serikali ilikuwa inadaiwa shilingi trillion 1.97. Kiasi kilicholipwa na PSPF kwa wastaafu kimezaa riba ya shilingi bilioni 698 na kusababisha deni la shilingi trillion 2.67. Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa na Mfuko, uwezo wa mfuko kulipa kulipa mafao kwa wanachama wake  unategemeana na namna serikali itakavyolipa michango yake kwa wakati  pamoja na kulipa deni  la wanachama kipindi cha utumishi kabla ya julai 1999.
Mheshimiwa Spika, Kundi la pili linatokana na  madeni ya uwekezaji . Kumekuwa na kukinzana baina ya serikali na mfuko wa PSPF . wakati serikali  inadai deni inalodaiwa ni  bilioni 290 , mfuko wa PSPF  unadai deni halisi  ni shilingi   bilioni 533. Pamoja na mkanganyiko huo , serikali imeshindwa  kutekeleza ahadi yake   ya kutoa  hati fungani  zenye  thamani  ya shilingi  bilioni 290 kwa ajili ya kulipa deni hilo. Na deni la tatu  ni madeni ya malimbikizo  ya mchango wa mwajiri (15% ya serikali kila mwezi)  Deni linalotokana na malimbikizo ya shilingi bilioni 253.78 ambalo  ni la kipindi  cha kuanzia  Julai 2015 hadi Februari  2016.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inadaiwa  madeni makubwa  katika Mifuko mingine, miongoni mwao ni NSSF,LAPF , NHIF ,PPF  n.k  kama ambavyo taarifa za Kamati za Bunge na Taarifa za Mkaguzi Mkuu wa  Hesabu Serikali zinazotolewa kila mwaka zinavyoaainisha.. Kambi rasmi ya upinzani inashangazwa na kushtushwa na pendekezo hili jipya la kutumia Mifuko hii hii  kujenga viwanda  vipya 27, wakati serikali  hailipi madeni inayokopa. 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiwezi kuruhusu wizi wa namna hii kuendelea kufanywa na Serikali dhidi ya fedha za wavuja jasho wa nchi hii! Ikumbukwe kwamba, hizi sio fedha za serikali, ni fedha za wanachama wanazochanga ili waweze kulipwa mafao punde wanapostaafu. Serikali inalazimisha mifuko kujenga viwanda wakati bado fedha za mifuko zilizotumika katika uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali (hususan sekta ya nyumba) zikiwa hazina uhakika wa kurejeshwa kutokana na maamuzi mabovu ya uwekezaji yaliyofanywa na Mashirika husika.[3]
Mheshimiwa Spika, Ni muhimu sana hapa ikaeleweka kwamba , hatupingi Mifuko ya hifadhi kushirikiana na serikali katika uwekezaji,lakini ni uwendawazimu tukiendelea kuiruhusu serikali kuifanya Mifuko hii ni mirija ya kuchota fedha pasipo kulipa! Tunamtaka waziri wa fedha  aliambie Bunge hili tukufu:
i)              Katika Bajeti ya mwaka 2017/18 wametenga kiasi gani maalum kwa ajili ya kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii?
ii)            Utaratibu wa utekelezaji wa malipo ukoje tofauti na makubaliano yaliyopita ambayo serikali haikuyatekeleza?
iii)           Viwanda 27 vinavyotarajiwa kujengwa na fedha za mfuko kila mfuko utachangia kiasi gani na kwa utaratibu gani wa mrejesho wa fedha za wanachama?
iv)         Viwanda husika vitajengwa wapi? Na vigezo gani vimetumika katika uchaguzi wa maeneo ya kujenga viwanda husika?
v)          Kama mradi wa viwanda tajwa unalipa, ni kwa nini sekta binafsi haijengi? badala yake zinatumika fedha za wanachama?

7.      DENI LA TAIFA  (Fungu 22)
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa linasimamiwa  na Sheria  ya Madeni , Dhamama na Misaaada ya Serikali ya Mwaka 1974 ((iliyorekebishwa  2004) na kulingana na vifungu namba  3 na 6  vya sheria ya madeni , dhamana na misaaada ya serikali ,1974. Waziri wa  Fedha  ndiye mwenye dhamana ya kukopa na kutoa dhamana kwa niaba ya serikali.
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa uchumi wetu. Kukua kwa Deni la Taifa kunasababisha bajeti ya Serikali kuendelea kuwa tegemezi na hivyo kushindwa kutatua kero za kiuchumi za wananchi. Kwa bahati mbaya wananchi wengi hawaelewi undani wa deni la taifa na athari zake katika maisha yao ya kawaida. Jambo la kusikitisha ni kwamba Serikali imekuwa ikitumia mwanya wa wananchi kutokufahamu kwa undani athari za deni la taifa kuendelea kukopa mikopo mikubwa yenye masharti ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, Kuendelea kukopa Kwa namna hiyo kunaendelea kuwabebesha walipa kodi wa Tanzania mzigo mkubwa wa madeni ambayo yanazidi kufanya hali ya maisha kwa wananchi iendelee kuwa ngumu kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kulipa madeni badala ya kuzitumia fedha hizo kugharamia miradi ya maendeleo.

7.1.      Mseto wa Deni la Taifa na Madhara yake Kibajeti
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Benki Kuu ya mwezi April, 2017 na Hotuba ya Bajeti 2017/18 inaonyesha kwamba Deni  la Taifa  limefikia  shilingi  trillion 50.8 (Ikumbukwe mpaka mwaka jana Juni 2016 deni la Taifa lilikuwa shilingi Trillion 41) .Deni la ndani likiwa  shilingi trillion 10.978. na deni la nje likiwa shilingi trillion 39.3 ( USD 17,578). Kwa kipindi cha mwaka mmoja deni la Taifa limeongezeka kwa  Dola za Kimarekani milioni 884.8 ( sawa na shilingi trilioni 2).
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba  kwa mwaka wa fedha 2016/17 kati ya  shilingi  8,671,038,922,510(Trillion 8.67) zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (Wizara  ya Fedha) shilingi 8,009,341,187,000 (Trilion 8) zilikuwa ni kwa ajili ya kulipia deni la Taifa.[4] Fedha zilizotumika kulipa deni,ni fedha nyingi kuliko  fedha zilizotumika kwa miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa deni la nje Serikali kuu peke yake  inadaiwa Dola za Kimarekani 13,792.9 (Tshs  Trillion 30.8). Kwa mwaka mmoja pekee nyongeza ya mkopo (deni la nje)  ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 455.4 ( Tshs Trillion 1. 018) Rejea Jedwali : External Debt Stock Borrowers katika Ripoti ya BOT ya Aprili, 2017.
Kwa upande wa Deni la Ndani:  Mpaka mwezi Mach, 2017 deni la ndani lilifika shilingi 10.976.8 bilioni. Ongezeko la mwezi la  shilingi  bilioni 327 na ongezeko la mwaka  kwa shilingi Trillion 1.53
Rejea Jedwali 5.1 :  Deni la Serikali (Government  Domestic Debt  Stock) 2007-2017 (Ripoti ya BOT mwezi April 2017)
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa deni la ndani wakopeshaji wakuu ni   Benki za biashara (41%) ,mpaka mwezi  Machi, 2017 wanaidai serikali  shilingi   4,578.8 bilioni (Trillion 4.578), wakifuatiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii,  (27%), ambayo mpaka Mwezi March  2017  wanaidai  serikali shilingi Trillion 2.995.3 , nyongeza ya shilingi Trillion 1.482 ukilinganisha na mwezi Machi, 2016.
Rejea Jedwali namba 5.4 (Ripoti ya BOT mwezi April 2017): Linaloonyesha mchanganuo wa deni  la ndani la serikali.

Mheshimiwa Spika, Imekuwa ni kauli za serikali kwamba deni la Taifa ni himilivu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumekuwa tukitoa tahadhari ya mara kwa mara kutokana na ukweli kwamba serikali imekuwa ikihamisha goli (Change of Goal Post) kila mara ili kujitafutia uhalali wa kuendelea kukopa huku Taifa likiingizwa kwenye matatizo makubwa. Katika hotuba yetu ya mpango wa Taifa wa mwaka 2017/18 tulilihoji hili pasipo kupatiwa majibu.Cha kushangaza ni kwamba kauli za uhimilivu zimeanza kutajwa toka 2008 wakati deni likiwa shilingi Trilion 7.8  mpaka 2017 deni likiwa limefika shilingi Trillion 50.8
Mheshimiwa Spika, Baada ya hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni za kipindi kirefu (2010/11; 2011/12; 2012/13, 2013/14, 2014/15; 2015/16 na 2016/17) hatimaye tahadhari juu ya uhimilivu wa deni la Taifa imetolewa na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali. Katika Taarifa yake ya mwaka iliyotolewa mwezi Machi, 2017 Mkaguzi Mkuu alikuwa na haya ya kusema :
1.   Deni la Taifa  lilianza kukua kwa kasi  tangu mwaka  2007/08 wakati nchi ilipopata msamaha wa madeni 
2.   Deni ya  Taifa limeongezeka kwa  149%  kwa miaka mitano iliyopita  bila kuhusisha madeni yaliyoachwa nje ya mseto
3.   Mikopo isiyo ya masharti nafuu yanaongezeka  kwa 17% . Kutoka shilingi  bilioni  7,835 mwaka  2014/15 mpaka shilingi  bilioni 9.155  mwishoni  mwa mwaka 2015/16 . Na mikopo yenye masharti nafuu kupungua . Mwaka 2012 mikopo ya masharti nafuu  ilikuwa 89% ya deni la nje  ikilinganishwa na  69%  mwishoni mwa mwaka 2015/16. Hii ni kusema kwamba  mikopo isiyo ya masharti nafuu (Mikopo ya Kibiashara) ilikuwa 31% ya deni la nje  mnamo mwezi Juni 2016 ikilinganishwa  na 11%  miaka mitano iliyopita.
4.   Ongezeko la madeni ya nje yenye masharti ya kibiashara unaongeza gharama za kuhudumia deni kadiri mikopo inavyoiva . Hii ni kutokana na vipindi vifupi  vinavyotolewa  katika kulipa deni ( mara nyingi miaka mitatu), riba kubwa  na muda mfupi wa deni kuiva!
5.    Taarifa ya uhimilivu wa deni la Taifa inaonyesha kwamba  kwa kuangalia gharama za kuhudumia  deni la Taifa ,ikilinganishwa  na mapato ya ndani ,gharama hizo ziko juu sana .Gharama  za kuhudumia  deni  zikichanganywa  na gharama  nyingine  kama vile  mishahara ya wafanyakazi ni gharama ambazo zinaiacha serikali na kiasi kidogo  sana cha fedha za kugharamia  miradi ya maendeleo  na huduma nyingine za kijamii.
6.   Kutokana  na rasilimali  kuelekezwa  katika kulipa madeni , ni kiashiria  kuwa serikali  itaendelea kutegemea mikopo ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Matokeo ya utegemezi huu ni kukua  kwa madeni ya ndani  na nje ambayo siyo  ya masharti nafuu. Mikopo husika pia inaendelea kuongeza gharama za kuhudumia deni.[5] ‘ ongezeko la mikopo isiyo ya masharti nafuu na mikopo ya ndani imesababisha gharama za kukopa kuwa juu, CAG  anatoa wito kwa watunga sera kuchukua tahadhari.

7.   Serikali kukopa ndani kwa wingi kunasababisha ‘msongamano’  wa sekta binafsi katika fedha  chache zitakazokuwa zimebaki katika mabenki. Kwa lugha nyingine CAG anasema kukopa kwa wingi kwa serikali katika mabenki ya ndani kunaua uwezo wa wafanyabiashara wa ndani kukopa! hata wakifanikiwa kukopa masharti yanakuwa magumu sana.

7.2.      Muundo na Usimamizi wa Deni la Taifa Kupitwa na Wakati
Mheshimiwa spika, Mkakati wa Taifa wa Madeni (NDS) wa mwaka 2002 uliandaliwa  kwa mazingira ya sheria ya Mikopo ya serikali , Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 (Miaka 43 iliyopita). Hali ya uchumi  na mazingira ya kuanzishwa  kwa sheria  na mkakati wa NDS yamebadilika  mno kutokana na mabadiliko ya kiuchumi ambayo yametokea.
Mheshimiwa Spika, Kutokana  na kupanuka  kwa wigo wa deni la Taifa  katika suala  la vipengele na mikopo mikubwa  ambayo imefanyika, sheria na miongozo inayosimamia  deni la Taifa haiko sambamba  na maendeleo hayo na vyombo vinavyotumika vimepitwa na wakati  na kwa sababu hiyo kufanya usimamizi wa deni la  taifa kuwa changamoto.
Mheshimiwa Spika, Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali anabainisha [6] katika ripoti yake aliyoitoa hivi karibuni kwamba wakati wa mahojiano na idara mbalimbali zinazosimamia deni la Taifa  chini ya wizara ya fedha ( idara ya uchambuzi wa sera (PAD), Mhasibu Mkuu wa Serikali (ACGEN), Idara ya fedha za Nje(EFD), Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Benki Kuu ya Tanzania amebainisha kwamba  mfumo uliopo sasa unaongeza uzembe katika uendeshaji,uratibu duni na  kutokuwa na taarifa za kutosha katika vitengo na taarifa sahihi  kupitia taasisi na kusababisha  kuwa na rekodi zisizosahihi  na  zisizojitosheleza  kuhusiana na deni !!haya ni maneno ya CAG !!!
Mheshimiwa Spika, katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza kulipa deni la Taifa linalokua kwa 149% kwa miaka 5. Bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato  au kusamehewa deni hili itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu. Hii ni kwa sababu uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa deni hata kidogo. Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa kuwa inakopesheka, na hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku holela.
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa  ya mikopo hii inakopwa katika soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.

7.3.      Mzigo Mkubwa wa Deni kwa Taifa (Debt Stress)
Mheshimiwa Spika, Matokeo ya uchambuzi  wa uhimilivu wa deni la Taifa  uliofanyika  mwaka 2015  na 2016  inaonyesha kuwa  uwiano wa gharama za kuhudumia deni na mapato ya  nchi (vyanzo vya ndani ya mapato) unakua kwa kasi sana [7]. Hili limejidhihirisha katika bajeti ya mwaka 2016/17 ambapo serikali kupitia vyanzo vyake vya ndani (mapato ya kodi, mapato yasiyo na kodi na mapato ya serikali ya mtaa) ilifanikiwa kukusanya shilingi trillion 13.5.[8] Fedha zilizotengwa kuhudumia deni la Taifa zikiwa shilingi 8,009,341,187,000 (Trilion 8). Na fedha zilizotengwa kwa ajili ya mishahara ni Trillion 7.2.
Mheshimiwa Spika,
 Mchanganuo hapo juu unatuonyesha kwamba Kwa mishahara na deni la Taifa peke yake fedha zilizotumika shilingi Trillion 15.2 huku makusanyo ya nchi yakiwa ni shilingi 13.5 Kwa tafsiri nyingine werikali ina uwezo wa kulipa mishahara na kuhudumia deni la Taifa tu! Huku ikiwa na upungufu wa shilingi Trillion 1.7. Bila mikopo serikali isingekuwa na ubavu wa kufanya shughuli yoyote ile!! Hii ni hatari
Mheshimiwa Spika, Hali kama hii inatarajiwa kujitokeza katika bajeti ya mwaka 2017/18 kwani kati ya shilingi Trillion 19 zinazotarajiwa kukusanywa kutokana na mapato ya Ndani , Shilingi trillion 16.6 zinatarajia kulipa misharaha na kuhudumia deni la Taifa.[9]
Mheshimiwa Spika, hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka huu sababu serikali imejiwekea maoteo makubwa ma makusanyo ambayo hayana uhalisia. Kama mwaka 2016/17 ilipanga kukusanya shilingi Trillion 29.53 ikaambulia kukusanya shilingi Trillion 20.7 (Pungufu ya Trillion 9) Ni miujiza gani itakayoiwezesha serikali kukusanya Trillion 31.7 kwa mwaka wa fedha 2017/18?!!

7.4.      Serikali Inakopa kwa Masharti ya Kibiashara Kulipa Mikopo: Maajabu!!!!!
Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Waziri,[10] inaonyesha kwamba  serikali inatarajia kukopa shilingi Trillion 7.763 kutoka soko la ndani  na nje kwa masharti ya Kiabiashara. Mikopo ya ndani  ikiwa shilingi  Trillion 6.168, ambapo  shilingi  bilioni 4.948.2 ni kwa ajili ya kulipia  dhamana za serikali zinazoiva.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa aina hii unachangia kwa kiasi kikubwa  kuongeza mzigo wa deni kwa nchi!  Serikali imeshindwa kulipa madeni kwa kutumiavyanzo vyake vya mapato!

Tabia hii inazidi kuota mizizi, kwani katika mwaka 2014/15 kati shilingi trilioni 1.8 zilizokopwa katika soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika kulipa madeni ya hati fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye miradi ya maendeleo. Hiki ni kiashiria cha karibu sana kwa serikali kufilisika.
Mheshimiwa Spika, Kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo au kwa uendeshaji wa kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha kutosha kuainisha maamuzi yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo ya kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.

7.5.      Imani ya Taasisi za Fedha za Kimataifa kwa Tanzania Imepungua
Mheshimiwa Spika, Imefikia hatua hata  kupata ‘hiyo mikopo ya biashara’  imekuwa shida. Katika bajeti ya mwaka 2016/17 serikali ilipanga kukopa kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara  shilingi trillion 2.1 ili kugharamia miradi ya maendeleo. Fedha hizo hazikupatikana kwa maelezo kwamba  soko la fedha za kimataifa kutokuwa na hali nzuri.
Mheshimiwa Spika, sababu inayotolewa na serikali haina ukweli. Ukweli ni kwamba taasisi za fedha za kimataifa zinakwepa kuikopesha serikali kwa sababu haina uhakika  juu ya uwezo wa serikali wa kulipa mkopo pamoja  riba kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imekuwa ikikwepa kufanyiwa tathmini/uhakiki wa uwezo[11] wa kukopesheka (Credit Rating)[12] kwa kipindi kirefu sasa,inashindwa hata na Rwanda!! sijui kuna siri gani inafichwa. Matokeo yake wanatarajia kupewa mikopo kwa huruma na hisani jambo ambalo halifanyika katika ulimwengu wa Biashara!
Mheshimiwa Spika, Ili kuweza kutanzua kutendawili na utata wa deni hili;
i)              Ni rai ya kambi rasmi ya  upinzani bungeni kurudia ushauri tulioutoa miaka minne na kulitaka Bunge liridhie na kumwelekeza Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi maalum (special audit) katika kitengo cha Deni la Taifa (fungu 22) ili kujua mikopo inayochukuliwa kila wakati inatumika kufanyia nini, na miradi iliyotekelezwa kama ni miradi ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
ii)           Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kuitaka serikali kama ambavyo tumesema miaka mitano iliyopita kulitaka  Bunge  litunge sheria  ili liweze  kudhibiti ukopaji na matumizi ya mikopo ya serikali. Vile vile tunapendekeza katika sheria hiyo iwe lazima kwa serikali kupata kibali kutoka katika Bunge  kabla ya kuweza kukopa. Hii inafanyika katika nchi nyingi  duniani kama vile Marekani na Uingereza.
iii)          Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali wakati wa majadiliano ya mikataba ya mikopo, kutumia utaratibu wa ‘Interest rate swap[13]’kutokana na ukweli kwamba sababu mojawapo inayosababisha deni kukua kwa kasi kunatokana ni kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu  na kuwa na riba ambazo zinabadilika mara kwa mara. Interest swapping maana yake ni kukubaliana kuweka kiwango cha riba kulingana na thamani ya shilingi ambayo inasaidia kuwa ni kiwango kilekile cha riba bila kujali kama thamani ya  shilingi itapungua  au itaongezeka. Hii inasaidia kufanya deni lisiongezeke kwa kasi kutokana na kupungua kwa thamani ya shilingi.
Mheshimiwa Spika, Ukirejea uchambuzi tulioufanya hapo juu kuhusiana na deni la Taifa na tishio lake katika mustakabali wa nchi hii, ni mwendawazimu pekee ambaye hataona hatari kubwa sana iliyo mbele yetu. Ni lazima sasa Bunge lako tukufu lichukue nafasi yake kuisimamia serikali kiukamilifu kama matakwa ya katiba yanavyolitaka ili kulinusuru Taifa.


8.   UPOTEVU WA MAPATO KATIKA SEKTA YA MADINI NA HADITHI ZA ‘MCHANGA’ ZA SERIKALI YA CCM
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni kumeibuka mjadala mpana juu ya rasilimali za nchi yetu baada ya sakata la Makinikia ama “Mchanga wa Dhahabu’.Katika hali ya kushangaza kuna upotoshwaji wa makusudi unaotaka kufanywa wenye dhamira ya kuonyesha kwamba ETI LEO kambi Rasmi ya upinzani Bungeni inapinga MAMBO ambayo kwa miaka mingi huko nyuma tumekuwa tukiyapambania dhamira ikiwa utajiri wa nchi hii uwanufaishe watanzania .
Mheshimiwa Spika,Nirejee hotuba yetu ya miaka ya karibuni  iliyosomwa na aliyekuwa waziri kivuli wa fedha na Uchumi  Ndugu James Fransis Mbatia wakati akiwasilisha HOTUBA MBADALA ya Bajeti  mwaka 2014/15  akiielezea serikali ya CCM juu ya upotevu wa MAPATO katika sekta ya Madini.  Naomba nirejee maelezo yake kama ifuatavyo:
i)             Taarifa za shirika la fedha Duniana (International Monetary Fund - IMF) zinabainisha kuwa kati ya mwaka (2008 – 2011) mapato ghafi ya dhahabu yaliongezeka toka Dola za Marekani millioni 500 hadi bilioni 1.5  kwa sababu ya kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu kuongezeka dhamani,  lakini mapato kwa serikali yalibaki kuwa  Dola za Marekani  milioni 100 kwa mwaka kwa wastani.Hali hii imesababishwa kwa kiasi kikubwa kwa msamaha wa kodi kwa makampuni (Corporate income tax holidays). Hakuna kampuni hata moja liliyolipa kodi hii hadi 2012. Taarifa ya IMF inaonesha pia kwa kuzingatia hali hii, hakuna mategemeo kuwa kipato kutokana na madini kitaongezeka hivi karibuni.

ii)           Mheshimiwa Spika, pamoja na kupitishwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, migodi iliyopo bado inaendelea kulindwa na mikataba iliyoingiwa kwa kutumia sheria iliyofutwa. Makubaliano ya kati ya Serikali na makapuni hayo inaonesha kuwa Tanzania inapoteza fedha nyingi sana, kwa mifano:

iii)          Taarifa ya Tume ya Bomani ilikadiria serikali ilipoteza  sh. bilioni 39.8  mwaka 2006/7 na sh. bilioni 59 mwaka  2007/8 kutokana na msamaha wa kodi ya mafuta tu (fuel levy exemptions)  kwa makampuni sita tu. Kufikia mwishoni mwa mwaka 2011, makampuni ya uchimbaji madini yalikuwa yanadai takribani Dola za Marekani miioni  274 kurejeshewa kutokana na msamaha wa kodi hiyo toka 2002. 

iv)         Makampuni yamepewa haki ya kumiliki  madini yake, ikiwemo haki ya kuuza hisa na mitaji yake bila kulipa kodi ya mapato (capital gains tax).

v)          Mikataba na sheria inawapa makampuni ruksa ya kutumia hasara wanazopata kufidia kulipa kodi.

vi)         Mwaka 2010, Tanzania Minerals Audit Agency (TMAA) ilikagua makampuni 12 na kugundua mapungufu/udanganyifu wa matumizi ya makampuni wa  Dola za Marekani milioni 705.8, ambapo serikali ilikosa  mapato ya Dola za Marekani 176 milioni. Hii ilikuwa mara ya kwanza TMAA kufanya ukaguzi, je, kwa miaka 10 kabla ya hapo serikali ilipoteza kiasi gani cha mapato?

vii)        Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Viongozi wa Kidini juu ya Haki za kiuchumi na Umoja (A report commissioned by the Interfaith Standing Committee on Economic Justice and the Integrity of Creation) iliyoitwa The One Billion Dollar Question iliyotokana na utafiti wa kutafuta mianya na kiasi cha upotevu wa mapato kwa nchi katika sekta ya madini, upotevu wa mapato ulikadiriwa kufikia  Dola za Marekani bilioni 1.07  kwa mwaka 2009/10 kwa njia ya misamaha ya kodi, ukwepaji kodi, uhamilishaji mitaji na vivutio vya kodi kwa uwekezaji.
viii)      Mheshimiwa Spika, upotevu huo wa  Dola za Marekani bilioni 1.07  (takribani sh trilioni 1.7) ilikuwa ni takribani  asilimia 17  ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka 2009/10.  Hoja hizo zote za kambi zilijibiwa kwa kejeli kubwa sana na wabunge walio wengi wa CCM zikiongezewa mbwembwe na mtoa hoja (WAZIRI mwenye dhamana ya Fedha) , Rais Magufuli akiwa sehemu yao!

Mheshimiwa Spika, Tukiwa mwaka wa pili wa utekelezaji wa bajeti ya serikali ya awamu ya tano ya CCM , bajeti  ambayo imevunja rekodi kwa kuwa utekelezaji mbovu kuliko uliowahi kutokea kwa upande wa miradi ya maendeleo  (0-30%),Huku Halmashauri zetu zikiwa HOI BIN TAABAN kwa kunyang’anywa mapato,  imeibuka hoja ya MCHANGA  WA DHAHABU. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  haihitaji Bunge lako tukufu kutumia misuli mingi kujadili ‘mchanga’ ambao kwa mikataba yetu NI MALI YA MWEKEZAJI.  Mchanga ambao hata kama wote ungegeuka dhahabu leo ,stahili yetu kama nchi ni  mrabaha wa asilimia nne tu!! Tunataka Bunge lijadili kuhusu DHAHABU yetu na madini yetu mengine yanayoibiwa kila uchwao NA SIO MCHANGA!
Mheshimiwa Spika, Tunataka Bunge hili lirejee makosa yaliyofanywa na wana CCM  wenzao mwaka 1997(KUJISAHIHISHA na kuwaomba Radhi watanzania)  walipoleta sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali  za fedha ( Financial Laws Miscellaneous Amendments Act 1997) ambayo ilifanya marekebisho makubwa katika sheria mbalimbali za kodi , tozo na ushuru mbalimbali kwa makampuni ya madini. Matokeo yaliyoisababishia nchi  kukosa mapato  ya kutosha  katika madini, matokeo yake nchi inashindwa kujitosheleza kibajeti ,inajiendesha kwa kukopa huko huko kwa wanufaika wa MADINI yetu na sasa deni la TAIFA limefikia shilingi Trillion 50.8
Mheshimiwa Spika, Tukifika hapo, TUTAMPOGEZA RAIS, lakini si kwa maigizo yanayofanyika sasa.

9.   WANANCHI WANATAKA BAJETI INAYOZINGATIA UKUAJI SHIRIKISHI – INCLUSIVE GROWTH
Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba mipango mbali mbali ya serikali imekuwa ikigonga mwamba kwa sababu mipango inakuwa mingi, fedha kidogo na hakuna mwendelezo (consistency). Jambo likipangwa kutekelezwa kwa miaka mitano , lisipofanikiwa tunarukia jambo lingine hata kama hatukufanya uwekezaji wakutosha, Matokeo yake hakuna kinachofanikiwa!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kwamba huwezi kuondoa umasikini  bila kuigusa sekta inayoajiri watanzania walio wengi! TUNARUDIA Kama Kilimo hakitaendelezwa, ina maana kwamba, itakuwa ni ndoto kuondoa 75% ya  Wananchi wetu katika lindi la umasikini. Sekta ya Kilimo imedumaa si kwa sababu nyingine yeyote zaidi ya Ukweli kwamba hakuna uwekezaji wa maana unaofanyika!
Mheshimiwa Spika, Ripoti zinaonyesha kwamba Shughuli za kiuchumi za kilimo zilikuwa kwa kasi ndogo ya asilimia 3.5 mwaka 2014/15 ikilinganishwa  na asilimia 2.3 mwaka 2025/16 .Mwaka 2017 kimezidi kudidimia  kufikia 1.7%...tusishangae mwaka 2018 tukiambiwa ukuaji wa sekta hii imefikia 0.5%!! ni wazi kwamba hakuna miugiza inayoweza fanyika kama serikali inatenga shilingi bilioni 3.3 kuhudumia watanzania milioni 30 , wakati huo huo  shilingi Trillion 1 zimelipwa ‘CASH’ kununua ndege ambazo zinahudumia watanzania 10,000[14].
Mheshimiwa Spika, Licha ya  kupuuzwa, bado sekta hii imeendelea kuongoza kwa kuwa na mchango mkubwa  katika pato la Taifa  kwa kuchangia kwa asilimia 29.0 ya pato la Taifa ikifuatiwa  na shughuli za ujenzi (13%), biashara na matengenezo (10.7%) na ulinzi na utawala 6.4%.
Mheshimiwa Spika, hata hotuba wa waziri [15]I naonyesha ni kwa namna gani serikali ya CCM haina mpango kabisa na wakulima wan chi hii (75% ya watanzania) kwa miradi inayopewa msukumo wa KIPEKEE kwa mwaka 2016/17-2020/21 kati ya vipaumbele 8, suala la KILIMO limezungumziwa katika kamradi kamoja ka uanzishwaji wa shamba la miwa  nakiwanda cha sukari,na pesa zilizotengwa ni shilingi bilioni mbili tu!! HII NI ZAIDI YA MZAHA!
Mheshimiwa Spika,
ILI Kilimo kiweze kupiga hatua:-
1.   Lazima tufanye utambuzi wa maeneo ya kipaumbele kwa Taifa
2.   Utambuzi wa  aina  ya mazao ambayo ni kipaumbele kwa Taifa  baada ya  kufanya utafiti [16]wa kina wa kujua   mahitaji ya soko; soko la ndani, kwenye ukanda wa Africa Mashariki, Afrika na Dunia ambayo yakifanyiwa uwekezaji maalum na ya kimkakati wa serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wakulima wadogo tutataweza ongeza pato la Taifa  na kupunguza umasikini lakini kubwa zaidi kusaidia ukuaji wa sekta nyingine!
3.   Lazima kuwe na mkakati maalum wa kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati ( Maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati)
4.   Miundombinu bora ya kuunganisha maeneo ya kimkakati na soko
5.   Ujenzi na Upanuzi wa mabwawa ya umwagiliaji (irrigation schemes) kwenye maeneo ya mkakati
6.   Hakikisha kuna pembembejeo za kilimo za kutosha sambamba na mbolea na mbegu kwa wakulima
Mheshimiwa Spika, Uchumi imara wa Brazil leo,unategemea KILIMO NA VIWANDA[17] Pamoja na mambo mengine ulianzia  katika uwekezaji wa zao la KAHAWA .Brazil ilitambulika Duniani kwa zao husika, hata mtikisiko wa uchumi ulipotokea miaka ya 1930 serikali ilihakikisha inafanya uwekezaji kupitia program maalum kuhakikisha zao husika halitetereki. Kilimo kilikwenda sambamba ya viwanda vidogo  na vya kati vya kuongezea thamani .  Hii ilikwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu  ya Barabara na reli kwa  ajili ya kuunganisha maeneo ya uzalishaji (yaliyotambulika kimkakati) na masoko.
Mheshimiwa Spika, Kukosekana kwa umakini kunaonekana kwenye  hotuba wa waziri wa fedha na mipango juu ya jukumu la Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB)[18]. Waziri anasema  katika mwaka 2017/18 Benki ya Maendeleo ya Kilimo itaboresha huduma za kibenki  kwa kuanzisha mazao maalum  kwa wakulima wadogowadogo  kulingana na mnyororo husika wa thamani  kulingana na vipaumbele vya Mikoa husika.. Na kwamba  Benki imepanga  kufanya maandalizi  ya kutoa Mikopo ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yaliyoainishwa  na Tume ya Taifa ya umwagiliaji.. vilevile benki imepanga kuwa jengea uwezo wakulima wadogowadogo, Wafanyakazi  wa Benki, benki nyingine  na Wadau mbalimbali  wa kilimo nk.
Mheshimiwa Spika, mbali na kwamba haijulikani hivyo vipaumbele vya mikoa vina uhusiano gani na Malengo Mapana ya Taifa ili kuelekeza Mikopo kwenye maeneo husika ni Ukweli usiopingika kuwa benki hii ni MFU.
Mheshimiwa Spika, Kwa wasiofahamu uanzishwaji wa benki hii mwaka 2009 , Benki hii ilikuwa shughuli ya pili kwa umuhimu  (Baada ya  shughuli ya  1 ya “kuongeza bajeti ya Serikali kwa ajili ya Kilimo kwanza “)Kati ya shughuli 15  za nguzo  ya pili ya Kilimo  Kwanza. Ilidhamiriwa   TADP ianzishwe ikiwa na mtaji wa dola za kimarekani  milioni 500 (kipindi kile  shilling bilioni 800, sasa hivi Trilion 1.1)….Fedha hizo zingepatikana iwapo  serikali ingetenda bilioni 100 kila mwaka …. Lengo likiwa ni kukopesha  wakulima  wadogo wadogo kwa masharti  na riba nafuu!! Benki hii muhimu iliishia kuambulia shilingi bilioni 60 tu mwezi April 2015.
Mheshimiwa Spika, Kwa nini tunaogopa kufanya utambuzi wa KITAALAM , kuwekeza, hatimaye  kurekebisha pale ambapo tunakosea pasipo kuchoka mpaka pale azma ya NCHI ikakapotimia?
Mheshimiwa Spika, Kwa hili, tuna la kujifunza kutoka India. Mapinduzi ya viwanda India ni Matokeo ya mkakati/mpango maalum wa miaka mitano mitano wa toka mwaka 1951 unaoendelea mpaka sasa, huku Mkakati mahsusi wa Maendeleo ya viwanda ukianza mwaka 1970. Iliwachukua zaidi ya muongo mmoja kwa India kugundua kwamba walikosea ‘kutaka kuanzisha viwanda vikubwa’ wakati rasilimali watu(ndani ya nchi) ya kuviendesha viwanda hivyo haipo. Kuziba mwanya huo wenzetu walianzisha mkakati maalum wa kutumia DIASPORA ambao wamekuja kuwa na mchango chanya sana katika mapinduzi ya Uchumi na viwanda![19]
Mheshimiwa Spika, Natambua kwamba kila nchi ina mazingira tofauti na fursa tofauti. Sisi kama Taifa tunajipambanua vipi? Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inasisitiza ,UKUAJI SHIRIKISHI wa uchumi hauwezi kuacha Maendeleo ya KILIMO .Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) akitoa utangulizi katika semina ya waheshimiwa  wabunge kuhusu kuanzishwa  kwa TADB alisema: “ili Tanzania  ifanikiwe  katika kupunguza  umasikini  na kujenga uchumi wa viwanda , ni lazima ifanye mapinduzi  kwenye sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Ni ukweli  unaouma kwamba, viwanda haviwezi kuwepo  bila malighafi. Lakini vilevile viwanda  (kama vitajengwa )  havitakuwa na msaada katika kupunguza tatizo la AJIRA  nchini  kama hatuna rasilimali watu ya ndani ya kutosha kuweza kuviendesha..Korea ya Kusini ilikuwa na POTENTIAL toka miaka ya 1970  ya kuanzisha viwanda  vya magari (automotive industries),lakini iliwachukua miongo miwili  kabla ya nchi kuibuka kama moja ya wazalishaji wa  magari toka bara la Asia. Waliwekeza katika rasilimali watu mahsusi kwa ajili ya viwanda husika kwa zaidi ya miaka 20.  Walipoibuka walipenya kiurahisi kabisa na kuwa washindani wakubwa katika uzalishaji wa magari!
Mheshimiwa Spika, Somo la Korea ya Kusini na India linatuambia kwamba BAJETI inayozingatia UKUAJI SHIRIKISHI wa uchumi unatutaka tuwekeze katika ELIMU na mafunzo kwa VITENDO. Na sio elimu kiujumla wake, bali mkazo uwekwe (toka ngazi ya msingi) kwenye maeneo ya kimkakati ambayo TAFITI zinaonyesha kwamba tukiwekeza ,tutapenya kwenye SOKO! Hivi Tanzania ya viwanda ambayo ndio Wimbo wa TAIFA wa kila mmoja wetu tumeihuisha vipi katika mipango yetu mbalimbali ya nchi ? Hivi nikiiuliza serikali leo,  kiwanda cha chuma cha liganga na mchuchuma kinatarajiwa kuendeshwa na nani?? Kwa manufaa ya nani?? Na kwa maandalizi gani?? Au ndio yale ya dhahabu, zinavunwa na wageni sisi tunaishia kugombana sababu ya MCHANGA
Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya sekta moja inategemea ukuaji wa sekta  nyingine. Viwanda sio mbadala (Substitutive ) wa Kilimo , bali ni sekta mbili  zinazotegemeana. Viwanda /Kilimo  haviwezi kukua  bila kukuza / kuboresha  sekta hizi mbili kwa pamoja . Kama Kilimo kitachukuiwa kuwa ni ‘ moyo’ wan chi, basi  viwanda  itakuwa ni ‘ubongo’.
10.               UCHAMBUZI WA KINA WA HALI YA UCHUMI WA TAIFA,
MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIAKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
10.1.  Siasa na Mwelekeo wa Serikali
Mheshimiwa Spika napenda watanzania watambue kwamba kama Taifa tumekamilisha Bajeti ya kwanza  ya Utawala wa awamu ya tano chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli. Ni wazi kwamba mwenendo wa Serikali kabla ya Bajeti yake hii ya kwanza  na baada ya  utekelezaji wa bajeti yake hii ya kwanza unatosha kutoa picha kamili juu ya aina gani ya Uongozi tulionao kama Taifa katika usimamizi wa Uchumi, Siasa na Maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla. Sitegemei kama bado kuna mtanzania anahitaji muda zaidi aweze kutafsiri Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Spika, Nathubutu kusema kwamba Taifa linapita kwenye kipindi kigumu cha utawala wa mtu mmoja, usioheshimu Katiba, Sheria, Taratibu na wala tamaduni zetu kama watanzania. Tunapita kwenye kipindi kigumu cha utawala wa mtu mmoja asiyeamini katika nguvu ya taasisi  za dola, Tunapita kwenye Utawala wa mtu mmoja asiyeamini katika Uhuru wa mihimili mingine kwa maana ya Bunge na Mahakama. Kwa kifupi ni utawala wa Kiongozi mmoja aliyejikusanyia mamlaka yote mkononi na mwenye kupenda kila kitu kwenye nchi hii awe yeye. Waingereza wanaita POPULIST LEADERSHIP.
Mheshimiwa Spika, Tabia ya Utawala wa namna hii umechambuliwa vizuri katika Makala ya Mwandishi na Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti Chuo Kikuu cha Central Europe university, Dr  Milkoz Harasz kwenye Jarida maarufu duniani la Washington post la Disemba 28, 2016, ambapo kwa kifupi naomba ninukuu maneno yake kuhusu  tabia za populist leaders  kwa faida ya Bunge lako na watanzania;
Mheshimiwa Spika, Mwandishi na Mtafiti na Milkoz Harasz,  anasema “ Populist govern by swapping issues as opposed by resolving them. They don’t mind being hated.Their two basic postures of defending and triumphing are impossible to perform without picking enemies.Populist can turn into peace nicks or imperialist depending on what they think could yield good spin that boost their support. Hypocrisy is in the genes of populists, in many countries they betray expectations of selfless strongman nd have lead to civic awekeny”..
Mheshimiwa Spika, Kwa tafsiri isiyo rasmi, Dr Miltoz anasema “ Kiongozi mpenda sifa na mwenye kujikweza hutawala kwa kufunika matatizo ya msingi badala ya kuyatafutia ufumbuzi, watawala hawa hawaoni shida  kuchukiwa.Dhamira zao mbili za kulinda utawala wao na kuwashinda wapinzani wao wanaamini hazifanikiwa bila kutengeneza maadui. Watawala wapenda sifa na wenye kijikweza  huweza ama kuwa wahubiri wa Amani ya uongo ama wakawa mabeberu madikteta kutegemea wanachodhani kinaweza kulinda matakwa yao.Unafiki ndio asili yao, hata hivyo katika nchi nyingi watawala wa namna hii hudhihirisha utawala wenye maslahi binafsi,  na mwishowe wananchi huwaelewa, huzinduka na kuasi’
Mheshimiwa Spika, Tabia hizo za viongozi wapenda sifa mara nyingi hutumia muda na akili nyingi kuzuia au kukabiliana na wakosoaji ndani na nje ya vyama vyao. Wanaposhindwa kukidhi matarajio waliyoyajenga kwa Umma hugeuka na kutumia mbinu za kikatili kwa mkono wa dola kutawala,na mara nyingi hukanyaga demokrasia na kuvunja katiba kama inavyonekana hapa nchini kwasasa ambapo kama Taifa tunashuhudia utawala wa Rais wetu ukikanyaga Katiba na misingi yake sambamba na kuminya demokrasia kwa hoja za kuleta maendeleo yasiyonekana.
Mheshimiwa Spika, Tawala za namna hii hutumia muda mwingi kutaka umma uamini kwamba demokasia ni kikwazo cha Maendeleo na kwamba Udikteta unaweza kuleta maendeleo(kituambacho hakijawahi kuonekana kwenye tafiti yoyote kuhusu maendeleo Tanzania).
Ni vema Rais wetu akaelewa na kuamini kwamba tawala anazochukulia mfano zina historia tofauti na Taifa letu, mataifa anayochukulia mfano watawala wake waliingia madarakani kwa mkono wa chuma, na sio sanduku la kura. Ni huzuni kuona Rais aliyetafuta madaraka kwa  kuomba kura nchi nzima mpaka anapiga ‘push up’ jukwaani kushawishi achaguliwe leo anatamani kutawala  kwa mkono wa chuma. Mwenendo wa mambo kwasasa unabainisha dalili zote za utawala anaozungumzia Dr milkoz Sarasz,
Hivyo, Tusigawanyike kwa  misingi ya itikadi za vyama katika vita hii kwani Taifa linaelekea kuparanganyika   tusiposimama na kukataa kwa sauti moja. Lazma wanasiasa, viongozi wa dini, wafanyabiashara, wanazuoni, wakulima na wafanyakazi wote kwa pamoja tusimame kama watanzania kupinga Taifa hili zuri kupelekwa kusikojulikana ambako Demokrasia inaelekezwa kuzimu, biashara zinapukutika, ukata unazidi na watanzania wanazidi kuzama kwenye lindi la umasikini na hofu ya dhidi ya utawala wao.
Mheshimiwa Spika, Haya ni maisha ambayo watanzania hawakutarajia, na hii ndio changamoto kuu kwa Bunge hili lenye dhamana ya mwisho kuhusu mustakabali wa Taifa hili kikatiba. (Parliament is the supreme organ of the state).

10.2.  Uchambuzi wa Bajeti na Hali ya Uchumi
§  Ukuaji wa Uchumi Usiopunguza Umasikini
Mheshimiwa Spika, Ni jambo lisilobishaniwa tena kuhusu kuongezeka kwa ukali wa maisha kwa kila mtanzania. Kwa muda mrefu, Serikali ya CCM imekua ikitumia kigezo cha ukuaji uchumi kupotosha kuhusu hali halisi ya uchumi wa taifa letu. Serikali ya awamu ya tano inatumia dhana ya ukuaji uchumi kwa asilimia 7% kama hoja ya kukaririsha watanzania waamini kwamba hali ya uchumi ni shwari na kwamba kiwango chetu cha ukuaji uchumi ni kikubwa ukilinganisha na nchi washindani wetu hususani Kenya ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 6%.
Mheshimiwa Spika, Kwanza, nivema tukafafanua kwamba uchumi wa Kenya ni  zaidi ya dola 65 billion, hivyo unapokua kwa asilimia6% ni sawa na ongezeko la dola 4bn , wakati uchumi wa Tanzania wa dola 45billion, unapokua kwa asilimia 7% ni sawa na ongezeko la dola 3bn  Hii ni tafsiri muhimu sana kujulikana kwa watanzania kwamba kwa mwaka uchumi wa Kenya unaongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko uchumi wetu badala ya kuwadanganya na takwimu za asilimia bila kuzingatia ukubwa wa uchumi wa kila nchi.
Mheshimiwa Spika, ni vema  ikaeleweka pia kwamba ukuaji huu wa uchumi kwa asilimia 7% haukuanza leo baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, ukuaji huu umekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, kwa maana tangu awamu ya tatu(rejea hotuba ya bajeti ya 2005/06), chini ya Benjamini Mkapa, uchumi ulikua kwa kiwango hicho cha asilimia7%, na ifahamike tu kwamba mwaka 2011, Ukuaji huo ulifikia asilimia 7.9.
Mheshimiwa Spika, Nivema ikafahamika kwamba changamoto tuliyonayo kama taifa kuhusu uchumi sio ukuaji tena, bali namna ya kufanya ukuaji huo utafsiri maisha ya watanzania. Ilitegemewa tangu kuingia awamu ya nne na sasa ya tano, kazi kubwa ingekuwa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unapunguza umasikini, badala yake imekua kinyume chake kwani awamu ya nne imeshindwa kupunguza idadi ya masikini, na mbaya zaidi awamu hii  inafanya vibaya zaidi kuliko awamu ya nne katika mkakati wa kupunguza umasikini kama inavyojipambanua kwenye ripoti mbalimbali za kiuchumi za kimataifa na kitaifa sanjari na hali halisi wanayopitia wananchi kwasasa.
Mheshimiwa Spika, Bado Uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unakuzwa na sekta zilezile, za Utalii, Madini, Huduma ya fedha,Mawasiliano, ambazo kwa hakika zinabeba watu wachache na ndio sababu ya uchumi kuendelea kukua bila kupuguza umasikini.Kwa zaidi ya muongo mmoja, Taasisi maarufu nchini inayohusika na tafiti za kiuchumi  ijulikanayo kama Research on Poverty Alleviation(REPOA) imebainisha wazi kwamba ili kupunguza umasikini ni sharti kukuza sekta ya kilimo katika dhana pana(mazao, uvuvi na ufugaji) kwa asilimia 8% mpaka 10%, na kwamba tukikuza Kilimo kwa kiasi hicho kwa miaka mitatu3 mfululizo tutakata umasikini kwa asilimia 50%.
Mheshimiwa Spika, Ni bahati mbaya kwamba tangu awamu ya tatu mpaka awamu ya nne kilimo kiliendelea kukua chini ya asilimia 4% na mbaya zaidi, katika mwaka wa kwanza wa serikali ya wamu ya tano inayojinasibu kama serikali ya masikini, kilimo kimekua kwa asilimia 1.7%, kiwango ambacho ni hafifu kupata kutokea tangu Utawala wa Mkapa na Kikwete.
Mheshimiwa Spika, Ndio sababu Kambi rasmi ya upinzani bungeni tunapenda watanzania watambue kuwa Rais John Pombe Magufuli ni adui wa wakulima wa nchi hii, bajeti hii tunayomaliza ya 2016/17 ruzuku ya mbolea ilitengewa billioni10 na katika Bajeti hii ya pili 2017/18 Ilipanga kutumia billioni15 kama ruzuku ya pembejeo ukilinganisha na billion 78 ya mwaka wa mwisho wa Kikwete  2015/16. Ni vema ikaeleweka kwamba moja ya tatizo kubwa katika sekta ya kilimo Tanzania ni matumizi duni ya mbolea kwani imesisitizwa kwenye ripoti mbalimbali za tafiti za uchumi na kilimo.Kwa  mujibu wa  Ripoti ya Umasikini na Maendeleo ya Binadamu 2014(Poverty and Human Development 2014),  Matumizi ya Mbolea Tanzania ilikuwa ni 9kg kwa ekari1 wakati nchi zenye chumi ndogo kama Malawi, wakulima wameweezeshwa kiasi cha kutumia 29kg kwa ekari1 na nchi zilizpiga hatua zaidi kwa kilimo kama China, ekari 1 wanatumianzaidi ya  260kg.
Kama tathimini hii ya matumizi ya 9kg kwa ekari1 Tanzania ni utafiti wakati ambapo serikali ya awamu ya nne walau ilikuwa ikitenga fedha kiasi cha kuonekana kwenye ruzuku ya mbolea, watanzania na hususan wakulima wanapaswa kujiuliza leo, ambapo Serikli inatenga 10billioni kutoka 78billioni hali itakuwaje?.
Mheshimiwa Spika, Ni vigumu kwa Serikali ya Tanzania kufanya mapinduzi makubwa kiuchumi yenye kupunguza umasikini bila kukuza kilimo katika dhana pana(mazao,ufugaji na uvuvi). Kwa mujibu wa Ripoti ya USAID ya 2014, asilimia  70% ya watanzania wanategemea Kilimo, na kati yao asilimia 75% ni wanawake. Hivyo masikini wakubwa Tanzania ni wanawake ambao ni asilimia 75% ya watu wote wanaotegemea kilimo, hiyo mwenendo wa sasa ambapo Bajeti ya Miradi ya kilimo katika mwaka huu wa fedha inatekelezwa kwa asilimia 2.2%, rekodi ambayo haijapata kutokea tangu Uhai wa Taifa hili ni ishara tosha kwamba Serikali hii haina mpango na masikini watanzania, na tabia ya Mhe Rais kujinasibu kuwa ni Rais wa masikini ni sawa na dhihaka kwa masikini wa Tanzania.
10.3.   Mkwamo wa Uchumi na Ongezeko la Ukata Nchini
Mheshimiwa Spika, imekuwa changamoto kubwa hata miongoni mwa wachumi kuhusu hali ya uchumi nchini hasa inapoonekana biashara nyingi zinafungwa, walipa kodi wakubwa kama TBL , Benki za biashara , Kampuni za simu zote zinatangaza hasara. Manunuzi ya nje(imports) kuzidi kushuka, sekta ya nyumba(real estate) inazidi kuporomoka, kampuni zinazidi kupunguza wafanyakazi, soko la mitaji(stock market) linazidi kufanya vibaya, ukata kwenye uchumi (decline in liquidity) unazidi kuongezeka, lakini bado serikali inatangaza uchumi kuwa ni imara na kwamba mwaka 2016 inakadiriwa kukua kwa asilimia 7% na kwamba utaendelea kukua kwa asilimia 7.2% mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, Ipo haja ya kuchunguza uhalisia wa takwimu zetu kuepuka kujenga uchumi hewa kwa takwimu za kupika , ndio sababu IMF hivi karibuni wametahadharisha kuwa mwenendo mbovu wa sera za kibajeti na kutokutabirika kwa utawala huu kutasababisha kuzorota kwa uchumi katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza hilo kwani hata ripoti za tathimini ya Uchumi ya robo mwaka inayotolewana Benki kuu(Quartely Economic review) inaonesha kuwa sekta zote kiuchumi zina hali mbaya, Rejea ripoti ya robo ya kwanza, robo ya pili na hata robo ya tatu .
Mheshimiwa Spika, Sekta ya fedha ni kichocheo kikubwa kwa sekta binafsi ambayo duniani kote ndio injini ya uchumi, kwa kigezo cha ulinganisho wa mikopo kati ya 2015/16 na 2016/17, takwimu za ripoti ya mwisho ya BoT ya Disemba 2016, iliyopo tovuti ya Bank Kuu inaonesha kwa mfano; Mikopo kwa sekta ya usafiri na Mawasiliano; mwaka 2015/16 ilikua kwa asilimia 33.1% ukilinganisha na ukuaji wa asilimia -0.1% kwa mwaka 2016/17, mikopo sekta ya uzalishaji viwandani mwaka 2015/16 ilikua kwa asilimia 22.3% ukilinganisha na asilimia 8.8% mwaka 2016/17. Mikopo ya Biashara ilikua kwa asilimia 16% mwaka 2015/16 ukilinganisha na asilimia -4.1% mwaka 2016/17. Mikopo kwa sekta ya ujenzi ilikuwa kwa asilimia 12.3% mwaka 2015/16 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia -4.15%. Ripoti zote za Bank Kuu kuhusu tathimini ya uchumi katika mwenendo wa mikopo kwa sekta mbalimbali inaashiria kuparanganyika kwa uchumi baada ya kuingia kwa awamu ya tano.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya robo ya pili ya tathimini ya kiuchumi inayotolewa na Bank Kuu BoT(Quartely Economic Reviews) ambayo ni ripoti ya robo ya pili ya utekelezaji wa bajeti hii ya 2016/17 inayoanza katika robo ya tatu ya tathimini ya uchumi ya BoT  iliyoanzia Oktoba mpaka Disemba , 2016, inaonesha kuwa ujazo wa fedha kwenye uchumi(M3) uliongezeka kwa kiasi cha billion 645.1billions  ukilinganisha na kiasi cha 3501.2 billions katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16 sawa na upungufu wa ujazo wa fedha kwa asilimia 540%.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonesha wazi kwamba nchi ina hali mbaya isiyovumilika na inayohitaji mpango wa maalumu kuokoa uchumi huu kwa maana ya Stimulus package kama tulivyofanya mwaka 2008 kufuatia mtikisiko wa uchumi duniani kwani hali ya sasa ni mbaya kuliko 2008, Kwani Ripoti hizo za Benki Kuu zinaonesha wazi kwamba kushuka huko kwa ujazo wa fedha kwenye uchumi kunatokana na kushuka kwa kiwango cha mikopo kutoka Benki za biashara kwa sekta binafsi, na hivyo kuyumba kwa sekta bbinafsi ambayo kimsingi ndio injini ya uchumi.Na ndio sababu Benk Kuu ya Tanzania, kama msimamizi wa sera ya fedha, ikachukua hatua mbili kama namna ya kutafuta ufumbuzi wa ukata wa fedha kwenye uchumi(liquidity tightness). Hatua ya kwanza ni ile ya tangazo la kupunguza riba(credit discount) kwa mikopo ya Bank kuu kwenda bank za  biashara kutoka riba ya asilimia 16% mpaka riba ya silimia 12%. Ikafuatiwa na tangazo la Bank Kuu la kupunguza dhamana za Bank za biashara zinazowekwa bank kuu kutoka asilimia 10% mpaka asilimia 8%
Mheshimiwa Spika, Hatua zote hizo zilichukuliwa kwa lengo la kukabili ukata kwenye uchumi kwa kuhakikisha sekta binafsi zinapata mikopo na kuchangamsha biashara kwenye uchumi na hivyo kukabili ukata mkali unaokabili uchumi kwasasa.
Hata hivyo, pamoja na juhudi zote hizo za Bank Kuu kwa kutumia sera ya fedha(Monetary Policy), bado ukata umebaki kuwa tatizo kwenye uchumi ikiwa ni kielelezo kwamba mzizi wa tatizo la uchumi kwa sasa chimbuko lake sio sera ya fedha( monetary policy)bali sera ya bajeti na mazingira ya biashara kwa ujumla(fiscal policy&Business environment).
Mheshimiwa Spika, Tatizo  la uchumi kwasasa sio benki kukosa fedha kukopesha sekta binafsi, tatizo ni Serikali imeshindwa kujenga mazingira rafiki kwa biashara na wawekezaji kwa ujumla.wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje  kwa ujumla wanakabiliwa na mazingira magumu kibiashara ndio sababu kiwango cha mikopo isiyolipika(Non Performing loans-NPL) kimezidi kuongezeka kwa kiasi ambacho hakijawahi kutokea kwa zaidi ya miongo miwili.Kwa mujibu wa ripoti ya BoT, kiwango cha mikopo isiyolipika kimefikia zaidi ya asilimia  10  ambapo wastani ni asilimia 5
Mheshimiwa Spika, Hii ni ishara mbaya sana kwa sekta binafsi ambayo ndio inapaswa kuwa injini ya uchumi katika uchumi wa soko.Sio kwamba wafanya biashara hawa wanapenda kushindwa kulipa mikopo hiyo bali mazingira ya biashara ni mabovu na hivyo kusababisha wafanyabiashara kuogopa kukopa kwajili ya biashara na pia mabenki kuongeza urasimu wa kutoa mikopo kwa hofu ya mikopo isiyolipika kutokana na mazingira mabovu ya kibiashara ambayo msingi wake ni sera duni za kodi na utawala unaoendesha nchi kwa amri zaidi ya sheria. Na ndio maana hata ripoti ya mwaka 2017 kuhusu urahisi wa kufanya biashara(EASY OF DOING BUINESS) inayotolewa na Bank ya Dunia, Tanzania bado iko nyuma ya Kenya, Uganda na Rwanda ambao ndio washindani wetu kibiashara.
10.4.  Wafanyabiashara Washirikishwe Kutatua Mgogoro wa Kiuchumi
Mheshimiwa Spika, Tangu awamu ya tatu chini ya Benjamini Mkapa kiliundwa chombo kinaitwa Tanzania National Business Council-TNBC, Chombo hiki ni jukwaa muhimu kati ya Serikali na wafanyabiashara nchini, na kimuundo kinaongozwa na Rais kama Mwenyekiti.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na umuhimu wa chombo hiki kwajili ya kukutanisha na kugonganisha fikra kuhusu majibu ya uchumi na biashara nchini, Mhe Rais hakuwahi kuitisha chombo hiki kwa zaidi ya mwaka mmoja, na hata baada ya kuitisha baada ya shinikizo kubwa, bado maoni ya wawekezaji na wafanyabiashara yameendelea kupuuzwa.  Ni wito wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kumtaka Mheshimiwa Rais na wataalamu wake  atumie jukwaa hili kusaka majawabu ya hali mbovu ya kibiashara inayoendelea nchini kwa kuchanga mawazo ya bongo za pande zote, wafanyabiashara na wataalamu wake. badala ya kusikia upande mmoja wa watendaji wake ambao wengi ni wanataaluma kutoka vyuo vikuu ambao kwa kiasi kikubwa hawajawahi kuwa practioners.


10.5.  Uamuzi wa Kuondoa Fixed Deposits za Serikali kwenye Benki za Biashara .
Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuachana na Sera na Mipango ya kubahatisha au majaribio kwenye Uchumi. Itambukwa mwaka 2016 mwanzoni Serikali ilifanya uamuzi wa kuondoa fedha zake zote zilizokuwa zikiwekwa kwenye benki za biashara na kuzipeleka benki kuu BoT kwa hoja kwamba benki za biashara zinafaidi fedha hizo za serikali kwa kuzifanyia biashara.
Mheshimiwa Spika, Baadaye mwaka huu, Serikali hiyohiyo imehamasisha benki za biashara zikakope fedha benki kuu kwa riba punguzo kutoka asilimia 16% mpaka asilimia 12%. Kambi rasmi ya upinzani tunajiuliza, hivi ni akili gani iliyoamua kuondoa fedha za serikali kwenye benki za biashara ambako zilikuwa zinazalisha riba ya mpaka asilimia 15% na kuzipeleka benki Kuu ambako hazizalishi chochote? Kama awali Serikali ilikuwa inaweka fedha zake benki za biashara kwa riba ya asilimia 15% ni sawa na kusema serikali ilikuwa inazikopesha benki za biashara fedha yake kwa riba ya asilimia 15% lakini sasa imeamua kuzikopesha kwa mlango mwingine benki hizo hizo kwa riba ya asilimia 12%. Kwa utaratibu wa uliofutwa ni serikali ilikuwa inapata riba ya asilimia 15 na sasa umeletwa utaratibu unaoitwa bora ambapo sasa serikali itapata riba ya asilimia 12%. Akili iko wapi katika jambo hili?


10.6.   Ni wajibu wa Serikali Kutekeleza Bajeti iliyoidhinishwa na Bunge

Mheshimiwa Spika, Jukumu la kujadili na kuamua kuhusu Bajeti ni  moja ya majukumu muhimu kabisa ya Bunge hili tukufu ambalo tumepewa kikatiba. Jukumu la Serikali katika Bajeti ni utekelezaji tu. Na ndio maana mwaka 2015, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Bajeti kwa lengo la kuhakikisha nidhamu na ufanisi katika kupanga, kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa Bajeti.
Mheshimiwa Spika, Ni bahati mbaya sana, kama nilivyoeleza awali kwamba Utawala huu unaongoza kwa kutokuheshimu sheria na Katiba, makosa hayo yanajidhihirisha pia katika utekelezaji wa bajeti hii ya kwanza katika utawala wa awamu ya tano.Serikali  kwa agizo la Mhe Rais imetumia fedha za bajeti hii kutekeleza baadhi ya mambo ikiwemo  kuhamishia Serikali Dodoma,mambo ambayo hayakupitishwa naBunge kwenye Mpango wa Bajeti wa 2016/17.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani haina tatizo na dhamira njema ya Serikali kuhamia Dodoma au utekelezaji wa mpango wowote kwajili ya huduma kwa wananchi. Tunachosisitiza ni kwamba uendeshaji wa Serikali lazma ufuate sheria na taratibu. Uendeshaji wa Serikali usiofuata Sheria na taratibu ni utawala wa fujo.Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015( The Budget Act 2015, Sect 34), inasisitiza wazi kwamba Serikali haitaruhusiwa kutekeleza mradi wowote ambao hakupitishwa na Bunge kwenye Mpango wa bajeti.Maamuzi ya namna hii yanapora mamlaka ya Bunge letu, na ni utovu wa nidhimu wa hali ya juu wa Serikali hii kwa Muhimili wa Bunge ambao kikatiba ndio Muhimili Mkuu wa dola (Supreme organ of the State).
Mheshimiwa Spika, Naomba kwa msisitizo, nitumie maneno yaliyotumiwa na Jaji Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya arusha aliyetoa dhamana kwa Mhe Godbless lema , akionekana kukemea tatizo la Mahakama kuingiliwa, alisema “Ni lazma Mahakama zionee wivu mamlaka yake”.
Mheshimiwa Spika, Hilo ndilo neno ningependa Bunge pia tulitumie kama sote tunajitambua bila kujali tofauti zetu:  Kwamba ni lazma Bunge lionee wivu Mamlaka yake . Na lisikubali Mamlaka yake yapokonywe na Serikali au Mamlaka nyingine ya dola. Ni lazma tuhakikishe Serikali inatekeleza majukumu yake ndani ya  ukomo wa mamlaka yake na sio vingineyo kwani kuacha Serikali ifanye maamuzi ya Bunge, itafanya pia ya Mahakama na kuingiza taifa hili kwenye kile waingereza wanaita ‘Kangaroo Governance”. Kwa maana ya Utawala usio na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Bajeti ndio kipimo cha uwezo wa uongozi kutimiza wajibu wake kwani ni bajeti inayotafsiri ahadi za Ilani ya Chama kilichopo Madarakani katika kufikia Dira ya Taifa, sanjari  na ahadiMgombea Urais. Mafanikio ya Rais yeyote yanapimwa katika namna anavyomudu kutekeleza bajeti na sio idadi ya purukushani au ziara za kushtukiza na matamko yasiyo na ukomo kila kukicha na yasiyo ya kimkakati kuweza kutolewa na Ofisi kuu ya Nchi.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti 2016/17, inaonesha wazi kwamba miradi ya maendeleo iliyotekelezwa ni asilimia 38% ya makadirio ya Bajeti. Kwamba, wakati makadirio ya matumizi kwa miradi ya maendeleo yalikuwa billion 11,820,503, Serikali imefanikiwa kutekeleza kwa kutoa billion 3,647.7 na fedha za nje billioni907. Ni wazi kwamba huu ndio msuli wa Rais wa awamu tano unapoishia, na bila shaka Mhe Rais atakuwa amejua kipimo cha uwezo wake kuwa ni asilimia 38%, tofauti na mafikirio makubwa aliyokuwa nayo kuhusu uwezo wake wa kutekeleza mipango katika Taifa hili kulinganisha na watangulizi wake.Utekelezaji huu wa asilimia 38% unamfanya Rais wetu atambue nafasi yake kuwa yeye ni rais wa kawaida sana ukilinganisha na watangulizi wake kwani miradi ya maendeleo tangu awamu ya tatu imekuwa ikitekelezwa kwa takriban asilimia 40% Na hii ndio changamoto kwake.
10.7.  Uwezo wa Kujitegemea Kiuchumi na Kibajeti
Mhe shimiwa Spika, Uchambuzi wa Bajeti hii unaonesha wazi kwamba chini ya CCM Taifa hili litasafiri zaidi ya karne bila kufikia uwezo wa kujitegemea. Kwa mfano, katika Bajeti ya 2016/17 , Makusanyo ya Kodi yalikuwa trilioni 11.6 dhidi ya makisio ya trilioni 15, na makusanyo yasiyo ya kodi yalikuwa trilioni 1.6  dhidi ya makisio ya trilioni 2.69 na makusanyo toka serikali za mitaa yalikuwa billion 399 dhidi ya makisio ya billion 665.
Mheshimiwa Spika, Wakati uwezo wa Serikali yetu yenye umri zaidi ya nusu karne ukiwa kiasi hicho, kiasi cha deni lililoiva mwaka 2016/17 ilikuwa trilioni 8 wakati msahahara peke yake ikiwa trilioni trilioni7?. Hii maana yake katika mwaka uliokwisha, makusanyo yetu jumla ya ndani trilioni 13.5 wakati hitaji la mshahara na deni peke yake likifika trilioni 15. Ni mazingira haya Rais Uhuru wa Kenya ataendelea kutukujeli kuwa Tanzania bado tuna serikali ambayo sio tu inakopa kugharimia miradi yote ya maendeleo bali inakopa kujiendesha kwa matumizi ya kawaida na hata mishahara ya walimu na watumishi haijimudu bila kukopa.
Mheshimiwa Spika, Hali ni hiyo pia katika Bajeti ya 2017/18, kwani Bajeti hii imekosa ubunifu wa vyanzo vya mapato, na hivyo itaendeleza aibu ya kushindwa kujimudu hata kugharamia mishahara ya watumishi kwani hakuna ubunifu wowote katika vyanzo vya mapato.  Ni Bajeti iliyojaa rhetorics. Imekosa ubunifu katika vyanzo vya mapato, imekosa mkakati wa kuchochea sekta binafsi iweze kuchochoa uchumi, haisemi kwa utekelezaji wa bajeti hii itatengeneza ajira ngapi wala haisemi bajeti hii itapunguza umasikini kwa kiasi gani ili iweze kupimika mwisho wa siku.Kifupi ni bajeti ya mazoea, iliyojielekeza kwenye vyanzo vya mapato kwa mazoea na hivyo kukosa nyongeza ya ubunifu.
Mheshimiwa Spika, Nasisitiza kuwa Bajeti hii ni ya mazoea kwasababu maeneo yaliyongezwa kodi ni yaleyale ya miaka yote. Bajeti hii haisemi lolote kuhusu mkakati wa kumwinua wakulima ambao ni70% ya watanzania hasa katika mazingira ya sasa ambapo kilimo kimeporomoka kufikia ukuaji wa 1.7%, zaidi kwenye kilimo imebaki na msimamo wa kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka 78bn ya mwaka 2015 mpaka 15bn ya mwaka 2017/18.Haina chochote kuhusu bank ya wakulima, iliyoanzishwa mwaka 2015 kwa kusudio la mtaji wa 1trilioni na kukopesha wakulima 200,000 kwa mwaka lakini sasa imeishia kukopesha wakulima 3700 na mtaji wa billion 60 tu kwa miaka3.
Mheshimiwa Spika Bajeti hii haisemi lolote kuhusu kujenga na kuimarisha wajasiliamali wadogo na wakati ambao ni asilimia 40% ya ajira zote.
10.8.  Kukwama kwa Mikopo toka nje na Utekelezaji wa Miradi ya Kibajeti
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania imekuwa kinara wa kupata misaada na mikopo nafuu toka nje kuliko Serikali zote ukanda huu wa kusini na Mashariki ya afrika. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Official Development Aid (ODA) ya mwaka 2013. Kwa mujibu wa Ripoti hii, Tanzania tunayokaririshwa kuwa nchi ya Amani na Utulivu imekuwa ikipata misaada (Grants) kuliko nchi zilizo vitani au zisizo na usalama kabisa duniani kama Kongo DRC na Sudan. Hii ni moja ya aibu kubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mwenendo huo wa miongo kadhaa ya Taifa hili kupata upenedelo huo wa misada zaidi ya kiwango cha nchi zilizo vitani, bado misaada hiyo haijaweza kuleta tija ya maana kiuchumi zaidi ya kujenga Serikali yenye akili tegemezi badala ya kujitegemea.
Serikali hii ya awamu ya tano, kuanzia kwenye hotuba ya Rais bungeni pamoja na hotuba ya wizara ya Bajeti 2016/17 lisisitiza kwa kiasi kikubwa dhana ya kutotegemea nje ingawa bajeti yake ni tegemezi kuliko ile ya awamu ya nne.
Kwa mfano, Katika Bajeti ya mwisho ya awamu ya nne, kiwango cha misaada na mikopo nafuu toka nje ilikuwa trilioni 2.6, wakati bajeti ya kwanza ya Rais John Pombe Magufuli anayejitangza kutotegemea nje, misaada na mikopo nafuu ilikuwa 3.6trilioni. Huu ni ushahidi wazi kwamba serikali hii inategemea nje kuliko Serikali iliyopita.
10.9.  Vita dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Transparency Inernational kwa mwaka 2016 kuhusu tathimini ya hali rushwa na ufisadi duniani,Tanzania ni miongoni mwa nchi tano katika Afrika ambazo ziliguswa mahususi katika Ripoti hiyo, Kwa kifupi, ushauri wa jumla kuhusu nchi hizo za Kenya, Nigeria, South Africa, Ghana kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi, ripoti hiyo inasema kwamba: “African Leaders that come to Office on an anti corruption ticket, will need to live up their pledges to deliver corruption free services to their citizen, they must implement their commitments to their principles of governance, democracy and human rights. This includes strengthening the insitutions that hold government accountable as well as electoral systems that allow  citizens to either re elect them or freely chose an alternative.
Mheshimiwa Spika, Kwa tafsiri isiyo rasmi, Ripoti hiyo inasema kwamba “ Viongozi wa Afrika walioingia madarakani kwa tiketi ya vita dhidi ya ufisadi wanapaswa kuishi ahadi zao kuhakikisha rai wanapata huduma bila rushwa,na ili kufikia hatua hiyo ni lazma Viongozi hao wahakikishe wanatimiza wajibu huo kwa misingi ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu. Hii ni pamoja na kuhakikisha Taasisi zinazosimamia uwajibikaji wa serikali zinaimarishwa  pamoja na mifumo ya uchaguzi inaimarishwa kuhakikisha wananchi wanaweza kuirudisha serikali hiyo madarakani au kuchagua serikali mbadala kwa hiari yao”
Mheshimiwa Spika, Hii ni ripoti Muhimu sana kwa utawala huu na ni vema Serikali hii ijenge tabia ya kusikiliza taasisi za kitaalamu zinasema nini kuhusu utawala wake. Kambi rasmi ya Upinzani inaunga mkono ripoti hii kwamba ili vita dhidi ya ufisadi iwe endelevu na yenye mafanikio ni lazma kama nchi tujenge taasisi imara za kuisimamia Serikali likiwemo Bunge.
Mheshimiwa Spika, Hali ya sasa ambapo Serikali inadhoofisha bunge kwa kuliweka gizani na kwa miongozo isiyokwisha toka Ikulu, Hali ya sasa ambapo Ofisi ya CAG inabanwa kibajeti ishindwe kutimiza majukumu yake ya ukaguzi ili kulisaidia Bunge kuisimamia Serikali, Hali ya sasa ambapo vyombo vya habari vinabanwa kuhakikisha vinaandika habari tamu kwa serikali, Ni mfano mbaya kabisa na ni kielelezo tosha kwamba serikali haipo serious katika vita dhidi ya Ufisadi nchini kwani kinachoendelea ni serikali inaharibu yenyewe na inataka ijikosoe yenyewe na kujisimamia yenyewe.

10.10.              UTAWALA BORA UNAVYOCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, Ni aibu kwamba ingawa Washirika wa Maendeleo toka nje wamendelea kupunguza kwa kasi kiasi chao cha mikopo na misaada, bado bajeti za Serikali ya CCM zimendelea kuongeza kiasi cha utegemezi wa mikopo na misada toka huko bila kutatua msingi wa tatizo la kukwama huko. Tangu mwaka 2014/15 Nchi za Ulaya zimekuwa kwenye mahusiano mabovu na taifa letu kutokana na Serikali kushindwa kusimamia misingi ya utawala bora na Demokrasia kama sharti lao  muhimu katika ushirikiano. Ni katika msingi huo Tanzania imekosa fedha toka Millenium Challenge Accounts (MCC II) zaidi ya 1trilion, ambapo nchi kama Ghana wamendelea kupata.
Mheshimiwa Spika, Kwasababu ya kuharibu uchaguzi mkuu zanzibara, Sheria mbovu ya makosa ya  mitandao, kuliweka bunge gizani, Kuzuia mikutano ya kisiasa kwa vyama kinyume cha Katiba, yote hii imesababisha mahusiano mabovu kati ya Tanzania na nchi washirika wa maendeleo na ndio sababu ya kukwama kwa mikopo nafuu kutoka mataifa hayo pamoja na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, Kibaya zaidi wakati Serikali ikikwama kupata mikopo nafuu kutokana na udikteta, bado pia imeshindwa kupata mikopo ya kibiashara kwasababu ya uzembe na kutojipanga. Nchi za Kenya na Rwanda imekuwa rahisi kupata mikopo ya kibiashara toka nje kupitia Eurobond/International Bond  kwasababu zimeshakikiwa kuhusu uwezo wake wa kukopa.
Mheshimiwa Spika, Tanzania tangu zama za Mhe Mkulo kama waziri wa fedha mpaka Mgimwa na baadae Saada Mkuya na sasa Dr Mpango inapiga stori za kufanyiwa uhakiki wa uwezo wake kukopesheka(CREDIT RATING).Huu ni mfano wa namna tulivyo na Serikali isiyo na akili ya kibiashara. Duniani kote kuna Agency tatu zinazofanya kazi hii, ambazo ni Moodys, Standard&Poor na Fitch, kwa muda mrefu kumekuwa na mazungumzo yasiyokwisha kuhusu kampuni ya Moodys kufanyia uhakiki uchumi wetu lakini hakuna kinachoendelea. Ni vema Serikali ikakamilisha mazungumzo hayo yasiyokwisha kwani uwezekano wa Tanzania kuendelea kupata mikopo ya kawaida toka nje umezidi kufifia.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza hili kwani hata ripoti ya IMF ya Januari 9,2017, kuhusu mwenendo wa uchumi wetu imesisitiza hili, kwamba ni lazma Serikali ihakikishe inapata mikopo toka nje ili kutekeleza miradi mikubwa ya kibajeti kwakuwa ukosefu wa fedha hizo kwenye miradi hiyo ni moja ya sababu za ukata kwenye uchumi kwani imepunguza mzunguko wa fedha kwa kiasi kiubwa nchini.
10.11.              Miradi ya Kimkakati katika Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kiasi kikubwa cha rasilimali lakini kwasababu ya ukosefu wa uongozi wenye maono bado rasilimali hizo hazijaweza kuliondoa taifa kwenye lindi na umasikini. Idadi ya watanzania masikini imezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka badala ya kupungua.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Poverty &human Development, inaonesha kwamba tangu kama taifa tuanze marekebishoya Uchumi (economic restructuring) katika miaka ya 1990, umaskini Tanzania ulikuwa asilimia 39% wakati idadi ya watu ilikuwa milioni 25, sawa na masikini milioni 9.750,000 na sasa kiasi cha umasikini ni asilimia 28, wakati idadi ya watu imefikia milioni 48, sawa na masikini milioni13.44.
Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa ya kuendelea kuongezeka kwa masikini ni sera mbovu mtazamo finyu wa CCM katika kujua mahitaji ya Taifa na namna ya kuweka vipaumbele ili kufikia malengo. Badala yake imebaki chama kilekile kinabadilisha majina ya awamu na watawala bila kubadili mbinu zenye kuleta majawabu ya matatizo ya umasikini wetu watanzania. Moja ya Agenda kwa Afrika kwenye mwaka huu kwenye World Economic Forum, ilikua ni “AFRICA FORGET ABOUT NATURAL RESOURCES BUT TECHNOLOGY”.
Mheshimiwa Spika, Naamini kama Mhe Rais angeshiriki mkutano huu wa kimkakati angeweza kupata mawazo zaidi ya dunia imefikia wapi na inahitaji nini kwasasa. Dunia kwasasa inahitaji tuwekeze zaidi kwenye kujenga rasilimali watu zaidi ya vitu. Ni utawala wa ajabu unaweza kuacha kuboresha elimu ya vijana wake ikatumia fedha hizo kununua ndege au kujenga barabara. Ndio maana sisi kama CHADEMA/UKAWA tulisistiza na tunaendelea kusisitiza kuwa Mradi pekee wa kimkakati kukwamua Taifa hili hapa ni kusuka mfumo wa elimu na kuhakikisha vijana wanapata elimu bora itakayowawezesha kushiriki dunia ya ushindani kama wadau sio watazamaji. Tunapaswa kujenga Taifa la watu ambao wanaweza kukabili maisha hata nchi hii ikigeuka kuwa jangwa lisilo na rasilimali yoyote kama ilivyo Israel. Inasikitisha kwamba huduma ya elimu nchini kuanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu imebaki vurugu tupu. India ambayo miaka ya 1970tulikuwa nayo sawa kiuchumi, sasa inauza wataalamu wake nchi za Ulaya na marekani, wakati sisi bado tunauza mchanga, tumbaku na ngozi.
10.12.              Mradi wa Chuma na Makaa ya Mawe
Mheshimiwa Spika, eneo la Liganga linakadiriwa kuwa na makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 428 kiwango ambachi kinaweza kutumika kwa takribani miaka 500 (Kwa mujibu wa utafiti wa NDC),na chuma tani milioni 126.
Mheshimiwa Spika, Tangu awamu ya tatu mpaka ya nne kumekuwa za masimulizi yasiokwisha kuhusu namna kuvuna utajiri huu wa makaa ya mawe na chuma.Lakini kwasababu ya mtazamo finyu kibiashara, awamu zote zimekuja na kuondoka na kuacha masimulizi hayo. Awamu ya tano, kwenye bajeti 2016/17, iliahidi kufanyia kazi suala hili, lakini ni bahati mbaya sana, maelezo kwenye kitabu cha utekelezaji wa bajeti, yanatoa picha kwamba hakuna jipya zaidi ya mwendelezo wa masimulizi.
Mheshimiwa Spika, Akiba hiyo ya chuma na makaa ya mawe ni biashara kubwa na kama Serikali ingeweka mkazo kukamilisha utaratibu wa kukamilisha miradi hiyo miwili kwa pamoja Tanzania ingeweza kufikia kiwago cha kuuza nje sio chini ya tani milioni 2 za chuma na makaa ya mawe, na kuvuna dola za kutosha kuendesha nchi hii. Ilikuvuna chuma, inahitajika umeme zaidi ya 250MW, wakati mradi uliokwama wa kuzalisha makaa ya mawe Liganga unaweza kuzalisha kwa kuanzia zaidi ya 600MW, kiasi ambacho kingetosha kuendesha mtambo wa kufua chuma na kubaki na ziada ya umeme ya 350MW.
Mheshimiwa Spika, Laiti kama tungekuwa na Uongozi makini, miradi hii miwili ilipaswa kuwa ya kwanza na yenye kupewa kipaumbele kabla hata ya kujielekeza kwenye ujenzi wa reli. Hii inatokana na ukweli kwamba ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa zaidi ya 2,400km itakayogharimu zaidi ya dola million 7,000, utahitaji mamilion ya tani za chuma, kiasi ambacho kama tungekuwa tumekamilisha mradi huo wa chuma tungeweza kupunguza gharama hizo kwa kiasi kikubwa na mradi huo ungekuwa soko kubwa kwa mradi wa chuma, kuliko sasa ambavyo Serikali itakapoanza ujenzi wa reli na kuhitaji kutumia fedha za kigeni kuagiza chuma nje  na kwa bei ambayo ni kubwa ukilinganisha na kama ingenunua chuma nchini
Hivyo ni ushauri wa Kambi rasmi ya upinzani kwamba serikali ikamilishe miradi hii ya Liganga na Mchuchuma ili kupunguza gharama kubwa za ujenzi wa reli ya kati.
10.13.              Mradi wa Liquified Natural Gas(LNG)
Mheshimiwa Spika, Tangu miaka ya 2011, Serikali ya CCM ilitangaza kwa matangazo makubwa kuhusu ujenzi wa uchumi wa gesi baada ya kuvumbuliwa kiasi kikubwa cha gesi nchini kinachozidi futi za ujazo trilioni 55. Mategemea makubwa katika biashara hii ya gesi yalitegemea sana uwekezaji mkubwa katika mradi huu ambao unakadiriwa kufikia dola billion 30, uwekezaji ambao kama ungeanza mwaka huu inakadiriwa ungesababisha uchumi kukua kwa asilimia 7.2 kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu wenye uwekezaji wa dola 30billion ni mradi wa kihistoria katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, na kwakweli katika historia ya Tanzania kwani dola billion 30 ni karibu asilimia 75% ya uchumi wa Tanzania ambao kwasasa ni takribani dola billion 45. Uwekezaji wa dola billion 30 ni zaidi ya theluthi moja ya uchumi wa Kenya, Dola billion 30, ni karibu sawa na uchumi wote wan chi ya Uganda unaokadiriwa kuwa dola billion 30.
Mheshimiwa Spika, Ni uchungu kusema kwamba ingawa taarifa ya utekelezaji wa bajeti serikali inasema mradi huu utaanza mwaka 2019/20 ,Ukweli ni kwamba wawekezaji katika mradi huu ambao ni kampuni za State Oil, BG/Shell, Exxon Mobile na  Orphir , wamekwishamua kuahirisha uwekezaji huu. Kwa mujibu wa Jarida la Reuters, la Novemba16, Meneja  wa kampuni ya Sate  amekaririwa akisema kwamba kutokana na kutoeleweka kwa Serikali ya Tanzaia, wao wameamua watafanya uamuzi kuhusu uwekezaji huo miaka mitano 5 kutoka 2016, yaani  20 kusisitiza kwamba ikiwa hivyo, wataingiza mtaji miaka mitano5 kutoka mwaka huo 2021, ikimaanisha kwamba ratiba ya kampuni hizi kuleta mtaji ni mwaka 2026.
Mheshimiwa spika, Huu ndio ukweli ambao Serikali haiusemi na badala yake inatoa maelezo yaliyojaa simulizi kwa suala muhimu na la kimkakati kama hili. Kifupi ni kwamba Serikali ya awamu tano haiaminiki, haitabiriki kwa wafanyabiashara wa ndani nanje kama IMF iliyosisitiza hivi karibuni. Na kwakuwa mitaji inatafutwa duniani, wawekezaji hawahawa ambao wameahirisha mradi huu hapa kwetu wanaendlea kuwekeza nchini Mozambique, na watakapomaliza, ni wazi Mozambique yenye gesi kuliko Tanzania, ikiwa na LNG Plant, itatawala soko lote la gesi kusini na mashariki ya Afrika, wakati Tanzania ikiendelea na utawala wake wa purukushani sio na maono wala mkakati.
         
11.      HALI YA SIASA NCHINI NA UCHUMI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yoyote unategemea hali ya utulivu wa kisiasa pamoja na uzingatiwaji wa misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu. Ni dhahri kuwa mambo hayo yakikosekana kutakuwa na athari za moja kwa moja za kiuchumi katika taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza kuhusu uchumi shirikishi ambao unalenga kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unaendana na kuboresha maisha ya wananchi. Malengo haya hayawezi kufikiwa kama bado hali ya nchi kisiasa sio nzuri kutokana na baadhi ya makundi kuminywa kupaza sauti yao na kutoa maoni juu ya masuala yanayoendelea katika taifa.
Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo ningependa kugusia masuala yafauatayo ambayo yanahitaji majibu na hatua za Serikali;

(a)       Daftari la Wapigakura (PVR)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalo jukumu la kuilinda Katiba ya nchi kwa kutekeleza matakwa ya kikatiba juu ya haki ya wananchi kushiriki katika uchaguzi kwa kupiga kura. Aidha Serikali inalo jukumu la kuhakikisha kuwa matakwa ya kisheria kuhusu masuala ya uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanazingatiwa ikiwemo maandalizi ya daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba: “Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, Ili kuhakikisha kuwa haki ya wananchi ya kupiga kura inalindwa, Ibara ya 5(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria ya uchaguzi na kuweka masharti ya kuanzisha daftari la kudumu la wapiga kura na kuweka utaratibu wa kuboresha daftari hilo.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi sura namba 343 toleo la mwaka 2015 kifungu cha 15(5) inaelekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuboresha daftari la kudumu mara mbili ikiwa na maana ya mara tu baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi mkuu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni toka Bunge la kumi imekuwa ikiitaka Serikali kutekeleza takwa hilo la kisheria lakini Serikali imekuwa ikiziba masikio.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili toka uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulipofanyika lakini hakuna dalili yoyote inayoonesha kuwa daftari la kudumu la wapiga kura litaboresha kama ambavyo sheria inataka. Ukisoma kwa makini Fungu 61 Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina kifungu ambacho kimetengewa fedha kwa ajili ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Spika, Hii maana yake ni kuwa tunaelekea mwaka wa tatu bila kuboresha daftari la wapiga kura. Huu ni ukiukwaji wa taratibu za kisheria ambazo kama taifa tumejiwekea. Ikumbukwe kuwa lengo la kuboresha daftari ni muhimu kwa sababu kumekuwa na chaguzi ndogo za Udiwani na Ubunge ambazo zote zimefanyika kwa kutumia daftari la wapiga kura lililoboreshwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ili kuepuka malalamiko ya wadau wa siasa nchini kwa kuboresha daftari la wapiga kura ili kukidhi matakwa kikatiba na kisheria kama ambavyo tumeeleza.
Mheshimiwa Spika, kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura haiondoi hoja ya hitaji la kuwa na Tume huru ya uchaguzi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa na madai ya muda mrefu ya  kuwa na Tume huru ya uchaguzi. Majibu ya Serikali kwenye hoja hii yamejikita kusubiri mchakato wa Katiba mpya kukamilika.
Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanajua kuwa mchakato wa Katiba mpya umekwama na Rais ameshasema hadharani kuwa wakati wa kampeni hakutamka popote kuhusu Katiba mpya na hivyo inaonekana si kipaumbele chake. Hii maana yake ni kuwa majibu ya hoja ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi itasubiri Katiba mpya hayatakuwa na mantiki baada kauli ya Rais.
Mheshimiwa Spika, ili kuwe na mwelekeo mzuri wa huko tunakoelekea Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwe na mabadiliko ya Katiba iliyopo ili kukidhi masuala ya kidemokrasia nchini na kuondoa malalamiko ya wadau wa siasa nchini. Ikumbukwe kuwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 kulikuwa na majadiliano ambayo hayakufikia mwisho yaliyokuwa yanasimamiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambayo yalipendekeza kuwe na marekebisho ya mpito ya Katiba iliyopo ya mwaka 1977 kwa ajili ya kuepuka mambo ambayo yanaweza kuharibu uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Mheshimiwa Spika, Ili kuwa Taifa linaloheshimu misingi ya kidemokrasia nchini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kurudia baadhi ya mapendekezo ya Kamati ya Kituo cha Demokrasia Tanzania ili kuwe na marekebisho ya Katiba ya mpito katika masuala yafuatayo yanayohusu Tume ya Uchaguzi;

·        Uteuzi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume uthibitishwe na Bunge na sio kuteuliwa na Rais pekee.
·        Tume ya Taifa ya Uchanguzi kuhakikisha kuwa inakuwa na ofisi kwa kila Jimbo la Uchaguzi na ofisi za Uratibu za Mikoa na sio kuwatumia Wakurugenzi wa Halmashauri na ofisi ambazo zipo chini ya TAMISEMI
·        Tume ya Taifa ya Uchaguzi iweke utaratibu wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kuwa wa kudumu. Hii ni kwa sababu kila mwaka kunakuwa na wapiga kura wapya ambao hufikia umri wa miaka 18.
·        Kuhakikisha kuwa Tume ya Taifa ya uchaguzi baada ya marekebisho inasimamia pia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
·        Katiba iruhusu baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu, matokeo ya Urais yapingwe Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, demokrasia ikishamiri vizuri katika nchi uchumi utakua na kufanya nchi yetu kuendelea. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha inalichukulia kwa uzito jambo hili kwa ajili ya mustakabali mwema wa yetu.

(b)       Hali ya Siasa Zanzibar
Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Machi, 2016 Shirika la MCC lilifikia uamuzi wa kusitisha misaada yake kwa Tanzania[20]. Sababu za kusitishwa kwa misaada hiyo pamoja na mambo mengine ni kutokana na kufutwa kwa uchaguzi halali wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 pamoja na Serikali kutumia sheria  ya makosa ya kimtandao kuzuia uhuru wa kutoa maoni.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kusisitiza kuwa kurudiwa kwa uchaguzi feki wa Zanzibar wa tarehe 20 Machi, 2016 hakujawa dawa ya kutatua mkwamo wa kisiasa Zanzibar. Wananchi wa Zanzibar walifanya maamuzi yao tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad lakini sauti yao haikusikika kwa sababu kuna kikundi cha watu ambao hawaheshimu misingi ya demokrasia nchini.
Mheshimiwa Spika, Aidha tunasisitiza kuwa marudio ya uchaguzi Zanzibar hayajawa dawa kwa wanachama wa Chama cha Wananchi CUF walioteswa na kupigwa na Mazombi huku vyombo vya dola vikishuhudia kama ambavyo ambavyo tulieleza kwa kirefu kwenye hotuba ya Kambi ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.
Mheshimiwa Spika, marudio ya uchaguzi wa Zanzibar hayajafanyika kwa mujibu wa Katiba wala Sheria bali kwa matakwa ya mtu mmoja ambaye aliamua kufuta uchaguzi huo bila kuwa na mamlaka ya kisheria wala Katiba.
Mheshimiwa Spika, thamani ya fedha zilizozuiliwa na MCC ni takribani 1.5 Trilioni[21], Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haishangai kuona miradi ya REA ikisuasua kutokana na ukosefu wa fedha. Hata bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini imeshuka (kutoka 1,056,354,669,000 hadi 938,632,006,000) tofauti na mwaka wa fedha uliopita. Ikumbukwe kuwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji suala hili Serikali ilijinasibu kuwa itagharamia miradi ya REA kwa fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba fedha za MCC zilikuwa muhimu kwa nchi lakini kutokana na kukiukwa kwa misingi ya demokrasia na kuwaziba wananchi midomo kunakofanywa na Serikali ya CCM fedha hizo zikazuiwa. 
Mheshimiwa Spika, tarehe 01 Juni, 2017   Balozi Msaidizi wa Marekani hapa nchini, alitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini[22].
At this same crossroads, however, is another path. One which leads to a Tanzania where people are afraid to use their voice, and where development stagnates.  Down this road, entrepreneurs hang back from starting new business due to stifling or inconsistently applied regulations. Government institutions remain susceptible to corruption and inefficiencies.  Schools and medical centers do not have the resources they need.  And are unable to serve those who need them.  The security forces are feared and operate outside the rule of law.  People distrust their neighbors and wonder where their loyalties lie.  Citizens are afraid to offer their views – limiting the debate that is so often needed to come up with the best way forward.  In this direction, the efforts of millions of hard-working, talented Tanzanians – especially young Tanzanians – will see a less certain future”.
Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi maoni haya yanaweza kujengwa katika dhana zifuatazo;
(i)                  Watanzani wamekuwa waoga kutoa maoni yao
(ii)                 Maendeleo ya nchi yetu yanarudi nyuma
(iii)                Wajasiriamali wanaogopa kufanya biashara zao kutokana na vikwazo vya kikanuni
(iv)               Jitihada za kupambana na rushwa hazina ufanisi
(v)                Shule na hospitali hazina rasilimali za kutosha
(vi)               Vyombo vya dola vinafanya kazi kinyume na utawala wa sheria
(vii)             Serikali inazuia mijadala- kama ilivyozuia kuzinduliwa kwa Kitabu cha Ndugu Alphoce Lusako ambaye alikuwa Mwanafunzi aliyefukuzwa masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara mbili.
(viii)            Hakuna mustakabali mwema kwa vijana ambao ni wachapakazi na wenye vipaji
Mheshimiwa Spika, Hii ndiyo hali ya siasa katika nchi yetu kwa jicho la kimataifa. Huu ndio ukweli ambao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliuweka wazi katika hotuba zake kwa Wizara mbalimbali. Japo mengine yalifutwa na kutoingia ndani ya Bunge lakini ukweli utabaki palepale kuwa hali sio nzuri ndani ya nchi yetu kwa sasa kwa sababu imejengwa hofu kubwa miongoni mwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Rais anapenda kusisitiza kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kuhoji kuwa ni ukweli upi ambao Serikali yake inapenda kuusikia? Hii ni kutokana na juhudi za kila namna ya kuzuia mawazo mbadala kusikika kwa wananchi. Ukweli upi ambao Rais anapenda kuusikia wakati amezuia kinyume na sheria mikutano ya vyama vya siasa? Ukweli ni upi anaopenda kuusikia wakati wananchi hawawezi kusikia na kuona moja kwa moja mijadala ya wawakilishi wao ndani ya Bunge?

(c)        Sheria ya Makosa ya Kimtandao na Uhuru wa Kujieleza
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Act) imekuwa mwiba wa uhuru wa kujieleza nchini.  Hii inatokana na vyombo vya dola kujizolea sifa ya kuendelea kuwakamata vijana mbalimbali na kuwafungulia mashitaka ya uchochezi au makosa ya kimtandao kutokana na kuamua kutumia uhuru wao wa kikatiba kutoa maoni na kujieleza. 
Mheshimiwa Spika, wapo vijana wengi ambao wamekuwa wakikamatwa na kuteswa hasa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi na Kituo cha Polisi cha Oysterbay Jijini Dar Es Salaam, kutokana na kuandika na kutoa maoni yao mtandaoni ambayo huonekana ikikosoa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni alikamatwa kijana kutoka Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe Mdude Nyagali pamoja na Nicas David, ambapo baada ya Mdude kukamatwa huko Mbozi aliteswa bila kupelekwa hospitali na baadae kusafirishwa kwenda Dar es Salaam ambapo pia alipata mateso akiwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay  bila ya kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, ni baada ya Wakili na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Mhe. Tundu Lissu (Mb) kuwaeleza Polisi kuwa angepeleka maombi Mahakama Kuu ya Habeas Corpus   ndipo aliporudishwa tena Mbozi na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi ambapo mwezi wa Aprili mwaka 2017 Mahakama imemkuta bila hatia yoyote.
Mheshimiwa Spika, mwendelezo wa Serikali kutumia Sheria ya Makosa ya Kimtandao “Cyber Crime Act” ya mwaka 2015 umekuwa mwiba mchungu kwa watu kutoa maoni yao ndani ya nchi. Ni ishara kuwa Serikali haipendi matumizi ya mitandao ya kijamii na ndiyo maana Mkuu wa nchi wakati anapokea ndege za Bombadier Jijini Dar es Salaam alisema kuwa anatamani malaika washuke kuizima mitandao hiyo na kusahau kuwa wakati wa uchaguzi mkuu 2015 alitumia mitandao hiyo hiyo kujinadi na kutafuta kura.
Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa Sheria hiyo inatumika kama malaika kuzuia uhuru wa kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii.  Mamlaka makubwa waliyopewa Polisi kukamata computer au simu za mikononi tuliyaeleza kwa kirefu wakati sheria hiyo ilipokuwa inapitishwa Bungeni kwenye Bunge la kumi.
Mheshimiwa Spika, Ndiyo maana mpaka sasa nchi washirika wa maendeleo na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Umoja wa Ulaya na Shirika la Millenium Challenge Corporations (MCC), wameikosoa sheria hiyo kuwa inakiuka misingi ya demokrasia na utawala bora kwa sababu inazuia uhuru wa raia wa kujieleza; na kwa sababu hizo Shirika la MCC iliamua kuinyima Tanzania fedha za misaada katika miradi ya umeme kutokana na Serikali kutumia sheria hiyo kuzuia uhuru wa kujieleza.
Mheshimiwa Spika, kuna orodha ndefu ya vijana wa Kitanzania ambao tayari walishapandishwa kizimbani kutokana na Sheria hii ya Makosa ya Kimtandao kwa kuikosoa Serikali ya awamu ya Tano na hususani Mkuu wa Nchi, orodha hiyo ya vijana ni kubwa kuliko matumizi ya vifungu vingine vya Sheria hii, jambo linaloifanya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iamini kuwa uwepo wa Sheria hii ulilenga kuzuia uhuru wa kujieleza ili Serikali hii iendelee na vitendo vya ukandamizaji wa haki nyigine na ikose kabisa watu wa kuikosoa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao ni ya kibaguzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wapo  makada wa Chama cha Mapinduzi  wanaotoa matusi mpaka ya nguoni  kwa viongozi wa Vyama vya Upinzani lakini sheria hiyo haitumiki  kuwachulia hatua. Kutokana na hali hiyo, mtu yeyote anaweza kujenga hoja kuwa sheria hiyo wametungiwa wapinzani pekee na si upande mwingine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta marekebisho ya sheria hiyo ili kuondoa vifungu kandamizi ambavyo vinalalamikiwa na wadau na wananchi kwa ujumla.

12.      UCHUMI NDANI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, ili nchi yetu iendelee ni lazima kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha kuwa inatumia kwa ukamilifu fursa zilizopo katika nchi jirani na hasa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Kwa takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa biashara inayofanyika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee ni ya thamani ya dola za kimarekani milioni 5,632.9.
Mheshimiwa Spika, Tanzania haijatumia vizuri fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa kwenye nchi za Uganda, Rwanda na Burundi. Izingatiwe kuwa Taifa changa la Sudani ya Kusini tayari limeshajiunga katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na kufanya soko la ndani ya Jumuiya kupanuka kwa kiasi kikubwa. Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inafanya sana biashara na Kenya kuliko Taifa lolote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa mwaka 2015 Tanzania iliuza bidhaa Kenya kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 852.7 ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 448.1 mwaka 2014. Aidha, kwa kipindi hicho hicho Tanzania iliuza bidhaa Uganda zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 56.4 kwa mwaka 2015 na dola milioni 73.7 kwa mwaka 2014[23].
Mheshimiwa Spika, kwa nchi za Rwanda na Burundi Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 41.9 na 41.3 kwa mwaka 2015 pekee. Ikumbukwe kuwa tayari Sudani ya Kusini imejiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na pia Tanzania inajinasibu na uchumi wa viwanda, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hatua ambazo inachukua kuhakikisha kunakuwa na mkakati wa kupanua soko la bidhaa za Tanzani kwenda nchi za Uganda, Rwanda na Burundi katika hatua za awali.
Mheshimiwa Spika, Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza Bunge lako tukufu kama kuna mkakati wowote wa kuhakikisha kuwa inawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kuhakikisha wanatumia vizuri fursa mpya ya soko la nchi ya Sudani ya Kusini ambayo ni nchi mshirika mpya ndani ya Jumuiya.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaweza kuja na majibu ya idadi ya watu na ukubwa wa soko katika nchi za Burundi na Rwanda, majibu kama hayo hayatakuwa na mantiki kwa sababu nchi ya Kenya pekee iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 250 kwa mwaka 2015 pekee. Huku Tanzania kwa hizo mbili ikiwa imeuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 83.2 tu kiwango ambacho ni cha chini mara tatu kuliko kile cha wenzetu wa Kenya.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi ni ishara kwamba hatujatumia vizuri fursa za soko lililopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ieleweke kuwa nchi yetu iko kimkakati ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo inapakana na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki isipokuwa Sudani ya Kusini. Ni dhahiri kuwa, Serikali ikitumia vizuri fursa zilizopo nchi yetu inaweza kupata soko kubwa la bidhaa kuliko nchi zingine za Jumuiya.
Mheshimiwa Spika, ni lazima kuwe pia na mkakati wa kuhakikisha kuwa uchumi wa maeneo ya mpakani na nchi washirika wa Afrika Mashariki unawanufaisha wananchi wanaoishi maeneo hayo kuanzia baadhi ya maeneo ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Mara, Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Badala ya maeneo hayo kukumbwa na kadhia za wahamiaji haramu au wakimbizi wa vita, migogoro ya mipaka na ujambazi ni lazima yanufaike kiuchumi na kuwafanya kuona umuhimu wa Jumuiya kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Benki ya mwaka 2016 iliyochambua mazingira ya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Doing Business 2016-Measuring Regulatory Quality and Efficiency), imeipa Tanzania kiwango cha chini cha mazingira bora ya kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Katika viasharia vyote na vipengele vyake, Tanzania ilikuwa na kiwango cha chini kabisa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika viashiria 21 wakiongozwa na Burundi ambayo katika imekuwa na viwango 26 vya chini kabisa (lowest regional performance). Wakati huohuo nchi ya Rwanda ikiwa na alama 29 katika viashiria vya kuwa nchi yenye mazingira bora ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi si ishara nzuri kwa nchi yetu kama moja ya nchi kongwe ndani ya Jumuiya Mashariki. Moja ya kiashiria ambacho Tanzania imefanya vizuri kuliko nchi zingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Best Regional Performance) ni kusimamia na kuheshimu mikataba. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina wasiwasi kama mwaka huu 2017 bado Tanzania itaongoza katika kiashiria hiki baada ya mgogoro unaoendelea kati ya Serikali na kampuni ya madini ya Acacia.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha akishirikiana na Waziri wa Viwanda na Biashara kuhakikisha kuwa inaboresha mazingira ya biashara na kuiondoa nchi yetu kwenye aibu ya kuwa na mazingira karibu sawa na nchi kama Burudni ambayo mara kadhaa imekumbwa na machafuko ya kisiasa  ya ndani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuifanyia kazi taarifa ya Benki ya Dunia na kubadili mfumo ili kuweka mazingira bora ya biashara kuliko kuwaona wafanyabiashara na wawekezaji ambao wamewekeza ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na hasa nchini mwetu kama maadui na si marafiki katika ukuaji wa uchumi.
13.      UTEKELEZAJI WA MIRADI MIKUBWA YA KIMKAKATI
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na ugumu wa kupata mikopo ya riba nafuu kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo hapa nchi kama vile miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme wa maji –Stigler’s Gorge, uzalishaji wa Chuma-Liganga, ujenzi wa Reli ya Kati na matawi yake kwa  Standard Gauge, ujenzi wa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha nguo mikoa ya Magharibi au Ziwa na ujenzi wa Kiwanda cha ku- liquify  Gas (LNG) na kuiweka kwenye mitungi tayari kwa usambazaji nchi nzima na nje ya nchi; basi Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kufanyia utaratibu wa kupata mikopo ya ndani kwa mfumo wa “Organized Local Loans Syndications”.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu ni kwa Mabenki ya ndani pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii kushirikiana kutoa mkopo ili kufanikisha utekelezaji wa mradi hiyo.
 Mheshimiwa Spika,  sambamba na utaratibu huo tuliopendekeza hapo juu, Serikali inaweza pia kutumia mfumo wa  “Build-Operate-Transfer rights” (BOT), kwa kutumia makampuni binafsi au taasisi zisizo za kiserikai kujenga vitega uchumi vikubwa na hatimaye wakisharudisha gharama zao, vitegauchumi hivyo vinakuwa vya Serikali au kama ambavyo Serikali inaweza kuamua vinginevyo. Kambi Rasmi ya Upinzani ina uhakika kuna makampuni yanayoweza kutekeleza program kama hizo ikiwa utaratibu utaandaliwa vizuri na kuyaonesha makampuni jinsi gani wakiwekeza kwenye miradi husika watakavyoweza kurudisha fedha zao, pale wakipewa fursa ya kujenga na kuanza kuuendesha mradi husika kwa kipindi kitakachokuwa kimefikiwa katika makualiano na baada ya kumalizika kipindi hicho mradi utarudi Serikalini au Serikali inaweza kuingia  makubaliano mapya ya jinsi ya kuendesha mradi husika. Jambo kubwa ni kuwa tayari utakuwa unafanyakazi tayari na Serikali haitakuwa na jukumu la kukopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi husika.

Mheshimiwa Spika, utaraibu huu ndio kwa sehemu kubwa umeinua uchumi  wa nchi za Taiwan, India, Canada, Croatia, Australia, Japan, China, Malaysia, New Zealand na Philippines. Utaratibu huu unatoa uhakika kuwa mradi utaendeshwa kwa faida, kutokana na mhusika atakavyokuwa anauendesha ili kurudisha gharama zake za ujenzi. Hoja ya msingi ni jinsi ya kuwa makini katika uingiaji wa mkataba baina ya pande mbili husika katika mazingira ya faida kwa wote ( win – win situation).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba Serikali imeshindwa kutumia fursa ya sheria ya uendelezaji wa miradi kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP), na kushindwa huko kunaweza kuelezewa  na mambo yafuatayo:
§  Inawezekana kwamba masharti yanayowekwa na Serikali yanakuwa magumu kiasi kwamba Sekta binafsi inaona itashindwa kufanya biashara na kurudisha gharama zake,
§   Inawezekana pia kwamba, Serikali inataka kuwa ndiyo iwe imeshika mpini katika kila kitakachokuwa kinaendelea na mshirika mwenzake kukosa kauli katika ushirika, na
§  Inawezekana pia kwamba, Serikali haitaki kuitekeleza kwa ubia miradi mikubwa ambayo ina uwezekano wa kurudisha gharama kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli pia mitaji ya ujenzi wa miradi au fedha za kuongeza mitaji kwa makampuni ambayo hayafanyi vizuri kama Shirika letu la Umeme inaweza kupatikana kwa kusajili shirika husika kwenye soko la hisa “Initial Public Offerings”. Hii itafanikiwa kama kutakuwa na uaminifu katika utayarishaji wa vitabu mahesabu ya Kampuni husika (Prospectus ya Kampuni).  Mfumo huu ungeweza pia kutumika kwa shirika letu la Reli kwani kuna uhakika kwamba pale mradi utakapokamilika shirika litakuwa linatengeneza faida. Aidha, wanunuzi wa mwanzo wa hisa wanaweza kuziweka hisa hizo katika soko la pili na hivyo mtaji kuendelea kuendelea kukua.

14.      VYANZO VYA MAPATO YA  KODI
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na kilio cha siku nyingi cha watanzania kuhusiana na kuongeza ufanisi wa makusanyo ya kodi kwa kuhuisha sera ya msamaha wa kodi  na sheria zilizopo ambavyo kwa muda mrefu imekuwa ni kichaka cha kukwepa kodi. Aidha, Serikali imeshindwa kuifanyia ukaguzi misamaha inayotolewa na Serikali kwa wahusika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kwamba fedha za misamaha ya kodi ni fedha halali za walipa kodi, hivyo ni muhimu na lazima fedha hizo au miradi husika ifanyiwe  Ukaguzi  wa “value for money”  na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani sambamba na Kamati ya Mheshimiwa Spika Mstaafu ANNE MAKINDA (Chenge I Report) tulishauri kwamba ni muda mwafaka kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato badala ya kuongeza viwango vya kodi kwa vyanzo vile vile. Jambo hili linapelekea walipa kodi kutafuta njia mbadala za kukwepa kodi hiyo kwa kushirikiana na watendaji wa Mamlaka ya Kodi.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba huwezi kuvuna pale usipowekeza, kauli hiyo ina ukweli mno katika muktadha wa sekta ya kilimo hapa Tanzania, Sekta hii kwa kwa takwimu zilizo katika nyaraka mbalimbali ni kwamba ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu katika utoaji wa ajira kwa watanzania na ndio inaongoza kwa uchangiaji  29.7%  kwenye Pato la Taifa na kutoa ajira kwa asilimia 56.5% na mchango wake kwa mauzo nje ni 24.9%, lakini kwa ukweli ni kwamba sekta hiyo inapokuja kwenye mchango wake katika mapato ya kodi-tax revenue (VAT, excise duty, corporation income tax and PAYE) ni  0.2% tu.

Mheshimiwa Spika, hii maana yake nini katika ukuaji wa uchumi wetu na maendeleo ya Taifa kwa ujumla? Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwa tafsiri rahisi ni kwamba uwekezaji wa kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na endelevu kama ilivyoainishwa kwenye sera ya Kilimo ili waajiriwa katika sekta hiyo waweze kutambulika bado mkakati huo haupo. Hata wawekezaji wanaowekeza katika kilimo bado wafanyakazi katika sekta husika  kwa mtindo wa vibarua, jambo linalopelekea kuwa hawapo katika mfumo wa kulipa kodi ya mshahara (PAYE). 
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Madini  ambayo ukuaji wake umekuwa ni kama ifuatavyo 2012 - 6.7%, 2013 - 3.9%, 2014 -9.4%, 2015 -9.1% na 2016-16.6%[24]  mchango wake katika Pato la Taifa ni 20.5%, lakini  inachangia 3.7% tu kama kodi ya mapato ikiwa  VAT 1.2%  Kodi ya Makampuni 2.2% na PAYE 8.2% [25].  Kwa mwenendo huo wa mapato ni dhahiri kwamba wachangiaji wakubwa wa kodi ni wafanyakazi ambao wanalipa PAYE na sio kodi zingine zinazotakiwa kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kodi zinazotakiwa kulipwa na Wamiliki wa migodi mikubwa kisheria ni:-
§  Kodi ya makampuni,
§  Kodi ya zuio (WHT)
§  Kodi kwenye mishahara (PAYE)
§  Ushuru wa stempu
§  Kodi ya kuendeleza ufundi stadi (SDL)
§  Ushuru wa barabara
§  Ushuru wa forodha
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kufahamu kati ya kodi hizo, ni kodi ngapi ambazo makampuni hayo yanazilipa kwa ukamilifu wake?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria zetu viwango vya mrabaha  au tozo inayotozwa na kulipwa Serikalini kwa makampuni yote yanayozalisha na kuuza madini kabla ya kusafirisha madini hayo  kwa mujibu wa  Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ni:
§  Vito, almasi na urani – 5%
§  Vito iliyokatwa na kusanifiwa – 1%
§  Chumvi na Madini ya Ujenzi – 3%
§  Madini mengine ikiwemo dhahabu – 4%
Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba mchawi wa kutokunufaika kwetu na sekta ya madini ni sheria ambazo zimepitishwa na Bunge letu hili, ambalo toka uwepo wake limekuwa “dominated” na maamuzi ya chama kimoja ambacho kimeongoza nchi yetu tangu uhuru.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ni muda mwafaka sasa sheria hii ya madini inayotoa viwango hivyo kufanya marejeo makubwa sambamba na sheria hiyo pia marejeo yafanyike kwenye sheria za mafuta na gesi zilizopitishwa mwaka 2015.
15.      MAPATO YASIYO YA KODI
Mheshimiwa Spika, mapato yasiyo ya kodi (maduhuli) yanajumuisha; gawio, ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Vyanzo vya mapato haya ni pamoja na shughuli za utalii, bandari, viwanja vya ndege, uchimbaji madini (mirabaha), bidhaa zitokanazo na misitu, kodi ya ardhi, uvuvi.  Japokuwa kuna fursa kubwa ya kuongeza vyanzo vya mapato yasiyo ya kodi katika sekta kadhaa za kiuchumi, lakini vyanzo hivyo bado havijafanyiwa tafakuri kama ambavyo Kambi Rasmi kwa miaka yote imekuwa ikiishauri Serikali kufanyia kazi. Takwimu zinaonesha kwamba Serikali inapata chini ya 2% ya GDP kama mapato yasiyo ya kodi na mapato hayo ni chini ya 10% ya jumla ya mapato yote ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuna tafiti kadhaa zilizokwishafanyika ni kwa jinsi gani vyanzo vya mapato vinavyoweza kuongeza, urasimishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinaweza kufanyiwa kazi katika ngazi za Serikali za mitaa kwanza kwa kuwekewa utaratibu mzuri na ukishakubalika ni dhahiri Serikali itaanza kupata haki yake katika shughuli hizo za kiuchumi.

16.      KODI YA MAJENGO KAMA CHANZO CHA MAPATO YA
         SERIKALI

Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha unaokwisha mwezi Juni 2017 Serikali iliweka utaratibu wa kisheria kuondoa mamlaka ya Halmashauri kukusanya kodi ya majengo (property tax)na kuipa haki hiyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku Serikali ikijua kuwa kodi hiyo ilikuwa sehemu muhimu sana ya mapato ya Halmashauri nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililiona jambo hili kama mkakati wa kuondoa mapato kwa Halmashauri ili kuzipunguzia nguvu Halmashauri nyingi za Majiji ambazo zinaongozwa na Wapinzani. Ieleweke kuwa halmashauri hapa nchini zimekuwa zikikusanya mapato kwa ajili ya kuendesha miradi yake ya maendeleo na shughuli nyingine za kawaida kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato kwa mujibu wa sheria ya fedha ya Halmashauri (Local Government finance Act, 1982) Haukuwa uamuzi sahihi kutunga sheria ya kuondoa chanzo cha mapato cha kodi ya majengo kutoka katika halimashauri nchini .
Mheshimiwa Spika, Kufutwa kwa kifungu kilichokuwa kinazipa Halmashauri jukumu la kukadiria na kukusanya kodi za majengo na kulihamishia TRA kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2016, kifungu cha 38 baada ya kufanya marekebisho kwa kuvifuta vifungu vya 31A na 31B vya sheria ya fedha ya Serikali ya Mitaa sura 290 kumeziyumbisha sana halimashauri katika kutekeleza majukumu yake kutokana na ukweli kwamba chanzo cha kodi ya majengo kilikuwa ni mojawapo ya chanzo kikubwa cha mapato ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa Ofisi ya Rais TAMISEMI tulieleza wazi kuwa taarifa ya Serikali inaonyesha kuwa kodi ya Majengo iliyokusanywa ni shilingi milioni 4,762.37 kati ya mIlioni 29,004 sawa na asilImia 17.4 tu ambayo ilitarajiwa kukusanywa na TRA.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo ni wazi kuwa TRA haina uwezo wa kufanya kazi ya kukusanya chanzo hiki cha mapato kwa ufanisi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili sababu za kuipa TRA mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo wakati haikuwa imejipanga kimikakati na kimfumo kufanya kazi hiyo, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta tena marekebisho ya Sheria ya Fedha ili kurudisha chanzo hiki cha mapato katika ngazi ya Halmashauri kama ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa baada ya kuziondolea Halmashauri haki ya kutoza kodi ya majengo, Halmashauri nyingi hasa za Vijijini zimeanza kutoza kodi ya majengo kwa wananchi huko vijijini jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi wetu ambao kwa waliowengi hawana vipato vizuri.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali  kulieleza Bunge lako tukufu, ni kwa nini wameondoa kodi ya majengo kama chanzo cha mapato na kuruhusu Halmashauri kuanza kuwatoza wananchi wa vijijini kodi ya majengo yao.
Mheshimiwa Spika, Kama Serikali bado inang’ang’ania chanzo hiki, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri majengo yagawanywe kwenye madaraja kama vile majengo makubwa ya kibiashara, residential apartments, na majengo mengine makubwa kama itakavyoamuliwa kodi zao zikusanywe na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) lakini majengo madogo ya biashara na nyumba za makazi kodi yao ikusanywe na Halmashauri ili kuongeza ufanisi wa TRA katika ukusanyaji.
Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha eneo hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba, kitendo cha Serikali hii ya awamu ya tano kuziondolea Serikali za Mitaa mamlaka ya ukusanyaji wa kodi ya Majengo na kurudisha mamlaka hiyo kwenye Serikali Kuu kupitia TRA, kunauwa kabisa dhana ya ugatuaji kamili wa madaraka (D by D) ambayo ilikuwa ndiyo kaulimbiu kubwa ya Serikali za awamu zilizopita na fedha nyingi zilitumika kutekeleza dhana hiyo. Kutokana na hali hiyo, uwepo wa Serikali za Mitaa hauna maana tena kwani madaraka yake ya msingi yamechukuliwa na Serikali Kuu, jambo ambalo litasababisha Serikali hizo zishindwe kujiendesha. Kwa maneno mengine ni kwamba Serikali Kuu inazifuta kinyemela kwa kuziondolea uwezo wa kufanya kazi na kujiendesha.

17.       MCHANGO WA VIWANDA KATIKA UKUAJI WA UCHUMI

Mheshimiwa Spika, Ili Tanzania ifanikiwe kuwa ya uchumi wa kati kiviwanda ifikapo mwaka 2025 basi sharti sekta ya uzalishaji (manufacturing) ichangie wastani wa chini wa asilimia 40 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, leo hii takaribani miaka 8 kabla ya mwaka 2025, sekta ya viwanda vya uzalishaji (manufacturing) inachangia asilimia 5.2 tu ya pato la Taifa kwa mujibu wa kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano (National Five Year Development Plan, 2016/17 – 2020/21. 

Mheshimiwa Spika, kwa mwenendo huo,  hata kama Rais Magufuli akifanikiwa kukaa madarakani kwa miaka 8 ijayo mpaka kufikia mwaka 2025, yeye na Serikali yake yote hataweza kabisa kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kiviwanda kwa sababu ili afanye hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inampa changamoto kuwa kila mwaka wa fedha ikiwamo mwaka huu wa 2017/2018, sekta ya uzalishaji (manufucturing) inapaswa kukua kwa asilimia 4.35 kila mwaka wa fedha mpaka ifikapo mwaka 2025 ili kufikia lengo la kuifanya ‘manufacturing’ ichangie asilimia 40 ya pato la Taifa na hatimaye Tanzania kuwa ya uchumi wa kati kiviwanda!

Mheshimiwa Spika, ukisoma kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano (National Five Year Development Plan, 2016/17 – 2020/21 Serikali ilijipangia kutumia jumla ya Shilingi Trilioni 5.78 kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mikubwa ya kimkakati kwenye sekta ya uzalishaji (manufacturing), wakati ahadi (commitment) ya Serikali pekee ikiwa ni bilioni 659 – angalia Jedwali la 1 hapo chini.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Uwekezaji wa Viwanda Kimkakati iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2017/2018 katika fungu Fungu 44, ilikuwa imetengewa jumla ya Shilingi Bilioni 2.38 ambayo ni sawa na asilimia 0.36 ya fedha zote za Maendeleo zilizotakiwa kutengwa na Serikali, kama sehemu ya ahadi yake katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano. – angalia Jedwali la 2 hapo chini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaposema hoja ya Tanzania ya uchumi wa viwanda ni hoja hewa, inamaanisha inachokisema. Kwa kiwango cha ‘facts’ ambazo tayari tumezianisha katika jedwali la 1 na 2, ni wazi kabisa kuwa hakuna Tanzania ya viwanda inayoimbwa kila kukicha na Serikali ya CCM.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ya CCM kulielezea Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla inapojinasibu kuwa nchi yetu ni Tanzania ya viwanda, je Serikali itajenga uchumi wa viwanda kwa bajeti ipi?
Jedwali 1:
Uwekezaji katika Sekta ya Uzalishaji (Manufacturing Sub Sector
Jina la Mradi
Mpango wa Bajeti 2017/2018
TZS Bilioni
Government Commitment
2017/2018
TZS Bilioni
Bagamoyo SEZ
3,412
402.1
Kurasini Logistics Center
220
Mtwara SEZ (Freeport Zone)
12
0.9
Kigoma SEZ
10
5
Tanga SEZ
5
2.7
Ruvuma SEZ
3
2.6
Bunda SEZ
3
2.8
Morogoro - Star City SEZ
337
13
Industrial Park Interventions
23
20.6
MSMEs Parks Strategic Choices
29
13.3
Automotive industry Strategic Choices
160
70.7
Petro and Chemical Industries Strategic Choices
1,144
30.5
Development of Pharmaceutical Industries Strategic Choices
27
5
Textile and Clothing Industries
10
9.5
Building and Construction Industries Strategic Choices
76
5
Leather Industry Strategic Choices
8
3
Agro processing strategic Choices
129
47.2
Iron and Coal Strategic Choices
179
25.01
JUMLA
5,787
659
Chanzo: URT (2016) National Five Year Development Plan 2016/17 - 2020/21, pp. 230 – 241


Jedwali 2:
Miradi ya Uwekezaji wa Viwanda Kimkakati iliyotengewa fedha 2017/2018 Fungu 44
Jina la Mradi
Kiasi cha Fedha za Maendeleo kilichotengwa kwenye Bajeti, 2017/2018
TZS
Lake Natron
            2,000,000,000
Revival of General Tyre and Rubber Plant
                  70,000,000
Integrated Industrial Development
                  10,000,000
Mchuchuma Coal to Electricity Project
                100,000,000
Liganga Vanadium Titanium
                100,000,000
KAIZEN
                100,000,000
JUMLA
            2,380,000,000
Chanzo: Volume IV - Public Expenditure Estimates Development Vote (PART A), Page 70 & 71


18.      UNYANYAPAA WA SEKTA BINAFSI KATIKA KATIKA UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya tano imeanzisha sera zisizo rasmi zenye msimamo mkali (extremist view) dhidi ya ukuaji wa sekta binafsi. Ni vema Serikali ikatambua kuwa nchi ya Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa ujumla ina uchumi dhaifu unaokuwa taratibu ukitegemea ukuaji wa sekta binafsi katika kuufanya kuwa uchumi imara. Hivyo hatua zozote zenye misimamo mikali dhidi ya ukuaji wa Sekta binafsi ni hatua za kudhoofisha juhudi za ujenzi wa uchumi imara ulio shirikishi (inclusive economic growth)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imemsikia Rais Magufuli akitoa ufafanuzi wa sera zisizo rasmi zenye msimamo mkali (extremist view) dhidi ya sekta binafsi nchini alipokuwa akifungua Kituo cha Kutunzia Taarifa (Data centre) na kuzindua Mfumo wa Ukusanyaji Mapato wa Serikali kwa Njia ya kielektroniki kwenye sherehe zilizofanyika Kijitonyama jijini Dar es salaam Juni 1, 2017, alinukuliwa akisema kuwa “TCRA wanapotoa faini , faini ndogo tu sijui milioni mia tatu, sijui milioni ngapi, kwa mtu anayepata mabilioni ataacha kujirejista kwenye Dar es Salaam Stock Exchange kusudi uwe una mpiga faini, kwa sababu faida nyingi anabaki nayo, TCRA msipige faini,  futeni haya makampuni” hii ni sera isiyo rasmi yenye mtazamo mkali (extremist view) ambao sio rafiki wa sekta binafsi nchini.  
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo huu, Rais anatuma ujumbe kwa sekta binafsi kuwa Serikali inakusudia kufuta makampuni nchini jambo ambalo sio sahihi kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa. Rais anadhani njia rahisi ya kukusanya kodi kutoka sekta binafsi basi ni kutumia vitisho vya kufungia makampuni. Kulipa kodi sio jambo moja tu ambalo nchi inanufaika nalo, bali makampuni haya makubwa kwa madogo ndio yanayotoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, ambao nao huilipa kodi ya mapato kwa Serikali (Pay As You Earn).
Mheshimiwa Spika, Moja ya njia ya kuboresha maisha ya Watanzania ni kwa Serikali kuweka mazingira rafiki ya makampuni katika Sekta binafsi kujiendesha kwa uhuru bila kuvunja sheria za kodi wala kukwepa kodi ili makampuni hayo yatoe ajira nyingi kwa Watanzania na mapato ya Serikali yaongezeke kutokana na tozo za kodi kwa makampuni. Lakini jambo la kustaajabisha ni kitendo cha Serikali kuwa na mawazo ya sera zenye msimamo mkali dhidi ya ukuaji wa Sekta binafsi nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutumia akili kukusanya kodi na sio matumizi ya nguvu na mabavu kama inavyoendelea kufanya Serikali ya awamu ya tano. Tanzania sio kisiwa na ni sehemu ya dunia haiwezi kujitenga na kujitegemea yenyewe inahitaji wawekezaji wa ndani ya nje ya nchi ili kunenepesha uchumi wa Taifa.

19.      MWENENDO WA BIASHARA NCHINI NA JINSI
UNAVYOATHIRI UKUAJI WA UCHUMI

19.1.  Kushuka kwa Mauzo ya Bidhaa nje ya Nchi
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Biashara nchini inaongozwa na Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003. Hata hivyo Seriali hii ya awamu ya tano inaonekana kutotekeleza Sera hiyo kwa ufanisi. Tafiti zinaonesha kuwa Sera hii haijafanikiwa kuendeleza sekta ya biashara hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Sera hii ya Taifa ya Biashara katika dira yake inaweka mkazo kwa Sekta nzima ya biashara kuwa ni kuugeuza uchumi kuwa wa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi (export-led); Dira ya Sera hiyo inasema hivi:-
“... to transform the economy from a supply constrained one into a competitive export-led entity responsive to enhanced domestic integration and wider participation in the global economy through national trade liberalisation”
Kwa tafsiri  isiyo rasmi ya Kiswahili ni kuwa:-
“…kubadilisha uchumi kutoka katika vikwazo vya usambazaji kwenda kwenye ushindani wa mauzo ya bidhaa nje ya nchi yatakayowezesha maingiliano ya ndani na ushiriki mkubwa wa uchumi wa dunia kupitia biashara huria kitaifa”

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini kuwa msingi mkuu wa Sera ya Biashara ya Taifa ni “mauzo ya bidhaa nje ya nchi” yaani “exports”. Msingi ambao ujenzi wake kwa vitendo umekuwa ni kitendawili kikubwa kutokana na Serikali hii ya CCM kushindwa kwa vitendo kuimarisha uzalishaji wa bidhaa na huduma ndani ya nchi ili hatimaye kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Shirika la Trading Economics iliyochapwa mwaka 2017 katika takwimu zake zimeonesha kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi (Exports) yameshuka kutoka Dola za Kimarekani milioni 932.90 mwezi Januari, 2016 mpaka Dola milioni 854 mwezi Disemba, 2016. Wastani wa mauzo ya bidhaa nje ya nchi uliendelea kubakia kuwa dola milioni 549.16 kutoka mwaka 2006 mpaka mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017 iitwayo “Ease of Doing Business Tanzania” (Wepesi wa Kufanya Biashara Tanzania) imeripoti kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 180 kati ya 190 (nafasi ya 10 kutoka mkiani) katika wepesi wa kufanya biashara baina ya mipaka ya nchi na nchi (Trading Across Borders)
Mheshimiwa Spika, kukamilisha nyaraka za mauzo ya bidhaa nje ya nchi hapa kwetu Tanzania inachukua saa 96 (karibuni siku 4) wakati Botswana huchukua takribani saa 8 tu, na Kenya majirani zetu huchukua muda wa saa 21. Kushuka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kumeendelea kushika kasi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya awamu ya tano ipo madarakani.
Mheshimiwa Spika,  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kutoa taarifa mbele ya Bunge lako tukufu juu ya hatua inazozichukua kuhakikisha inaongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi (Exports) ili kukuza uchumi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa inaboresha mazingira ya biashara katika mipaka ya nchi na nchi (Trading Across Borders). Ili nchi yetu iendelee kuaminiwa na wawekezaji wa ndani na nje, ni lazima sera na sheria zetu za biashara ziaminike, ziheshimiwe na ziwe shirikishi (Predictable and participatory).

19.2.  Mazingira Magumu ya Kufanya Biashara Nchini
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Ease of Doing Business Tanzania 2017 imeonesha kuwa Tanzania imeongeza ugumu zaidi katika hatua za kuanzisha bishara kwa kuongeza tozo za usajili. Jambo hili linaathiri juhudi za kuongeza ajira kwa vijana wetu. Tanzania imeshika nafasi ya 135 kati ya 190 katika wepesi wa kuanzisha biashara mpya. Unapokuwa na ugumu wa kuanzisha biashara, unawafanya wajasiriamali wasifanye shughuli rasmi ya kuingiza mapato yao na mapato ya Serikali, na hivyo kupunguza kiasi cha ajira zitokanazo na biashara rasmi.

Mheshimiwa Spika, ili mjasiriamali aanzishe biashara Tanzania anatakiwa kuruka vihunzi 9 vya utaratibu wa usajili ndani ya siku 26 na gharama ya asilimia 21.5 ya mapato ya Mtu mmoja kwa mwaka (per capital income). Biashara za ujenzi wa majengo ikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi unakabiliwa na changamoto kubwa ya muda mrefu unaotumiwa kutoa Kibali cha Ujenzi (Construction Permit). Utafiti wa ‘Ease of Doing Business 2017’ unaonesha kuwa inachukua takribani siku 205 na taratibu 18 ili mfanyabishara apate kibali cha ujenzi.  Kuingiza umeme kwenye biashara mpya kama vile kiwandani inachukua siku 109 na hatua 4 za ukamilishaji wa nyaraka mbalimbali.  Kupata hati ya nyumba kwa ajili ya biashara mbalimbali inachukua hatua 8 ndani ya siku 67 kukamilisha mchakato wa kupata hati hizo.
Mheshimiwa Spika, nchini Rwanda, ambako ndiko Serikali ya awamu ya tano inapendelea sana kwenda kuchukua ushauri wa masuala mbalimbali ikiwemo jinsi ya kukusanya kodi, inachukua muda wa siku 1 tu kufungua Kampuni bila kulipia gharama zozote zile. Hapa nchini inachukua siku 4 kufungua kampuni na ada inayotozwa ni kati ya Shilingi 20,000 na 440,000 jambo linazuia biashara nyingi kurasimishwa, ajira kupotea na sekta binafsi kuendelea kudumaa. 

Mheshimiwa Spika,  kutokana na mazingira magumu ya kuanzisha na kuendeleza biashara nchini, utafiti uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2012, (National Baseline Survey Report – Micro, Small and Medium Enterprises in Tanzania) unaonesha kuwa  asilimia 96.4 ya biashara za chini (Micro-Entprises) hazijasajiliwa na BRELA, na asilimai 84.4 ya biashara ndogo (Small Enterprises) hazijasajiliwa na BRELA, huku asilimia 63 ya wafanyabishara waliohojiwa wakisema hawajui chochote juu ya masuala ya usajili wa biashara.

Mheshimiwa Spika, hii ni ishara kuwa mazingira ya kuanzisha biashara nchini sio rafiki kiasi cha kuwa na kiwango kikubwa cha biashara zinazoanzishwa bila kusajiliwa rasmi. Ni ishara pia kuwa mipango ya Serikali haiwezi kuwafikia kundi hilo kubwa la wafanyabiashara nchini ili kuboresha mazingira yao ya biashara na kuongeza mapato ya Serikali kwa namna itakayofaa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuboresha mazingira ya kuanzisha biashara kwa kupunguza idadi ya siku mpaka kufikia siku moja na kuondoa tozo za usajili wa makampuni ili kuchochea wajasiriamali kufungua makampuni kwa wingi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuweka mazingira rafiki na yanayovutia wafanyabisahara wa kada zote kusajili biashara zao kwa namna itakayoiwezesha Serikali kubaini wafanyabishara walipo ili kuwapelekea Maendeleo kwa wepesi na haraka zaidi, tofauti na ilivyo hivi sasa, ambapo ni vigumu mipango ya Serikali kuzifika biashara ndogo ndogo zaidi ya asilimia 90 ambazo hazijasajiliwa na kutambuliwa.

19.3.   Kufungwa kwa Biashara zaidi ya 2,000 Nchini
Mheshimiwa Spika, Waziri Uchumi na Mipango, Mhe. Dr. Philip Mpango alinukuliwa na gazeti la Mwananchi, tarehe 3 Januari, 2017 akikubali kuwa Serikali imebaini kuwa karibu wafanyabiashara 2,000 wamefunga biashara zao. Gazeti hilo hilo la Mwananchi, lilimnukuu mwenyekiti wa Wafanyabiashara nchini, Bw. Johnson Minja akidai kuwa kufungwa kwa biashara hizo kunatokana na Serikali kutosikiliza kilio cha muda mrefu cha wafanyabiashara, na kuwa Serikali imeweka mazingira magumu sana ya kufanya biashara hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Suala hili la kufungwa kwa biashara nchini limetolewa angalizo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Ripoti ya IMF kuhusu utekelezaji wa Sera Tanzania (Policy Support Instrument for Tanzania) iliyotolewa tarehe 9 Januari, 2017 imeionya Tanzania kuwa moja ya masuala yanayohatarisha ukuaji wa uchumi ni pamoja na “kuyumba kwa sekta binafasi kutokana na mikakati mipya ya Serikali ya awamu ya tano” (private sector uncertainty about the government’s new economic strategies.)

Mheshimiwa Spika, kama biashara 2,000 zilizofungwa wastani kila biashara inaajiri watu 5, inamaanisha kuwa ajira 10,000 za Watanzania zimepotea kutokana na sera mbovu za uratibu wa biashara nchini zinazosimamiwa na Serikali ya awamu ya tano. Serikali imevuruga mazingira ya biashara nchini na hivyo kupelekea wananchi wengi kuishi maisha ya dhiki na taabu.
Mheshimiwa Spika, muendelezo wa sera hizi zinagharimu ajira na biashara nchini ni kinyume cha ushauri uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF tarehe 14 Aprili, 2017 Tanzania kuifikia malengo ya uchumi wa kati sharti iwe na sekta binafsi yenye nguvu na yenye mazingira bora ya biashara. Ni wazi kuwa kudorora huku kwa biashara na kuendelea kufungwa kwa biashara nchini ni ishara kuwa Serikali ya awamu ya tano haielewi inataka kulipeleka wapi Taifa letu kwa kuendelea kuharibu mazingira ya biashara nchini.
Mheshimiwa Spika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kutoa taarifa za kina kwanini biashara zaidi ya 2,000 zimefungwa nchini. Aidha, tunaitaka Serikali iseme kuwa ni hatua zipi inazozichukua ili kuondoa mdororo wa biashara nchini na hatua zilizochukuliwa kuzuia kuendelea kufungwa kwa biashara nyingine nchini.

19.4.  Hali Duni ya Wafanyabiashara Wadogo
Mheshimiwa Spika, Taifa letu limekosa dira muafaka (a right vision) juu ya kuendeleza watu wake kupitia sekta isiyo rasmi iliyojaa wafanyabiashara wengi wa biashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga. Kwa ufupi, Tanzania kwenye sekta ya Biashara ni Taifa la wachuuzi, ambao kwa muda mrefu biashara zao zimekuwa zikiathiriwa na ukosefu wa dira muafaka ya Serikali kuhusu biashara ndogo ndogo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inaendelea kusisitiza kuwa ‘Maendeleo ni ya watu na sio ya vitu’ hivyo ni jukumu la Serikali kuangalia Maendeleo ya kila mtu mmoja mmoja kwa makundi yao kama vile ilivyo kwa kundi la wafanyabiashara ndogondogo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pamoja na kufanya tafiti mbalimbali kupitia mashirika yake mbalimbali lakini inashindwa kuzitumia tafiti hizo kwa umakini wakati wa kupanga vipaumbele kwenye sekta ya ukuzaji wa biashara kwa ajili ya Maendeleo ya watu nchini.
Mheshimiwa Spika, Moja ya tafiti ambazo hazitumiki ipasavyo na kwa kiwango cha kuridhisha katika kupanga Maendeleo ya wafanyabiashara ndogo ndogo ni pamoja na utafiti uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2012 juu ya Sekta ya Biashara za Chini, Ndogo, na Biashara za Kati (National Baseline Survey Report – Micro, Small and Medium Enterprises in Tanzania).

Mheshimiwa Spika, Utafiti huo ulibaini kuwa vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 25 na 34 ndio kundi kubwa kwa asilimia 36 linalojihusisha na biashara ndogo ndogo nchini, wakati kwa ujumla wake asilimia 14.6 hawajawahi kumaliza elimu ya shule ya msingi, na asilimia 73.5 ndio wamemaliza elimu ya shule ya msingi na asilimia 72.1 katika maisha yao yote hawajawahi kabisa kupata mafunzo yoyote kabla hawajaanza biashara. Bila kuwa na ‘picha kubwa’ yaani maono makubwa ya kuliangalia taifa letu miaka 100 mbele, taifa haliwezi kupiga hatua za Maendeleo ya kibiashara kwa haraka, bali tutaenda kwa kusuasua kama ilivyo hivi sasa.

19.5.  Hasara Benki za Biashara zinazochangiwa na Sera za Serikali
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano imendelea kuasisi sera mbovu ambazo zinaathiri sekta ya fedha inayotarajiwa kuimarisha sekta binafsi nchini. Sekta Binafsi imeendelea kuyumba kutokana na Sera ya Serikali ya kuzuia mashirika ya Serikali kutunza fedha katika mabenki ya kibiashara na kuondoa jumla ya Shilingi bilioni 5 kutoka mabenki ya biashara na kuzitunza katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu (BoT).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini kuwa ongezeko la riba za mikopo katika benki za biashara linatokana na uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano kuondoa fedha katika mabenki ya biashara jambo lililopunguza kiasi cha fedha ‘liquidity’ na kupelekea kupungua kwa amana katika benki hizo jambo linalolazimisha benki za biashara kuongeza kiwango cha riba ili kujipatia unafuu wa kibiashara.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali kuondoa fedha katika mabenki ya biashara ni hatua ya kuamua kuiangamiza sekta binafsi ambayo inauhusiano wa moja kwa moja na ukuaji wa pato la kila Mtanzania na pia ukuaji wa pato la Taifa. Mpaka sasa Benki kadhaa za kibiashara zimerekodi hasara katika hesabu zao kutokana na uamuzi huo. Gazeti la The Citizen, tarehe 11 mwezi Agosti, 2016[26]  liliripoti kuwa uamuzi wa Serikali kuhamisha fedha kwenye mabenki ya biashara kumesababisha benki kadhaa kupata hasara. Benki zilizorekodi hasara ni pamoja na Barclays Bank Tanzania (hasara ya Shilingi bilioni 8.2), TBI Development Bank (hasara ya Shilingi bilioni 6.27), Stanbic Bank Tanzania (hasara ya shilingi bilioni 2.40)
Mheshimiwa Spika, Gazeti hilo hilo la The Citizen, tarehe 31 mwezi Oktoba, 2016[27] liliripoti benki kadhaa kuendelea kupata hasara iliyopelekewa na uamuzi wa Serikali kuondoa fedha katika mabenki ya biashara. Benki zilizorekodi hasara ni pamoja na CRDB Bank (hasara ya shilingi bilioni 1.9) na Amana Bank (hasara ya milioni 195)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kutekeleza sera za kutunza fedha za umma kwenye akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu, sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulielezea Bunge lako tukufu kuwa ni hatua zipi inazozichukua ili kuhakikisha mifumo ya matumizi ya fedha za umma katika mashirika ya umma na Serikali kuu inaimarishwa ili kuzia ubadhirifu, wizi, ufisadi wa kimikataba na kuziba mianya ya rushwa kubwa kubwa za kimfumo zinazowanufaisha ‘PEP’ (Political Exposed Personalities) kama vile Wakurugenzi, Makatibu wakuu, na Mawaziri na viongozi wa ngazi za juu zaidi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ya awamu ya tano kuelewa kuwa njia salama ya Serikali kuzuia wizi, ubadhirifu, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma sio kuzificha fedha katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu; kwa kuwa, kwa vyovyote vile, lazima zitatolewa ili zikatumike kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya umma, njia sahihi ya kuzuia wizi ni kuimarisha usimamizi wa fedha (finance management) ndani ya mashirika ya umma na Serikali, kuimarisha sera za matumizi ya fedha kwenye miradi ya kimkakati na kuziba mianya ya rushwa katika mifumo rasmi ya matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Spika, Mtindo unaotumiwa na Serikali ya awamu ya tano kutuza fedha za umma Benki Kuu badala ya kuziweka kwenye benki za biashara ili zisisimue uchumi wa nchi na kuimarisha sekta binafsi kwa kukuza biashara nchini ni njia za kizamani (traditional methods), zimepitwa na wakati na hazina tofauti na baba wa nyumba anayeficha fedha kwenye kibubu chini ya uvungu wa kitanda wakati angeweza kwenda kuzihifadhi katika amana za benki ili ziingizwe katika mfumo rasmi wa mzunguko wa fedha.

20.      WINGI WA KODI KATIKA SEKTA YA UTALII NA ATHARI ZAKE KATIKA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, ni masikitiko makubwa kuona kwamba serikali ya Chama cha Mapinduzi katika mapendekezo yake ya bajeti haijazungumzia kwa namna yoyote uboreshaji wa sekta ya utalii. Ni masikitiko makubwa kwa sekta binafsi zinazopambana kuhakikisha zinachangia pato la taifa yaani GDP kwa 17.5% kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya Benki Kuu ya mwaka 2016, sekta inayotoa takribani ajira rasmi 500,000 na jumla ya ajira zisizo rasmi 1,500,000 kwa mwaka kuona kuwa bajeti hii haijachukua mapendekezo yao licha ya sekta binafsi katika utalii kuonyesha vyanzo mbadala vya mapato. Wafanyabiashara katika sekta ya utalii ndio wanao kamuliwa kodi nyingi na kuwekewa mazingira magumu ya biashara. Serikali ya CCM imesahau kabisa ili ng’ombe aweze kukamuliwa maziwa vizuri ni lazima aweze kulishwa vizuri. Bajeti hii ya Serikali ya awamu ya tano haijawagusa kabisa maelfu ya wananchi wanaoishi na kujipatia riziki na kulipa kodi kwa kupitia sekta hii ya utalii. Hii ni bajeti ya ajabu kabisa ambayo haijawahi kutokea. Ni bajeti inayokwenda kuizika sekta ya utalii ambayo kihistoria imekuwa ni sekta ya pili baada ya kilimo katika kuchangia pato la taifa na kipato cha wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Spika, ni ajabu kabisa bajeti hii ya serikali ya CCM haijaanisha vipaumbele vyake katika sekta ya utalii wala vyanzo vipya vya mapato vinavyotokana na utalii huku nchi yetu ikiwa na utajiri mkubwa wa rasilimali asili. Wakati nchi ya Kenya ikitoa kipaumbele katika sekta ya utalii ambayo uwekezaji wake ni mdogo na ikilinganishwa na faida (low investment - high return).Nchi hiyo imeainisha chanzo chake kipya cha mapato katika utalii ikiwemo utalii wa michezo (sport tourism), utalii wa fukwe (beach tourism) na utalii wa huduma ya afya (medical tourism) kama ilivyo kwa nchi ya India iliyowekeza zaidi katika huduma za matibabu ambapo wageni kutoka nchi mbalimbali hutembelea katika nchi hiyo kwa dhumuni la kununua huduma za kitabibu. Kwa mwaka 2012 nchi ya India iliingiza takribani dola za kimarekani bilioni 22.2 kwa huduma za kitabibu pekee. Pamoja na hilo nchi ya India imekuwa ikijipatia fedha nyingi za kigeni kwa kuuza visa za matibabu yaani (medical visas).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 serikali ya Kenya imejikita katika ukarabati mkubwa wa ngome ya Yesu (Fort Jesus) ya Mjini Mombasa kama chanzo kikuu cha kuongeza mapato huku ikiboresha huduma katika viwanja vya ndege, maeneo ya kupumzikia na kutafuta masoko ya watalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hapa Tanzania mambo ni tofauti kabisa kwani serikali imejikita kufanya siasa na hadaa kwa Watanzania kama ilivyozoea, kwani bajeti iliyowasilishwa na serikali imejikita katika kutoa ahuweni kwa watu wa tabaka la juu na kati huku zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania masikini waishio vijijini ikiwa haijawagusa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, huko vijijini ndiko kuna mbuga mbalimbali za wanyama, ndiko wananchi wanapotunza hifadhi za misitu yetu, ndipo kwenye WMA’s ambazo kimsingi ndizo zinazosaidia uharakishaji wa maendeleo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi.Hivyo basi, kushindwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya maliasili na utalii ni dhahiri kuwa hakujawagusa moja kwa moja wananchi hawa.
Mheshimiwa Spika, kukumbuke kuwa kufutwa kwa ada ya mwaka ya leseni ya magari haina mguso wa moja kwa moja kwa mwananchi anayeishi katika lindi la umaskini vijijini. Lakini kwa  kuboresha mazingira ya uwekezaji katika utalii wa asili (cultural tourism),kuboresha WMA’s, kutoa kipaumbele cha ajira katika maliasili zetu ,kuwekeza katika mazingira ya hifadhi na misitu kuna faida ya moja kwa moja kwa wanachi hawa. 
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa tisa na kumi wa kitabu cha hotuba ya Waziri kifungu kidogo cha (iv) na (vii) vinaelezea kwamba serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinawanufaisha wananchi. Ni lazima hapa tujiulize wananchi hawa wananufaika vipi na maliasili endapo serikali hii haiwajali wala kuthamini mchango wa sekta binafsi. Jambo hili limejidhihirisha wazi katika ukurasa wa 22 na 23 wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha  2017/18. Serikali imejinasibu kuwa inaamini sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na inathamini sana na kupongeza mchango mkubwa wa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, serikali imekwenda mbali zaidi na kujitutumua kuwa imendelea na jitihada za kuimarsiha utulivu wa uchumi,kupunguza urasimu,kuharakisha maamuzi,kuimaisha ulinzi na usalama na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu ikiwemo umeme na mikopo. Mambo haya yanayosemwa na serikali hii ya CCM ni mambo ya ubabaishaji kabisa na usanii mtupu. Katika sekta ya utalii imeghubikwa na urasimu wa kutisha kuanzia kwenye kufungua kampuni na kulipa kodi, msururu wa tozo zinazowanyonya wafanyabiashara, rushwa ya kutisha, upendeleo kwa makampuni makubwa yale yanayolinda maslahi ya watu wachache, na kauli zinazokatisha tamaa zinazotolewa na viongozi wakubwa wa serikali ambazo kimsingi zina athari za moja kwa moja katika ukuaji wa sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Spika,  mnamo Mwezi Julai 2016, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Fedha 2016/2017 (Finance Act 2016/2017). Sheria hiyo ilianzisha kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT kwa asilimia 18 kwenye shughuli za utalii. Katika maelezo ya Waziri wa Fedha alieleza kwamba kuongeza kwa kodi hiyo ni mpango wa serikali wa kukusanya kodi na kuongeza mapato ili kuondokana na utegemezi,kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na shughuli za utalii
Mheshimiwa Spika, wakati huo huo katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Mwaka wa fedha 2016/2017 ya nchini Kenya serikali iliamua kuondoa gharama ya VAT ya 16% katika huduma za utaliii. Kwa mujibu wa taarifa ya SATOA (www.satoa.com) ya tarehe 15/06/2016 yenye kichwa cha habari “Tanzania Tourism Industry worry about VAT on services” ambayo ilianisha kwa kina sababu hasa ya nchi ya Kenya kuondoa kodi hiyo ya VAT ambapo kimsingi iliondolewa ili kuisaidia nchi hiyo kuweza kumudu soko la ushindani ambalo lilikuwa limeathiriwa na changamoto za kisiasa na matishio ya ugaidi. Lakini zaidi ikiwa ni moja ya mbinu ya kibiashara katika kuwavutia watalii wengi zaidi ambapo wanaweza kupata huduma ya utalii kwa gharama nafuu na kwa ubora zaidi kuliko nchi nyingine yoyote Afrika Mashariki. Mwaka 2013 sekta ya utalii nchini Kenya ilianguka kwa 4.6 % kutokana na matishio ya ugaidi na mpaka mwaka 2016 sekta ya Utalii nchini humo imekuwa kwa 15% huku Tanzania ikikuwa kwa 11% pekee.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri katika nchi za Afrika Mashariki nchi ya Kenya ndio mshindani hasa wa nchi yetu katika ushindani wa biashara ya utalii. Ni lazima tujue kuwa na mshindani katika biashara ni jambo zuri ambalo linatupa changamoto ya kubuni mbinu zaidi ili kuweza kuimarisha biashara hiyo. Kwa mantiki hiyo kama taifa tuna kila sababu za kuhakikisha tunakuwa na mbinu bora ili kuweza kuongeza idadi ya watalii.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maliasili na utalii kwenye semina kuhusu umuhimu wa uhifadhi ya Mwezi Mei 2017, inaonyesha kwamba idadi ya watalii walioingia nchini kwa mwaka 2016 ni 1,284,279 ambapo kwa nchini Kenya waliingia watalii 1,307,351. Hii inaonyesha kuwa kuna watalii 23,073 zaidi walioingia nchini Kenya. Ikumbukwe kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa wingi wa vivutio vya maliasili lakini katika ushindani wa kibiashara ni nchi ambayo haifanyi vizuri ikilinganishwa na Kenya.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya serikali ya Kenya 2017/2018 imeondoa VAT katika kuunda bodi za magari ya utalii ili kuwavutia wafanyabiashara wa utalii kuweza kuunda magari hayo maarufu kama (hardtop) kwa shughuli za utalii nchini humo kwa bei nafuu zaidi. (Kenya exempted locally assembled tourist vehicles in a move aimed at encouraging tour operators to buy locally assembled vehicles at a lower cost). Hii ina maana kwamba hata wafanyabiashara wa sekta  ya utalii kutoka Tanzania watavutiwa kwenda nchini Kenya kuunda magari yao kwa bei nafuu. Mpaka sasa biashara hii ya kuunda bodi za magari , pamoja na viti inafanyika sana hapa nchini.Kwa bei ya kuanzia shilingi milioni 50 kwa gari. Kwa tafiti mbalimbali za masoko ya magari zinaonyesha kuwa kwa sasa bei ya magari haya ya kitalii huanzia shilingi milioni 150 mpaka milioni 170. Hivyo basi kuondoa VAT kwenye kuunda magari haya ni msaada mkubwa sana kwa wafanyabiashara na hivyo ni wazi kuwa tutapoteza wateja ambao walikuwa wakiunda magari haya hapa nchini kutokana na gharama kubwa na hivyo serikali kupoteza mapato hayo kabisa.
 Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo serikali  imeshindwa kuwasaidia kabisa wawekezaji wa ndani na nje kwa kuwabebesha mzigo mkubwa wa kodi ambao hauendani kabisa na mapato wanayoyapata kutokana na shughuli za utalii. Pamoja na kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imelizungumzia sana jambo hili na kutoa ushauri mara kwa mara bado Serikali ya CCM kwa mwendo ule ule wa kupuuza mambo imeendelea kuwatoza wafanyabiashara takribani kodi 36 ambapo kati ya kodi hizo 12 ni za usajili wa biashara na udhibiti wa leseni (business registration and regulatory license fees),11 zikiwa ni ada mbalimbali za usafiri na usafirishaji wa watalii  (duties for tourist vehicles) na 13 zikiwa ni tozo nyinginezo (miscellaneous fees) na hivyo kuifanya Tanzania kuwa  ni nchi yenye gharama kubwa zaidi  katika huduma za utalii Afrika ya Mashariki kwa zaidi ya 25% tofauti na miaka ya nyuma ambapo Tanzania ilikuwa na gharama zaidi kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa 7%.
Mheshimiwa Spika, tukirejea kauli ya Rais aliyoitoa tarehe 18 Julai, 2016 akiwaapisha Wakuu wa Mikoa alizungumzia suala la  tozo za kodi katika shughuli za utalii alisema “ni bora waje awatalii wachache wanaolipa kodi kuliko kuja watalii wengi wasiolipa kodi”.Ni dhahiri kuwa kwa kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais katika suala hili la kodi katika sekta ya utalii ni kuwa alipitiwa au hakuwa na maelezo ya kutosha kuhusiana na wingi wa kodi katika sekta hii ambayo wawekezaji wengi wameanza kuikimbia kutokana na mzigo mkubwa wa kodi unaowaumiza hasa wawekezaji wazawa.
Mheshimiwa Spika, Ongezeko kubwa la kodi katika sekta ya utalii limekuwa na madhara makubwa ya kibiashara kwa wawekezaji, madhara kwa uchumi wa nchi na hata uchumi binafsi wa wale wanaoitegemea sekta hii kwa ajili ya kujipatia kipato tofauti kabisa na maelezo ya Waziri aliyoyatoa tarehe 24 Mei 2017 alipokuwa akihitimisha hoja
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hoteli maarufu zilizokuwa zinategemewa na watalii wengi hapa nchini zimefungwa na nyingine kubadilisha matumizi yake kutokana na kushindwa kujiendesha kutokana na kuporomoka kwa soko. Mfano kwa Mwaka 2016 pekee Hotel ya Land Mark ilibadilishiwa matumizi na kuwa hosteli za wanafunzi, kufungwa kwa  hoteli zote za JB Belmont za Dar es Slaam na Mwanza zilifungwa kutokana na madeni na kushindwa kujiendesha, Impala hotel,  Ngurdoto Arusha, Malindi hotel, Mtendele hotel , Mount Meru hotel Arusha pamoja na kampuni mbalimbali yakiwa na hali mbaya na hivyo kuamua kupunguza wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, kufungwa kwa hoteli , kubadilisha matumizi ya hoteli hizi za kitalii au kwa makampuni  makubwa ya utalii ni ushahidi tosha kuwa sekta ya utalii nchini iko katika hali mbaya. Jambo hili la wazi kabisa halihitaji mbwembwe na kelele za kisiasa za kuendelea kuwadanganya Watanzania na tarakimu zisizo na tija.  Hivyo ni lazima kutafuta mbinu mbadala za kibiashara ikiwa ni pamoja na mbinu ya kutafuta masoko na kuvutia wateja ikiwa ni pamoja na kupunguza kodi zisizo za lazima kwa wafanyabiashara ili waweze kuboresha huduma. Endapo wafanyabiashara hawa wataboresha huduma ni dhahiri kuwa watalii wengi zaidi watavutiwa kuingia Tanzania kutokana na kuwepo kwa maliasili za kipee kabisa.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii imekuwa ikitumia fedha nyingi kupitia Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu yenye Manaibu Mawaziri wawili katika kutafuta ajira kwa vijana.  Tujiulize Wizara hii ina faida gani kama imeshindwa kumshauri Mheshimiwa Rais katika kuona umuhimu wa kutumia kauli itakayowatia moyo zaidi wafanyabiashara ili waboreshe huduma na kuwavutia watalii wengi zaidi na hivyo wananchi wapate ajira. Katika biashara ya ushindani kauli ni mali. Tunatambua kabisa kauli ya Mheshimiwa Rais ni  amri na hivyo ni  sawasawa na sheria (presidential decree) hivyo kutokana na uzito wa kauli zake ni vyema zikapimwa ili zisiwe na madhara  katika uchumi na hivyo kuathiri jamii nzima.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuyumba kwa sekta hii ya utalii serikali ya CCM ituambie imejiandaaje kuhakikisha inakabilina na athari za wimbi kubwa la vijana kukosa ajira  ikiwa ni pamoja na matokeo yake kama vile kuongezeka kwa uhalifu nchini,utelekezaji wa familia,Watanzania hawa kushindwa kulipa kodi nyingine mbalimbali na kununua huduma kama vile afya, elimu, chakula, na nyinginezo ambazo ni muhimu kwa binadamu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo ni dhahiri kuwa serikali itapoteza mapato.Katika tafiti mbalimbali za utalii kwa  wastani wageni wanaokuja nchini huja na fedha za ziada yaani Pocket money ambapo wengi huja na zaidi ya $ 6,000 kwa wastani . Fedha hizi huingia katika mizunguko mbalimbali ya kibiashara inayoinufaisha nchi pamoja na wananchi. Endapo wafanyabiashara wataelemewa na mzigo wa kodi na kushindwa kufanya biashara katika soko la kibiashara la ushindani basi ni dhahiri watalii watapungua na serikali itakosa mapato.
Mheshimiwa Spika, athari nyingine inayojitokeza ni uzoroteshaji wa wazi wa sera ya diplomasia ya kiuchumi. Mpaka sasa taifa letu lina tatizo kubwa la kushindwa kutekeleza sera ya diplomasia ya kiuchumi.Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikilizungumzia jambo hili kwa kina sana lakini ni wazi kuwa kukosekana kwa maono na watu wenye maono ndani ya serikali ya Chama cha Mapinduzi kunasababisha watu hao kushindwa kumshauri Mheshimiwa Rais ipasavyo ili kuona umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya  utalii kwa jicho pana zaidi. Mfano, Katika nchi ya Kenya ambayo ina vivutio vichache zaidi kuliko Tanzania  inapokea wageni wengi zaidi kwa mwaka ikilinganishwa na Tanzania. Hii ni kwa sababu nchi ya Kenya kwanza inapeleka Mabolozi wenye ujuzi na uwezo mkubwa wa kiakili ( great minds) katika balozi zake ili kuweza kutafuta masoko  ya kimataifa ya kibiashara ya utalii (foreign markets),wenye uwezo wa kiushawishi kwa wawekezaji wakubwa kwenye sekta hii (skills in sensitizing potential foreign investors), wenye uwezo mahususi katika lugha za kimataifa ( competent in key international languages) ambao wana uwezo wa kushikiri katika makongamo makubwa ya kibiashara ili sasa waweze kuwasaidia wawekezaji hasa wa ndani katika kuwapungumzia mzigo mkubwa wa kodi na tozo mbalimbali ambazo serikali ya CCM inadhani kuwawekea mrundikano wa  kodi serikali itapata mapato. Hii ni aibu kubwa kwa nchi na wachumi ambao humshauri Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, serikali ya awamu ya tano itambue kuwa nchi yetu imeingia katika mikataba mbalimbali ya kulinda haki za watalii na kanuni za utalii (tourism bill of rights and tourist code ).Moja ya mikataba hii ni ile iliyotokana na Azimio la Bulgaria la mwaka 1985 ambalo  linatambua jukumu jipya la utalii ikiwa ni pamoja na kunyanyua maisha ya watu wote,kama njia ya kuleta amani na mahusiano bora duniani “it recognizes the new role of tourism as an appropriate instrument for improving the quality of life of all people and as a vital force for peace and International understanding and defines the responsibility of States for developing tourism and in particular ,for fostering awareness of tourism among the people of the world and protecting and enhancing the tourism resources which are part of mankind’s heritage.
Mheshimiwa Spika, hii ikiwa na maana kwamba biashara ya utalii ina kazi muhimu zaidi ya kuleta au kuboresha mahusiano baina ya nchi yetu na mataifa mengine. Hii ni pamoja na kuondoa dhana kuwa watalii wanaokwenda kwenye nchi nchi nyingine ni watu wenye fedha nyingi; bila kujali haki zao kimsingi ikiwa ni pamoja na kujifunza, kupumzika na kuburudika.Serikali ya CCM ielewe kuwa  Watalii wanaotembelea nchi nyingi za Afrika ni wale wenye uchumi wa kati. Hivyo hujinyima na kujichanga ili waweze kuja kutembelea hifadhi na vivutio vingine katika nchi zetu.Hatuna budi kuhakikisha kuwa nchi yetu inanufaika na safari zao lakini pia serikali inapaswa kutokuwatoza tozo nyingi zenye kuwaumiza na kuwafanya watalii hao kushindwa kutembelea vivutio hivi ambavyo ndio fahari yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa mustadha wa sekta hii ya utalii, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri serikali kufanya yafuatayo:
1.   Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri Kamati ya Bajeti ihakikishe kuwa sekta ya utalii inatambuliwa katika bajeti hii hasa kwa kuzingatia umuhimu wake mkubwa katika kuchangia pato la taifa yaani GDP.Kwani kwa kupunguza kodi zizsizo za lazima na masharti magumu kwa wafanyabiasha katika sekta hii kutayafanya makampuni ambayo hayajasajiliwa (kampuni bubu) kujitokeza kufanya biashara kihalali kutokana na unafuu wa kodi. Kwani mpaka sasa kuna makampuni zaidi ya 700 ambayo hayajasajliwa kutokana na ugumu wa masharti ya kuanzisha biashara ikiwa ni pamoja na idadi ya magari na kodi ya leseni.Badala ya wafanyabaisha hawa kuanza kufanya biashara akiwa na gari tatu (3) ambapo kwa gari moja linagharimu milioni 150-200, na hvyo kufanya jumla ya milioni 450-600 kwa ununuzi wa magari pekee ambapo Mtanzania wa kawaida hawezi masharti haya, au kutoza dola 2000 kwa leseni ya kuanza biashara ambayo ni sawa na shilingi milioni 4,474,000, huku kukiwa na ada nyingine zaidi ya 35 ni uonevu mkubwa kwa wananchi wenye nia ya dhati ya kuwekeza katika sekta ya utalii.Hivyo ni muhimu masharti haya yakapunguzwa ikiwa ni pamoja na kuondoa VAT, na kodi zinazojirudia rudia bila ulazima wowote
2.   Kuzingatia ushauri unaotolewa mara kwa mara na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, serikali ituambie ni nini kipaumbele chake katika sekta ya utalii nchini. Na je, inawekeza katika vyanzo vipi vya mapato ili faida (return of investment) iweze kupatikana na kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni (foreign currency)
3.   Katika Malengo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017-2020/2021 serikali ilijiwekea lengo la kufikisha watalii milioni 2 na kuhakikisha kuwa mpaka mwaka 2020 Tanzania itakuwa na jumla ya vitanda 1,735,000 seikali ituambie inatumia mikakati gani kufikia ili sasa kama nchi tuweze kumudu soko hili la uhsindani ndani ya Afrika Mashariki kwani mpaka mwaka 2016 nchi ya Kenya ilikuwa na takribani vitanda milioni 3.6 ikiwa ni ongezeko la 14.6 % ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo ilikuwa na vitanda 3.1huku Tanzania tulitaka kufikia idadi tajwa tu kwa mwaka 2020.
4.   Serikali kuanzisha kituo kimoja mahususi cha kulipia tozo mbalimbali (onestop centre) kuliko ilivyo sasa ambapo huchukua takribani masaa 2,000 kwa mwaka katika ulipaji wa tozo mbalimbali katika sekta ya utalii kama ilivyoelezwa kwenye utafiti wa Dr.Sinare.
5.   Serikali kuangalia upya utalii wa asili (cultural tourism) kwa kuwaalika wawekezaji katika maeneo hayo pamoja na kuvitambua vivutio mbalimbali kama jambo la kisera ili vivutio kama hot springs,maeneo ya camping, maeneo ya kihistoria, maeneo yenye jiografia na sifa za  kipekee ambayo yanaweza kuendeshwa na halmashauri na  kuwa sehemu ya mapato ya halmashauri.
21.      KATIBA MPYA NA UCHUMI WA NCHI
Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa Katiba ndio sheria mama. Katiba ndio taswira hasa ya taifa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na hata katika mambo mbalimbali ya utoaji wa huduma kwa wananchi .Katiba ndio msingi wa utoaji haki na wajibu wa kila raia.   Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa kuwa na Katiba Mpya inayokidhi matakwa ya wananchi na inayoendana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na hata kutatua kero mbalimbali za kijamii serikali ya awamu ya Nne iliona ni vyema ikatoa fursa kwa wananchi kuleta maoni yao kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka ili kuweza kunufaika kwa pamoja kama taifa.
Mheshimiwa Spika, hakuna uchumi bora wa nchi kama hakuna Katiba bora. Katiba  ndio chombo pekee cha kulinda uhuru wa kila raia, ni chombo cha kuonyesha dira ya kule tunapotaka kuelekea  na miiko yetu kama taifa. (Constitution is the only safeguard of our liberties; it is a solid expression of our vision and values as a nation). Kwa mantiki hiyo hatuwezi kamwe kuendelea kiuchumi kama hatuna katiba inayotoa taswira ya kule tunapotaka kwenda.
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa Katiba mpya ;rasimu ya pili ya katiba imejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulisadia taifa hili kujikwamua kutoka katika lindi la umaskini wa kujitakia, maradhi na ujinga uliopindukia  uliosababishwa na Chama cha Mapinduzi na serikali zake zote zilizotangulia Rasimu hii pia  inazungumzia mchakato wa kupata viongozi katika ngazi mbalimbali, muundo wa tume huru ya uchaguzi ambapo inapendekeza tume hiyo iteuliwe na tume maalum kuliko ilivyo sasa ambapo tume huteuliwa na Mwenyekiti wa Chama tawala, Katiba pendekezwa ya wananchi inalenga maadili ya viongozi wa umma, mamlaka ya viongozi ambayo hayawezi kukiuka haki za binadamu, lakini zaidi rasimu hii ya pili ya katiba inaonyesha taswira ya taifa huru, lenye watu huru ,mawazo huru na yanayojikita kuheshimu maamuzi ya wananchi kuliko ilivyo sasa ambapo Katiba tuliyonayo inawapa viongozi wengine mamlaka yanayopitiliza kitendo ambacho kinaweza kuhatarisha haki za raia, vyama vya siasa, na kuingiza nchi yetu katika utawala wa kiimla au udikteta jambo ambalo ni hatari sana kwa amani na usalama wa nchi yetu na pia ni hatari kwa uchumi wa wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa matamanio ya kuwa na katiba mpya; serikali ilitumia mabilioni ya fedha  ikiwa ni sawa na fedha za maendeleo za Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Kilimo, Wizara ya elimu, Wizara ya maji na Umwagiliaji, Maliasili na Utalii, Wizara ya Afya,Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2016/2017 pekee kama ilivyoainishwa kwenye fedha za maendeleo za Wizara mbalimbali kwenye kitabu cha Matumizi ya Maendeleo Juzuu ya Nne kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mabilioni hayo yaliyotumika serikali ilitumia muda mrefu wa takribani miezi mitatu ikijumuisha wajumbe zaidi ya 600 ambapo kila mjumbe alilipwa posho isiyopungua shilingi 300,000 kwa siku huku watendaji mbalimbali nao wakilipwa posho. Hii ikiwa na maana kwamba fedha za walipa kodi wa nchi hii ndizo zilizotumiwa na serikali ya CCM katika kutafuta Katiba mpya . Kwa umuhimu huo miradi ya huduma za kijamii kama maji, hospitali, madawa, nishati ya umeme ambapo huduma hizi muhimu kwa kila mwananchi hazikupewa kipambele kwa wakati huo kama mchakato wa Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika, kila raia wa nchi hii alitambua umuhimu wa kuwa na katiba mpya ambayo ilikuwa tegemeo la matumaini mapya ya kuwepo kwa utawala bora ambao ungechochea kasi ya ukuaji wa uchumi  na kujenga dhana ya uwajibikaji kwa kila raia na viongozi wao. Kinyume na mategemeo ya wananchi walio wengi mchakato wa upatikaji wa Katiba Mpya umekuwa  na kiza kinene hasa katika serikali hii ya awamu wa Tano chini ya John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 4, Novemba 2016, Mheshimiwa Rais alinukuliwa akisema hakuwahi kuzungumzia Katiba mpya wakati wa kampeni zake, kwa hiyo katiba  siyo kipaumbele chake na kwamba anachotaka kwanza ni kunyoosha nchi. Kauli hii ya Mheshimiwa Rais inataka kutuaminisha kuwa fedha zote zilizotumika katika mchakato huu ni kwamba zimekwenda kwenye mifuko na matumbo ya watu bure. Inaaminisha kuwa muda uliotumika katika kutafuta maoni ya wananchi umepotea bure, imenyang’anya sauti Mwenyekiti wa tume, na zaidi ya yote inaonyesha dhahiri kupuuzwa kwa sauti za wananchi ambapo ndio wenye mamlaka ya kuiweka serikali yoyote madarakani.
Mheshimiwa Spika, nchi hii haiwezi kunyooka kama hakuna Katiba mpya ambayo imezingatia maoni ya wananchi na sio ile iliyopendekezwa na kikundi fulani au iliyofanyiwa uhuni wa kuyaondoa yale yanayopendekezwa na wananchi wenyewe. Nchi inaweza kunyooka tu pale ambapo Katiba yake inatoa taswira chanya ya namna bora ya kunufaika au kumiliki na  kulinda rasilimali za nchi, na zaidi nchi inaweza kunyooka pale inapokuwa na  katiba yenye kujenga umoja wa kitaifa, katiba yenye kuzingatia ugawaji wa mapato, mfumo mzuri wa kimaamuzi, fidia kwa shughuli za uwekezaji katika rasilimali hasa madini na gesi na zaidi katiba inayolinda matarajio ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, imeweka misingi ya uwajibikaji katika usimamizi wa maliasili ya Taifa kama inavyosomeka kwenye Ibara ya 27 (1) na (2) na Ibara ya 28 (1) ya Katiba.
(1)        Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano,mali ya Mmlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi ,na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine
(2)        Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi nay a pamoja ,kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhiifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.
28 (1) Kila raia ana wajibu wa kulinda,kuhifadhi na kudumisha uhuru,mamlaka,ardhi na umoja wa taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa vifungu hivi katika Katiba ya Mwaka 1977 bado maliasili za nchi hii kama wanyamapori, misitu, madini, gesi, hewa, mafuta, maji na uvuvi, na hata mgawanyo wa ardhi umegubikwa na rushwa. Rasilimali zetu hususani madini na wanyapori yamekosa usimamizi mzuri kiasi kwamba wachache ndio wanaonufaika na wananchi wetu hususani wale wanaozunguka maeneo hayo wamebaki kuwa maskini wa kutupwa. Vijiji vinavyozunguka misitu ya hifadhi na migodi imekuwa ikikumbwa na mapigano ya mara kwa mara,manyanyaso makubwa kutoka kwa baadhi ya wawekezaji na hata vifo kwa raia wema wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika,mfano dhahiri ni mauaji yaliyowahi kutokea katika mgodi wa Geita ambayo yamekuwa yakiripotiwa ikiwa ni pamoja na  mauaji ya mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Kivukoni  marehemu Hoja Juma, vitendo vya mauaji, utesaji na kuwabambikizia kesi wanavijiji  katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara (NMGM), madhara ya kiafya pamoja na ucheleweshaji wa fidia katika maeneo mbalimbali ambayo serikali imewakaribisha wawekezaji bila kujali mustakabali wa wananchi katika maeneo hayo. Katika bonde la Loliondo wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakiishi kama wakimbizi kutokana na manyanyaso makubwa wanayopata kutoka kwa baadhi ya wawekezaji wa kigeni huku serikali ikiyafumbia macho kutokana na rushwa kubwa kubwa zinazowanufaisha vigogo wa juu serikalini. Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikiipigia kelele kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) kutoka falme za kiarabu ambae amekuwa mwiba mkubwa kwa wananchi wa Loliondo na kuona kama wametengwa katika taifa lao.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo kwa malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kuhusu ushirikishwaji katika maamuzi yanayohusu utumiaji wa maliasili katika maeneo yao. Wananchi  katika maeneo mbalimbali yenye rasilimali wamekuwa wakiyatunza vizuri na bila uharibifu wowote lakini pale wanapoanza kuletwa wawekezaji bila kuwashirikisha na kinyume na matarajio yao basi wananchi hao wamekuwa wakileta vurugu jambo ambalo sio afya kwa wawekezaji na haileti taswira nzuri katika sekta ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje. Mfano, vurugu zilizowahi kutokea Mwezi Januari na Februari mwaka 2013 mkoani Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza kwa kina sana katika hotuba ya nishati na madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kuhusu katiba na mustakabali wa madini, mafuta na gesi asilia ikitoa mifano hai ya uzoefu wa  nchi mbalimbali  zilizofanikiwa baada ya kutatua changamoto mbalimbali za kikatiba, kisheria na kisera ili kulinda rasilimali za nchi. Mfano, nchi ya Norway imeweka mwongozo wa uwajibikaji katika matumizi ya maliasili kwenye Katiba yao Ibara ya 110 (b) ambapo ibara hiyo inasema “every person has a right to an environment that is conducive to health and to natural surroundings whose productivity and diversity are preserved. Natural resources should be made use of on the basis of comprehensive long-term considerations whereby this right will be safeguarded for future generations as well”. Mwaka 2009 nchi ya Bolivia ilianza mchakato wa kupata katika mpya ambao pamoja na mambo mengine katiba hiyo ililenga kuhakikisha kuwa mafuta na gesi asilia yanawanufaisha wananchi wa Bolivia.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi ni dhahiri katiba ya sasa ya mwaka 1977 haitaweza kutuhakikisha kuwa rasilimali zetu zinatukomboa katika lindi la  umaskini ambao umetukabili kwa takribani miaka 56 sasa hata baada ya uhuru. Msimamo wa katiba pekee ndio utakaoweza kufafanuliwa vizuri katika sheria zetu zinazolinda rasilimali zetu. Mfano, katika Katiba ya Bolivia imeeleza bayana kuwa serikali ya nchi hiyo itakapoingia ubia na makampuni binafsi katika utafutaji na uvunaji wa mafuta na gesi asilia itakuwa na hisa zisizopungua asilimia hamsini na moja (51%) ya hisa zote. Jambo hili limewekwa bayana ndani ya katiba.
Mheshimiwa Spika, kwa mifano hii iliyo wazi ni kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa katika usimamizi wa rasilimali zetu na ili kujikwamua katika hili tunahitaji maoni ya rasimu ya pili ya katiba ambayo ilipendekeza  namna bora ya kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali zetu ili ziweze kumnufaisha kila mwananchi.
Mheshimiwa Spika, tulipofika sasa kama taifa hatuhitaji kuwa na katiba yenye viraka viraka. Tunahitaji kuwa na katiba mpya inayoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na ushindani wa kibiashara, mabadiliko ya kimfumo katika teknolojia, mashirikiano ya nchi mbalimbali na misimamo ya taifa na utaifa wetu, utawala bora, inayozingatia demokrasia , haki za binadamu na utawala wa sheria. Hivyo, rasimu ya pili ya katiba imetoa maoni ya wananchi ambayo kimsingi yanashabihiana na uhitaji huo.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanataka kuona katika ikiwashirikisha katika kumiliki faida zitokanazo na rasilimali zao ,ikiwa ni pamoja na michakato ya wazi ya utoaji wa leseni,katiba inayotoa mamlaka kwa Bunge kupitia na kuridhia mikataba mbalimbali inayohusu uvunaji wa maliasili ya Taifa ili kuongeza uwazi. Lakini pia, katiba itoe fursa kwa wananchi kuwa na sauti dhidi ya bunge lao, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata taarifa ya kila kinachoendelea ndani ya Bunge kwa kuwa Bunge ndio mkutano mkuu wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kurejesha mara moja mchakato wa rasimu ya pili ya katiba kwani katiba pendekezwa haikuzingatia maoni ya wananchi . Vilevile, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutatua mkwamo wa mchakato wa katiba uliojitokeza katika serikali hii ya awamu ya tano bila sababu mahususi. Kuendelea kwa mkwamo huu kunatoa taswira hasi kwa serikali ya awamu ya tano sio tu  ndani ya nchi bali pia katika medani za kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Kwa umuhimu huu wa katiba mpya Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli kurejea katika Ibara ya kwanza ya Katiba ya Japan inayosema “The Emperor shall be the symbol of the State and of the unity of the People, deriving his position from the will of the people with whom resides sovereign power”. Ikiwa na maana kwamba Mheshimiwa Rais azingatie matakwa ya wananchi katika kuwaletea kile walichokiomba kwa muda mrefu ambacho ni rasimu ya pili ya Katiba.

22.      MCHANGO WA USAFIRI WA RELI KATIKA UJENZI WA
UCHUMI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kitabu cha Mpango wa pili wa Maendeleo, kati ya mataifa 189 yanayotumia usafiri wa Reli duniani, Tanzania inashika nafasi ya 84 kiutendaji katika sekta hiyo. Hata hivyo, pamoja na Tanzania kuonekana kushika nafasi nzuri kwa wastani, bado kuna changamoto kubwa katika ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya reli.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba mkakati wa ujenzi wa Reli ya kati kwa  awamu ya kwanza kwa kujenga reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Hata hivyo, changamoto kubwa inaonekana ni upatikanaji wa fedha za kuhakikisha Reli hiyo inajengwa kwa ukamilifu wake kwa maana ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, unatarajia kukamilika mwaka 2021 na utagharimu Sh trilioni 7.6. Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi huo inahusisha kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, na tayari ujenzi huo umeshawekewa jiwe la msingi na unakadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni1.21 (Sh trilioni 2.6).
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Uhusiano kwa Jamii wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,011 (Dar es Salaam – Mwanza) umegawanyika katika awamu tano. Awamu ya kwanza ni kipande cha Dar es Slaam – Morogoro ambapo ujenzi umeshaanza; awamu nyingine itahusisha vipande vya Morogoro hadi Makutupora kilomita 336, Makutupora-Tabora (km 294), Tabora-Isaka (km 133) na Isaka-Mwanza (km 248); huku  Serikali ikiwa imetenga kiasi cha shilingi trioni 1 katika bajeti yake  kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa za kujenga reli ya kati kwa  kiwango cha standard gauge ni sababu za kiuchumi ambazo lazima zizingatiwe kwa kiwango ambacho kitaliwezesha taifa kupata faida. Kwa mantiki hiyo bado, kuna sintofahamu katika tathimini ambazo mamlaka husika zimefanya na tathimini hizo zikapelekea kufanyika kwa maamuzi ya ujenzi wa reli ya kati kutoka Da es salaam hadi Mwanza badala ya kwenda Kigoma.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali kuanza kujenga Reli ya kati  ya Dar es Salaam na Mwanza (kama taarifa inavyotolewa, japo kuwa Reli ya Kati ni Reli ya kutoka Dar es salaam kwenda mkoani Kigoma na si vinginevyo),unapaswa kuangalia vipaumbele vya maeneo ambayo shughuli za reli hiyo itasaidia kwa kuangalia takwimu ni wapi Serikali inapaswa kujenga reli ili mradi huu wa ujenzi wa reli uweze kuzalisha fedha za kujenga reli nyingine aukuliletea Taifa faida.
Mheshimiwa Spika, inavyoonekana tafsiri ya reli ya kati ambayo ilijulikana ni kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, reli nyingine inayounganishwa nayo inakuwa ni tawi la reli ya kaati na si vinginevyo. Kusema reli ya kati ni kutoka Dar mpaka Mwanza ni kupotosha tafsiri ya reli ya kati.  Kwa muktadha huo Mheshimiwa Spika, ujenzi wa  'Standard Gauge' kwa hatua hizo za awali unaotoka Dar es salaam kwenda Mwanza ulipaswa kuwa ni ujenzi wa standard gauge kutoka jijni Dar es salaam kwenda mkoani kigoma.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi nchini ya mwaka 2015/2016, takwimu zinaonesha kwamba mizigo ambayo Tanzania inahudumia kwa nchi za maziwa makuu ni tani Milioni tano kwa mwaka. Katika hizo Zambia ni 34%, Kongo ni 34%, Rwanda12% Burundi 6% na Uganda ni 2.6%. Tafsiri yake ni kwamba Ujenzi wa 'Standard Gauge' utakaotumia matrilion ya fedha wakati huo huo reli hiyo imeelekea Isaka na Mwanza maana yake ni kwamba reli hiyo itakayokuwa kwa kiwango cha standard gauge itahudumia 15% ya mizigo yote tunayoipitisha, kwa maana ya mizigo kutoka Rwanda na Uganda, wakati huo huo kama Taifa tumeacha kuhudumia mizigo 40% kwa maana ya mizigo inayotoka katika nchi za Kongo na Burundi ambayo yote inapita mkoani Kigoma.
Mheshimiwa Spika, mujibu wa aya ya 25 ya  hotuba ya Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/18 tarehe 8 Juni, 2017 ni kwamba nchi zinazofanya biashara na Tanzania kwa wingi katika bara la Afrika, ukiachilia mbali Afrika ya Kusini inayoongoza kwa asilimia 12.2; nchi inayofuatia ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ni asilimia 5.6 ikifuatiwa na Kenya kwa  asilimia 5.5
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitarajia Serikali ijenge reli ya Standard Gauge katika maeneo ya kimkakati kibiashara; na kwa maana hiyo reli ya kati ijengwe hadi Kigoma ili kuunganisha Tanzania na Congo DRC ambayo ni nchi ya kimkakati kibiashara, na pia reli ya kaskazini ijengwe kwa standard gauge na iunganishwe na reli ya Mombasa – Nairobi iliyozinduliwa hivi karibuni kwa Kenya nayo ni nchi ya kimkakati kibiasahara.
Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu haipingi ujenzi wa reli ya kati kupitia Isaka – Mwanza, lakini inapendekeza Serikali ikamilishe kwanza ujenzi wa reli hiyo hadi Kigoma kwa kuwa kule kunza mzingo mwingi kutoaka DRC na kwa maana hiyo faida itapatikana haraka.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa reli hii ya kati kwa kiwango cha standard gauge kuna fedha za Benki ya Dunia kwa ajili ya ukarabati wa reli, kiasi cha Bilioni 200, Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inasahauri kwamba, fedha hizi za ukarabati wa reli ambao upo kipindi hiki zipelekwe maeneo mengine ambayo ujenzi huu wa reli kwa kiwango cha standard gauge haufanyiki ili kuleta uwiano wa utekelezaji wa miradi hii ya reli.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani katika wasilisho lake la mwaka 2013  kuhusu bajeti ya Serikali ilipendekeza kuanzishwa kwa kodi maalum (Special Railways development levy) ya manunuzi na mauzo ya bidhaa nje. Tunapendekeza tozo ya asilimia moja (1 %) ya bei ya bidhaa zinazoagizwa toka nje na asilimia 0.5 (0.5%) ya thamani ya bidhaa kwa zile zinazouzwa nje. Mapato ya tozo hii maalumu yote yatumike kujenga miundombinu ya Reli hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kitabu cha Mpango wa pili  miaka mitano wa Maendeleo  ukurasa wa 92  kuna wakfu(Fund) wa Maendeleo ya Reli ambao ulikadiriwa kwamba  angalau asilimia 70 ya mtaji wake uwe ni kwaajili ya miradi ya Reli.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwa kiwango gani wakfu huo umeanza kazi na fedha zake zinatoka wapi na unaendeleaje kuongezeka?

23.      MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA-TCAA
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwa mujibu wa sheria kwamba biashara yote ya usafiri wa anga hapa nchini inathibitiwa na kuongozwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Mamlaka hii iliundwa rasmi na kuanza kufanyakazi zake kwa mujibu wa sheria ya Bunge namba 10 ya mwaka 2003 ambayo ilifanyiwa marejeo mwaka 2006.  Aidha, sheria hii ndiyo inaangalia kwa jinsi gani Sheria Namba 80 ya Usafiri wa Anga ya mwaka 1977 na kanuni zake zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga nchini zilizowekwa kwa lengo, hususan, kuhakikisha usalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa anga sambamba na kulinda usalama wa umma na mali wakati wa matumizi ya vyombo husika.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huu, ni dhahiri kwamba utendaji wa shirika letu la ndege unaathari za moja kwa moja na utendaji wa mamlaka hii ya usafiri wa anga. Kwani uendeshaji wa kampuni yoyote inayotoa huduma za usafiri wa anga ni lazima ithibitiwe na matakwa ya Mamlaka hiyo, hivyo kama mamlaka haina watendaji ambao wenye weledi wa kutosha katika tasnia ya usafiri na usafirishaji wa anga ni dhahiri hata kampuni inayotoa huduma itakuwa katika mtanziko wa kiutendaji.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali, katika kuhakikisha kuwa usafiri wa anga hapa nchini unaboreshwa ni lazima utendaji wa ofisi ya mdhibiti wa usafiri wa anga unakuwa na watu wanaoelewa kwa undani biashara nzima ya usafiri wa anga, na sio tu watendaji ambao walikuwa kwenye nafasi za juu katika wizara husika.
23.1.  Kampuni ya Ndege Tanzania- ATCL
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa historia nzima ya uwepo wa shirika letu la ndege hadi sasa inafahamika  vyema na kwa jinsi gani limehujumiwa na wale ambao ndio waliopewa dhamana na watanzania kuliangalia kwa niaba yao. Kwa muktadha wa hotuba hii itaweka zaidi wazi ni kwa jinsi gani uendeshaji wake ufanyike ili shirika letu liweze kuwa shindani katika medali za usafiri wa anga.

Mheshimiwa Spika,  kabla ya kuangalia na kushauri naomba nitoe rejea kwa mashirika mengine ya usafirishaji ambayo yanafanya vizuri sana japokuwa yameanzishwa muda mfupi kwa kulinganisha na shirika letu.  Shirika la Ndege la Emirates, lilianzishwa rasmi mwaka 1985, hadi sasa shirika hilo lina jumla ya ndege 231 kati ya hizo  ndege 68 ni  aina ya Airbus, A.380 zinazobeba abiria  800. Lakini shirika lilianza biashara na ndege mbili (2). Katika kuonesha kuwa biashara ya ndege sio biashara ya kila mtu, wamiliki walimtafuta mtaalam wa uendeshaji masuala ya ndege raia wa Uingereza, Sir Maurice Flanagan ambaye ameliendesha shirika hilo hadi mwaka 2006 na akafariki May 2015.

Mheshimiwa Spika, Shirika la ndege la Rwanda ambalo lilianza kufanyakazi rasmi mwaka 2002 na hadi sasa lina umri wa miaka 17 na lina jumla ya ndege 13 zinazofanyakazi na ndege nyingine moja inasubiriwa ili kuifanya idadi kuwa 14. Hoja ya msingi ni je wenzetu wamefanyaje mpaka shirika lao limefikia hapo lilipofikia?

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shirika la ndege la Kenya ambalo muda wa uanzishwaji wake ni sawa na shirika letu. Hadi mwezi januari 2015 shirika hilo lilikuwa na ndege 6 Dreamliners  B787-8 ambazo zinaenda kila siku Nairobi-London na hivyo kulifanya shirika hili kuongeza ndege zake kutoka 44 hadi kufikia 107  kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015, na hivyo  shirika hilo kuwa na vituo (destinations) 115 kutoka vituo 62.

Mheshimiwa Spika, tukirudi kufanya ulinganisho na shirika letu la ndege ambalo lina umri sawa na wetu ni dhahiri kwamba bado tuna safari ndefu ili tuwakute wenzetu. Ni ukweli pia tunapanua uwanja wetu wa Julius Nyerere ili uweze kuwa shindani, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ili Tanzania inufaike zaidi na uwanja huo ni lazima shirika letu liendeshwe kisasa zaidi, na mamlaka ya usafiri wa anga iwe na watendaji wenye taaluma na uzoefu wa kuendesha shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli pia wakati Mwalimu Nyerere anastaafu mwaka 1985 aliacha shirika likiwa na ndege 11 ikiwa ni; Douglas DC-9-32  ndege moja (1), Boeing 737 mbili(2), Fokker F 27 ndege nne(4), na Twin Otter DHC-6-300 ndege nne (4).

Mheshimiwa Spika, ndege hizo zote wajanja wamekunywa kama vijana wa mjini wanavyosema na hiyo itabakia kuwa ni historia kama ilivyoachwa na muasisi wa taifa hili.

23.2.   Ukiukwaji wa Sheria katika Manunuzi ya Ndege
Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali kwa mujibu wa kitabu cha fedha za Maendeleo Volume IV Part A fungu 62 kasma 4294 ilitenga jumla ya shilingi Bilioni 500 fedha za ndani kwa ajili ya kununua ndege za abiria kwa ajili ya shirika la Ndege la ATCL.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya waziri wa Fedha akiwakilisha taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2016 na mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2016/17 ameeleza kuwa serikali imeshasaini mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine 4 na malipo ya awali ya dola milioni 56.89 ambayo ni sawa na shilingi 126,125,130,000.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali itoe taarifa kamili juu ya masuala yafuatayo kuhusu ndege ambazo zimenunuliwa na zile zinazotegemea kununuliwa;
(i)                  Je mradi wa ununuzi wa ndege utagharimu kiasi gani cha fedha mpaka ndege zote zitakapowasili nchini?
(ii)                 Utaratibu upi uliotumika kuagiza ndege hizo kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya umma?
(iii)                Je, kiasi cha dola milioni 56.89 kilichotumika kulipia malipo ya awali kilitengwa kutokana na fedha zipi za Bajeti kwa mujibu wa sheria?
(iv)               Je, serikali ilitumia utaratibu gani mpaka kuamua kuchagua kampuni ambazo imeamua kuingia nazo mikataba ya ununuzi wa ndege?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa majibu ya mambo tuliyoyaainisha kwa sababu bila kutoa  taarifa za kina kuhusu mradi huu wa ndege, mashaka yatakuwa makubwa kuhusu matumizi hayo ya fedha nyingi za walipakodi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kwa sasa duniani sio kununua ndege kwa fedha taslimu za walipakodi kama ambavyo serikali ya CCM inafanya, bali serikali huingia makubaliano na kampuni zinazozalisha ndege ambapo kwa kushirikiana na sekta binafsi ndege zinaanza kufanya biashara na kujilipa kutokana na faida inayopatikana. Utaratibu huu wa kuondoa mabilioni ya fedha kwenda nje ya nchi yetu unaathiri si mzunguko wa fedha ndani ya nchi bali pia huathiri miradi mingi ya huduma za jamii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi kuwa ni lazima ATCL iendeshwe kwa weledi na watu ambao wanajua kufanya biashara ya usafiri wa anga kuliko kutegemea kila mara kupokea maelekezo ya viongozi wa serikali ambao pengine hawana uelewa wa kutosha wa kuendesha biashara hiyo. Haitashangaza kuona ATCL inafanya biashara kwa hasara kuliko mategemeo ya sasa kwa sababu ya kuchanganya siasa na utendaji.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa ndege hizo ni mali ya Serikali  na hivyo ndege hizo zinakodishwa kwa Kampuni ya ATCL na ATCL inatakiwa kulipa kiasi cha dolla za kimarekani 160,000 sawa na takriban shilingi 360,000,000/= kila mwezi na kwa mwaka shilingi 4,320,000,000/=, na kiasi kinachobakia kinauwezo wa kuifanya kampuni kurejea kwenye ushindani, kwa kuajili wataalam wabobezi wa masuala ya uendeshaji shughuli za usafiri wa anga au mambo ni yale yale ya Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kuteua anaohisi wanaweza. Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali kwamba, kwa kuwa Kampuni ndio kwanza inaanza kutambaa ni kwani fedha hizo inazoilipa Serikali kila mwezi zisilipwe baada ya miaka mitano ambapo tayari itakuwa imesimama?

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba ATCL inakabiliwa na matatizo mengi sana. Miongoni mwa matatizo hayo ni pamoja na:-
                     i.        Kushindwa Kupata Vyeti Muhimu vya Usafiri wa Anga
ATCL  inatakiwa kuweke utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi au kuwajiri watumishi wapya wenye sifa stahiki pamoja na kuwa na mpango wa kurithishana ujuzi kwa nafasi muhimu za uongozi wa Shirika ili kuwa na watumishi wasomi, wazoefu, waliohamasika na wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani katika soko linalokuwa kwa kasi la usafiri wa anga. Kwa njia hiyo ATCL inatakiwa kupata vyeti vyote kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kimataifa (IATA) pamoja na ukaguzi wa usalama wa usafiri wa anga. Kulingana na taratibu na kanuni za uendeshaji wa makampuni yote ya ndege kufuata taratibu za usalama za usafiri wa anga.

                   ii.        Kukosekana kwa Mkakati Mahususi wa Kufufua Shirika
ATCL  inatakiwa kuwa na mkakati utakaoiwezesha kurudi katika hali nzuri ya kifedha kwa kufanya tathmini ya kina kubaini sababu na matatizo yaliyopelekea kuwa na matatizo ya hali ya kifedha iliyopo, pamoja na kuboresha mifumo na namna ya kuendesha biashara hiyo ili kuwa na Shirika jipya lenye ufanisi na kujiendesha kwa faida. Mwezi April, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi, alinukuliwa akisema shirika lake limefanikiwa kukusanya Sh Bilioni 9 kwa Miezi minne tu kwa kutumia ndege mbili za Bombardier.

Mheshimiwa Spika, hii inatokana na ukweli kwamba, ATCL hadi sasa bado halifanyi kazi kama Kampuni ya biashara badala yake linatoa huduma, mfano mzuri ni pale linaposhindwa kutunza muda wa ndege zake kuruka mapema au kuchelewa na kulazimika kuwakodishia abiria wake ndege zingine zenye gharama/bei au nauli kubwa kulinganisha na nauli inayotozwa na kampuni  hiyo.


24.      UFANISI WA BANDARI NA MCHANGO WAKE KATIKA UCHUMI

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba uwezo wa bandari yetu katika kuhudumia meli kubwa bado ni duni sana na jambo hilo halina ubishi kutokana na takwimu zilizopo. Jambo hili linapelekea kwa kiasi kikubwa meli kubwa kushindwa kutia nanga hapa nchini kwetu na badala yake kwenda Bandari za Beira na Mombasa.

Mheshimiwa Spika, uwezo wa bandari yetu ni kupokea meli zenye uwezo wa deadweight tonnage (DWT) 4.1 million “dry cargo” na   DWT 6.0 million “bulk liquid cargo”. Kwa mujibu wa  “Port master plan  2008-2028” inaonesha kuwa kulikuwa na mkakati wa kuongeza ufanisi na upitishaji wa mizigo kwa 30% toka tani 13.5milioni kwa mwaka 2013 hadi tani 18milioni mwaka 2015. Katika kufikia hapo uwekezaji mkubwa ulitakiwa kufanyika katika milango ya kuingizia meli na maegesho yake. Ukweli ni kwamba uwekezaji uliotakiwa hadi sasa haujafanyika.

 Mheshimiwa Spika, bandari ya Dar es Salaam ni fursa muhimu ya kijiografia kwa nchi yetu, kutokana na mataifa yaliyotuzunguka kutokuwa na huduma hiyo wakati huo huo yanazo raslimali za kutosha kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Tukumbuke kwamba biashara ni muda, ukishindwa kuupima muda basi muda huo utakupima wewe.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya nne kwa kuliona jambo hilo, iliingia makubaliano na  Exim Bank ya China ili kupata mkopo kwa ajili ya kupanua lango na kujenga gati namba 13 na 14 lakini cha kushangaza hadi sasa ujenzi huo haujaanza. Wakati sisi tukishindwa kuchukua hatua, jirani zetu wa Kenya wamemaliza ujenzi wa gati namba 19 ya bandari ya Mombasa na bandari hiyo inafanyakazi. Katika kuonesha kuwa wako mbele zaidi kulinganisha na sisi  Reli yao ya Standard Gauge ya kuanzia Mombasa kwenda Nairobi hadi Kampala imeanza kazi rasmi.

Mheshimiwa Spika, meli za mizigo zinaongezeka ukubwa na uwezo wa kubeba mizigo kulingana na imetengenezwa lini (Generations), hapa inaonesha jinsi muda wa utengenezaji meli unavyokwenda sambamba na ukubwa pamoja na uwezo wa kubeba mizigo. Bandari yetu inauwezo wa kuingiza meli za Generations  1 hadi 3.Generations
Generation
Years
Type
TEU's
1st Gen.
1956-1970
Converted GCS/Tanker
135-200 m
9 m
500-800
2nd Gen.
1970-1980
Cellular
215 m
10 m
1000-2500
3rd Gen.
1980-1988
250-290 m
11-12 m
3000-4000
4rt Gen.
1988-2000
275-305 m
11-13 m
4000-5000
5th Gen.
2000-2007
335 m
13-15 m
5000-8000


Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu ni kwanini Serikali ya CCM inakuwa na kigugumizi   kuanza ujenzi wa gati 13 na 14 wakati mradi tayari ulishapatiwa fedha tangu Mei, 2012, na hadi sasa utekelezaji haujaanza. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaka kufahamu inapotokea kuvunjwa kwa mkataba wa kupata mkopo pande husika inatakiwa kufidia vipi hasara iliyopatikana?
Mheshimiwa Spika, imetulazimu kuomba ufafanuzi huo kutokana na ukweli kwamba, mikataba inaingiwa na Serikali na baadae hatupatiwi mrejesho wa utekelezaji. Mfano mzuri ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Kuingiwa na kuvunjwa maana yake walioshiriki hawakuangalia maslahi ya nchi? Na kama ndivyo hivyo ni kwanini hatujasikia wakiwajibishwa kwa hilo?

Mheshimiwa Spika, juhudi zinazofanyika sasa hivi bandarini ni za kuongeza ufanisi wa kazi tu, jambo ambalo kwa upande wa kuingiza meli kubwa halitahusika, jambo hilo lilitakiwa kwenda sambamba na mpango wa upanuzi wa Gati na 13 na 14.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo juhudi za kuongeza ufanisi haziendani na uhalisia wa ushindani wa kibishara baina ya nchi yetu na washindani wetu katika miundombinu ya Bandari. Mfano:
1.   Mgongano wa tozo za uhifadhi wa mzigo ambapo TRA wanatoza storage na TPA wanatoza Custom warehouse rent. Hiki ni kitu kile kile.
2.   Tozo ya dola za kimarekani 23 kwa tani moja ya mzigo wa shaba ambapo bandari ya Durban kwa mzigo huohuo  wa uzito huo wanatoza dola 17.86
3.   Tozo kubwa kwa mizigo yote inayokwenda Zambia, kwa mfano kasha la urefu wa futi 40 linatozwa dolla 530, badala ya dolla 320 ambazo hutozwa kwa mzigo kwenye kasha la urefu wa futi hizo hizo kwa mzigo unaokwenda Rwanda na Burundi.
4.   Single Custom Territory (Himaya ya Forodha) ambapo nchi ya DR-Congo (nchi na wafanyabiashara) inatumia bandari yetu kwa mizigo yote inayokwenda nchi hiyo. Lakini kitendo hicho wafanyabiashara wa DR-Congo wanaona kuwa ni gharama kwa biashara zao na hivyo kulazimika kuhama bandari na kuhamia  bandari za Beira, Durban au Mombasa. Hii inatukosesha mapato ambayo yangelipwa na wafanyabiashara toka DRC kwa kigezo tu cha kufanya kazi ya mamlaka ya Mapato ya DRC.
5.   Bandari yetu inatoa “grace period of transit of bulk liquid” fupi sana ya siku 30 kwa kulinganisha na washindani wetu wanaotoa siku 60 hadi 90.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuyafanyika kazi mapungufu hayo ya kimfumo ili ufanisi katika badari yetu uweze kuonekana. Kinyume cha hapo tutafukuza matendaji wote na kuleta wapya kwani matokeo hayatonekana.
 aidha, kitendo cha kushindwa kupanua ukubwa wa maegesho kwa meli kubwa ni dhahiri hata ujenzi wa Reli kwa kiwango cha kimataifa bado “economic viability” yake inatia mashaka. Kwani ujenzi wa Reli kwa standard gauge lengo kubwa ni kuhakikisha inachukua mzigo mkubwa toka ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, na mzigo huo uweze kuingizwa moja kwa moja kwenye meli zinazolingana na mizigo husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali kutathmini upya mkakati wake wa uwekezaji katika Reli ya Kati ikienda sambamba na upanuzi wa bandari ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia mizigo mingi, kwani gharama za ujenzi wa reli zitalipwa kwa reli kupokea mizigo mingi kupitia bandari.

25.      MRADI WA UJENZI WA RELI YA KATIKA KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA – STANDARD GAUGE:
 Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua umuhimu wa mchango wa usafiri wa reli katika kukuza uchumi wa taifa. Aidha, hapinngi ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa – Standard Gauge kutokana na umuhimu wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapata shida kuelewa ni kwa nini Serikali kutekeleza mradi huo kwa kutumia kampuni yenye bei ya juu na kuacha iliyokuwa tayari kujenga reli hiyo kwa gharama za chini.
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, unatarajia kukamilika mwaka 2021 na utagharimu Sh trilioni 17.6. Kwa kujenga jumla ya kilometa 2400 kwa mujibu wa mkataba na Wachina na ikalazimu Serikali kupata mkopo wa riba nafuu toka benki ya Exim ya China.  Mkataba  na Waturuki wa ujenzi wa kipande cha kilomita 205 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, na tayari ujenzi huo umeshawekewa jiwe la msingi na unakadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni1.21 (Sh trilioni 2.6).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka majibu sahihi ni kwanini hasa mkataba nafuu wa Wachina wa trilioni 17.6 ambapo kilometa moja ilitakiwa kujengwa kwa dola bilioni 3.16 ulivunjwa na Serikali ikaingia mkataba na Waturuki  ambao ni ghali wa kujenga kilometa moja kujengwa kwa bilioni 5.8?
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ilieleza kuwa ujenzi huo utakamilika mwaka 2021 kutokana na mfumo unaotumika wa kutoa zabuni kwa vipande vipande badala ya kutoa zabuni yote kwa kampuni moja. Alisema mfumo huo unapunguza muda wa ujenzi kutokana na kampuni nyingi kufanya kazi hiyo kwa wakati mmoja, lakini ikitokea kampuni inayojenga ikaomba tenda na kushinda na ikabainika kuwa na uwezo wa kufanya shughuli hiyo kwa wakati, itapewa zabuni.
Mheshimiwa Spika, awamu nyingine itahusisha vipande vya Morogoro hadi Makutupora kilomita 336, Makutupora-Tabora (km 294), Tabora-Isaka (km 133) na Isaka-Mwanza (km 248). huku Serikali katika bejeti yake, serikali ikiwa imetenga kiasi cha shilingi trioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa za kujenga reli ya kati kwa  kiwango cha standard gauge ni sababu za kiuchumi ambazo lazima zizingatiwe kwa kiwango ambacho kitaliwezesha taifa kupata faida. Kwa mantiki hiyo bado kuna sintofahamu katika tathimini ambazo mamlaka husika zimefanya na tathimini hizo zikapelekea kufanyika kwa maamuzi ya ujenzi wa reli ya kati kutoka Da es salaam hadi Mwanza badala ya kwenda Kigoma.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa serikali kuanza kujenga Reli ya kati baina ya Dar es Salaam na Mwanza (kama taarifa inavyotolewa, japo kuwa Reli ya Kati ni Reli ya kutoka Dar es salaam kwenda mkoani Kigoma na si vinginevyo),unapaswa kuangalia vipaumbele vya maeneo ambayo shughuli za reli hiyo itasaidia kwa kuangalia takwimu ni wapi serikali inapaswa kujenga reli ili mradi huu wa ujenzi wa reli uweze kuzalisha fedha za kujenga reli nyingine ama kuliletea Taifa faida.
Mheshimiwa Spika, inavyoonekana serikali ni kama serikali imesahau tafsiri mpya ya reli ya kati, au inafanya kwa makusudi, kwa kuweka sawa kumbukumbu, ukisema reli ya kati tafsiri yake ni kwamba unazungumzia reli ya kutoka mkoani Kigoma hadi jijini Dar es salaam au kutoka jijini Dar es salaam hadi mkoani Kigoma na maeneo mengine yote ni matawi ya reli ya kati. Kwa muktadha huo Mheshimiwa Spika, ujenzi wa  'Standard Gauge' kwa hatua hizo za awali unaotoka Dar es salaam kwenda Mwanza ulipaswa kuwa ni ujenzi wa standard gauge kutoka jijni Dar es salaam kwenda mkoani kigoma.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi nchini ya mwaka 2015/2016, takwimu zinaonesha kwamba mizigo ambayo Tanzania inahudumia kwa nchi za maziwa makuu ni tani Milioni tano kwa mwaka. Katika hizo Zambia ni 34%, Kongo ni 34%, Rwanda12% Burundi 6% na Uganda ni 2.6%. Tafsiri yake ni kwamba Ujenzi wa 'Standard Gauge' utakaotumia matrilion ya fedha wakati huo huo reli hiyo imeelekea Isaka na Mwanza maana yake ni kwamba reli hiyo itakayokuwa kwa kiwango cha standard gauge itahudumia 15% ya mizigo yote tunayoipitisha, kwa maana ya mizigo kutoka Rwanda na Uganda, wakati huo huo kama Taifa tumeacha kuhudumia mizigo 40% kwa maana ya mizigo inayotoka katika nchi za Kongo na Burundi ambayo yote inapita mkoani Kigoma.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inataka kupata majibu kutoka serikalini, ni utaalamu gani na au upembuzi upi wa kiuchumi umetumika hadi kufikia maamuzi ya kujenga reli hii kwa kiwango cha standard gauge kwenda Isaka hadi Mwanza sehemu ambazo kwa takwimu za serikali yenyewe, zinaonesha kwamba haziwei kuleta faida kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa reli hii ya kati kwa kiwango cha standard gauge kuna fedha za Benki ya Dunia kwa ajili ya ukarabati wa reli, kiasi cha Bilioni 200, Kambi Rasmi ya Bunge lako Tukufu inasahauri kwamba, fedha hizi za ukarabati wa reli ambao upo kipindi hiki zipelekwe maeneo mengine ambayo ujenzi huu wa reli kwa kiwango cha standard gauge haufanyiki ili kuleta uwiano wa utekelezaji wa miradi hii ya reli.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani katika wasilisho lake la mwaka 2013  kuhusu bajeti ya Serikali ilipendekeza kuanzishwa kwa kodi maalum (Special Railways development levy) ya manunuzi na mauzo ya bidhaa nje. Tunapendekeza tozo ya asilimia moja (1 %) ya bei ya bidhaa zinazoagizwa toka nje na asilimia 0.5 (0.5%) ya thamani ya bidhaa kwa zile zinazouzwa nje. Mapato ya tozo hii maalumu yote yatumike kujenga miundombinu ya Reli hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kitabu cha Mpango wa pili  miaka mitano wa Maendeleo  ukurasa wa 92  kuna wakfu(Fund) wa Maendeleo ya Reli ambao ulikadiriwa kwamba  angalau asilimia 70 ya mtaji wake uwe ni kwaajili ya miradi ya Reli.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwa kiwango gani wakfu huo umeanza kazi na fedha zake zinatoka wapi na unaendeleaje kuongezeka?

26.      KUSAHAULIKA KWA SEKTA YA AFYA KATIKA MAENDELEO YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii ya serikali suala la afya halijapewa kipaumbele kabisa.Hii inaonyesha wazi kabisa bajeti hii ni ya ajabu kabisa na haijawahi kutokea. Ni ajabu kuona serikali hii haifahamu kuwa afya ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani. Hakuna taifa lililowahi kuendelea kiuchumi pasipo kuwekeza kwenye afya ya wananchi wake.Hakuna uchumi bora bila kuwa na watu wenye afya bora. Maendeleo ya viwanda, kilimo, elimu,nishati, miundombinu na michezo yanaweza kufikiwa endapo tu nchi ina mifumo bora ya utoaji wa huduma za afya na wananchi wake wana uhakika wa maisha .
Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii ambayo serikali imejigamba ni bajeti ya wananchi imeshindwa kuonyesha unaafuu katika suala la upatikanaji wa huduma ya afya ambalo ni suala linalogusa maisha ya kila Mtanzania wa kila rika, jinsia, rangi n.k. Afya huunganisha taifa.  Lakini cha ajabu ni kuwa bei za vipimo mbalimbali kama vile CT-Scan vimekuwa ni vya gharama sana na hivyo kutokana na wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za vipimo hivyo wengi wamepoteza maisha.Nchi hii imekuwa na gharama kubwa sana katika ununuzi wa vifaa tiba jambo linalowafanya hata wawekezaji wa ndani  kushindwa kuwekeza vya kutosha katika sekta hii ya afya. Vilevile, kumekuwa na urasimu mkubwa katika kufungua viwanda vya kutengeneza dawa hapa nchini pamoja na tozo nyingi zisizokuwa na tija badala ya kutoa unaafuu na kutengeneza mazingira wezeshi ili dawa hizi zipatikane moja kwa moja hapa nchini na kupunguza mzigo mkubwa kwa serikali katika kununua madawa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,tunapoteza nguvu kazi kubwa ya taifa kutokana na vifo visivyo vya lazima kwa sababu tu ya kukosekana kwa vifaa tiba,wataalamu na madawa. Mfano; kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2015-2016 (Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey) inaonyesha kuwa kati ya watoto 1,000 chini ya umri wa miaka mitano watoto 67 hufariki. Hii ina maana kwamba kati ya hao 67 wanaofariki tunapoteza nguvu kazi kama wataalamu,walipa kodi, tunapunguza pato la taifa na zaidi tunapunguza juhudi zetu katika kukuza uchumi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo bajeti hii haijagusa ipasavyo afya ya wanawake na watoto wa kike (women and girls) licha ya kuwa ndio kundi lenye wapiga kura wengi nchini .  Kundi hili hukabiliwa na changamoto lukuki za kiafya ikilinganishwa na makundi mengine (most vulnerable group). Watoto wa kike wamekuwa wakitaabika sana wakati wa hedhi. Wengi wao wakilazimika kukatisha masomo, kupata msongo wa mawazo na hivyo kuathiri kabisa kiwango cha ufaulu kwa watoto wa kike. Wengi wa watoto hawa wamekuwa wakitumia vitu mbalimbali katika kujihifadhi na wengine wakilazimika kutumia vitambaa au matambara ambayo ni hatari kwa afya zao hususani kwenye via vya uzazi.
Mheshimiwa Spika, kupunguza kodi kwenye taulo za kike (sanitary pads) kungeweza kabisa kuwasaidia wanawake walio wengi kuendelea kufurahia uanamke wao,kujisikia huru na kufanya kazi za uzalishaji vizuri  na hata kuongeza kiwango cha ufaulu  kwa walio mashuleni.Mpaka sasa bei ya taulo hizi za kike hugharimu kuanzia shilingi 2,500 mpaka shilingi 5,000. Wakati mwingine wanawake hulazimika kutumia pedi zaidi ya moja kutokana na wingi wa hedhi na hivyo kila mwezi anahitaji kuanzia 5,000- 8,000 /-ili kujisitiri.
Mheshimiwa Spika, gharama hii ni kubwa sana. Tafiti zinaonyesha ni 11 % tu ya wanawake waliofikia umri wa kupata hedhi wana uwezo wa kutumia taulo hizi maalum za hedhi, Kwa mujibu wa gazeti la the citizen la tarehe 10 June ,2017 lenye kichwa cha habari “Women decry levy on sanitary towels” imeeleza kwa kina umuhimu wa serikali kupunguza kodi katika taulo za kike kwani pia taulo hizi zinategemewa sana na kina mama pale wanapojifungua.
Mheshimiwa Spika, badala ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kupiga makofi kishabiki ni lazima sasa kama taifa kuweka ukada pembeni na kuchambua kwa kina bajeti hii kwa kuangalia sekta muhimu zinazogusa maisha ya kila Mtanzania na makundi mbalimbali. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia upya bajeti yake na kuzingatia mambo ya msingi hususani kwenye sekta ya afya kwani bila mfumo bora wa utoaji wa huduma na unaafuu wa upatikaji wa huduma za afya, tujue wazi hakuna nguvu kazi yenye afya na kwa maana hiyo  uzalishaji utapungua na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi.

27.      SEKTA YA MAFUTA NA  GESI ASILIA
Mheshimiwa spika, katika historia ya Tanzania, tafiti za uchimbaji wa mafuta na gesi asilia zilianza mwaka 1952. Mafanikio ya shughuli za utafiti kwa mara ya kwanza yalipatikana miaka 22 baadaye ambapo mwaka 1974 gesi asilia iligunduliwa Songo Songo, katika mkoa wa Lindi. Baadaye, mwaka 1983 ugunduzi mwingine ulifanyika katika eneo la Mnazi katika mkoa wa Mtwara.Tokea wakati huo, shughuli madhubuti za utafiti wa uchimbaji ulikuwa ukiendelea na ilipofika Juni, 2015 ugunduzi wa gesi asilia ulikadiriwa kuwa trilioni za ujazo 55.08.
Mheshimiwa spika, mfumo wa udhibiti katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia hapa Tanzania unasimamiwa na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ambayo imechukua nafasi ya Sheria ya Utafiti na Uzalishaji wa Petroli ya mwaka 1980 sura ya 328 kama ilivyorejewa mwaka 2002. Sheria zingine zinazotumika katika sekta ya mafuta na gesi kwa shughuli za uchimbaji kwenye mkondo wa juu ni Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, na Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003.
Mheshimiwa spika, Hivi sasa, Tanzania imepitisha sheria tatu mpya ikiwa ni pamoja na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015 na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Shughuli za Utafutaji wa Mafuta, gesi asilia na madini Tanzania ya mwaka 2015, aidha ilielezwa kuwa lengo la sheria hizo ni kuboresha ubora wa usimamizi wa huduma, na shughuli katika sekta ya mafuta na gesi kwa maslahi ya Tanzania na watu wake.
 Mheshimiwa spika,  Sekta ya mafuta na gesi inajumuisha shughuli na taratibu mbalimbali ambazo kwa pamoja zinachangia mabadiliko ya rasilimali ya awali ya mafuta ya petroli na mwishowe kuwa bidhaa inayoweza kutumika na yenye thamani kwenye viwanda na watu binafsi. Shughuli hizi tofauti kwa asili yake zinahusiana (kinadharia, kimkataba, na/au kivitendo/kiutekelezaji), na mahusiano haya hutokea ndani ya makampuni binafsi, na pia ndani ya nchi au yanaweza kuvuka mipaka ya kitaifa.
27.1.  Ushirikishwaji wa Wadau katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia Tanzania:
Mheshimiwa spika, Kuna wadau wakubwa kadhaa katika usimamizi wa sekta hii ya mafuta na gesi asilia Tanzania. Wadau hawa wamegawanyika katika makundi mbalimbali yakiwemo taasisi binafsi, makampuni ya kimataifa ya mafuta pamoja na taasisi zinazotoa huduma katika sekta hii. Aidha serikali kama mdau mkubwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ina wajibu wa kusimamia sekta ya mafuta na gesi asilia nchini. Mbali na wajibu huu, Wizara ina kazi ya kutengeneza na kupitia upya sera na kanuni katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini. Taasisi nyingine za uangalizi ni pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Usimamizi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hizi ni taasisi za serikali ambazo zina wajibu wa kusimamia shughuli za kila siku za makampuni ya kimataifa ya mafuta, mazingira, usalama na afya mahali pa kazi, pamoja na kusimamia mapato.
Mheshimiwa spika, kwa upande mwingine Makampuni ya Mafuta ya Kimataifa kama wadau mhimu kwenye sekta hii, hufanya shughuli zinazohusiana na mafuta katika maeneo ya mikataba kulingana na sheria zinazokubalika, pia kulingana na sheria za utendaji za kimataifa. Aidha kuna taasisi   zinazotoa huduma katika Sekta hii kama vile Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, na Wizara ya Kazi. Wizara hizi kwa kupitia taasisi zake za mafunzo kama vile vyuo, na vyuo vya ufundi na usanifu zina wajibu wa kujenga uwezo wa Watanzania ili waweze kushiriki na kujihusisha na uchumi wa mafuta na gesi asilia. Aidha, zinapaswa kulinda ushiriki wa wenyeji na kutekeleza sheria za kazi katika sekta hii.
27.2.  Upotevu wa Fedha Zinazotokana na Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.
Mheshimiwa spika, Taarifa ambazo kambi rasmi ya bunge lako tukufu inazo zinaonesha kwamba utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa wazawa na uhakiki wa gharama rejeshwa katika makubaliano ya kugawana mapato ni hafifu na kuna hatari ya kutopata manufaa ya kutosha yatokanayo na ugunduzi wa mafuta na gesi asilia.  Athari ya jambo hili mheshimiwa spika ni kupungua kwa mapato ya serikali kunakotokana na ushiriki hafifu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika biashara ya mafuta na gesi asilia katika hatua ya uzalishaji. Taarifa zinaonesha kuna makubaliano ya mgawanyo wa mapato ambayo yanawapa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania fursa ya kushiriki katika biashara ya mafuta na gesi. Aidha makubaliano ya Kugawana Mapato yanaruhusu ushiriki wa kati ya 5%-20% wakati wa kipindi cha uzalishaji na zaidi ya hapo ili mradi tu wachangie mtaji unaohitajika kuwekeza katika mradi husika.
Mheshimiwa spika, Ili kuhakikisha kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linashiriki katika makubaliano yote ya kugawana mapato katika hatua ya uzalishaji, Shirika lilitakiwa kujumuisha kipengele hicho katika mikakati, mipango, na bajeti zake. Katika mantiki hiyo hiyo, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ilitakiwa kutoa msaada unaohitajika kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli ili kupata mtaji unaohitajika kuweza kujiingiza katika kila Makubaliano ya Kugawana Uzalishaji wakati uzalishaji wa kibiashara unapoanza.
Mheshimia spika, ushiriki wa TPDC usioridhisha kunako tokana na kutofanyika kwa uhakiki wa gharama rejeshwa kunasababisha kupotea kwa mapato yanayotokana na mafuta na gesi . Kulingana taarifa za Mkataba wa Makubaliano ya Mgawanyo wa Uzalishaji, Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) linatakiwa kufanya uhakiki wa gharama rejeshwa za kila Mkataba katika kipindi cha ndani ya miaka miwili baada ya kufungwa kwa mwaka unaohusika. Pamoja na kutakiwa kufanya hivyo, taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, zinaonesha kwamba, gharama rejeshwa zilizorekodiwa na makampuni ya mafuta na gesi zinazofikia kiasi cha dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hazijahakikiwa hadi sasa.
Mheshimiwa spika, Uchambuzi zaidi unaonesha kwamba takribani dola za Kimarekani Bilioni 1.5 zilikuwa ni gharama rejeshwa zisizohakikiwa kwa kipindi kirefu, na hii maana yake mheshimiwa spika ni kwamba, gharama hizo ambazo hazihakikiwi zinasababisha serikali kupoteza mapato yatokanayo na mafuta na gesi, kwa sababu mapato hukusanywa baada ya marekebisho ya gharama rejeshwa kama sehemu ya gharama.
27.3.  Madhaifu ya Mamlaka ya Mapato Kukadiria na Kukusanya Mapato katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.
 Mheshimiwa spika, yapo mapungufu yanayotokana na uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kukadiria na kukusanya mapato yatokanayo na kodi katika sekta ya mafuta na gesi asilia.  Taarifa zinaonesha  Mamlaka haina taratibu zinazowataka wakaguzi wa kodi kupima uhalali na uhakika wa taarifa kutoka vyanzo vingine mbali na taarifa kutoka kwa walipa kodi. Hii ni maana yake ni kwamba maafisa hao hulazimika kutumia taarifa anazotoa mlipa kodi mwenyewe bila kwa kuwa na utaratibu wa kutosha wa kutumia taarifa kutoka vyanzo vingine ili kujazia ushahidi ambao haukuonekana kwenye taarifa ya mlipa kodi.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inazotaarifa kuwa Mamlaka ya Mapato bado haijaunda mfumo wa taarifa ambao unasaidia katika ukaguzi wa kodi. Vilevile, taasisi hii haijabuni mfumo wa habari na mawasiliano ambao utasaidia wakaguzi wa kodi katika kutumia taarifa zinazopatikana ndani ya nchi hususani katika taasisi za serikali.  Pamoja na hayo, Mamlaka yaMapato haina kanzidata yenye taarifa za kiasi cha hasara kilichopitishwa kutoka kwa makampuni ya mafuta na gesi asilia yaliyokadiriwa kodi .
Mheshimiwa spika, Mbali na uwepo wa taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zinakusanya taarifa ambazo zinaweza kutumika kwa makadirio ya kodi za aina mbalimbali, Mamlaka ya Mapato haijawahi kufanya utafiti kuona njia zinazoweza kutumia vyanzo hivi katika makadairio ya kodi wanazokusanya.  Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo ni kwamba, mfumo wa taarifa uliopo umejikita zaidi katika kusaidia ukokotoaji wa kodi katika biashara za kunua na kuuza nje ya nchi pamoja na ukaguzi wa miamala ambayo haiakisi bei halisi ya soko. Huduma hii inatolewa na Kitengo cha Kodi za Kimataifa chini ya Idara ya Walipakodi Wakubwa.
Mheshimiwa spika, kambi Rasmi ya bunge lako tukufu inaona kwamba matatizo yaliyo ainishwa ni matokeo ya sera mbovu na mikakati isiyo endelevu ambavyo vinachangia kudidimiza sekta ya Gesi Asilia na Mafuta huku watanzaia wengi waliokwenye lindi zito la umasikini wakipewa matumaini hewa ya kunufaika na rasilimali hizi. Kwa mukitadha huo, Kamabi Rasmi ya Bunge hili inaitaka serikali kupitia taasisi zake kuacha uzembe unaosababisha Taifa kukosa mapato na kudidimiza uchumi wa nchi. Aidha mamlaka ya Mapato nchini lazima wawe na uwezo wa kufanya tathimini ya mlipa kodi kwa kuangalia pia taarifa nyingine nje na zinazotolewa na mlipa kodi mwenyewe.
Mheshimiwa spika, Pamoja na hayo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati  na Madini lazima iwe na miongozo ya ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kuelewa maeneo yanayohitaji maboresho zaidi katika utekelezaji wa mpango wa uendelezaji wa mtaji wa rasilimaliwatu. Hatuwezi kunufaika na rasilimali zetu ikiwa hatuna rasilimali watu wenye uwezo na weledi wa kutosha kwenye sekta ya Gesi asilia na Mafuta. Ikumbukwe kwamba uzalishaji wa wataalamu katika sekta ya mafuta na gesi asilia ni jambo moja lakini pia serikali kuhakikisha inaondoa tatizo la upungufu wa fedha na kuandaa miongozo ya ufuatiliaji ni jambo la pili, ili kuhakikisha kwamba shughuli za ufutiliaji na tathmini katika uendelezaji wa shughuli za kuwezesha ujuzi katika mafuta na gesi asilia zinafanyika kwa ufanisi, kinyume na hapa Taifa litaendelea kukosa mapato kama ambavyo bado hatujanufaika katika sekta ya Madini. 
27.4.  Maamuzi dhaifu kuhusu mradi wa ujenzi wa  Bomba la Usafirishaji Gesi Asilia Kati ya Mtwara na Dar es Salaam
Mheshimiwa spika, ujenzi wa Bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lilijengwa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Company (CPTDC) kwa gharama ya Dola za Kimarekani bilioni 1.283 ambapo kati ya hizo, dola za Kimarekani bilioni 1.225 zilipatikana kama mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China. Marejesho ya mkopo huo yalitegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara.
Mheshimiwa spika, kwa masikitiko makubwa sana, taarifa zilizopo zinaonesha kwamba serikali ilikurupuka kufanya maauzi ya ujenzi wa bomba hilo,kabla ya kutafuta wateja na kusainiana mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wateja lengwa wa gesi asilia. Matokeo yake mheshimiwa spika ni athari katika malipo ya mkopo kwa vile mauzo halisi ya gesi asilia yako chini ya kiwango cha makadirio ya awali cha futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku (mmscfd). Aidha, kwa sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo mteja pekee wa gesi asilia; ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku. Tafsili yake ni kwamba makubaliano ya awali ambayo ilikua TANESCO liweze kutumia takribani futi za ujazo milioni 80 kwa siku kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya mkataba wa mauziano ya gesi asilia (GA) ni tofauti na hali ilivyo kwa sasa.
Mheshimiwa spika, pamoja na maoni ya wadau kuhusu ama kuanza kujengwa kwa visima vya gesi au kuamua kujenga bomba la kusafirishia gesi, serikali iliamua kufanya maamuzi ya ajabu kwa kuanza kujenga bomba la gesi kuliko visima vya kuchimba gesi yenyewe, hali hiyo ilipelekea, mradi huu kujaribiwa kwa matumizi kwa kutumia kiwango cha wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku ikiwa ni kiwango cha chini sana ukilinganisha na ukubwa (capacity) halisi wa bomba. Maana yake ni kwamba, shirika la mafuta nchini TPDC itawajibika endapo itatokea hitilafu yoyote itakayotokana na majaribio ya upitishwaji wa gesi asili kufanyika chini ya kiwango cha bomba la gesi hilo. Hali inatokana na kipindi cha uangalizi wa bomba (defect liability period) kwa sehemu kubwa kuisha tangu mwezi Agosti mwaka 2016.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Bunge lako tukufu inashangaa kuhusu maamuzi haya ya kukurupuka yaliyofanywa na serikali hii ya chama cha mapinduzi kwa kuwa maamuzi kama haya, hata kama yangetakiwa kufanywa na chombo kingine chochote chenye maamuzi, basi tunaamini chombo hicho kingeamua kuanza na ujenzi wa visima ili kuupatia mradi huo tija kama ambavyo wadau mbalimbali walitahadharisha. Katika mkitadha huo huo Kambi Rasmi inataka jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa Serikali.
27.5.   Matumizi ya Bomba la Gesi Asilia Chini ya Kiwango kwa 94%
Mheshimiwa spika, matokeo ya maamuzi ya kukurupuka yamepelekea Bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam lililojengwa ili kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kwa ajili ya kupikia majumbani na kwa matumizi ya kwenye magari, sasa taarifa zinaonesha kwamba hapakuwa na maandalizi ya kupata wateja wa gesi hiyo na hadi sasa kwa mujibu wa taarifa ambazo kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo zinaoesha kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ndilo mteja pekee aliyeunganishwa kwenye bomba la gesi asilia toka Mtwara.
Mheshimiwa spika, kuunganishwa kwa TANESCO kama mteja pekee wa gesi hiyo kumepelekea kutumika wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku sawa na asilimia sita (6%) tu ya ujazo wa bomba; ambapo, kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba. Hali hii mheshimiwa spika, ni tofauti na taarifa za mkataba wa mauziano ya gesi asilia kati ya TPDC na TANESCO kuweka wazi kwamba TANESCO ingetumia gesi asilia kwenye mitambo yake sita (6) ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II, Tegeta na Symbion kwa kima cha chini cha matumizi cha futi za ujazo milioni 80 kwa siku na futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku kama kiwango cha juu.
Mheshimiwa spika, hadi sasa taarifa za Kambi Rassmi ya upinzani Bungeni zinaonesha kwamba mtambo wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I ndio pekee unaotumia gesi asilia kuzalisha umeme; na unatumia kiwango cha asilimia (34%) ya kiasi cha gesi yote iliyolengwa kutumiwa na TANESCO. Aidha mitambo mingine mitano iliyokuwa imekadiriwa kutumia kiasi cha futi za ujazo milioni 92.19 kwa siku, sawa na asilimi sitini na sita (66%) bado haijaanza kutumika; na haijulikani ni lini mitambo hiyo itaanza kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa spika, TANESCO bado lina mikataba ya muda mrefu na wazalishaji wakubwa wa umeme ambao ni kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Songas; ambapo mikataba yao inaisha mwaka 2022 kwa ule wa IPTL na mwaka 2023 kwa Songas. Hii inaiongezea TPDC na TANESCO ugumu kwenye kutimiza vifungu walivyokubaliana kwenye mkataba wa mauziano gesi asilia (GA).
Mheshimiwa spika, kama kweli serikali hii ya chama cha mapinduzi inadhamira ya kuliepusha taifa hili na malipo ya mkopo huo ambao kimsingi haufanyi kazi kama livyokusudiwa kwa matokeo ya vitendo vya serikali yenyewe kukurupuka, nilazima sasa TPDC iwasiliane na TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini ili wajadiliane ni kwa namna gani mitambo ya uzalishaji umeme ya TANESCO itaweza kumalizika kwa wakati ili bomba la gesi litumike kwa ufanisi na kuweza kulipa mkopo wa bomba la gesi kutoka Benki ya Exim ya China kwa wakati. Kwa upande mwingine, nguvu zaidi zielekezwe kwenye kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia ili kuongeza mapato ya gesi na kuiwezesha TPDC kutimiza wajibu wa kulipa madeni inapostahili.
27.6.  Uzembe wa Wizara ya Nishati na Madini, TRA na FCC na kuisababishia serikali hasara ya takribani dola mil 700.
Mheshimiwa spika, kampuni ya ORPHIR ilipouza shares zake kwa kampuni ya PEVELION kwa vitalu 3 vya mtawara serikali ilivuna zaidi ya dola 230m mwaka 2013 kutokana na malipo ya capital gain tax iliyopo kwa mujibu wa sheria ya fedha ya 2012.
Mheshimiwa spika, kampuni ya Shell iliponunua shares za BG kwenye soko la mitaji London, ilikuja nchini na kufanya uhamishaji wa shares za BG kwenda shell kuptia mamlaka za wizara ya Nishati na Madini, FCC na TRA kabla ya kodi kulipwa na kusababisha serikali kupoteza kodi ya takribani dola 700m. Matokeo yake mheshimiwa spika, Leo hii TRA inahangaika kuidai Shell kwenye tribunal kutokana na uzembe wake na hakuna uhakika wa kulipwa kutokana na uzembe wenye kila sura ya ufisadi.
Mheshimiwa spika, kutokana na uzembe huo, ambao umesababisha serikali imepoteza kodi ya takribani kiasi cha mil 700 dola za kimarekani, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ni lini itawatumbua wahusika wa wizara ya nishati na madini, TRA na FCC kutokana na uzembe huu wenye sura ya ufisadi hasa ukizaingatia ukweli kuwa sheria hii ya fedha imekuwepo tangu 2012 na imepata kutumika mara kadhaa, iweje katika hili la Shell mamlaka hizi zifanye maamuzi bomu kama haya.

27.7.  Kiasi cha Gesi iliyogunduliwa na Maeneo ilikopatikana
Mheshimiwa spika, Sekta ya Gesi na mafuta hapa Tanzania ni sekta ambayo kama ikitumika vizuri italitoa taifa hapa lilipo na kutuweesha kupiga hatua nyingi mbele za kimaendeleo ikiwa tutakuwa na utashi wa kisiasa wa kufanya hivyo. Hadi sasa, kwa takwimu za mwaka 2015 kwa mfano, gesi ilikuwa imekwishapatikana sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Mkuranga 2007 (0.2 TCF), Kiliwani 2008 (0.07 TCF), Songo Songo 1974 (2.5 TCF), MnaziBay 1982 (5 TCF), Ntorya 2012 ( 0.178 TCF), Deep Sea 2010-12 (44.8 TCF), Ruvu Basin 2015 (1.9) TCF ) ambapo jumla ya kiasi cha gesi kilichogunduliwa nchini kwa kipindi hichi ilikuwa ni futi za ujazo Trilioni 55.05 .
Mheshimiwa spika, nchi yetu imejaliwa utairi wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi na Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa kama tutaweka mstari wa mbele upeo, umasikini na uadilifu katika sekta ndogo ya gesi na mafuta.katika miaka ya nyuma imekuwepo miradi inayohusu  shughuli za uendelezaji, uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia hapa Tanzania.
Mheshimiwa spika, kwa mujibu wa ripoti  ya BMI, (Business Monitor International Ltd) kuhusu “Tanzania and Gas Report –Q4-2016”, ripoti inayohusu pia matarajio kwa miaka 10 ijayo, miradi inayohusika na sekta ya Gesi na Mafuta hapa Tanzania ambayo bado iko kwenye utafiti ni 10, makampuni yaliyoko kwenye hatua ya Appraisal ni 5 na makampuni yaliyofikia hatua ya ugunduzi ni 5, kampuni 1, ilikuwa katika hatua ya uendelezaji, na kampuni 1 pia ilikuwa katika hatua ya uzalishaji.
Mheshimiwa spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, makampuni hayo ya uwekezaji yana kumbwa na tishio kubwa la hali ya sintofahamu kuhusu sheria za nchi zinazohusu sekta ya Gesi na Mafuta. Sintofahamu hiyo inakwamisha na kupunguza shauku ya wawekezaji na hivyo kusababisha kudorola kwa miradi husika. Aidha ripoti hiyo inasema, ukosefu wa miundombinu na hali ya mazingira ya sintofahamu dhidi ya sekta hii ni kikwazo kikubwa dhidi ya wawekezaji kwenye sekta hii.
27.8.   Changamoto katika sekta ya Gesi na Mafuta Nchini
Mheshimiwa spika, Serikali ilipaswa kuiangalia sekta ya Gesi na Mafuta rikali ili kuhakikisha kuwa inakuwepo mipango na mikakati na inatekelezwa kikamilifu. Taarifa zinaonesha kwamba vyombo vya serikali vyenye wajibu katika sekta ya mafuta na gesi havitekelezi vya kutosha mipango na mikakati iliyopangwa kama ipo au havjapanga kabisa mipango ama mikakati yeyote. Aidha mipango kama ya kuendeleza rasilimali watu, katika sekta ya mafuta na gesi asilia; kufanya au kuwezesha kufanyika kwa utafiti kwenye petroli na gesi; na kutoa ushauri kuhusu teknolojia sahihi na mbinu muhimu za utendaji mzuri katika sekta ya petroli ilipaswa kufanyika na inaonekana kutofanywa na serikali hii ya chama cha mapinduzi.
Mheshimiwa spika, taarifa ambazo kambi rasmi ya bunge lako tukufu inazo ni kwamba kumekuwepo na kushindwa kufikia malengo ya manunuzi na utoaji wa mikataba na leseni. Taarifa ambazo KRUB inazo zinaoesha kwamba malengo ya serikali kupitia TPDC kuhusu usimamizi wa mchakato wa uandaaji na utoaji wa mikataba na leseni za utafutaji wa gesi asilia halikufanikiwa kutokana na ukosefu wa mwongozo wa muda maalumu; na kukosekana kwa sera sahihi, mikakati na miongozo. Aidha taarifa hizo zinaonesha kwamba, malengo yaliyopangwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli yalifikiwa kwa kiasi kwa sababu ya matarajio madogo ya sekta nchini, na uwezo mdogo wa kiufundi na kifedha.
Mheshimiwa spika, Mapungufu mengine yaliyoonekana ni katika uwasilishaji wa majibu ya zabuni zilizotangazwa kuwa chini ya matarajio. Katika mzunguko wa nne wa leseni, kati ya zabuni za vitalu nane (8) zilizotangazwa, vitalu sita havikuguswa ambayo ni sawa na asilimia 75 ya jumla ya zabuni za vitalu vyote. 25% tu ya zabuni za vitalu iliwavutia wawekezaji. Hali hii ilibainika katika mizunguko yote minne ya leseni, ambapo jumla ya zabuni za vitalu 32 zilitangazwa, lakini ni mikataba ya vitalu 5 tu ndiyo ilifanikiwa kutolewa ambayo ni sawa na 16%. Aidha taarifa zinaonesha kwamba kulikuwa na upungufu katika utoaji wa zabuni kwa makampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi asilia. Mapungufu haya yalisababishwa na lengo la manunuzi halikukidhi vigezo kama gharama za kuendesha shughuli na mapato yanayotarajiwa, pamoja na muda utakaotumika kukamilisha kazi au hata uzalishaji, ubora, na utaalamu wa makampuni yaliyonunuliwa.
Mheshimiwa spika, katika ule mwendelezo wa wawekezaji kuendelea kuzifaidi rasilimali za watanzania chini ya sera ambovu za chama cha mapinduzi, sekta ya Gesi na mafuta nayo inaonesha kukumbwa na tatizo la utelekezaji duni wa masharti ya mkataba wa ugawanaji wa mapato yatokanayo na uzalishaji na uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uendeshaji. Taarifa za mikataba hiyo zinaonesha kwamba  Mkataba wa Ugawanaji wa Mapato yatokanayo na Uzalishaji ambao ulitiwa saini kati ya Serikali ya Tanzania, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania pamoja na Makampuni ya Kimataifa ya Mafuta; Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa kipengele cha Ushiriki wa Wazawa kimewekwa kwenye Mkataba wa Ugawanaji wa Mapato yatokanayo na Uzalishaji pamoja na Sheria ya Uzalishaji na Utafutaji wa Petroli ya mwaka 1980 zinatekelezwa kwa ufanisi.
Mheshimiwa spika, katika kuonesha kwamba yanayotokea kwenye sekta ya Gesi na mafuta siyo ajali, kama ambavyo bajeti kuu haitaji ni ajira kiasi gani serikali inakusudia kuongeza, huenda ni kutokana na serikali kupuuza dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata ajira. Kwenye sekta ya Gesi na mafuta pia, wajibu wa utoaji Ajira kwa Watanzania hautekelezwi. Hii inasababishwa na upembuzi hafifu wa kutambua nafasi za ajira katika sekta ya mafuta na Gesi asilia na pia ukosefu wa mipango mkakakati ambayo ingehakikisha kupatikana kwa ajira kwa Watanzania katika makampuni ya kimataifa ya mafuta ya na gesi asilia na ukosefu wa miongozo na utaratibu wa kutoa ajira kwa wafanyakazi wa kigeni.
Mheshimiwa spika, hali hii ya watanzania kushindwa kupata ajira katika sekta hii, kunasababishwa na mapungufu ya kisheria, udhibiti, na mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya usimamizi wa utekelezaji wa kipengele cha Ushiriki wa wazawa katika Mkataba wa Ugawanaji wa Mapato yatokanayo na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia. Aidha kuna ushiriki usioridhisha Katika Biashara ya Mafuta na Gesi Asilia, kwa mfano Shirika la Maendelelo ya Petroli Tanzania lilipaswa kushiriki katika mradi wa Songosongo pamoja na mradi wa Mnazi Bay ambayo ni miongoni mwa mikataba michache ambayo ilishafikia  katika hatua za uzalishaji, lakini taarifa zilizoo ni kwamba TPDC ilishiriki katika mradi wa ghuba ya Mnazi pekee.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa mbadala ufuatao dhidi ya sekta ya Gesi na mafuta hapa nchini.
     i.        Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingehakikisha inashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo sekta binafsi katika michakato ya utafiti, uchimbaji na usambazaji wa gesi asilia ili kuhakikisha kwamba sekta binafsi zinapewa nafasi ya kushiriki katika kujenga uchumi wa Taifa hili.
    ii.        Kambi Rasmi ya upinzani bungeni ingehakikisha inaondoa mazingira yote yanayoonesha viashiria vya sintofahamu ili kuruhusu wawekezaji wakubwa kufanya maamuzi ya mwisho katika uwekezaji ili kuinusuru miradi ambayo inachechemea kutokana na sintofahamu ya sheria na viashiria vya hofu.
   iii.        Kambi rasmi ya upinzani Bungeni ingehakikisha , sekta ya gesi na mafuta inatoa ajira kwa watanzania waliowengi ili kupiunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini, kuweka miongozo na kusimamia sheria kwa ukaribu ili kuhakikisha wazawa wanapewa ajira na makampuni ya kigeni yanayowekeza katika sekta hii. kwa kufanya hivyo, vipato vya wananchi vingepanda, lakini pia serikali ingepata kodi inayolipwa kutokana na vipato vya mishahara yaani  (PAYE)
  iv.        Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni ingehakikisha kuna fungamanisho la sekta ndogo ya gesi asilia na sekta nyingine ili kuongezeka na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunaposisitiza fungamanisho la sekta ndogo ya gesi asilia na sekta nyingine, hapa tunataka gesi iwe kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine hapa nchini kama Ajira, kilimo, viwanda, Nishati na uvuvi.28.      USAWA WA JINSIA KATIKA BAJETI (GENDER BUDGETING)
Mheshimiwa Spika, JINSIA ni dhana inayoelezea tafsiri ya jamii kuhusu wajibu na haki za KE na ME katika jamii, tofauti na JINSI ambayo ni dhana inayoelezea tofauti za kimaumbile au kibaiolojia – yaani hali ya kuzaliwa mwanamke au mwanaume. Kwa kuwa jinsia inahusika zaidi na wajibu au shughuli wanazofanya wanaume au wanawake, basi kwa vyovyote vile shughuli hizo zitakuwa na uhusiano wa moja kwa moja au vinginevyo katika kujenga na kukuza uchumi wa taifa.
Mheshimiwa Spika, Taifa letu linatambua umuhimu wa mchango wa jinsia zote mbili katika kulijenga taifa na ndio maana waasisi wa taifa letu waliafiki kuweka picha au taswira ya mwanaume na mwanamke katika Nembo ya Taifa wakimaanisha kwamba taifa litajengwa na wanaume na wanawake katika kazi zao na nafasi zao mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, ili wanaume na wanawake waweze kutekeleza jukumu hilo la kujenga taifa, ni lazima wapatiwe fursa sawa ili waweze kutumia maarifa yao na uwezo walio nao  kutoa mchango wao katika ujenzi wa taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha hakuna ubaguzi wa kijinsia, ili watu wote waweze kupata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi na hivyo kutoa mchango wao katika ujenzi wa uchumi wa taifa. Miongoni wa hatua hizo ni pamoja na kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusu kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ikiwemo:
                     i.        Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ukatili Dhidi ya Wanawake (CEDAW 1979)
                    ii.        Maazimio ya Beijing
                   iii.        Ajenda ya Umoja wa Afrika Kuhusu Usawa wa Jinsia au Katika Mkakati wa AGENDA 2063
                  iv.        Itifaki ya Usawa wa Jinsia wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) (2007)
                   v.        Malengo Makuu ya Milenia na Sasa Malengo 17 Endelevu ya Dunia (SDGs) nk
Mheshimiwa Spika, pamoja na dhamira hiyo njema ya Serikali, bado kuna changamoto kubwa katika kuzingatia usawa wa kijinsia katika sekta mbali mbali za kiuchumi. Changamoto hizo ni kama ifuatavyo:
                     i.        Wanawake na wasichana wengi hapa nchini hawana fursa na haki sawa katika takriban maeneo yote ya jamii ikiwemo kufikia, kutumia na kumiliki rasilimali zikiwemo ardhi, fedha, taarifa, teknolojia nk. Kwa mfano utafiti wa TDHS 2010 ulibaini kuwa ni asilimia 8 tu ya wanawake wanamiliki ardhi yao peke yao ikilinganishwa na asilimia 30 ya wale wanaomiliki katika mfumo wa pamoja. Aidha, utafiti uliofanywa na Oxfam, 2012 ulibaini kwamba ni asilimia 5 tu ya wanawake wanaofanya kazi za kilimo wenye kumiliki ardhi yao, na asilimia 44 wanafanya shughuli za kilimo kwenye ardhi inayomilikiwa na waume zao na asilimia 35 wanafanya kilimo katika ardhi inayomilikiwa na ukoo. Katika utafiti huo, ilibainika pia kwamba ni asilimia 13 tu ya kaya zinazoongozwa na KE wanapata mikopo ikilinganishwa na asilimia 33 ya kaya zinazoongozwa na wanaume. Hali hii inazuia wanawake kupata fursa za kujiendeleza kiuchumi.
                    ii.        Wanawake na wasichana bado hawana fursa sawa na wanaume kufikia huduma bora za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji , nishati na huduma za ugani. Kwa mfano Demographic Health Survey 2010 ilibainisha kuwa asilimia 19.1 ya wanawake wenye umri kati ya miaka  20 – 24  hawana elimu kabisa ikilinganishwa na asilimia 10.5 ya wanaume.
                   iii.        Wanawake hawana fursa sawa na wanaume katika maamuzi kuhusu maslahi yao kuanzia ngazi ya familia hadi taifa. Utafiti wa DHS 2010 ulibaini pia kwamba katika uongozi wanawake katika ngazi za wilaya na serikali za mitaa wanawake walikuwa ni asilimia 10tu au pungufu.
Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali ubaguzi huo wa kijinsia katika fursa mbalimbali bado kuna ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya wanawake na watoto, vitendo vya ubakaji kwa wanawake, mimba za utotoni kwa wasichana na mila kandamizi dhidi ya wanawake hususan ukeketaji, utakasaji, nyumba ntobhu, nk.
Mheshimiwa Spika, licha ya manyanyaso wanayopata wanawake, imebainika kwamba wao ndio nguvu kazi kubwa inayotegemewa katika ukuzaji wa uchumi. Kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi ya 2012, zaidi ya nusu ya watanzania ni Wanawake katika makundi yote ya jamii ambao fursa zao katika uchumi ni ndogo zaidi ikilinganishwa na wanaume. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema kwama Usawa wa kijinsia ukizingatiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi utasaidia kufikia haraka malengo ya uchumi wa ngazi ya kati – ambao kwa sasa ni uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali kutekeleza mambo yafuatayo:
                     i.        Kuweka lengo mahusi la kuzingatia usawa wa kijinsia ili lielekeze jinsi ya kutafsiri jinsia katika malengo/ vipaumbele vingine vyote na pia kuendeleza juhudi zilizokwishakufanyika kaitka kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali za jamii.
                    ii.        Kuweka mazingira ya kuwajengea uwezo wasichana katika kujenga wataalam wenye ujuzi maalum.
                   iii.        Kuweka mfumo wa bajeti unaozingatia usawa wa kijinsia.

29.      SEKTA YA FEDHA
29.1.  Mikopo ya Kibiashara na Riba
Mheshimiwa Spika, kabla ya Mwezi machi, 2017 riba katika mikopo ya kibiashara ilifikia kati ya 18-26% jambo ambalo lilipelekea kushuka kwa kiwango kikubwa cha mzunguko wa fedha katika uchumi wetu. Hali ya ongezeko la riba katika mikopo hiyo kulitokana na kuongezeka kwa hali ya uhaba wa fedha katika mabenki pamoja na ku-discourage wananchi kukopa ili kukabiliana na kupungua kwa ukwasi wa fedha katika taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Benki Kuu kupunguza kiwango cha mabenki ya kibiashara  kukopa katika benki kuu ya Tanzania toka kiwango cha awali cha 16% mpaka  12% na pia kupunguza amana za mabenki ya kibiashara (statutory minimum reserve requirement) toka 10% mpaka 8% bado hali ya riba na mikopo ya kibiashara ni ngumu kwa wananchi kwa kawaida.  Kwani bado riba zipo juu na wananchi wa kawaida hawawezi kumudu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuchukua hatua ya kuwaeleza mabenki ya kibiashara kupitia BOT kupunguza riba kama ambavyo na wao wamepunguziwa ili wananchi waweze kukopa.


29.2.  Serikali Kukopa Mikopo ya Ndani na Athari zake katika Biashara
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha miaka 3 mfululizo Serikali imekuwa na tabia ya kuendelea  kukopa katika mabenki ya ndani kwa masharti ya kibiashara ili kuhudumia malipo ya madeni ya amana. Kitendo hicho kimepunguza uwezo wa mabenki na taasisi za kifedha kukopesha wananchi kutokana na kukabaliwa na ushindani wa serikali kukopa kwenye mabenki. Mfano katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 serikali inatarajia kukopa ndani tril 7.7 fedha ambazo haziendi katika uwekezaji wa miradi ya kimaendeleo na badala yake ni mkopo wa kulipa mkopo. Hali hii imeathiri sana mzunguko wa fedha katika mabenki na kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaishauri serikali kurudi katika utaratibu wa awali wa kukopa nje mikopo yenye riba nafuu (concessional loans) kwa kukubali kutengeza utaratibu mzuri wa kidiplomasia.

29.3.  Wafanyabiashara Kushindwa Kulipa Mikopo
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali ya kibiashara kuwa mbaya hali ya marejesho ya mikopo katika mabenkI kwa wafanyabiashara imekuwa mbaya katika historia ya nchi yetu kwani imevuka kiwango cha chini cha 5% kinachoruhusiwa. Mpaka sasa mikopo chechefu imefikia 10.3% ya watu kushindwa kulipa madeni kutokana na mikopo iliyokuwa imechukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kupitia BOT kunusuru hali hii ili mabaenki yetu yasije kufilisika.

30.      VYANZO  MBADALA VYA MAPATO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa takriban miaka kumi (10) imekuwa ikitoa ushauri na mapendekezo kuhusu njia mbadala za kuongeza mapato ya Serikali.  Bunge, kwa kuona mapungufu yaliyopo Serikalini katika kubuni vyanzo vipya au vilivyopo kutokuwa na uthibiti navyo, lililazimika kuunda kamati maalum ili kuishauri Serikali jinsi ya kuongeza mapato badala ya kuongeza viwango vya kodi kwa vyanzo vile vile.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna baadhi ya vyanzo tumeishauri Serikali kuvifanyia kazi na imeshindwa inatulazimu kurudia tena, na vyanzo hivyo pia vilifafanuliwa vyema na kamati maalum ya Spika Mstaafu -Anne Semamba Makinda kwenye taarifa ya mapendekezo kuhusu mapato na matumizi ya serikali”,vyanzo hivyo ni vifuatavyo:
1.   Mapato Yatokanayo na Uvuvi katika Bahari Kuu
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa mbali ya kutoza fedha kidogo za leseni kwa ajili ya meli zinazofanya uvuvi katika bahari kuu (deep sea fishing) bado Serikali haipati hata shilingi moja ya mrabaha wa samaki zinazovuliwa na meli hizo.

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa wastani wa meli 41 zinapatiwa leseni kwa mwaka kwa ajili ya kufanya uvuvi katika bahari kuu. Kwa ujumla ni kwamba kiwango cha chini cha ada ya leseni na kukosa mrabaha pamoja na biashara nyingine ambazo zingefanyika kama kungekuwa na bandari ya samaki.  Tanzania inapoteza mapato ya dola za Kimarekani milioni 220  sawa na Tshs. 492,140,000,000/- kila mwaka kutokana na uvuvi haramu.

2.   Mapato Yatokanayo na Sekta ya  Madini ya Vito
Mheshimiwa Spika, eneo hili la madini ni chanzo kikubwa sana cha mapato, lakini ukweli ni kwamba toka hujuma ilisababisha kufa kwa minada ya vito pale Arusha. Baada ya minada kufa, wafanyabiashara hawa, wakaja kwa sura za wawekezaji lakini kiuhalisia walikuwa ni wachuuzi (traders) na waliweza kupata haki zote za kukaa na kufanya biashara mpaka kufikia kutawala soko la ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika,  taarifa ya Kamati maalum ya  Spika Mstaafu - Makinda inaonesha kuwa kuna ofisi zisizopungua hamsini (50) za wageni mjini Arusha zinazonunua Tanzanite na kwamba Wizara ya Nishati na Madini inatoza dola za Kimarekani 200 kwa kila leseni kwa mwaka. Bei hii ni ndogo sana ikilinganishwa na ilivyo katika nchi za jirani zenye vito vyenye thamani ya chini ikilinganishwa na Tanzanite. Kwa mfano Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leseni hutolewa kwa dola za Kimarekeni 50,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo za kampuni za kigeni ada ya leseni ikiwa dola za Kimarekani 50,000 kwa mwaka maana yake mapato yatakuwa dola 2,500,000 ukitumia kiwango cha USD 1 =Tshs 2,237. Mapato yanakuwa Tshs. 5,592,500,000/-
Mheshimiwa Spika, mbali ya ada ya leseni ni kwamba ilikwisha kubalika kwamba madini hayo yasiuzwe nje ya nchi bila ya kusafishwa/ kuchongwa. Lakini kwa sababu ambazo haziko wazi bado madini ya vito yanasafieishwa yakiwa ghafi na hivyo ajira kubwa kuhamishwa na kupelekwa nje ya nchi, katika mchakato huo mapato mengi yanapotea.
Mheshimiwa Spika, India, Jaipur Germs imeajiri vijana/ wafanyakazi wapatao laki moja kwa ajili ya kukata na kusafisha madini ya Tanzanite yanayotoka Tanzania, lakini kwetu vijana walioajiriwa ndani hawazidi elfu tano. Unaweza kuona ni kiasi gani cha TANZANITE kinachokwenda India kwa njia ambazo Serikali haizifahamu. Hii yote ni kukosa uthibiti wa madini hayo.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kuwa na mitambo au vifaa vya kusafisha TANZANITE hapa ni kuzidisha uthibiti wa madini hayo, jambo linalozidisha thamani yake katika soko la kimataifa. Bei nzuri ya madini ya PARAIBA TOURMALINE yanayotoka Nchini Brazil inatokana na udhibiti makini unaofanywa na Serikali ya Brazil. Hivyo kuyafanya yauzwe kwa bei ghali kwa sababu ya uadimu wake katika soko tofauti na Tanzanite ambayo haijafanyiwa udhibiti makini na umiliki wake (branding) halali haujulikani. Mfano kuna Tanzanite- Tanzania, Tanzanite- Kenya, Tanzanite- India, Tanzanite- Sri lanka, Tanzanite- South Africa, nk. Kama Tanzanite ingefikia thamani ya PARAIBA TOURMALINE mauzo yake yangefika dola za kimarekani bilioni moja kwa mwaka (dola za Kimarekani 1,000,000,000).

Mheshimiwa Spika, hali hii huifanya Tanzanite kuuzwa kwa bei ya chini sana ikilinganishwa na PARAIBA TOURMALINE ya Brazil inayouzwa mara kumi ya bei ya Tanzanite ambayo ni kati ya Dola za Kimarekani 1,500-20,000 kwa Karati wakati Tanzanite huuzwa kati ya dola za Kimarekani 150-300 kwa Karati.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo ni dhahiri mapato yatokanayo na mrabaha  ambayo ni asilimia 5 na asilimia 1 kwa kodi ya kukata na kusanifu vito ukiweka na kodi ya PAYE. Hivyo basi, mapato yanakadiriwa kuwa  shilingi 270 bilioni.

3.   Mapato Kutokana na Dhahabu na Madini Mengine
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kuna  makampuni 12 ya uchimbaji wa madini nchini na makampuni hayo mbali ya kulipa mrabaha kwa dhahabu inayochimbwa kwa kiwango cha asilimia 4 tu, lakini bado makampuni hayo hayalipi kodi ya makampuni (corporate tax) kwa ukamilifu wake. Hivyo fedha ambazo hazijalipwa na hivyo  zinatakiwa kulipwa ni takriban kiasi cha dola za kimarekani 265,687,434.9 (Tshs 425,099,895,840/=). Hizi fedha ni mapunjo yanayotakiwa kulipwa, lakini kodi stahiki kwa mwaka .

4.   Kupunguza misamaha ya kodi kuwa 1% ya pato la Taifa
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi kwa sasa ni 1.14% ya pato la taifa na ili kufikia kiwango ambacho kitaleta tija katika uchumi inatakiwa misamaha iwe asilimia 1 au chini ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kwamba 0.14% iliyoongezeka  ya pato la Taifa la shilingi milioni 103,744,606 kuwa ni mapato ya Serikali. Hivyo basi kiasi cha shilingi 145,242,448,400/- kitapatikana.

5.   Uuzaji wa Hatifungani za Kimataifa (EURO BOND FLOATS)
Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza hapo awali kwamba, miradi ya kimkakati kama vile, ujenzi wa mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge, Ujenzi wa Reli ya Kati n.k inaweza kujengwa kwa fedha kwa Serikali kutoa hatifungani kimatifa. Katika chanzo hiki ni dhahiri zinaweza kupatikana shilingi 2.2 trilion.
6.   Mapato kutoka katika Sekta ya Utalii
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya utalii, kampuni zinazojihusisha na shughuli za utalii takwimu zinaonesha kuwa ni 1050, lakini kati ya kampuni hizo zilizosajiliwa kwa biashara hiyo ni kampuni 350 na hivyo kuziacha kampuni 700 bila ya kusajiliwa.  Kama kampuni hizo zikilipa TALA license ya USD 500 inayotakiwa kulipwa na kuacha kodi zingine. Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi 782,950,000/ = ikiwa dola moja ni sawa na shilingi 2237
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna makampuni 1,050 na tukichuulia kuwa kila kampuni ina  wastani wa magari 20 na kila gari moja la kubeba watalii mbugani linalipiwa dola 100 kama vehicle fee. Hapa tutapata jumla ya shilingi 4,697,700,000/-
Mheshimiwa Spika, kuna utalii wa kiasili ambao hadi sasa kivutio hiki hakija rasimishwa, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba hapa itaweza kupata mapato ya shilingi bilioni 300.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 watalii  walioingia nchini ni 1,284,275  na tunatarajia idadi hiyo itaendelea kuwa hiyo au zaidi kwa mwaka wa fedha unaokuja na kila mtalii akilipa Visa fee ya dola 100, maana yake kiasi cha shilingi  287,293,212,300/-
Mheshimiwa Spika, hivyo basi kwa sekta ya Utalii itatoa mapato ya jumla shilingi 592,773,862,300/-
7.   Mapato kutoka kwenye sekta ya michezo ya kubahatisha-Gaming.
Mheshimiwa Spika, mchezo wa kubahatisha ni mchezo ambao hapa nchini unakua kwa kasi kubwa sana na hivyo mchezo huu kama ukiwekewa utaratibu mzuri na mazingira ya kuridhisha kama nchi za wenzetu ni dhahiri ni chanzo kingine cha mapato kwa Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kwa chanzo hiki kitatoa kiasi cha ziada ya shilingi bilioni 30.59

31.      MUHTASARI WA VYANZO VIPYA YA MAPATO MBADALA
NA
MAELEZO
KIASI (TSHS)
KIASI(TSHS)
1.
Mapato yatokanayo na uvuvi katika bahari kuu
492,140,000,000.

2.
Mapato yatokanayo na sekta ya  madini ya vito;
a)   Kutokana na Leseni

 5,592,500,000.


b)    Kodi, Mrabaha na PAYE
270,000,000,000.

3.
Kupunguza misamaha ya kodi kuwa 1% ya pato la Taifa
145,242,448,400.

4.
EURO BOND FLOAT
2,200,000,000,000.

5.
Mapato kutoka katika sekta ya Utalii

592,772,862,300.

6.
Mapato kutoka kwenye sekta ya michezo ya kubahatisha-Gaming
30,000,000,000.59


JUMLA YA VYANZO VYA MAPATO VYA NYONGEZA

3,735,747,810,700.5932.      SURA YA BAJETI MBADALA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
MAELEZO


                         KIASI KATIKA SHILINGI (TZ)

MAPATOA
Mapato ya Ndani

20,725,442,810,700.59       


i. Mapato ya Kodi
17,521,578,448,400.00ii.Mapato yasiyo ya kodi
3,203,864,362,300.59


B
Mapato ya Halmashauri

387,306,000,000.00


JUMLA YA MAPATO YOTE YA NDANI
                                               21,112,748,810,700.59
C
Mapato na mikopo  nafuu kutoka nje

5,071,103,000,000.00


D
Mikopo toka nje masharti ya kibiashara

3,794,985,000,000.00


JUMLA YA MAPATO YOTE(A+B+C+D)
                                29,978,836,810,700.59


MATUMIZI

E
Matumizi ya Kawaida:
i.Deni la Taifa

9,461,433,000,000.00


ii. Mishahara

7,205,768,000,000.00


iii. Wazee

1,200,000,000,000.00


iv. Matumizi Mengineyo:-

2,200,000,000,000.00


a.Wizara -40%
880,000,000,000.00b.Halmashauri-60%
1,320,000,000,000.00JUMLA YA MATUMIZI YA KAWAIDA (i+ii+iii+iv)
                                                       20,067,201,000,000.00

F
Matumizi ya Maendeleo
i.Kilimo -10%
99,116,358 ,070.06ii. Elimu-20%
1,982,327,162,140.12iii. Viwanda-15%
1,486,745,371,605.09iv. Nishati-15%
1,486,745,371,605.09v. Mengineyo 40%
3,964,654,324,280.24JUMLA YA MATUMIZI YOTE YA MAENDELEO (i+ii+iii+iv+v)
9,911,635,810,700.59

JUMLA YA MATUMIZI(MAENDELEO  NA KAWAIDA)


29,978,836,810,700.59


MUHIMU:
1.   Serikali yetu mbadala itafanya “CREDIT RATING” ili iweze kuaminika kimataifa kwa minajili ya kukopeshwa mikopo yenye riba nafuu na pia mikopo ya kibiashara toka nje.
2.   Mapato ya mikopo ya kibiashara kutoka nje yataongezeka kufikia trilioni  3.794t kutoka trillion 1.594 ya Serikali ya sasa kwa sababu, Serikali mbadala itatoa EURO BOND zenye thamani ya DOLA BILLION 1 kimataifa ili kupata fedha za kugharamia bajeti.
3.   Kutokana na kuaminika huko, tutapata mikopo nafuu kutoka nje ya thamani ya shilingi trilioni 5.071
4.   Mapato ya Halmashauri yatashuka kufikia shilingi bilioni 387 kutoka shilingi bilioni 687 ya sasa ili kuziwezesha halmashauri kufanya miradi yake ya maendeleo.33.      HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwakumbusha watanzania kuwa Serikali hii ya CCM inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM John Pombe Magufuli imekuwepo madarakani miaka mingi toka taifa letu lipate uhuru na hivyo matatizo tuliyonayo kama Taifa yana unasaba wa moja kwa moja na serikali hii.
Mheshimiwa Spika, Aidha niwakumbushe pia kuwa Rais aliyepo sasa alikuwepo kwenye serikalini kwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita na kwa hiyo masuala ya ufisadi, sheria mbovu za uwekezaji, sheria za madini na zingine zinazoratibu matumizi ya rasilimali zilitungwa yeye akiwa sehemu ya serikali na kwa hiyo kuwahadaa watanzania kuwa anajenga Tanzania mpya ni mchezo wa kuigiza na propaganda ambazo hazitatujenga kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, Tanzania mpya tunayoiona ni Tanzania ambayo  serikali inaziba wananchi midomo kwa kutumia sheria ya makosa ya kimtandao, Tanzania ambayo wananchi wake hawana haki ya kuona Bunge live ili kuona wawakilishi wao wakitekeleza majukumu yao, Tanzania ambayo vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara kueneza sera zao kwa wananchi tofauti na utaratibu tuliojijengea kwa miaka takribani 25 ya vyama vingi, Tanzania ambayo Katiba ya nchi inakanyagwa kwa kauli na matendo ya baadhi ya viongozi wa serikali, Tanzania ambayo wafanyakazi katika mwaka wa pili wa bajeti hawajashuhudia ongezeko la mishahara yao, Tanzania mpya ambayo watumishi wa umma wanafukuzwa kwenye mikutano ya hadhara kinyume cha sheria ya utumishi wa umma, Tanzania ambayo wasimamizi wa uchaguzi hawatakiwi kuwa na itikadi za vyama lakini sasa wameteuliwa wakurugenzi na makatibu Tawala wa CCM, Tanzania ambayo vyombo vya dola badala ya kulinda mali na raia vinashiriki kwenye matukio ya utekaji na utesaji.
Mheshimiwa Spika, kweli serikali ya awamu ya tano inajenga Tanzania mpya ambayo ni Tanzania biashara zinafungwa, Tanzania ambayo Mamlaka ya Kodi inatisha walipa kodi kwa mitutu ya Bunduki, Tanzania ambayo mauaji yanaendelea huko Kibiti bila jitihaa za dhati za serikali, Tanzania ambayo inaendekeza ubaguzi wa itikadi za kisiasa, Tanzania ambayo vyombo vya habari vinavamiwa na kiongozi wa serikali na mteule wa Rais akiwa na silaha za moto.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Davidi Ernest Silinde (Mb)
Kny: MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
12 Juni, 2017
KIELELEZO A
MCC Statement on Decision of Board of Directors to Suspend Partnership with Tanzania March 28, 2016
Washington, D.C. — In December 2015, the Millennium Challenge Corporation’s (MCC) Board of Directors deferred a vote on the reselection of Tanzania for compact eligibility, citing the nullification of election results in Zanzibar and the need for a prompt, fair and peaceful conclusion of the electoral process.  The Board also sought assurances from the Government of Tanzania that the Cybercrimes Act would not be used to limit freedom of expression and association, in light of arrests made during the elections.  These concerns were repeated on a number of occasions, including in a statement of Ambassador Mark B. Childress
On March 20, 2016, Tanzania moved forward with a new election in Zanzibar that was neither inclusive nor representative, despite the repeated concerns of the U.S. Government and the international community.  The Government of Tanzania has also not taken measures to ensure freedom of expression and association are respected in the implementation of the Cybercrimes Act.
MCC’s model has a partner country’s commitment to democracy and free and fair elections at its core.  The elections in Zanzibar and application of the Cybercrimes Act run counter to this commitment.  As a result, while the United States and Tanzania continue to share many priorities, the MCC Board of Directors determined that the Government of Tanzania has engaged in a pattern of actions inconsistent with MCC’s eligibility criteria, and voted to suspend the agency’s partnership with the Government of Tanzania.  MCC will therefore cease all activities related to the development of a second compact with Tanzania.

KIELELEZO B
Statement on Election Re-Run in Zanzibar[28]
The High Commissioners and Ambassadors to Tanzania of Belgium, Canada, Denmark, the European Union, Finland, France, Germany, Ireland, Italy, the Netherlands, Norway, Spain, Sweden, Switzerland, the United Kingdom and the United States, today issued the following statement regarding the election re-run which took place in Zanzibar on March 20th, 2016:
“We regret the Zanzibar Electoral Commission’s decision to hold a re-run of the 25 October 2015 election, without a mutually acceptable and negotiated solution to the current political impasse.
“In order to be credible, electoral processes must be inclusive and truly representative of the will of the people.
“We reiterate our call on the Government of Tanzania to exercise leadership in Zanzibar, and to pursue a negotiated solution between parties, with a view to maintaining peace and unity in the United Republic of Tanzania.
“We commend once again the population of Zanzibar for having exercised calm and restraint throughout this process, and call on all parties and their supporters to re-start the national reconciliation process to find an inclusive, sustainable and peaceful resolution.”
By U.S. Embassy Dar es Salaam | 21 March, 2016 | Topics: Press Releases


[1] Iliyowasilishwa  tarehe 16/5/2017
[2] Price waters Coopers ,Comparative world studies  of Tax Regimes  2014
[3] Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha na Mipango, fungu la msajili wa hazina imefanya uchambuzi wa uwekezaji wa kizembe usiofuata kanuni na miongozo ya Mifuko  husika kulikopelekea hasara kubwa kwa  baadhi ya mifuko.
[4] Hotuba ya waziri wa fedha na Mipango, Mhe. Dr. Philip I Mpango (MB), akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato  na matumizi yam waka 2017/18, pg,12
[5] Tanzania economic Update Report , May 2016
[6] Ripoti  kuu yam waka ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali, kuhusu taarifa za fedha  za Taasisi za Serikali Kuu kwa mwaka unaoishia  Tarehe 30Juni ,2016. Machi 2017, uk.76
[7] Ofisi ya Taifa ya UKAGUZI, Ripoti kuu ya mwaka  ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Machi 2017
[8] Hotuba  ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. DKT Philip I. Mpango,Mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha mwaka 2017/18, 8 Juni 2017, Uk 26 & 27
[9] Trillion 7.2 zinalipa mshahara   na trillion 9.461 zikihudumia deni la Taifa.
[10] Uk. 79
[11] Kiwango/thamani
[12] Credit Rating is an assessment  of creditworthiness of a borrower  in general terms  or with respect  to a particular  debt or financial obligation. Credit ratings  determines  the likelihood that the borrower  will pay back  a loan  within the confined time of the loan agreement without defaulting.
[13] Interest rate Swap is a contractual agreement  between two parties  to exchange interest  payments
[14] Rejea Hotuba ya Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, wizara ya fedha 2017/18. Ofisi ya Msajili ya Hazina juu ya hali ya Kampuni ya Ndege.
[15] Hotuba ya waziri wa fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (MB), Taarifa ya Hali ya uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2017/18
[16] Hoja ya kutenga 1% ya GDP kwa shughuli za utafiti ililenga kupatia ufumbuzi maswali kama haya.
[17] How can Tanzania move, From  poverty to prosperity? Edited  by L.A. Msambichaka- J.K .Mduma – O .selejio- O.J Mashindano, pg 173
[18] Benki hii ilianzishwa kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia mapinduzi ya Kilimo . Uanzishwaji wa benki hii  ilikuwa  moja ya maazimio kumi ya KILIMO KWANZA yaliyofikiwa mwaka 2009.
[19] India ina diaspora wanaokadiriwa kufikia milioni 20 wanaoishi katika mataifa mbalimbali 70 duniani.
[20] https://www.mcc.gov/news-and-events/release/stmt-032816-tanzania-partnership-suspended
[21] http://www.mwananchi.co.tz/Marekani-yaipoka-Tanzania-Sh-1-4-trilioni/-/1596774/3139372/-/ewa7s1z/-/index.html
[22] https://tz.usembassy.gov/tanzania-at-the-crossroads/
[23] EAC Facts and Figures 2016 Report.
[24] Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18
[25] L. RUTASITARA*, N. OSORO, J. AIKAELI AND G. KIBIRA- DEPARTMENT OF ECONOMICS, UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM - Domestic Resource Mobilization in Tanzania  March, 2010

[26] Banks hit by public entities’ withdrawal of Sh500bn, imetolewa http://www.thecitizen.co.tz/magazine/businessweek/1843772-3340626-57jbnmz/index.html

[28] https://tz.usembassy.gov/statement-election-re-run-zanzibar/
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO