Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Obama aishika Dar • Ulinzi kila kona, FBI,CIA watamba

JIJI la Dar es Salaam leo litakuwa kwenye heka heka kubwa za kumpokea Rais wa Marekani, Barrack Obama anayetarajia kuwasili saa nane mchana.

Ujio wa kiongozi huyo umesababisha kufungwa kwa barabara na kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.

Kwa takribani wiki moja sasa ulinzi umeendelea kuimarishwa zaidi kwa kuwashirikisha makachero wa Marekani wakiwemo FBI, CIA na wale wa  Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Obama anayeongozana na familia yake anatarajiwa kupokelewa jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete na baadaye atakwenda Ikulu kwa mazungumzo rasmi.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa Obama atapata fursa ya kufanya mkutano na wafanyabiashara Ikulu pamoja na kuhudhuria dhifa ya kitaifa.

Kesho atakwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Symbion iliyopo Ubungo, Dar es Salaam na kuzindua rasmi Mpango Maalum wa Maendeleo ya Nishati Barani Afrika ulioanzishwa na Marekani wa Power Africa Initiative.

Kutokana na ujio huo wa Obama, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yalikuwa na ulinzi mkali wa makachero wa Marekani na Tanzania pamoja na barabara atakazopita kiongozi huyo kufanyiwa usafi.

Barabara atakazopita Obama pia zimefanyiwa matengenezo madogo madogo hususani zile zilizokuwa na mashimo, huku nyingine zikiwekewa taa za barabarani pamoja na bendera za mataifa hayo mawili.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao pembeni mwa barabara anazopita kiongozi huyo, wamehamishwa na usafi umekuwa ukifanyika kwa kiwango cha juu.

Katika viwanja vya Karimjee ambako kulikuwa kukitolewa vitambulisho vya watu watakaoshiriki kwenye matukio hayo, kulikuwa na idadi kubwa ya magari ya kisasa yatakayowabeba.

Magari hayo mengi yakiwa ni mabasi madogo, yalikuwa na bendera za Marekani na maandishi maalumu ya kuelekeza ni watu wa aina gani wanaopaswa kuyatumia.

Mpango wa nishati ya umeme

Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi saba ambazo zinatarajiwa kufaidika na ziara ya Rais Obama katika mpango wake maalumu wa maendeleo ya nishati barani Afrika ulioanzishwa na nchi yake wa ‘Power Africa Initiative’.

Mpango huo utazinduliwa kesho na Rais Obama anayetarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya siku mbili.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, jana jijini Dar es Salaam imeeleza kuwa nchi nyingine zinazotarajiwa kufaidika na mpango huo utakaogharimu dola bilioni 7 katika awamu ya kwanza mbali na Tanzania, ni Ethiopia, Kenya, Liberia, Nigeria, Uganda na Msumbiji.

Taarifa hiyo ilielezea sababu za nchi hizo kuchaguliwa ni kutokana na malengo yao kabambe ya kufanya mageuzi ya sekta ya nishati kwa ajili ya kusafisha njia kwa ajili ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, ilielezea kuanzishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Nishati barani Afrika kumechangiwa na wakazi wengi kukosa huduma hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa “zaidi ya mbili ya tatu ya watu wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara hawana huduma za umeme, na wengine zaidi ya asilimia 85 wanaoishi maeneo ya vijijini hawapati huduma ya umeme.”

Ilisema kuwa mpango huo kwa eneo la nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara unahitaji zaidi ya dola bilioni 300 kwa ajili ya kukamilika hadi ifikapo mwaka 2030.

Obama yuko katika ziara ya Afrika akiwa tayari ametembelea nchi za Senegal na Afrika Kusini na leo anatarajiwa kumalizia nchini Tanzania.

Akiwa Senegal

Akiwa katika ziara yake nchini Senegal, Obama alijikuta katika wakati mgumu kutokana na mwenyeji wake, Rais Macky Sall kupinga kauli yake ya kumtaka kurekebisha sheria zao za kutoa haki kwa makundi ya mashoga.

Rais huyo alipinga kauli hiyo, mbele ya wanahabari ambako alisema; “ingawa Senegal ni nchi tulivu sana, lakini haiko tayari kuruhusu maingiliano ya ngono kati ya watu wenye jinsia moja, na hatuko tayari kubadili sheria kwa ajili ya kuwatambua kwa sababu nchi hii watu wake wengi ni waumini wa dini ya Kiislamu ambao wanakataa kusikia hilo likitokea.”

Baada ya kuona sheria yake imeshindwa kupenya, Obama alisema kuwa nia yake katika mkutano huo haikuwa kufanya majadiliano ya suala hilo na Sall.

Afrika Kusini

Akiwa Afrika Kusini, Obama alipata fursa ya kuzungumza na rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma. Pia alimtakia afya njema mpigania haki za watu weusi, Nelson Mandela ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya Pretoria nchini Afrika Kusini kwa muda wa wiki tatu sasa.

Alitoa wito kwa viongozi wa Afrika na duniani kwa jumla kufuata mfano wa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini, kwa kulitanguliza mbele taifa zaidi ya nafsi yake.

Obama alisema viongozi wanaoshikilia nyadhifa hizo kwa muda wanatakiwa kutodanganyika na kujua kuwa hatima ya nchi zao haitegemei watakavyoendelea kuwa madarakani.

Akiwa nchini humo, alipata nafasi ya kuwajulia hali ndugu wa Mandela ikiwa ni pamoja na jana kutembelea katika kisiwa cha Robben, ambako Mandela alifungwa kwa muda wa miaka 18 kati 27 aliyokuwa amehukumiwa.

Baada ya hapo alizungumza na wananchi wa Afrika Kusini kupitia Chuo Kikuu cha Cape Town.

Akiwa nchini humo alieleza kuwa amekuja Afrika kwa dhumuni la kusaidia uwekezaji, sekta ya afya ikiwamo na kukuza demokrasia.

Akizungumzia kuhusu China, alisema kuwa hana tabu nao katika uwekezaji wao kwa nchi za Afrika ambako imefanikiwa kuwekeza kwa zaidi ya mabilioni ya dola ikilinganishwa na wao Marekani ambao hawajawekeza kwa kiasi kama hicho.

Obama ameisifia China kwa kuwekeza Afrika, lakini alitoa angalizo kwamba wasitumie fursa hiyo kwa kujinufaisha wenyewe na badala yake wawanufaishe na Waafrika kiuchumi kutokana na uwekezaji huo.

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO