Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MAKALA: Upendo Peneza, mwenyekiti wa wabunge vijana aliyependa siasa akiwa shuleni
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Gazeti Mwananchi
(ssauwa@mwananchi.co.tz)


Dodoma. 
Alianza kuonekana kwenye kwenye runinga katika mashindano ya stadi za maisha, maarufu kama Maisha Plus. Katika mashindano hayo ya mwaka mwaka 2009 alionyesha vipaji vyake mbalimbali na kuwashawishi watazamaji hadi akapigiwa kura kuwa mshindi wa pili.
Licha ya umri wake mdogo wakati huo, uwezo alioonyesha katika kujibu maswali na kupambana na changamoto za maisha katika shindano hilo lililowakusanya vijana mbalimbali kwenye mazingira ya kijijini, ulimfanya aonekane mtu kati ya watu na inawezekana ndio sababu akaibukia kwenye siasa na sasa ni mbunge.

Huyu ni Upendo Peneza (28), mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) kutoka Mkoa wa Geita. Ni miongoni mwa wabunge walioingia bungeni kwa mara ya kwanza katika Bunge la 11 na anasema silaha yake kubwa ni kutokata tamaa.
Kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Vijana Bungeni, umoja unaohusisha wabunge wa itikadi tofauti zilizoko bungeni – chama tawala na upinzani.
“Mimi ndiye mwenyekiti mwanzilishi wa umoja wa wabunge vijana, nafurahia sana tumeweza kutengeneza umoja huu wa kuwasemea vijana wenzetu bungeni,” anasema na kuwashukuru wabunge wenzake vijana kwa kumchagua kuwa mwenyekiti wao.
Umoja huo una wanachama 48 wenye umri chini ya miaka 35, lakini Upendo ana hoja ya kuongeza idadi hiyo kwa kuhusisha wabunge wengine hadi miaka 40, ili kuwawezesha kupata wanachama wengi zaidi katika umoja huo ambao umeanza katika Bunge la 11.
“Tukiwa wengi katika Bunge hili kutatuwezesha kuunganisha nguvu kuwatetea wananchi waliotutuma kuwawakilisha bungeni,” anasema.
Tofauti na makundi mengine ya wabunge, Peneza anasema changamoto zilizopo katika uongozi wa umoja huo hazitokani na kubaguana kiitikadi bali ni za kiutendaji.
“Ni chama kichanga ndani ya Bunge, bado hatuna resources (rasilimali) za kutosha lakini Spika anatuunganisha na vyama vya mabunge ya nchi nyingine, hilo nalo ni la kumshukuru sana kwa sababu anatusaidia kutuhakikishia tunakua na kupata sauti katika Bunge letu na hivyo kujifunza mambo mengi,” anasema.
Anamuomba Mungu amsaidie katika miaka mitano ya ubunge wake aweze kufanya vizuri kwa kuwa huo ndio wakati pekee aliopewa na Mungu.
“Mimi ninaamini kuwa wakati Mungu alionipatia ni sasa, ninamuomba anipatie uwezo, anipatie akili njema ili niweze kuwatumikia Watanzania kwa upendo na uwezo wangu wote waweze kupata maendeleo,” anasema.
Anasema anamuomba Mungu amwongoze kupata fursa kubwa zaidi ya hiyo ili aweze kuitumia kwa faida ya Taifa.
Upendo ametokea wapi?
Kijana huyo baada ya kumaliza elimu yake ya kidato cha sita alijiunga (akijitolea) na taasisi ya Kimataifa ya Vijana (Youth of United Nations Association).
Anasema kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwaelimisha wananchi kwa jinsi gani wanavyoweza kushirikia katika maendeleo kupitia bajeti ili kufikisha malengo ya milenia.
“Katika kuwasaidia wananchi kuhakikisha tunafikia malengo ya milenia mwenyewe nikajikuta navutiwa na suala zima la siasa,” anasema.
Hatua hiyo ilimsogeza zaidi na fursa ya kuwatumikia wananchi na anasema kutokana na hali hiyo aliona haja ya kugombea ubunge ili kushiriki katika kutekeleza mambo yanayomhusu mwananchi moja kwa moja, hivyo akaamua kujiunga na Chadema mwaka 2009.
Mwaka mmoja baadaye aliingia katika kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalumu katika uchaguzi mkuu wa 2010 lakini hakushinda. Hiyo haikumkatisha tamaa kufikia malengo yake. Upendo aliendelea kupambana.
“Vijana wengi huwa wakati fulani wanahisi unahitaji kubebwa, hii si kweli. Ukiangalia safari yangu ya kufika hapa, nimeshiriki katika operesheni zote zilizokuwa zikianzishwa na chama tena kwa kujitolea,” anasema.
Peneza anasema yeye ni miongoni mwa vijana wa Chadema ambao walijitolea katika shughuli za chama bila kulipwa chochote na alikuwa akitumia fedha ambazo alikuwa anapewa na wazazi wake kwa ajili ya kujikimu.
Wazazi hawakupenda siasa
Upendo anasema wazazi wake hawakupenda aingie kwenye siasa kwa wakati huo alioingia. Walitaka asome kwanza.
Ushauri huo ulimsaidia, alilazimika kujiunga na Chuo Kikuu Huria (OUT) mwaka 2009, lakini sababu ya siasa, alichelewa kuhitimu Shahada ya Sosholojia hadi mwaka 2014.
Upendo anasema wakati anasoma kwa kuwa wazazi wake walikuwa Geita na yeye akiwa Dar es Salaam, alikuwa anajiiba na kwenda kwenye shughuli za kisiasa.
“Saa nyingine nilikuwa siwaagi wazazi, siku nyingine namuaga mama na siku nyingine siagi kabisa ilimradi ninatimiza malengo yangu,” anasema.
Shughuli za ujasiriamali
Kijana huyo anasema baadaye alibuni biashara ya kuchapisha fulana zenye nembo ya Chadema, Mwalimu Nyerere na kuziuza na fedha alizokuwa anapata zikawa zinatumika kulipia nyumba ya kulala anapokuwa kwenye ziara za chama.
Anasema anajivunia kwamba alipigania maisha yake hadi hatua aliyofikia kwa kutumia nguvu na ubunifu.
Waliomvutia katika siasa
Mbunge huyo anawataja wanasiasa kadhaa wa Chadema aliovutiwa nao na mifano yao katika siasa, akiwamo Benson Kigaila (mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma); Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare; aliyekuwa mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo (sasa marehemu); Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki); Freeman Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) na Profesa Abdallah Safari na ndio watu ambao walimfundisha hadi amefika hapo.
“Mara yangu ya kwanza kuongea jukwaani ilikuwa ni Tanga katika Operesheni Sangara. Walionifundisha ni Kigaila na Lwakatare. Nilianza kuongea kwa dakika moja nikajitambulisha, nilisalimia tu na kukaa chini,” anasema.
Anasema baada ya hapo ndipo aliongeza muda wa kuongea akiwa jukwaani hadi kufikia dakika 20.
Safari ya ubunge
Anasema baba yake alikuwa hamuungi mkono katika siasa akiamini katika kusoma na kupata kazi ya kuajiriwa. Mwaka 2014 anasema baba yake alimpatia fedha kwa ajili ya kuanzisha biashara, lakini yeye alikuwa mkweli akamweleza asingeweza kufanya vizuri katika eneo hilo.
“Nilimwambia nachotaka kwa sasa ni siasa, nataka nikagombee uenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha) na hata ubunge Geita Mjini. Baba alikuwa anasitasita. Nilimwendea nikiwa na Mawazo lakini bado aliendelea kusisitiza kuwa huko siko,” anasema.
Hata hivyo, baada ya kumsisitizia na kuonyesha wazi hiyo ndiyo nia yake baba yale alikubaliana naye.
Anasema sehemu ya fedha alizompatia kwa ajili ya kufungua biashara alizitumia kufanyia kampeni. “Kwa hiyo hapo alinipa zaidi ya Sh10 milioni kwa ajili ya kufanyia kampeni za kugombea uenyekiti wa Bavicha,” anasema.
Anasema kwa jinsi alivyofanya kampeni kwa kuchapisha mabango, baba yake alikubaliana naye na kuanza kumuunga mkono katika safari yake.
Katika kinyanganyiro hicho, walikuwa wagombea 13, yeye akiwa mwanamke pekee. Alishinda katika mzunguko wa kwanza, ingawa hakufikisha asilimia 50, lakini uchaguzi akapitwa na Patrobas Katambi.
“Baadaye nikaja kugombea ubunge katika Jimbo la Geita Mjini na viti maalumu ndani ya chama. Ingawa nilishindwa kura za jimboni, lakini nilipata ubunge kupitia kundi la viti maalumu, anasema mwanasiasa huyo.
Akiwa mbunge, Upendo anasema hatua ya Rais John Magufuli kusitisha semina elekezi ni moja ya mambo yaliyompa tabu sana.
“Ndio, kuna vitabu tunaweza kusoma lakini ufafanuzi ni jambo muhimu sana kwetu wabunge wapya. Kwa hiyo nilikuwa na kazi ya ziada ya kujifunza. Inabidi ufuatilie uweze kufahamu masuala ya Bunge. Kwa semina elekezi ungeweza kuelewa kwa siku mbili lakini unachukua muda mrefu,” anasema.

Anasema miongoni mwa mambo aliyowahi kufanya ni kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka fedha za kununulia dawa nchini ziwekwe kwenye fungu la matumizi ya kawaida ili kuwezesha fedha kutolewa kila mwezi badala ya kutolewa kwenye fungu la maendeleo.
Anasema kwa kufanya hivyo, itakuwa sio mara ya kwanza kufanyika kwa jambo hilo kwa sababu Afrika Kusini na nchi za Sadc zinatumia utaratibu huo.
Hata hivyo, anasema hoja hiyo hadi leo haijapata nafasi tangu aiwasilishe Ofisi za Bunge mwaka jana.
Nini kinamkwaza?
Mbunge huyo anasema pamoja na kuwa Bunge limekuwa chuo cha mafunzo kwake kila siku kwa kuwa amekutana na wabunge wenye taaluma na itikadi tofauti, kitendo cha hoja kuamuliwa kwa misingi ya vyama ni mambo ambayo yanampa shida katika Bunge.
“Sijajifunza kwa wabunge wa chama changu tu, bali hata kwa wabunge wa chama tawala wamenifundisha mambo mengi. Hata kama mtu hana elimu kubwa, lakini unakuta kuna eneo lake alilobobea ukiongea naye unaongeza jambo katika utendaji wa kisiasa kila siku.
Mafanikio anayojivunia
Upendo anasema ameunda vikundi vya wanawake katika Mkoa wa Geita ambao wanajishughulisha na ujasiriamali.
“Hawa wanawake wananifurahisha, nilifanya ziara ya kuhamasisha wanawake kutengeneza vikundi, walikusanyika na miongoni mwao wapo wanaojishughulisha na ufugaji wa bata, nguruwe na hili ndilo nahangaika nalo kuhakikisha wanafika mbali,” anasema.
Anasema hadi sasa kuna vikundi zaidi ya 30 ambapo wanawake wanajiwekea akiba kupitia Vicoba walivyoviunda.
“Nimeweza kutoa bima ya afya kwa wanawake kama 200 ambao walifika katika siku ya maadhimisho ya wanawake duniani ni kama motisha,” anasema.
Anasema lengo lake ni kuhamasisha wanawake wengi wanajiunga na bima ya afya ili kuwawezesha kupata huduma za uhakika za matibabu.
“Hapa sasa linabaki jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa wananchi hawakosi huduma ya afya pindi wanapohitaji huduma hizo,” anasema.
Pia, anashauri kupanua wigo kwa wananchi kutibiwa katika maeneo yote nchini iwapo watapata kadi za bima ya afya.
Mambo yanayomuumiza
Anasema wanafunzi wa kike wamekuwa wakipata tabu ya kujihifadhi wakati wa siku zao, hali ambayo inawafanya wengine kushindwa kufika shule kwa kukosa taulo na maeneo ya kujihifadhia. “Nahangaika kuhakikisha watoto wa kike waliopo shule wanapata taulo za kujihifadhi, ipo siku nitafanikiwa ili kuwawezesha kusoma vizuri,” anasema.
“Hata katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nimechangia kwa njia ya maandishi kuwa watoto wa kike waliopo shuleni wapate sanitation towels (vifaa vya kujihifadhia lakini nilikuwa nina mpango wa kushika shilingi lakini sikupata nafasi,” anasema mbunge huyo.
Suala lingine linalomsumbua ni wachimbaji wadogo wa madini Geita kupata maeneo ya uchimbaji ambayo anasema anaendelea kuyapigania.
“Tunaendelea kuiambia Serikali wananchi wa Geita wanaomba maeneo ya kuchimbia. Kipindi cha nyuma Rais alitoa magwangala (mabaki ya mawe ya dhahabu) yale si suluhisho, wananchi walikwenda kuyaangalia wakakuta hayana dhahabu,” anasema.
Mfumo dume wamtesa
Upendo anasema jambo jingine linalomuumiza katika miaka yote aliyoishi katika siasa ni mfumo dume uliotawala nchini, hasa katika kuwania nafasi za kisiasa.
“Hata wakati ninagombea uenyekiti wa Bavicha nilipambana nalo, sio kwa sababu ya uwezo ulionao mtu bali watu wanataka kukukandamiza,” anasema.
Anasema wakati mwingine huwa ni changamoto ambazo ziko ndani ya vyama katika kumwezesha mwanamke kupiga hatua kwenye jambo fulani.
“Changamoto kubwa wakati mwingine ilikuwa kwa sababu ya umri wangu, hawakupimi kwa sababu ya uwezo ulionao katika jambo unalolitaka kulifanya bali wanaangalia umri ulio nao,” anasema mwanasiasa huyo.
Anasema umbo pia lilikuwa likisababisha watu kumuona ni mdogo kwa hiyo asingeweza kumudu baadhi ya nafasi za uongozi.
Pia, anasema katika kampeni watu wengi hutanguliza fedha kuliko uwezo wa mtu katika nafasi anayogombea na wananchi wengi hawaangalii mtu atakuwa na uwezo wa kuwawakilisha, bali fedha kiasi gani anazowapa.
“Wanaangalia huyu mtu anaweza kutupa leo Sh5,000, hawaangalii huyu bungeni ataweza kunisemea kwa kiasi gani ili matatizo yangu yaweze kupata utatuzi,” anasema.
Kitu asichosahau
Katika maisha yake, Penaza anasema hawezi kusahau mauaji ya kikatili ya mwenyekiti wake, Mawazo na hasa kutokana na hatima ya waliohusika na mauaji hayo kutofahamika.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO