Kenya imetangaza siku tatu za maombolezi baada ya kifo cha Waziri wa Usalama wa Kenya, Profesa George Saitoti, na naibu wake, Orwa Ojode, kwenye ajali ya helikopta ya polisi katika eneo la Ngong, nje ya Nairobi.
Rais Mwai Kibaki alisema kifo cha Bwana Saitoti ni msiba mkubwa kwa taifa, na serikali imetangaza kuwa baraza la mawaziri litakutana Jumatatu, kujadili tukio hilo.
Idara ya polisi imesema uchunguzi utafanywa kujua sababu ya ajali hiyo, na balozi wa Marekani mjini Nairobi, amesema Marekani iko tayari kusaidia kwenye uchunguzi huo, ikiwa itatakiwa kufanya hivo.
Msemaji wa polisi alieleza kwamba inavoelekea kuanguka kwa helikopta hiyo lilikuwa tukio la ajali.
Raia wa Kenya walikuwa na masikitiko Jumapili, baada ya taarifa ya ajali hiyo kujulikana, na watu wamekuwa wakizuru nyumba ya kuhifadhi maiti mjini Nairobi kutoa heshima zao.
Makamo wa rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka, alipofika kwenye tukio la ajali alitoa rambi-rambi zake na alieleza wale waliokuwamo ndani ya ndege ambao wote wameteketea:
"Ndege hiyo ya aina ya Eurocopter ya police airwing, ambayo ilikuwa inaelekea Yugis, ilikuwa imembeba Waziri George Saitoti, naibu waziri Orwa Ojode na maafisa rubani wa ndege, Nancy Gitwanja na Luke Oyugi, na vilevile askari wawili ambao wanakuwa wanaandamana na Waziri Saitoti, Inspector Tonkei na Thomas Murimi"
Rambi-rambi zimekuwa zikimiminika nchini Kenya, pamoja na za Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ambaye alipatanisha baada ya ghasia za uchaguzi uliopita nchini kenya.
Profesa Saitoti alikuwa akizungumza kwa ukali dhidi ya al-Shabaab na inaaminiwa alihusika na uamuzi wa jeshi la Kenya kuingia Somalia mwaka jana.
Bwana Saitoti aliwahi kuwa makamo wa rais na waziri wa fedha katika serikali ya Rais Moi, na akitarajiwa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Alikuwa na umri wa mika 67
Source: BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment