Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Makala ya Mwananchi - Je, sababu hizi zinatosha kuiangusha Ukawa 2015?

Siasa inabadilika kadri siku zinavyokwenda, hivyo kitendo cha kuungana kwa vyama vikubwa vya siasa  katika taifa lolote Afrika siyo jambo la kushangaza.

Ipo mifano ya vyama katika nchi kadhaa za Afrika vilivyojaribu hatua hiyo na kufanikiwa.

Kwa mara ya kwanza hapa nchini, vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF vimeamua kuunda kambi moja ya kuelekea Ikulu ili kuongeza nguvu na ushawishi, umoja uliochochewa na mwenendo wa CCM wakati wa mchakato wa Katiba.

Baada ya kukerwa na mwenendo wa mchakato ndani ya Bunge la Katiba, vyama vya upinzani viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa lengo la kutetea Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Lakini umoja huo sasa umejiegemeza katika  mkakati wa kuimarisha upinzani na kuiondoa madarakani CCM.

Msukumo wa kuunda umoja huo ulitokana na CCM kudaiwa kuhodhi mchakato huo kwa lengo kupenyeza ajenda zake, ikiwamo kulazimisha ajenda ya ya muundo wa serikali mbili kwenye Rasimu ya Katiba, ajenda ambayo haimo kwenye mapendekezo hayo.

Fukuto lao kwa sasa linaendelea nje ya Bunge kupitia ziara za Ukawa kwenye mikoa 17 huku CCM nayo ikifanya mikutano yake kwenye mikoa mbalimbali kudhibiti kukua kwa Ukawa.

Mmoja kati ya viongozi wa Ukawa ambaye ni mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anasema  matumaini ya mpango wao kufanikiwa ni makubwa kutokana na maandalizi yao.

Anasema baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, umoja huo uliunda kamati yenye wajumbe watatu kutoka kila chama kwa ajili ya kufanya kazi ya kuandaa tathmini, mipango na mikakati ya kutengeneza uwezekano wa kufanikiwa harakati hizo.

“Tulichokubaliana kwa sasa ni kukamilisha kwanza chaguzi za ndani kwa kila chama halafu ndiyo tuingie kwenye hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya kamati hiyo,” anasema.

“Baadhi ya wajumbe wake ni pamoja na makatibu wakuu wa Chadema ambaye ni Dk Wilbroad Slaa, Julius Mtatiro (CUF) na Mosena Nyambabe (NCCR-Mageuzi). Matumaini ni makubwa kwani hata Watanzania wamepokea uamuzi huo kwa furaha na uzalendo mkubwa.”

Uchambuzi wa wadau

Hata hivyo, ajenda hiyo imejengewa hofu ya kukwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mtandao wa CCM uliotapakaa nchi nzima, elimu ndogo ya kupiga kura ya wananchi, mchakato wa Katiba mpya na nyingine kadhaa.

Dk Benson Bana kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema dhambi itakayowatesa Ukawa katika uchaguzi mkuu ujao ni pamoja na kuhamishia ajenda ya Ukawa kwenda uchaguzi mkuu 2015.

Anasema kukubalika kwenye ajenda ya Katiba mpya, hakumaanishi kukubalika kwenye mambo mengine na hivyo  kubadilisha ajenda hiyo kuwa chombo cha kuwapeleka Ikulu.

“Watanzania wanaelewa kila kitu, waliwaamini kwenye Bunge la Katiba, lakini ipo tofauti kubwa kwani kuna mambo mengi yanayojenga hofu ya kufanikisha hilo,” anasema Dk Bana.

“Hivi mgombea urais watakayempitisha, ataongoza kwa sera za chama gani? Je, wananchi watakubaliana kwa pamoja. Hivyo dosari hiyo inaweza kuwakwamisha katika uchaguzi mkuu ujao.”

Akiunga mkono hoja hiyo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mkufunzi wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Dk Maria Semakafu anasema endapo wanahitaji kuongeza nguvu ni vyema waunganishe kwanza sera, itikadi na falsafa zao.

“Wasitumie hoja ya Ukawa, warudi nyuma na kujipanga upya. Waangalie jambo lipi litasimamiwa na chama kipi ndani ya Muungano wao, isije ikawaathiri zaidi badala ya kuwaletea tija,” anasema.

“Endapo wataendelea na hoja ya Katiba mpya kwa kupinga muundo wa serikali. Watanzania wengi wanaweza kuwakwepa wakiwamo Wazanzibari wanaokubaliana na serikali mbili, hivyo  watakuwa wamepoteza kisiasa.”

Mtazamo wa wengine

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, vyama vyote vya upinzani viligawana asilimia 49 ya kura zote zilizopatikana katika nafasi ya mgombea wa kiti cha urais baada ya Rais Jakaya Kikwete kuibuka kidedea kwa zaidi ya asilimia 61.

Mbali na hatua hiyo, Dk Semakafu anasema hoja mpaka sasa ni idadi ya wapigakura imekuwa ni ugonjwa unaotesa nchi nyingi duniani kutokana na kufifia matumaini kwa wanasiasa.

“Watu wanaangalia tija ya kupiga kura kama hawaoni umuhimu wowote hakuna sababu hiyo. Mataifa mengine yanaamua kutumia nguvu ya mahakama kulazimisha watu kupiga kura. Sasa Ukawa wanaungana, lakini wapiga kura je,” anahoji.

“Ni vigumu kumshawishi mwananchi anayemwamini mgombea wa chadema kupigia kura mgombea wa CUF. Anayekubalika Bara, siyo lazima akubalike Zanzibar.”

Nguvu ya CCM vijijini

Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa hivi karibuni, katibu mkuu wa CCM, Abdulrahiman Kinana anasema mpaka sasa  chama kina hazina ya asilimia 94 ya viongozi ngazi ya serikali za mitaa, asilimia 74 katika uwakilishi wa viti vya wabunge na asilimia 86 katika ngazi za halmashauri.

Pamoja na hazina hiyo, Kinana anasema pia kuna mabalozi 986,000 katika vijiji kote nchini huku kukiwa na akiba ya wanachama hai zaidi ya milioni 6 hadi sasa.

Kutokana na mazingira hayo, Kinana anasema nafasi ya upinzani ni ndogo katika uchaguzi mkuu ujao. Anaongeza akisema CCM bado inaaminiwa na Watanzania kwa kiwango kikubwa tofauti na mitazamo ya makundi yanayoipiga vita CCM.

“Hata wakiungana hawawezi kufikia mtaji wa CCM tulionao vijijini, hizo kelele zinazoishia mjini , ambako kuna asilimia ndogo sana ya wapigakura, wengi wao wako vijijini ambao pia wanaoona matunda ya CCM japokuwa bado zipo changamoto,” anasema Kinana.

Kinana anasema ahadi nyingi zilizoahidiwa mwaka 2010 zimeshatekelezwa katika maeneo mbalimbali na kwamba hiyo ndiyo sababu ya CCM kupewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.

Hata hivyo, Kinana anasema kwa sasa hakuna vyama pinzani  vinavyoonyesha ushindani wa siasa safi.

“Badala yake tunaona makundi ya wanaharakati tu, tunahitaji vyama pinzani vya kuikosoa, kuishauri CCM, lakini  hawa kazi yao kutukana CCM tu,” anasema.

Uzoefu wa uchaguzi Kenya

Uchaguzi mkuu uliofanyika majimbo 290 nchini Kenya mnamo Machi 4, mwaka jana ulifanyika chini ya upinzani mkali kutoka vyama vya siasa vilivyoungana katika makundi manne ambayo ni Amani Coalition, Pambazuka Coalition, Eagle Alliance na Jubilee Alliance.

Katika uchaguzi huo, muungano wa Jubilee kupitia vyama vya TNA, URP na UDF uliibuka kidedea katika safari ya Ikulu nchini humo chini ya Rais wake, Uhuru Kenyata.

Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, mmoja kati ya viongozi wa umoja huo ambaye ni mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia anasema hakuna aliyekuwa akiwaza kwamba leo Ruto (William) angekuwa Makamu wa Kenyatta (Uhuru) kwenye Serikali ya Kenya.

Mbatia anasema muungano wa vyama hivyo kupitia Ukawa umekuwa darasa kwa viongozi wakuu wa vyama husika kutafakari walikotoka, walipo na wanakokwenda.

“Tunapata nafasi ya kutafakari na kujifunza kwa kurejea tulikotoka,” alisema.

 

CHANZO: GAZETI MWANCHI JUNI 25, 2014

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO