Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MBUNGE NASSARI ASOTA POLISI AKIDAIWA KUMPIGA KADA WA CCM MAKUYUNI

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari jana alishikiliwa na jeshi la polisi mkoani Arusha kwa saa tatu na nusu kwa tuhuma za kumshambulia kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Warsama siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.

Nassari aliyefika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha saa 2:30 asubuhi jana ili kuitikia wito wa kutakiwa kuripoti kituoni hapo, alinusurika kuswekwa mahabusu baada ya kujidhamini mwenyewe majira ya saa saa 6:02 mchana na hivyo kuachiwa kwa dhamana.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha (RCO), Nassari anadaiwa kumshambulia Warsama Juni 16, mwaka huu, eneo Makuyuni alikokuwa wakala mkuu wa mgombea udiwani kupitia Chadema, Japhet Sironga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu zake zote mbili za kiganjani kuita bila kupokewa wakati RCO, Duwan Nyanda alisema Nassari aliripoti kwake.

Hata hivyo, alikataa kuzungumzia suala hilo kwa undani na kuelekeza atafutwe RPC ambaye ndiye msemaji wa polisi mkoani humo.

“Niko njiani nakwenda Dodoma, mtafute Afande RPC ndiye msemaji wa Polisi Mkoa,” alisema RCO Nyanda alipozungumza kwa njia ya simu jana.

Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatikana kutoka duru za polisi zimeeleza kuwa jeshi la polisi, lilianza kumsaka Nassari tangu Jumanne iliyopita, kupitia kwa Mkuu wa upelelezi wilaya ya Arumeru.

Habari hizo zilizothibitishwa na Nassari mwenyewe, zimeeleza kuwa Jumatano ya Julai 24, mwaka huu, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Polisi, Kamishina Isaya Mngulu, alimpigia simu mbunge huyo kumtaka afike polisi ndipo walipokubaliana kuwa angekwenda jana.

“Nilipofika polisi na kuripoti kwa RCO, nikawekwa chini ya ulinzi na kutakiwa kutoa maelezo kuhusu madai ya kumshambulia mtu mmoja, anayejulikana kwa jina la Hussein Warsama siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni,” alisema Nassari.

Mbunge huyo alisema baada ya kuwekwa chini ya ulinzi alikabidhiwa kwa ofisa  mwingine wa polisi kwa ajili ya mahojiano, lakini alikataa kuandikisha maelezo yoyote kwa sababu hakufuatana na wakili wake.

Alisema maelezo hayo yalionekana kuwakera polisi na RCO, kuagiza awekwe mahabusu hadi wakili wake, Tundu Lissu na Mabero Marando watakapofika, ambapo polisi kutoka wilayani Monduli walifika tayari kwa ajili ya kumchukua kumpeleka huko, kwa sababu tuhuma zinazomkabili zilifanyikia wilayani humo.

“Baada ya mimi kuwa tayari kuwekwa mahabusu na kuanza kukabidhi vifaa vyangu, RCO na maofisa wengine wa polisi, waliokuwepo walifanya majadiliano mafupi na baadaye kunikubalia kujidhamini mwenyewe, huku polisi wakiahidi kunipigia simu wakati wowote nitakapohitajika,” alisema Nassari.

Hata hivyo, wakati polisi wakimshikilia na kumhoji Nassari kwa tuhuma hizo, mbunge huyo pia alitoa tuhuma ya kushambuliwa hadi kulazwa hospitali ya Seliani, Arusha na watu aliodai kuwa makada wa CCM siku hiyo hiyo ya uchaguzi mdogo.

“Julai 14, mwaka huu nilivamiwa na watu wakiongozwa na Warsama huyu huyu anayedai nilimshambulia, nilitoa taarifa polisi lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa,” alisema Nassari.

Alisema ingawa hajajua aina ya makosa yanayomkabili, lakini ameshangazwa na hatua ya polisi kumweka chini ya ulinzi yeye aliyepigwa na kunusurika kuuawa na wafuasi wa CCM siku hiyo ya uchaguzi.

Kamanda wa operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi, Kamishina Paul Chagonja aliwahi kuwaeleza waandishi wa habari Jijini Arusha, kuwa jeshi hilo lilikuwa linamsubiri Nassari amalize kutibiwa na kutoka hospitali, ili wamhoji kuhusu tuhuma za kumshambulia kada wa CCM.

Aliporejea Arusha akitokea Dar es Salaam baada ya kutoka hospitali, Nassari aliwaeleza waandishi wa habari kuwa yuko tayari kutiwa mbaroni na polisi kujibu tuhuma hizo.

Naye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema kuwa wameshangaa kuona Polisi wanageuza kibao kwa Nassari wakati yeye ndiye alipigwa na kuumizwa na aliyepigwa hawakuwahi kumsikia hadi leo.

"Suala ili tutakutana kesho kujadiliana ili tuone cha kufanya, huku tukishauriwa na wanasheria wetu," alisema Golugwa.

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO