MKUTANO wa Nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaanza vikao vyake leo ambapo mbali na shughuli nyingine, wabunge walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, akiwemo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, watakula kiapo.
Kwa mujibu wa ofisi ya Bunge, mara baada ya wateule hao, Prof. Sospeter Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini), Saada Salum na Janeth Mbene, ambao ni manaibu waziri wa Fedha na Mbatia kuapishwa, kamati za vyama vya siasa bungeni zitaketi na kujadili mambo mbalimbali.
Pia taarifa hiyo ilisema kuwa bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2012/13 itasomwa Alhamisi wiki hii na kwa mujibu kanuni ya 97(1) ya kanuni za Bunge toleo la 2007, imeweka kiwango cha juu cha siku zitakazotumika kwa ajili ya mjadala wa hotuba ya bajeti ya serikali kuwa ni siku tano.
Katika mkutano huo pia miswada ya sheria itasomwa kwa mara ya kwanza ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 na Muswada wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2012.
Hotuba ya Waziri Mkuu juu ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika mwaka wa fedha unaomalizika, na matarajio yake kwa mwaka fedha ujao itasoma Juni 25 na kujadiliwa hadi Juni 29.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kutakuwa na uchaguzi wa mwenyekiti wa Bunge ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na George Simbachawene mbunge wa Kibakwe (CCM) aliyeteuliwa na Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini
Chanzo: Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment