Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA wafungua kesi ya madai dhidi ya madiwani waliowatimua

na Grace Macha, Arusha

DSC09812CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefungua shauri la madai ya gharama za kesi ya zaidi ya sh milioni 35.1 dhidi ya waliokuwa madiwani wake watano waliowatimua katika Jimbo la Arusha Mjini.

Madiwani hao na kata walizokuwa wakiongoza kwenye mabano ni Charles Mpanda (Kaloleni), John Bayo (Elerai), Estomih Mallah, (Kimandolu), Rehema Mohamedi (Viti Maalumu) na Reuben Ngowi (Themi).

CHADEMA wamefungua madai yao kupitia kwa wakili wao, Method Kimomogoro, ambapo yanatarajiwa kutajwa kesho (Julai 24) mbele ya Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Wilbad Mashauri.

Shauri hilo linatokana na hatua ya madiwani hao kushindwa kuhudhuria kwenye shauri lao walilofungua Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, mbele ya Jaji Kakusolo Sambo wakiiomba ifanyie mapitio uamuzi wa kulipa gharama za kesi uliotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Arusha, Charles Magesa.

Hata hivyo Jaji Sambo aliamua kutoa uamuzi wa kufuta shauri hilo Aprili 2, mwaka huu baada ya madiwani hao kutoonekana mahakamani hapo bila taarifa mara mbili mfululizo, ambapo aliwataka kulipa gharama za usumbufu.

Novemba 22, 2012 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha iliwaamuru madiwani hao waliotimuliwa CHADEMA kulipa zaidi ya sh milioni 15, ambapo kila mmoja alitakiwa kulipa sh milioni 3.1 ndani ya miezi miwili kama gharama za kesi waliyokuwa wamefungua kupinga kufukuzwa uanachama, vinginevyo watapelekwa gerezani.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Magesa, alitoa hukumu hiyo baada ya chama hicho kushinda kesi hiyo na kuwaamuru kulipa sh milioni 15 ndani ya miezi miwili, wakishindwa watapelekwa gerezani.

Hata hivyo tayari wadaiwa hao walikwisha kulipa deni hilo, isipokuwa Bayo ambaye anadaiwa sh laki 5.7 na Mpanda anayedaiwa sh milioni 1.5, ambapo tayari mahakama hiyo ilishatoa hati ya kukamatwa kwao tangu Februari 19, 2013.

Wakili wa CHADEMA kwenye shauri hilo, Kimomogolo, alisema kuwa wateja wake walishawasilisha mahakamani hapo fedha kwa ajili ya kuwahudumia waliokuwa madiwani wakati wakiwa gerezani.

Madiwani hao walitimuliwa CHADEMA baada ya kufikia muafaka wa uchaguzi wa umeya wa Jiji la Arusha bila kupata baraka za chama, ambapo tayari uchaguzi wa kata hizo umeshafanyika na CHADEMA walifanikiwa kutetea viti hivyo.

Source: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO