Taarifa fupi kutoka CHADEMA kupitia kwa Mh John Mnyika inaeleza kuwa heshima za mwisho kwa marehemu Bob N. Makani z(pichani) itatolewa kesho,Juni 11, 2012 kuanzia saa 6 mchana, Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Jakaya Mrisho Kikwete ameitumia familia ya Mzee Bob N. Makani salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mzee huyo kilichotokea usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesema kuwa amehuzunishwa na kusikitishwa na habari za kifo cha Mzee Makani ambaye alilitumikia taifa la Tanzania kwa uadilifu na uzalendo katika nafasi mbali mbali alizozishikilia katika maisha yake ikiwamo ile ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo katika mtandao wa Wavuti, zinaeleza kuwa, Mdogo wa marehemu, Hassan Makani amesema marehemu, Bob Makani anatarajiwa kuzikwa Jumatano katika kijiji cha Negezi, Shinyanga.
Makani alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.
Kazi ambazo amewahi kuzifanya serikalini; alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 na elimu yake ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere nchini Uganda.
Marehemu Makani ameacha mke na watoto saba na wajukuu wanane.
Source: vyanzo mbalimbali
0 maoni:
Post a Comment