UCHAGUZI Mkuu wa mwaka 2015 ulikuwa na hamasa kubwa kutokana na vyama vikubwa vya upinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo.
Hamasa hiyo ilizidi pale wanasiasa wakongwe na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kujiunga na vyama hivyo huku Lowassa akiwa mgombea urais. Kutokana na hilo wagombea wa CCM katika majimbo mbalimbali walipata wakati mgumu huku wengine wakiangushwa. Lakini kwa upande wa Jimbo la Nyamagama ambalo lilikuwa likiongozwa na Ezekiah Wenje kutoka Chadema ilikuwa tofauti baada ya Stanslaus Mabula kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushinda.
MTANZANIA imefanya mahojiano na Mabula ambaye pia alipata kuwa Meya wa Jiji la Mwanza, ambapo pamoja na mambo mengine anasema alitumia udhaifu wa Wenje kushinda jimbo hilo.
MTANZANIA: Tueleze historia yako kwa ufupi
MABULA: Ni marafiki…unajua unapokuwa karibu na marafiki ambao unakaa nao inatokea wewe ukawa na rafiki yako akakushawishi kwamba unaweza kufanya jambo fulani na kwangu ndivyo ilivyokuwa nilishawishiwa na marafiki zangu basi nikakubali.
Nilipojaribu nikawa serious na nikapata ukamanda wa Kata ya Mkolani mwaka 2007. Baadaye nikaendelea na harakati na mwaka 2010 nikawa Diwani wa Kata hiyo ya Mkolani.
Nikaendelea kufanya jitihada baada ya uchaguzi mkuu nikagombea umeya mwanzoni sikupata kwa sababu mimi nilikuwa natokana na CCM na by then madiwani wa upinzani walikuwa ni wengi kwa hiyo sikupata na mwaka moja baadaye Halmashauri ya Jiji la Mwanza likagawanywa kuzaa Manispaa ya Ilemela kwa sababu ilikuwa ni jiji moja lakini ilikuwa na wilaya mbili. Kwa hiyo utendaji kazi wake ilikuwa ni ngumu na option ilikuwa either kuvunja wilaya moja na kubaki na halmashauri moja au kuwa na wilaya mbili na halmashauri mbili.
Septemba 2012 lakini kabla ya kuteuliwa mimi, Halmashauri ya Jiji la Mwanza, madiwani wake walimkataa meya ambaye alitokana na Chadema baada ya hapo ikatulazimu tukae kama miezi mitatu hivi ndio tukafanya uchaguzi na mimi nikachaguliwa hivyo nikawa meya mpaka tunamaliza hiyo awamu ya nne na baada ya hapo nikaona ninaweza kuwa Mbunge wa Nyamagana.
MABULA: Kwa upande wangu uchaguzi ulikuwa mgumu haukuwa mwepesi generally kama ambavyo ilivyo lakini maeneo ambayo naweza kusema kwamba ujue siku zote kwenye vita unatumia ‘weakness’ ya mwenzako, unapotumia udhaifu wa mwenzako unakupa faida ya kwenda mbele ndicho nilichokifanya mimi.
Na moja ya faida kubwa ni mbunge wetu wakati huo kutofanya wajibu wake, kutokaa kwenye jimbo alikuwa anafanya siasa za kitaifa akasahau kuwa wapo watu ambao walimtuma huko sasa hizo kwangu ilikuwa ‘advantage’. Nilipokuwa meya nilikuwa natumia kusimamia majukumu yangu kwa sababu mbunge hakuwepo muda mwingi jimboni hivyo shughuli zote za maendeleo zikawa chini yangu. Na wananchi wakanipima ndio maana sikupata sana tabu kwa hilo japo ushabiki ulikuwepo kuliko uhalisia lakini namshukuru Mungu wananchi walinielewa nini tunachokimaanisha kuwa tunatafuta fursa za kuwasaidia.
MTANZANIA: Kwa hiyo hata kwenye kampeni ulitumia udhaifu wa mbunge wa zamani?
MABULA: Hapana! Kwanza kwenye kura ya maoni, kwanini nasema uchaguzi ulikuwa mgumu sisi ndani ya CCM tulikuwa wagombea 20, kwa hiyo mimi ndio nikachaguliwa kwa zaidi ya kura 9000 baada ya kuchaguliwa, nilichokuwa nafanya kwenye kampeni si tu kueleza udhaifu wa mpinzani wangu japo hiyo ni moja ya faida.
Lakini pili wananchi nao wanataka kujua ni kitu gani ambacho ulichokifanya kwenye nafasi hata ndogo ulizopata kushika ili wapate taswira wakikutuma wajue unakwenda kuwafanyia nini.
Mimi nikawa na fursa ya kuwaeleza yale niliyoyafanya nilipoingia nikiwa meya niliikuta halmashauri ilikuwa katika hali gani na mpaka naondoka nimeifikisha kwenye kiwango gani na moja ya mambo ambayo niliyafanya sana ni yapi hilo ndio ilikuwa faida kubwa kwangu.
MTANZANIA: Ni kitu gani kikubwa ambacho ulikifanya katika Halmashauri ya Mwanza na ambacho wananchi wanakukumbuka?
MABULA: Kwanza kubwa sana ambalo l ni tatizo kubwa la ukusanyaji hafifu wa makusanyo ya mapato ya ndani yalikuwa ni Sh bilioni tatu, kazi kubwa niliyofanya ni kuhakikisha tunaimarisha ukusanyaji wa mapato. Kuanzia mwaka 2012 mpaka nakabidhi halmashauri tayari tulikuwa tunakusanya zaidi ya Sh. bilioni 11. Hiyo ilikuwa ni hatua kubwa sana kwangu ambayo ilinisaidia kutekeleza baadhi ya mambo kwa mfano ukienda kule Kata ya Igoma ambayo sasa imezaa Kata ya Kishiri kuna maeneo ya Fumagira Mashariki, Fumagira Magharibi na Kanenwa na Bukaga maeneo haya hayajawahi kuwa na maji kabisa.
Kwa hiyo nilijitahidi kuhakikisha tunajenga mradi mkubwa wa maji ambao umesambaa zaidi ya kilomita 18 lakini ukiwa na matoleo zaidi ya 25 ambayo watu 50 wanaweza kuchota maji kwa wakati moja kwenye tenki kubwa sana ambalo inahifadhi maji zaidi ya lita 220,000. Sasa ukigawa kwa lita 20 hivyo 11,000 wanaweza kupata maji kwa wakati moja, sasa unaweza kuona mtu ambaye alikuwa ananunua maji ndoo moja Sh. 500 mpaka 1000 leo anapata maji kiwango hicho bila gharama na hata akitumia gharama si zaidi ya Sh. 200.
Si hilo tu yapo maeneo ambayo yalikuwa hayajafunguka kimiundombinu tumejitahidi kuyafungua tumeongeza upimaji kama maeneo ya Buhongwa, Bulale na mengineyo. Kwa hiyo yote haya tumejenga jengo la kitega uchumi cha Rock City Shopping Mall ambayo ni ya kwanza na ya kipekee kwa nchi yetu na tafsiri ya mall ile ni kwamba tunaweza sisi kupata mapato zaidi ya asilimia kumi kutoka kwa wawekezaji na faida kutokana na ardhi tuliyowekeza sisi tunaweza kukusanya kodi za ushuru mbalimbali lakini pia kodi ya jengo.
Lakini vile vile tumejenga barabara za lami zaidi ya kilomita 18 kwa kushirikiana na World Bank kwa hiyo mambo yote haya na si hilo tu hii itatusaidia kupata awamu ya kwanza na ya pili ambayo inatekelezeka hivi sasa ambayo na yenyewe ina kilomita nne kwa hiyo pale mjini katikati yote kufika Julai au Agosti zitakuwa zimejaa lami. Tumejenga pia barabara za mawe kwa kilomita 3.5 tumejenga kwa Sh. milioni moja gharama hii ni nafuu na kilomita inakuwa ndefu huu ni ubunifu na kwa sasa tunasisitiza mfuko wa barabara. Tukipata mfuko wa barabara tutajenga barabara za mawe zaidi yote hayo ni mambo ambayo nimeyafanya huko nyuma.
Kwa fursa hii ya kupata ubunge sasa ni namna ya kushirikiana na meya wa sasa wa Jiji la Mwanza kama team na baraza la madiwani ili yale niliyokuwa nayafikiria nikiwa meya tuyafanye na kazi ya mbunge ni kusukuma Serikali kuu. Kwa mfano mji wa Mwanza una ongezeko kubwa na unakua kwa kasi kubwa, msongamano wa watu ni mkubwa lakini wageni wanaingia kwa asilimia 8.2 na tafsiri yake tunaongeza wajasiriamali na wawekezaji pamoja na biashara zingine zisizo rasmi nyingi.
yote yanatokana na viwanda vyetu kutofanya kazi kwa hiyo tunayaangalia ni namna gani ili tuweze kupiga hatua. Kwa mfano kilio changu kikubwa hivi sasa ni kuunganisha barabara ya kutoka Buhongwa, Ruhanima, kutokea Kishiri kwenda Kanindo hadi Igoma tutakuwa tumeunganisha Nyamagana na kata zingine hivyo hiyo itasaidia kufungua fursa kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo. Lakini pia kuna matatizo ya umeme tumejitahidi kuweka umeme, tuna mitaa 175, 90 kwa jiji bado haitoshi tunaposema jiji lazima vitu muhimu kama haya yanareflect na mahitaji ya wananchi.
MTANZANIA: Wenje alilalamikia ushindi wako mpaka akaenda mahakamani, hili unalizungumziaje?
MABULA: Kwanza Watanzania wajifunze tabia ya kukubali…maana na mimi nashukuru amekwenda mahakamani kwa sababu sehemu pekee ya kupata haki ni mahakamani. Mahakama ikampa haki ya kumsikiliza, inawezekanaje unasema umepokonywa ushindi halafu huna vielelezo vya kuonyesha ushindi uliopata. Mfano ndugu mwandishi nikisema hii simu ni ya kwangu na wewe unasema hii simu ya kwako kitakachothibitisha kuwa ni ya kwangu ni risiti ya manunuzi. Unaposema umeshinda mimi nilikuwa na mawakala na yeye alikuwa nao pia.
Alipewa siku kumi kuwasilisha vilelezo vyake halafu hajafanya hivyo, kura zimepigwa kwenye mitaa na kazi ilikuwa ndogo tu ni yeye kuleta hivyo vielelezo lakini yeye katika mawakala 693 akaleta 600 tu unaweza kuona kwamba huyu hakujiandaa na alichokuwa akisema hakikuzungumzika maana mimi leo nikisema nilikuwa mshindi nitakuja na vielelezo vyangu huwezi kuja na laptop kwenye chumba cha kujumlishia matokeo halafu unataka watu waendane na matokeo yako, hilo haliwezekani. Wananyamagana walishaamua kwamba sasa wampe mtu mwingine kwamba tulimpa mtu miaka mitano hakutekeleza kama alivyoahidi sasa tumeamua kumpa mtu mwingine.
Ilivyofika hatua kwamba anatakiwa kuleta vielelezo na muda aliotumia haukutosha, lakini sheria alizotumia haikuwepo na Mahakama ikatumia utaratibu kwamba hakujiandaa kwa sababu alishindwa kuwasilisha vielelezo kwa muda.
MTANZANIA: Vipi kuhusu fidia, amekulipa?
MABULA: Aahh! Tunasubiri muda wa pili kwake ni siku 30 na mimi nina siku 60 za kuamua aidha nimdai au vipi lakini na mimi ni binadamu pia nitaangalia.
MTANZANIA: Kwa hiyo unaweza kumsamehe?
MABULA: Lolote linaweza kutokea lakini kama nilivyosema tumetumia muda wetu mwingi tumepata usumbufu, tungekuwa tumeshaanza kufanya shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Nyamagana kwa hiyo lolote tunaweza kufanya kumdai hizo fedha tuzichukue ziwasaidie wananchi au tuziongeze kwenye zile milioni 50 za kila kata ambazo Rais John Magufuli aliziahidi ili zisaidie maendeleo ya wananchi.
MTANZANIA: Una matarajio gani kisiasa kwa ziku zijazo?
MABULA: Ni kuwa mwanasiasa mkubwa. Namaanisha kwamba sifikirii kama nitakuwa mbunge wa term moja, nifanye kazi yangu kwa bidii na kwa maono ya mbali sana.
MTANZANIA: Unazungumziaje mwenendo wa Bunge kwa sasa na lililopita?
MABULA: Sisi tumekuwa nje ya Bunge, kikubwa ambacho ninakiona na ambacho ninajifunza inashangaza wabunge wanapokuwa nje wanakuwa marafiki lakini ninaumia wanapokuwa ndani wanakuwa maadui wanatukanana hakuna anayemheshimu mkubwa. Mimi naamini kama ndani tungekuwa marafiki tungewasaidia sana wananchi.
MTANZANIA: Unazungumziaje kuhusu kusitishwa kwa matangozo ya Bunge ya moja kwa moja?
MABULA: Unajua mfumo wa mabunge yetu tunachukua kwenye mabunge mengine si lazima tuige kila kitu na kutokana na haya yanayoendelea sioni sababu ya Watanzania kushuhudia upuuzi unaofanyika.
0 maoni:
Post a Comment