Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mukama awatibua CHADEMA msibani

•  MBOWE AKEREKA, AMJIBU KWA VIELELEZO

na Asha Bani

MUKAMA Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akitoa neno lililowaudhi CHADEMA, kabla ya kuagwa mwili wa marehemu Bob Makani (Picha: http://bashirnkoromo.blogspot.com)

********

KATIKA kile kilichoonekana kama vijembe vya kisiasa kuutawala msiba wa muasisi wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Bob Makani, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kauli yake kupingwa vikali na Freeman Mbowe.

Mukama wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya chama chake katika viwanja vya Karimjee zilikofanyika shughuli za kuuaga mwili wa marehemu, alimsifu Makani akisema alikuwa ni Katibu Mkuu wa Kwanza wa CHADEMA kutoka nje ya kanda ya kaskazini kati ya waasisi wenzake tisa.

Mbali na sifa nyingi alizommwagia marehemu, Mukama pia alisema CHADEMA wanatakiwa kuweka kumbukumbu hiyo kwa kuwa alikuwa ni mtu shupavu asiyependa kuongea wala kuhubiri kwa muda mrefu na asiyekumbatia udini, ukabila na ukanda.

Hata hivyo, wakati Mukama akieleza hayo, viongozi wengi wa CHADEMA walionekana kushangazwa na kauli ile ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, katika salamu zake alitumia mwanya huo kumjibu kwa vielelezo.

Mbowe alisema kuwa kitendo cha kusema kuwa CHADEMA kiliasisiwa na watu tisa kutoka eneo moja la kanda ya kaskazini ni uchafuzi wa kihistoria ndani ya chama hicho.

Katika kuonesha kukerwa na kauli hiyo, Mbowe alilazimika kuwataja waasisi na mikoa yao kuwa ni Edwin Mtei (Arusha), Makani (Shinyanga), Marehemu Brown Ngwilupipi (Iringa), Edward Barongo (Kagera), Mary Kabigi (Mbeya), Menrad Mtungi (Kagera), Costa Shinganya (Kigoma), Evalist Maembe (Morogoro) na Steven Wassira (Mara).

“Mimi wakati huo nilikuwa mdogo na shughuli zangu zilikuwa ni kuandaa vikao na mikakati ndani ya chama. Nashangaa sana wakati nakumbuka historia ya chama hiki, hivyo watu wasijaribu kuipotosha,” alisema Mbowe.

Mbowe pia aligusia suala zima la uanzishwaji wa mchakato wa Katiba mpya akisema ni lazima kufanyike na marekebisho ya mfumo wa kisheria ili kuwapa nafasi wenye uwezo kuingia bungeni na kutoa michango ya maendeleo kwa jamii.

Alisema mwaka 1995, 2000 na 2005 Makani aligombea ubunge Shinyanga Mjini akashindwa, hivyo ni vema watu kama hao wenye mchango mkubwa wakaingizwa bungeni kwa ajili ya kuleta changamoto mbalimbali.

Rais Kikwete amlilia

Rais Jakaya Kikwete naye alielezea kuhuzunishwa kwake na msiba huo na kusema kuwa Bob Makani alikuwa ni mtu muhimu na msaada mkubwa katika michango yake aliyowahi kuitoa katika kukuza uchumi wa nchi.

“Nilisikia taarifa za msiba ambao ulinihuzunisha na kushtuka sana nikajaribu kumpigia simu Mwenyekiti wa Chama, Mbowe, lakini hakupatikana kwa kuwa alikuwa katika shughuli kubwa huko Ruangwa, nikamtumia ujumbe mfupi na baada ya kuupokea akanipigia na mimi nilikuwa katika shughuli sikupatikana, hivyo nikampigia tena baadaye ndipo tukazungumza,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema kuwa ni vema kuhuzunika kwamba tumepoteza mtu muhimu lakini pia iendane sambamba na kusherehekea na kuyaenzi mambo yake mazuri ambayo ameyafanya wakati wa uhai wake.

Prof. Lipumba akumbusha enzi

Kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba, alimwelezea Makani kuwa alikuwa mtu mzuri na kwamba CHADEMA inatakiwa kuiga mfano wake wa kuunganisha watu.

Alisema alikuwa ni mwana mageuzi aliyeasisi harakati za mabadiliko ya Katiba na kusema alipata suluba pamoja naye katika mapambano hayo. Pia alikumbushia enzi zao za shule akisema Makani alikuwa na akili nyingi darasani.

Muasisi wa CHADEMA ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu na Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, Erdwin Mtei, alimtaka Makani kuwa alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu, na ameeleza masikitiko yake ya kuondokewa na mwenzake.

Mtei alisema Makani kwa nafasi yake katika BoT alikuwa ni mtu aliyejali maslahi ya nchi na pia mwepesi wa kutoa taarifa za fedha.

Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema walifaidi utawala wa sheria na aina ya uongozi wa Makani kutokana na kuwa mwanasheria.

Alisema Makani ni mfano wa kuigwa kwa kuwa alikuwa ni mtu wa watu aliyekuwa na kipaji cha kuelewa wananchi ambapo urefu wake uliweza kuonekana kila mahali alipoenda sambamba na ucheshi wake.

Asema kuwa Makani alizaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Kolandoto, Shinyanga na kusoma shule ya msingi Ibadakuli mkoani humo. Alifauru sekondari na kupelekwa Chuo Kikuu cha Makerere, ambako alifuzu na kupata Shahada ya Kwanza katika Uchumi (BA Economics).

Mwaka wa 1961 alikwenda Chuo Kikuu cha Liverpool, nchini Uingereza na 1965 akatunukiwa Shahada ya Sheria (LLB) alirudi nchini ambapo aliajiriwa na serikali kama Mwanasheria wa Serikali kwa muda mfupi kabla hajapandishwa cheo na kuwa Exchange Control Manager wa Benki Kuu.

Makani ni mwasisi wa CHADEMA mwenye kadi namba tatu baada ya Edwin Mtei, na marehemu Brown Ngwilulupi. Mwaka wa 1998 akachaguliwa kuwa mwenyekiti chama hadi 2003.

Makani pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi za wakurugenzi katika Shirika la Ndege Tanzania, Williamson Diamond, Tanzania Breweries, Benki ya Taifa ya Biashara na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO