Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Bajeti ya 2012/13 ni bajeti ya kilio

 

•  KODI ZA VINYWAJI BARIDI, BIA, SIGARA, SIMU JUU

IMG_1670 Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa  akionyesha mkoba wenye Bajeti ya Serikali ya  2012/13 Bungeni Mjini Dodoma Juni 14, 2012. (Picha kwa hisani ya http://freebongo.blogspot.com)

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, jana alitangaza bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, ambayo imeongeza kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi pamoja na bidhaa mbalimbali.

Bajeti hiyo ya sh trilioni 15 imeonesha kuwa kufanikiwa kwa shughuli za maendeleo ya nchi zitategemea zaidi misaada ya wafadhili na marafiki wa nje, ambao sasa watahitaji kuisaidia serikali kwa zaidi ya nusu ya fedha zilizotengwa kwa mwaka ujao wa fedha.

Akiwasilisha hotuba hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, Waziri Mgimwa alitaja ongezeko la kodi katika bidhaa kadhaa za ndani na nje, muda wa maongezi wa simu za mkononi pamoja na kuongezwa kwa kodi katika mishahara ya wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi.

Aidha, bajeti hiyo haikuwaacha nyuma wafanyabiashara wadogowadogo, ambao sasa watalazimika kulipa kodi ya mapato kati ya sh 100,000 hadi sh 575,000.

Pamoja na kuongezwa kwa viwango hivyo vya kodi, kwa mara ya kwanza serikali imetangaza kutoza kodi katika bidhaa za muziki, filamu na mikanda ya video (DVD, VCD, CD).

Katika hotuba yake iliyochukua saa 2:30; tangu saa 10:00 jioni hadi saa 12:30, Waziri Mgimwa alisema kodi ya mishahara ya wafanyakazi itatozwa kulingana na ongezeko la mshahara wa mfanyakazi. Hata hivyo, hakuweka wazi kiwango cha chini cha kodi kilichoongezwa.

Kodi nyingine zimeongezwa katika juisi ya matunda zinazozalishwa hapa nchini kwa sh 8 kwa lita, wakati zile zinazotoka nje ya nchi zitatozwa sh 83 na kwamba mabadiliko haya yamekusudia kuondoa ushindani usio wa haki.

Vinywaji baridi vimeongezeka kodi kutoka sh 69 hadi sh 83, mvinyo wa zabibu kutoka nje ya nchi unaongezeka kodi kutoka sh 1,345 hadi sh 1,614 kwa lita.

Navyo vinywaji vikali kodi yake imepanda kutoka sh 1,993 hadi sh 2,392 kwa lita, wakati bia ya hapa nchini imepanda kutoka sh 248 hadi sh 310 kwa lita huku zile za nje sasa zitatozwa kodi ya sh 525 badala ya sh 420.

Kwa upande wa sigara zisizo na vichungi, kodi yake imepanda kutoka sh 6,820 hadi sh 8,210 kwa sigara 1,000 wakati zile zenye vichungi zilizotengenezwa na tumbaku ya hapa nchini, sasa zitatozwa kodi ya sh 16,114 hadi sh 19,410, sigara zenye sifa mbali na hizo zitatozwa kodi ya sh 35,117.

Vitu vingine vilivyoongezewa kodi ni pamoja na michezo ya kasino na ile ya kubahatisha kutoka asilimia 13 hadi 15, michezo ya utabiri wa matokeo ya michezo kwa asilimia sita na asilimia 43 kwenye michezo ya bahati nasibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu.

Aidha, serikali pia imeamua kuanzisha utozaji wa ada kwa wamiliki wa magari ambao watataka kusajili namba zenye utambulisho maalumu kwa ada ya sh milioni tano kwa kila miaka mitatu.

Kodi nyingine zilizoongezeka ni za viwanja vya ndege kutoka kiwango cha sasa cha dola 30 hadi 40 kwa safari za nje ya nchi na sh 5,000 hadi sh 10,000 kwa safari za ndani.

Watumiaji wa simu za mkononi sasa watalazimika kulipa kodi ya asilimia 12 badala ya asilimia 10.

Vipaumbele vya bajeti

Hata hivyo, Waziri Mgimwa alitaja vipaumbele vya bajeti kuwa ni pamoja na kukuza pato la taifa kwa asilimia 6.8 kutoka asilimia 6.4 kwa mwaka 2011.

Serikali pia imelenga kuimarisha miundombinu ya uchumi, ikijumuisha sekta ya umeme, barabara, reli na bandari, huduma za kifedha na kuongezeka kwa mapato ya ndani ili kufikia uwiano wa pato la taifa la asilimia 18 kwa mwaka 2012/13.

Vipaumbele vingine ni kudhibiti mfumko wa bei ili urudi katika viwango vya tarakimu moja, kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje pamoja na kujengea uwezo wananchi ili kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha.

Katika bajeti iliyotangazwa jana, serikali inatarajia kutumia sh trilioni 15.119, kati ya hizo, trilioni 4.527 zikielekezwa katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Hata hivyo, kiasi cha sh trilioni 2.314 za fedha hizo za maendeleo, zitapatikana kutoka kwa nchi wahisani watakaokubali kuisaidia nchi, huku uwezo wa serikali kuchangia shughuli hizo ukiwa ni sh trilioni 2.213.

Matumizi ya kawaida yamechukua kiasi kikubwa cha bajeti, huku wizara zote zikitengewa sh trilioni 3.311, mikoa yote sh bilioni 49.7 na halmashauri zote sh bilioni 704.5.

Matumizi yanayoitwa mengineyo, yametengewa sh trilioni 4.065, mishahara sh trilioni 3.781 na kulipa deni la taifa sh trilioni 2.745.

Katika mchanganuo wa vipaumbele hivyo, Dk. Mgimwa alisema kuwa kwenye miundombinu, umeme utawekewa mkazo ili upatikanaji wake uwe wa kuhakika kwa kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, ambapo jumla ya sh bilioni 498.9  zimetengwa kwa ajili hiyo.

Aidha, serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya dola za Marekani milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.

Kwenye usafirishaji na uchukuzi, serikali itaimarisha Reli ya Kati ikijumuisha ukarabati wa injini na mabehewa ya treni na upande wa barabara, miradi inayopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi.

Katika usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika ambapo sh bilioni 1,382.9 zimetengwa katika eneo hili.

Kuhusu maji safi na salama, serikali itaongeza upatikanaji wake mijini na vijijini ambapo sh bilioni 568.8 zimetengwa.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), serikali itaimarisha mawasiliano kwa kutumia Tehama ili kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali, ikiwa imetengewa sh bilioni nne.

Kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji, waziri alisema kuwa watashirikiana na sekta binafsi na katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, huku sh bilioni 192.2 zimetengwa katika eneo hili.

Dk. Mgimwa aliongeza kuwa sh bilioni 128.4 zimetengwa katika maendeleo ya viwanda huku maendeleo ya rasilimali watu na huduma za jamii zikitengewa sh bilioni 84.1.

Katika utalii, alisema kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii, kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii

Chanzo: Tanzania Daima, June 15, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO