ALIYEKUWA mgombea Ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ng’umbi amewasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya kesi ya uchaguzi iliyompa ushindi John Mnyika.
Ngh’umbi, alifungua kesi dhidi ya Mnyika wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akipinga matokeo yaliyompa ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu kanuni na sheria ya uchaguzi katika uchaguzi huo .
Lakini Mahakama Kuu katika hukumu yake ilitupilia mbali madai na maombi ya Ngh’umbi na badala yake ikamthibitisha Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo la Ubungo. Katika hukumu hiyo aliyoisoma Mei 24, 2012, Jaji Upendo Msuya alisema kuwa Ngh’umbi alishindwa kuthibitisha madai yake na kuonesha jinsi madai hayo yalivyoathiri matokeo ya uchaguzi huo.
Baada ya hukumu hiyo Ngh’umbi alielezea kutokuridhika na uamuzi huo na kudai kuwa anakwenda kujadiliana na wakili wake ili kuona ni hatua gani ya kuchukua. Jana Ngh’umbi kupitia kwa wakili wake, Issa Maige, alianza rasmi mchakato wa kupinga hukumu hiyo baada ya aliwasilisha Mahakama ya Rufani hati ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Chanzo: Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment