Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob amebaini matumizi ya Sh392 milioni zilizoandikwa kwenye taarifa ya manispaa hiyo kuwa zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Sinza - Igesa ambao haukufanyika.
Katika taarifa ya manispaa hiyo, fedha hizo zilidaiwa kutumika kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hiyo.
Akizungumza kwenye ziara ya Kamati ya Uchumi na Fedha ya Manispaa hiyo, Jacob alisema ni ajabu kuona hakuna matengenezo yoyote yaliyofanyika kama taarifa hiyo inavyoelezwa huku fedha zikionekana kulipwa.
Alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika kwenye matumizi hayo huku akiiomba Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuchunguza matumizi ya fedha hizo.
“Fedha hizi zinaonekana zimelipwa kwa mkandarasi Skol Building Contract Ltd wakati barabara ina mahandaki na mashimo makubwa, ikionyesha kwamba haijakarabatiwa,” alisema.
Alisema kama wasingeamua kukagua thamani ya fedha za halmashauri hiyo zinavyotumika kwenye miradi hiyo katika kipindi cha Jaruari hadi Machi mwaka huu wasingegundua udanganyifu huo.
Meya huyo aliyeonyesha kukasirishwa na hali hiyo, aliwataka wataalamu wa halmashauri hiyo waliohusika kuandika ripoti hiyo kutoa maelezo ya kina kuhusu udanganyifu huo.
“Hivi kama tungenyamaza tusiamue kukagua miradi hii nani angesimama kueleza hayo? Mnaleta hadithi wakati tayari mmeshalidanganya Baraza la Madiwani kwamba fedha hizi zimetumika kukarabati barabara hii?” alisema.
Akitetea matumizi ya fedha hizo, mchumi wa manispaa hiyo, Huruma Eugen alisema zilizoandikwa kwenye taarifa hiyo zimetumika kwa ajili ya kulipa madeni ya nyuma.
Huku kukiwa na mabishano baina yake na Meya, Eugen alisema awali, ujenzi wa barabara hiyo ulifanyika kwa kukopa kutoka fedha za Mfuko wa Barabara, jambo lililowafanya watumie fedha za mapato ya ndani ya halmshauri kulipa deni hilo.
“Hela ilitoka kwenye mfuko wa barabara na imerudishwa kwenye akaunti, japo huku imeandikwa imelipwa kwa mkandarasi aliyejenga barabara hii,” alisema Eugen.
Hata hivyo, Meya huyo alisema kama fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kulipa madeni zingeonyesha wazi kwenye taarifa hiyo badala ya kuandikwa kwamba zimeelekezwa kwenye ukarabati wa barabara, wakati jambo hilo halijafanyika.
Diwani wa Sinza, Godfrey Chindaweli alieleza kushangazwa na taarifa inayoonyesha ukarabati wa barabara hiyo wakati ni miongoni mwa barabara zenye mashimo kwenye kata yake.
Alisema mara kadhaa amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ubovu wa barabara hiyo na kuahidi kuikarabati akidhani ipo kwenye mpango.
“Nimeshangaa kuona miongoni mwa miradi iliyotumia fedha za robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha, barabara ya Sinza ambayo haijaguswa ipo kwenye orodha, jambo hili linahitaji majibu ya haraka,” alisisitiza.
Diwani wa Makongo, Ndeshukuru Tungaraza aliwataka wataalamu wa halmashauri hiyo kueleza ilikuwaje fedha ziandikwe kwamba zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara wakati hazikutumika kwa kazi hiyo.
Tungaraza alisema hakuna sheria ya matumizi ya fedha inayoelekezwa kufanya kama ambavyo manispaa hiyo imefanya, jambo ambalo madiwani hawatakubaliana nalo.
Katika eneo la Mwananyamala kwenye Barabara ya Akachube inayoelekea kwenye kituo cha daladala cha Makumbusho, Meya huyo aliwaagiza wahandisi aliowakuta wakiendelea na ujenzi kukamilisha haraka ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Alisema malalamiko mengi ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara yanatokana na uzembe wa kutosimamia kwa ukamilifu miradi iliyopo.
Hata hivyo, mkandarasi wa kampuni ya Delmonto, Rajab Athman alisema wanashindwa kukamilisha kwa wakati barabara hiyo kutokana na kupasuka kwa mabomba ya maji.
“Maji yanamwagika mengi, hivyo tunawasubiri Dawasco wakishakamilisha kutengeneza mabomba yaliyopasuka tutaendelea kujenga,” alisema.
Mwananyamala
Katika ujenzi wa Jengo la Bima ya Afya, katika Hospitali ya Mwananyamala linaloendelea kujengwa, Meya Jacob alionyesha wasiwasi wa jengo hilo kukamilika mapema kabla mpango wa matumizi ya bima kwa wananchi wote kuanza.
“Mpango huu unatarajia kuanza Julai lakini mpaka sasa hali inaonyesha halitakamilika kwa wakati, jambo hili linanipa wasiwasi,” alisema.
Chanzo: ChademaBlog
0 maoni:
Post a Comment